- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Vita Virefu Zaidi vya Amerika
(Imetafsiriwa)
Vyombo vya Habari vya kilimwengu vimejaa taarifa ya kuondoka kwa vikosi vya Amerika nchini Afghanistan. Vita vya Amerika hadi sasa vimewagharimu walipa kodi wa Amerika zaidi ya dolari trilioni 2, vifo vya askari 2,488, huku wengine 20,722 wakiwa walemavu. Katika tamko la Ikulu ya White House mnamo siku ya Jumatano April 15, Raisi wa Amerika Joe Biden alisema ni “wakati sasa wa kumaliza vita virefu zaidi vya Amerika, mimi hivi sasa ni raisi wa nne wa Amerika kuongoza vikosi vya Amerika vilivyopo Afghanistan, Wana-repulican wawili, Wana-democrat wawili. Sitolipokeza jukumu hili kwa (raisi) wa tano.” Lakini wakati Amerika inazungumza juu ya jeshi lake kuondoka Afghanistan, nchi hiyo haiachii maslahi yake ya kimkakati.
Amerika ilicheza dori muhimu nchini Afghanistan wakati wa uvamizi wa Usovieti kutoka mwaka 1979 hadi 1989. Lakini wakati wa kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991 na kuibuka kwa jamhuri mpya 5 katika Asia ya Kati, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni kubwa ya huduma za mafuta alisema: “Siwezi kufikiria muda ambao tungekuwa na eneo lenye kuibuka kwa haraka na kuwa muhimu na la kimkakati kama eneo la Caspian.” Makampuni ya nishati ya Amerika yameiona nishati ya Asia ya Kati kama Mashariki ya Kati Mpya. Wakati Urusi ikiendeleza tu maeneo ya nishati nchini Urusi, hii inapelekea nishati katika Caspian na Asia ya Kati kubakia bila kuendelezwa na kusafirisha nishati kutoka Asia ya Kati kwendea masoko ya magharibi kuwa ni (suala) lenye kutawala utungaji sera wa Amerika.
Maeneo ya Caspian na Asia yakiwa yamefungika na kukosa njia ya kufikia baharini, kusafirisha nishati ya eneo hilo kunahitaji njia mpya ya mabomba. Kuunganisha Asia ya Kusini na Asia ya Kati kupitia njia mpya ya mabomba kumeonekana ni mkakati wa umuhimu. Njia hiyo inahitaji kupitia Iran au Afghanistan, na hivyo kuifanya Afghanistan kuwa na umuhimu. Kampuni ya mafuta ya Amerika UNOCAL ilianza maelewano mwaka 1995 kujenga njia ya mabomba ya mafuta na gesi kutoka Turkmenistan, kupitia Afghanistan kuelekea bandari za Pakistan kwenye bahari ya Arabuni. Hatimaye njia hii haikufanikishwa kwa kuwa UNOCAL haikuwa na uhakika wa kufanikiwa kiuchumi. Lakini wawekaji sera wa Amerika wakabadilisha mradi wa UNICOL kwa TAPI (Turkmenistan, Afghanistan, Pakistan, India) njia ya mabomba ya gesi inayounganisha Caspian na Asia ya Kati kutokea Turkmenistan kupitia Afghanistan hadi Pakistan na India. Amerika imetoa msukumo wa nguvu kwa njia hii kwani itakuwa ni njia ya kudhibiti rasilimali za hydrocarbon za Bahari ya Caspian pamoja na usalama na upitishaji.
Lakini Taliban iliingiza miguu yake na Amerika ikapoteza uvumilivu kwao na ikaona kuwa kubadilisha utawala ni njia bora zaidi ya kuwashughulikia Wataliban na kuhifadhi malengo yake ya mikakati juu ya kuibuka kwa Asia ya Kati. Uvamizi wa Afghanistan ulitokea wakati maafisa wa Amerika, waundaji sera na makampuni yake ya nishati yalipoiona Kabul (Afghanistan) kuwa ni njia ya kuelekea Asia ya Kati. Mabadiliko ya utawala nchini Afghanistan kupitia uvamizi wa kijeshi na kuitwaa ilikuwa njia ya kufikia sera ya kigeni ya Amerika katika Eurasia.
Wakati Amerika na muungano wa washirika wake walipoivamia Afghanistan mwaka 2011, iliweza kuwatoa Wataliban nje ya mji wa Kabul. Kisha Amerika ikaendelea na uundaji wa serikali ya wababe wa kivita mafisadi walioungana pamoja kutokana na chuki zao kwa Taliban. Serikali kuu ya Kabul iliendelea na uraisi wa kubahatisha wa Hamid Karzai kwa miaka kadhaa lakini haikuwa na uwezo wa kuiunda nchi zaidi ya afisi zake za serikali. Vikosi vya usalama ambavyo Amerika imevijenga kwa gharama na kuvifunza, hadi leo, baada ya miaka 20 haviwezi kuweka usalama katika nchi. Amerika imeangukia kuwa muhanga wa hali sawa kama ya Umoja wa Kisovieti na Uingereza ilivyoangukia kabla na kuwa vikosi vamizi, katika kipindi kirefu cha mbele vinajiangamiza vyenyewe katika jaribio la kuishinda Afghanistan. Amerika ilianza kuilenga Iraq kutoka 2005 lakini katika nchi zote mbili ambazo Amerika imezivamia imekuwa wazi kuwa inaweza kuzivunja tawala lakini kikawaida inashindwa katika uwezo wa ujenzi wake wa kitaifa.
Kutokea 2010 Amerika imeona chaguo la kijeshi limekuwa ni kushindwa na imegeukia kwenye diplomasia kufikia malengo yake ya kimkakati ya kuitumia Afghanistan kuifikia Asia ya Kati. Katika hili imetumia mataifa yote yanayoizunguka kuituliza Afghanistan. Pakistan, Iran, Urusi, India na China zote zilicheza dori muhimu katika kuisaidia serikali ya Kabul iliyoundwa na Amerika na kuwaleta Taliban katika meza ya mazungumzo. Hivi sasa Wataliban sio tu wameshakuja kwenye meza ya mazungumzo bali mwaka 2020 walitia saini mkataba wa amani na Amerika. Mkakati wa kisiasa wa Amerika wa kuishirikisha Taliban unahusisha kuwapatia nafasi ya kugawanya madaraka pamoja na Kabul. Hii itawapatia wanachama wa Taliban nyadhifa katika utawala na hivyo kuituliza Afghanistan.
Baada ya vita vilivyochukua muda mrefu zaidi ya Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia, Amerika haikutaka kubakisha uwepo wa kudumu nchini Afghanistan. Inataka kuidhibiti Afghanistan kwa kutumia gharama ndogo kabisa na uwepo wake kijeshi umeshachukua muda mrefu kuliko ilivyotegemea. Amerika ikiwa ni dola kuu ya ulimwengu ina masuala kadhaa ya kiulimwengu ya kuyashughulikia na Afghanistan ni sehemu moja tu ya masuala hayo mengi. Uvamizi wa kijeshi wa Amerika ni njia ya kufikia lengo, umekuwa ni kwa ajili ya tamaa ya kupata vyanzo vya nishati kwa njia haramu, kusafirisha na njia za mabomba ya mafuta za Asia ya Kati. Amerika hivi sasa imekuwa ikitumia diplomasia ambapo mikakati yake ya kijeshi imeshindwa kufikia malengo yake ya kimkakati kwa ajili ya Asia ya Kati. Wakati jeshi la Amerika likiondoka Afghanistan, Amerika haitoiacha nchi hiyo au maslahi yake ya kimkakati.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Adnan Khan