Jumatano, 01 Rajab 1446 | 2025/01/01
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Vita nchini Ukraine na Vidokezo Vinavyotegemewa kwa Amerika

(Imetafsiriwa)

Vita vya sasa nchini Ukraine vimechokonoa boksi la Pandora la mjumuiko mpya wa mambo magumu na mizozo kote duniani ambapo vita havielekei kumalizika karibuni. Vita vingi kupitia historia vimekuwa na athari kubwa juu ya muelekeo wa kipindi cha baada ya vita. Ni jambo lililo wazi kuwa vita vya Urusi na Ukraine havitokuwa tafauti ambapo vita vikimalizika vitaacha nyuma athari ya kumbukumbu juu ya hali ya mandhari ya siasa ya kidunia inayoathiriwa na jiografia ambapo vita vijavyo huenda vikatokana na vita vya sasa vya Urusi na Ukraine. Ni kama vita vilivyopita, vyote viliweka vitangulizi kwa ajili ya vita vijavyo kuweza kutokea. Vita vya Kwanza vya Dunia vilitokana na uzawa wa vita vya Ulaya wakati wa zama za mfumo wa uzani wa nguvu za Ulaya; Vita vya Pili vya Dunia vilitokana na vya Kwanza; Vita Baridi vilitokana na vya Pili na vita vya Iraq, Somalia na Afghanistan vilitokana na mpango wa baada ya 1991 - baada ya Vita Baridi.

Hivyo, ni muhimu kuiweka hali ya sasa ya dunia kuweza kutambua namna mazingira ya baadaye yatakavyo weza kubainika ndani ya mandhari ya kisiasa ya kiulimwengu na hatari mpya za kisiasa zitakazotokea kutokana nayo, kwa kuwa ni katika maslahi ya ummah kufahamu fursa mpya na mashaka yawezayo kutokea, ambayo yanaweza kutumika kwa ajili ya kusimamisha Dola ya Khilafah (kwa njia ya Utume). Bwana wetu Muhammad (saw) alikuwa katika ufuatiliaji wa kuendelea wa matukio ya kisiasa ili kuzitumia fursa mbali mbali zinazotokea kwa kipindi kifupi kwa kuisimamisha, kuimakinisha na kuitanua dola ya Kiislamu ili kuwainua watu na kueneza uadilifu na neema kote ardhini. Kutokana na juhudi za awali za Mtume (saw) na Masahaba zake, hadhara ya Kiislamu ilistawi kwa karne nyingi. Makhalifah wengine wengi, magavana na viongozi wa kijeshi walirithi fikra sawa ya kisiasa ya kupatiliza fursa kwa ajili ya kueneza umuhimu wa Uislamu. Kwa mfano, Sultan Muhammad Fatih aliendelea kufuatilia matukio halisi ndani ya Ulaya, yaliyompelekea kuunda sera ya kutumia mfarakano baina ya Magharibi na Mashariki (Himaya ya Roma). Ya mwanzo ilipelekea ukombozi wa Konstantinopli (ilioitwa baadaye Istanbul) ambayo ilikuwa ni ishara kiongozi ya hadhara ya Kiislamu.

Mwanzo, ni muhimu kufahamu sababu za vita vya Ukraine na msukumo wa Amerika na Urusi na wadau wengine wanaohusika, katika nukta zifuatazo:

1. Kwa Urusi, Ukraine ni sehemu kiunganishi ikiwa kama ni fahari yake kuu ya kihistoria na fikio la mandhari ya kisiasa inayoathiriwa na jiografia: Ukraine bila Urusi inabakia ni Ukraine, lakini Urusi bila Ukraine inasita kuwa dola kuu iliyovuka mipaka ya bara. Tokea wakati wa zama za Czar, Urusi ilikuwa na maeneo matatu - hadi 1991 ambayo ni muhimu kwa ubwana wa Urusi. Urusi nyeupe (Belarus), Urusi ndogo (Ukraine) na Urusi kubwa. Cheo cha Czar kilikuwa ni “mfalme wa Warusi wote”. Zaidi ya hayo, hadi leo, kiongozi wa Kanisa la Mashariki la Moscow anaitwa “Askofu Mkuu wa Warusi wote”. Rus inajumuisha maeneo ya zamani ya Belarus na Ukraine. Hivyo, historia hii ya ndani imekita miongoni mwa tabaka teule la Warusi na sehemu kubwa ya watu wake hadi hivi leo. Kwa sababu hii, Urusi haitoiwacha Ukraine. Kwa namna moja au nyengine, Urusi lazima itekeleze jukumu fulani la uongozi ndani ya Ukraine. Kutokana na sababu hiyo, ndio inaonekana kwa nini Vladmir Putin ameamua kukusanya idadi kubwa ya vikosi mbele ya mipaka ya Ukraine ili, matokeo yake, apate uhakikisho wa kuwa Ukraine haitopata kuingizwa ndani ya mamlaka ya muundo wa usalama wa Amerika - NATO. Kwani wakati huo itakatisha moja kwa moja matumaini ya kuipata tena Ukraine.

Pia, kile kilichomkasirisha zaidi Putin kuchukua hatua hizo kali ni kutokana na mazoezi ya kijeshi ya NATO kufanyika ubavuni mwa Ukraine jirani kabisa na mipaka ya Urusi mnamo 2021. Mbali na kutaja ushindi wa Azerbaijan inayopitia kwa muungaji mkono mwengine Uturuki ambayo pia ni mwanachama wa NATO na rasilimali ya Amerika, imedhoofisha mandhari ya kisiasa ya kijiografia ya eneo la kusini la Urusi. Hata hivyo, mazoezi ya kijeshi ya mwaka jana yalikuwa ni mstari mwekundu, ambayo yaliilazimisha Kremlin kuchukua hatua za adhabu kuzuia muingilio wa Amerika kwenye maslahi ya kisiasa yenye kuathiriwa kijiografia ya Urusi.

2. Kimsingi Putin hakukusudia kuivamia Ukraine; bali, alipanga kutumia ukusanyaji wa vikosi ili ifikie lengo la kisiasa la kuigawa Ulaya na, pia, kuilazimisha Ukraine kusitisha mapenzi yake na NATO na kinyume chake. Mshangao kwa vikosi vya Urusi karibu na mipaka ya Ukraine mwanzoni ulikuwa ni mkakati wa adabu kusababisha hali ya kuwa na mashaka na wasiwasi miongoni mwa watu wa Ulaya kuhusiana na hali ya kijeshi mpakani. Kremlin ilihitaji kutumia askari 100,000 jirani na mipaka ya Ukraine kucheza na hali ya mashaka kwa watu wa Ulaya na kupanda mbegu za kuwagawa. Kabla ya uvamizi, Ufaransa, na Ujerumani hasa, hawakuwa na ufasaha unaolingana kama watu wa Ulaya ya mashariki mfano Poland, Lithuania na Ukraine zilizojaribu kukusanya msaada madhubuti wa kila mtu dhidi ya matendo tata ya kijeshi kwenye mipaka ya Ukraine. Ufaransa, kwa upande mwengine, imeendelea kufuata urafiki wa Urusi katika juhudi za kuitenga Amerika na Ulaya. Kwa miaka mingi, kauli za Macron juu ya NATO ni “Akili iliokufa”, Ulaya inahitaji “Muundo wa usalama ulio kando na Amerika” na “Uhuru wa kimkakati wa Ulaya” zote ni kauli za kuimarisha sera ya kihistoria ya Ufaransa ya usawazisho wa Amerika kwa bara (la Ulaya) kupitia Urusi, kwa kutegemea badala yake kupata matumaini mapya ya ubwana wa Ufaransa barani Ulaya. Ujerumani pia, imekataa kuchukua msimamo usio dhahiri kuelekea mkusanyiko wa vikosi kwenye mipaka ya Ukraine. Pia, Berlin imekataa kusimamisha ununuaji wa gesi kutoka Urusi na kukataa kutoendelea na mradi wa bomba la mafuta la Nord Stream 2. Mwishoni mwa Disemba 2021, Ukraine iliisuta Ujerumani kwa kuzuia mahitaji ya NATO kuelekea Kyiv, ambapo waziri wa ulinzi wa Ukraine alisema, “Wanaendelea kujenga Nord Stream 2 na wakati huo huo wanazuia silaha zetu za kujihami. Hii sio sawa”. Kwa hiyo, kabla ya uvamizi wa kijeshi usio na maana, Kremlin iliimarisha msimamo imara kwa kuwa ilichochea wasiwasi, mkanganyiko na mgawanyiko miongoni mwa watu wa Ulaya, kitu ambacho, kwa kweli kiliiweka Amerika katika hali ya mashaka.

3. Kwa mujibu wa uoni wa Amerika, mkakati pekee unaoweza kutumika kuhifadhi na kumakinisha ubora wa Amerika kwa Ulaya ni kukemea uvamizi. Kama Urusi, ingebakia katika mipaka ya Ukraine bila kufanya uvamizi wa kijeshi, ingeweza bila shaka kuandalia njia kwa maslahi mapana ya mataifa ya Ulaya kuwa mawindo ya usaliti wa Urusi. Ujerumani ingebakia kuwa imara juu ya mradi wa Nord Stream 2, Wafaransa wangeweza kuendelea na juhudi za ghilba zao za usuhuba wa Ufaransa na Urusi kuitenga Amerika na Ulaya, na watu wa Ulaya mashariki wangeweza kuutilia shaka uaminifu wa Amerika kutokana na matukio ya awali -kama yatakuwa na umuhimu mkubwa - kwamba namna gani Amerika inaweza kuruhusu matukio kama hayo kufanikiwa wakati usalama wao ulikuwa chini ya tishio la Urusi likigonga mlango. Hata hivyo, kabla ya uvamizi wa Urusi, Amerika ilipanga kuikemea Urusi kwa kipindi fulani.

4. Mnamo miaka ya 1990, Amerika ilitumia mtazamo hasi wa watu wa Ulaya mashariki kwa Usovieti mpya kubakisha uhusiano na NATO. Ambapo baada ya Vita Baridi, Amerika ilihalalisha utanuzi wa NATO kuelekea mashariki, lakini sio kwa sababu Urusi ilikuwa tishio kubwa bali, kuizuia Ujerumani au Ufaransa kutoa hakikisho lao wenyewe la ulinzi kwa Poland, Hungary na mataifa mengine ya mashariki. Kwa hakika, mazingira ya Urusi wakati wa miaka ya 1990 hayakutoa tishio lolote kwa Ulaya tokea Urusi iliposambaratika kabisa na kuangamia kiuchumi. Hivyo, utanuzi wa NATO katika eneo la mashariki ulikuwa ni jibu kwa Amerika, kuhusiana na ukataliwaji wa baada ya 1991 wa uzito wa muungano huo ambapo iliisaidia Amerika kuimarisha uhusiano wa NATO na Amerika kuwa ni mpatanishi wa mkuu wa masuala ya Ulaya.

5. Katika kulinganisha na matendo ya sera za Amerika barani Ulaya, utawala wa Biden umehitimisha kuwa kuimarisha nafasi ya Amerika Ulaya, inabidi kuliunganisha bara hilo kuelekea tishio lilio wazi. Hili sio tu litaweza kugeuza uharibifu wa Trump Ulaya, bali pia itasaidia Amerika kufikia malengo mengine kama kumaliza Nord Stream 2, kuhujumu upatanifu wa Ufaransa na Ujerumani kwa Urusi, kuidhoofisha Urusi, kuongeza idadi ya wapiga kura wa Biden, kuongeza faida za viwanda vya kijeshi vya Amerika na mwisho, kuiwezesha Urusi iisaidie Amerika katika kuizingira China.

Amerika badala ya kuharakisha mchakato wa uanachama wa Ukraine kwa NATO au kuipatia mwamvuli wa kinyuklia wa kujilinda na uvamizi wa Urusi, imefanya mazoezi ya NATO karibu na mpaka wa Urusi na Ukraine mwishoni mwa mwaka uliopita, ambapo ulikuwa ni ukiukaji wa wazi wa maslahi ya kiusalama ya Urusi. Pia, utawala wa sasa wa Amerika umeyafanya kwa makusudi mahusiano ya Amerika na Urusi kuwa ya chini zaidi kwa kipindi chote tokea vita baridi. Biden ameendeleza suala la ukiukaji wa haki za binadamu na uvamizi wa Crimea. Tokea mwaka uliopita, Biden, ameonyesha kutokuwa na maslahi yoyote katika kukuza mahusiano ya Amerika na Urusi, kwa mategemeo ya kumsukuma Putin kwenye maamuzi ya pupa. Mnamo Disemba 2021, Biden, aliendelea kutozingatia onyo la Putin la “mahusiano kamili yenye furaha tele ya Amerika na Urusi” kama atachagua kuweka vikwazo visivyo vya kawaida kwa Urusi. Hata hivyo, Biden aliendelea na msimamo wake mgumu na usio na umuhimu kwa Urusi.

Vikwazo havipaswi kutumika kwa kiwango kikubwa kwani vinakuwa si vyenye ufanisi na ni hatari. Kwa sababu vikwazo havimyayushi adui, bali vinamkasirisha adui na wakati huo huo kumdhoofisha kunakoongezeka. Kama Japan katika Vita vya Pili vya Dunia, ambapo Amerika iliiwekea vikwazo na vizuizi Japan iliyopelekea kukatiwa rasilimali muhimu, na hatimaye kuibinya Tokyo kusalimu amri. Ukweli nyuma ya maamuzi ya sera hiyo ni kuwa Amerika ilitaka kisingizio cha kulishawishi Bunge la Congress kwa Amerika kuachana na sera yake ya kujitenga na kuirekebisha kuelekea kwenye kujihusisha na masuala ya kimataifa na kwa hivyo kukawekwa vikwazo vya wazi. Pamoja na hayo, utawala wa Biden uliendelea kukuza kauli za madaha kuhusiana na Urusi kuivamia Ukraine, ambapo pia umewaweka watu wa Ukraine katika hali ya kukosa raha. Jen Psaki, msemaji wa White House, ameelezea mara nyingi kuwa uvamizi wa Urusi “uko wazi”, wakati Jake Sullivan, mshauri wa usalama wa taifa, alisema unaweza kutokea wakati wowote. Serikali ya Ukraine hatimaye iliikabili Amerika juu ya upotoshaji na kuifanya hali ngumu zaidi kuliko ilivyo kuwa. Licha ya hayo, Biden aliendelea kukataa mazingatio halali kuhusiana na NATO na badala yake alitoa kauli akitaja “muingilio mdogo unaokubaliwa” ikimaanisha mambo mawili kwa Warusi, ruhusa ya uvamizi na kukosa uzingatiaji kwa madai muhimu ya Urusi.

6. Vita nchini Ukraine vimeipelekea Amerika kufikia mengi ya malengo yake. Hadi sasa, watu wote wa Ulaya wameangukia katika mwamvuli wa Amerika wakiiruhusu Amerika kuimarisha nguvu zake kwa mara nyengine. Amerika imeweza kuidhoofisha Urusi na kufanikiwa kuisukuma Ujerumani kuongeza mchango wake wa GDP kwa NATO, ambapo imenyanyua bei ya hisa za mashirika ya ulinzi ya Amerika kutokana na Ujerumani kuingiza dolari bilioni 100 kuimarisha jeshi lake. Na mwishowe, kumaliza Nord Stream 2 moja kwa moja.

Hata hivyo, utawala wa Trump ulikuwa na malengo hayo hayo, lakini mikakati baina ya makundi haya mawili ya kisiasa ilitafautiana. Chini ya Trump, Amerika ilipenda kuidhoofisha Ulaya na kwa namna fulani kuligawa bara baina ya Urusi na Amerika; hivyo, kuunga mkono harakati za kupinga Umoja wa Ulaya (EU) na Brexit, na wakati huo huo, Amerika kuibinya Ulaya kuongeza mchango wake kwa NATO. Kwa sababu chini ya utawala wa Trump, lengo lilikuwa ni kuigawanya EU kufaidika na Urusi na Amerika, lakini kuiweka NATO katika hali ya uzima ambapo itaweza kuendelea kubakisha ufahari wa Amerika. Amerika pia ilitaka kuumaliza mradi wa Nord Stream 2; hata hivyo, juu ya suala hili, Urusi na Amerika zilibaki kutafautiana japo ushirikiano mkubwa uliendelea baina ya Urusi na Amerika katika masuala mengine mbalimbali kulinganisha na wademokrat wa Biden. Mwishowe, Amerika chini ya Trump ilipanga kula njama na Urusi kuidhibiti China.

Hivyo, sio ajabu kwa nini Trump wakati wa kuanza kwa uvamizi wa Urusi ilionyesha kuwa angeliruhusu maeneo ya mashariki ya Ukraine kukaliwa na Urusi. Trump alisema, “Huyu ni mwenye kipaji. Putin ametangaza sehemu kubwa … ya Ukraine, Putin ameitangaza kuwa ni huru.” Kauli ya awali inaelezea kuwa hili ni jambo ambalo utawala wa Trump ungeweza kuruhusu kutimizwa kwa kuwa Amerika ilitaka kuitiisha Ulaya kwa kuikurubisha Urusi, ambapo ingeisaidia Amerika kuweka uzani sawa wa nguvu kwenye bara na wakati huo huo kuiruhusu Amerika kulinda maslahi yake.

7. Hakuna tafauti za msingi baina ya Biden au Trump; bali, tafauti zipo kwenye mtazamo. Wanademokrat siku zote wana tabia ya kuharibu taswira ya Amerika ya kuchukua imani zake za kiliberali na maadili kwa ushupavu wakati ikitekeleza sera za kigeni. Hivyo kutekeleza sera ngumu kuelekea Urusi kunakwenda sambamba na ghilba za wanademokrat wa awali. Hata hivyo, juu ya ugumu wa wanademokrat wakijaribu kudhibiti mapatano baina ya kauli za madaha na ukweli, muda wote wanaishia kujikanganya wenyewe, kama Obama, aliyetekeleza uingiliaji wa Amerika nchini Syria, iliyopelekea kuwashtua waungaji mkono wa ndani wa uraisi wake. Wanarepublican kwa upande mwengine, ni watu wa vitendo zaidi katika utendaji wao kwenye sera za kigeni kwani wanakubali ukomo na kutotekelezeka kwa maadili ya kiliberali katika sera ya kigeni. Kwa sababu hii, chini ya Trump, mahusiano ya kusisimua yalidhibitiwa kuelekea Urusi kulinganisha na wanademokrat.

Vidokezi vya sasa na vijavyo juu va vita

Katika mustakbali wa karibu, vita nchini Ukraine vitaigharimu Amerika mtaji wake wa kisiasa zaidi na kuharakisha mporomoko wa taifa hilo. Ni wazi kuwa Amerika inataka kuidhoofisha Urusi nchini Ukraine kwa maslahi yake. Hata hivyo, kurefuka kwa vita Ukraine pia kutapelekea kuharibu heshima ya Amerika, ambapo itamaanisha kuwa wanademokrat wa Biden hawakuchukua masuala yote katika mazingatio kabla ya kuiingiza Urusi mtegoni nchini Ukraine. Mwanzo, kukosekana kwa mshikamano wa kisiasa ndani ya Amerika kumefungua upangaji mpana wa masuala kwa ajili ya utawala wa Biden. Sera ya kigeni imekuwa muda wote ni muendelezo wa siasa za ndani na mgawanyiko nyumbani kunatatiza sera za sasa za Amerika kuelekea Urusi na Ukraine. Pili, ikihusiana na ya mwanzo, kupanda sana kwa bei ya nishati na kukosekana kwa mauzo ya nje ya ngano kutoka Ukraine na Urusi katika soko la dunia kumeongeza mbinyo kwa utawala wa sasa ambapo rasilimali kadhaa za Amerika kote duniani ziko chini ya tishio au kukataa kujifungamanisha kikamilifu na sera za Amerika kuelekea Urusi. Tatu, mawakala wengi wa Amerika wamefichua mwanya wa kumdhoofisha Biden, katika jitihada za kudhuru nafasi yake na kutafuta bwana muafaka badala ya Biden atayekuwa ni rafiki zaidi kwao.

Japokuwa mengi ya malengo ya Amerika, kwa sasa, yamezaa matunda; hata hivyo, kwa Amerika kupita kwa wepesi na kutuliza malengo yake ya kisiasa kutokana na vita vya Ukraine inaweza kuwa shida sana. Na hii ndio sababu.

Kama Amerika itaiwezesha Urusi nchini Ukraine na kwa kiasi fulani kuweza kuweka maelewano na Kremlin ambapo mataifa yote mawili yatashirikiana dhidi ya kuidhibiti China, haitochukua muda mrefu kwa Waukraine kuamua kuwa Amerika sasa inafanya kazi na taifa ambalo limeuwa maelfu ya Waukraine wasio na hatia katika wanawake, watoto na wanaume. Uamuzi huo utazusha shaka miongoni mwa Waukraine kuhusiana na tabia halisi ya Amerika. Haitochukua muda mrefu, hadi maamuzi hayo kuenea kwa majirani wa Ukraine na mataifa mengine kama Ufaransa ambao wataweza kuyatumia kwa ajili ya ajenda yake yenyewe.

Hali hiyo pia itadhuru makadirio ya uungaji mkono ambapo milioni 80 ya wapiga kuwa wa republican wa Trump na chama chenyewe cha republican kuweza kuongeza kampeni ya kumsulubu Biden kwa sera za ovyo ovyo, wakimshutumu Biden kwa kudhoofisha ubwana wa Amerika. Wanarepublican wataweza kutumia zaidi makosa ya Biden kukidhoofisha Chama cha Demokrat na kumbadilisha Biden kwa Mike Pence - mshindani wa Trump aliyegeuka - au Trump mwenyewe. Hivi sasa Biden anafanya bidii kupitisha sheria zinazohusu afya na elimu, na maeneo mengine kadhaa, ambayo yote yanawekewa vikwazo na wanarepublican wa congress na seneti. Kwa hakika, hata wanademocrat kadhaa wanajaribu kumzuia Biden kuwapa tahafifu kikosi cha ulinzi cha taifa cha Iran, ambayo inaonyesha kuwa ima wanasiasa wa kidemocrat wanaanza kuona usaliti uliopo baina ya Iran na Amerika au wanajinufaisha na nafasi dhaifu ya Biden kwa maslahi binafsi, au wanawafichua wanarepublican waliopandikizwa katika Chama cha Democrat, kwa kuwa haikuwa ni mara ya mwanzo ambapo wanademocrat fulani wameunda maelewano ya siri na wenzao wa republican.

Mwezi uliopita, msaada wa Biden wa dolari bilioni 13.6 kwa Ukraine ulipingwa na wanarepublican wa seneti, wakati huo huo, wanarepublican wamemsukuma Biden kuongeza juhudi zake kuihifadhi Ukraine. Moja ya malengo ya ubunifu wa vita nchini Ukraine ni kuwa utawala wa Biden ulitaka kutumia vita kuiunganisha serikali na kuongeza idadi ya wapiga kura wa Biden. Hata hivyo, migawanyiko imebaki serikalini ambapo wanarepublican wengi wameharakisha mgawanyiko na kulinda maslahi yao na kupunguza uaminifu wa Biden.

Pia, big oil (mkusanyiko wa makampuni makubwa ya mafuta na gesi) ambao wengi wao ni wafadhili wa republican wametumia vita kufaidika na nafasi dhaifu ya Biden ili kuongeza udhibiti wao katika ikulu ya White House. Big oil pia imetumia mgogoro wa Ukraine kuongeza faida ya wamiliki wake; Joe Biden alisema kuwa big oil ndio wa kulaumiwa kwa bei kubwa kwa kukataa kwao kuchimba na kusukuma mafuta na gesi zaidi. Katika kujibu, big oil imemlaumu Biden kwa kanuni kali juu ya mazingira, ambazo zinaikwaza big oil katika kuchimba mafuta na gesi zaidi. Pia, big oil imetetea msimamo wake kwa kueleza kuwa hawana nyenzo za kuchimbia kiasi hicho kikubwa cha mafuta na gesi kwa kipindi hiki. Japokuwa hilo sio kweli kwani inagharimu bilioni kwa makampuni ya big oil kuzalisha teknolojia ya uchimbaji; hivyo, ni jambo lisiloleta manufaa kwamba thamani yote ya mafuta na gesi inayochimbwa ni ndogo kulinganisha na kiasi kinachowekezwa katika kutengeneza teknolojia hiyo. Ukweli unaonyesha kuwa big oil inampendelea Trump au anayemfuatia, Mike Pence, ambapo chini ya utawala wa Trump ajenda ya suala la mazingira imekombwa kuwa sera iliyopo mezani. Wakati wa zama za Trump, Amerika iliamua kujiondoa kutoka Makubaliano ya Paris juu ya Mazingira kwa sababu tabaka la wafadhili wa uraisi wake walikuwa ndugu wa Koch (mjumuiko wa makampuni unaomilikiwa na familia ya Koch)  na big oil ambao wanachuki na kanuni za mazingira, zinazozuia faida zao za mafuta, kwa kulinganisha na Biden, ambaye anafadhiliwa kimsingi na mashirika ya Silicon Valley-tech. Licha ya maendeleo yote hayo, mashirika ya kiasili ya Amerika hayataki kuachia utawala kwa warasilimali wapya wa teknolojia ya Amerika wanaochipuka; hivyo, kuna mpambano baina ya wawili hao ambapo vyama vyote viwili vinachukua sera tafauti za mabwana zao, ambapo imezusha mgawanyiko wa wazi.

Kuyafanya mambo yawe mabaya zaidi, kukataa kwa big oil kusawazisha bei na uingiliaji wake unaoogezeka katikati ya vita kumemlazimisha Biden kubakisha baadhi ya sekta za nishati za Urusi kuwa mbali na vikwazo. Hii imeidhoofisha nafasi ya Biden ambapo kwa upande mmoja anawaunga mkono Waukraine na upande wa pili anasaidia kuwauwa. Siku chache nyuma, democrat ilitangaza mpango wa kupambana na big oil ili kushusha bei ya nishati. Ni kejeli kuwa Biden alitegemea kuiunganisha nchi na kurejesha mshikamano wa kisiasa jijini Washington, lakini hali imeelekea upande mwengine. Ama kwa wanarepublican na wanufaikaji wake kama big oil wamepanga kuwadhoofisha wanademocrat na kutoa mwanya kwa “uokozi” wa republican. Pia, hali inaonyesha kuwa big oil na sekta ya viwanda vya silaha ni wajanja zaidi wa kisiasa kuliko mashirika yanayochipuka ya teknolojia.

Nchi kama Saudi Arabia na umbile la Kiyahudi zimegundua mapambano ya ndani miongoni mwa Waamerika na kuamua kumdhoofisha Biden kutokana na msimamo wake wa kuwa karibu na Iran. Sababu ya Saudi Arabia kukataa takwa la Amerika kuongeza uzalishaji wa mafuta ni juu ya shutuma za Amerika kwa matendo ya sera jumla za MBS (Moh’d bin Salman) na msimamo wa Amerika kuwa na Iran. Hivyo, mtu pekee anayeweza kuuhifadhi utawala wa MBS kutokana na kuhuika kwa Iran ni Trump au kiongozi mwengine wa republican. Mbali na hayo, muongo mmoja uliopita Aramco ilimilikiwa na big oil na hadi sasa Aramco imewaajiri Wamarekani 40,000 katika ngazi za wakurugenzi, majiolojia, na washauri wenye historia ya kuwa waajiriwa wa big oil mwanzoni! Hivyo, sio ajabu kwa nini Saudi Arabia iko sambamba na msimamo wa wahafidhina/big oil kuliko wanademokrat na warasilimali wa teknolojia mpya. Saudi Arabia haiegemei kwa China, kwa kuwa haikubaliani na uhalisia kwani China haitoweza kuchukua manufaa ya Amerika kwa kibaraka wake Saudi Arabia. Sababu ya Saudi Arabia ya kuwauwa Waislamu wa Yemen bila kizuizi ni kutokana na Amerika kuwapatia vifaa, mazoezi ya kijeshi, na ulinzi wa Amerika kutoka taasisi za kimataifa za mpango wa kiliberali. China haiwezi kuipiku Amerika; hivyo, Riyadh haitoelekea kwa China. Itabakia kuwa ni kibaraka wa Amerika, bali itapenda kuona bwana wa sasa kuchukuliwa nafasi yake kwa aliye bora zaidi. Mbali ya mikataba ya kibiashara hakutakuwa na maendeleo ya maana katika mahusiano ya Saudia na China.

Ama kwa India, ni mshirika muhimu sana wa Amerika wa kuidhibiti China. Chama cha BJP chenye kuungwa mkono na Amerika kimeweza kukusanya nguvu zake katika bunge la Congress la India kutokana na kutangaza bendera ya uongo ya Kargil na wahafidhina mambo leo ambao kwa kiasi kikubwa wamejigamba kwa uungaji mkono wao kwa chama cha BJP. India inafahamu kuwa inacheza dori muhimu katika mpango wa hatua kwa hatua wa kuizuia China; hata hivyo, India kwa miaka miwili imekuwa ikiteseka kwa maandamano ya wakulima wakiwa wengi wao ni - Makalasinga - jambo ambalo limetupia macho zaidi kwa sera za Modi zisizopatana kwa sababu hadi sasa, Modi amekuwa akisukuma msimamo ulio dhidi ya Uislamu, ambao haukuisaidia nchi katika muundo au aina yoyote; badala yake, imeifanya India kuwa na hali mbaya zaidi na kutokuwa imara. Hivyo, ni katika maslahi ya Modi kumakinisha nafasi yake kwa kusaidia sekta ya kilimo ya uchumi wa India ili kuficha kasoro zake.

Kwa kuwa uchumi wa viwanda wa India kimsingi unafanya kazi kwenye mafuta na gesi na kwa kuwa kuna uhaba wa ngano kote duniani, Modi ameamua kujaza nafasi ya uhaba wa ngano ya Urusi na Ukraine kwenye soko la dunia ili kusaidia kunyanyua faida ya wakulima wa India. Karibuni, wakulima wa India wamevuna faida ya kuuza nje ngano kote duniani. Kwa sababu hii, Modi amekuwa akinunua gesi ya Urusi kwa bei rahisi kusaidia kuongeza ufanisi wa sekta ya kilimo India, ambayo itamsaidia kudhibiti nafasi yake ya nguvu na kuwaweka vizuri wapiga kura wake. Mwisho, ni kuwa India inahifadhi dolari nyingi zaidi katika akiba yake kwa kusafirisha nje ngano na kwa kununua nishati ya Urusi kwa kutumia sarafu ya rubbles. Amerika hata hivyo, imeanza kukosa subira kwa sababu msimamo wa Biden kwa Urusi umekuwa ukidhoofishwa ambapo mshirika muhimu ameudharau msimamo wa Amerika kwa Urusi. Kwa sasa, Amerika imekuwa haitoi moja kwa moja lawama zake kwa tabia ya India; hata hivyo, Amerika itaendelea kidogo kidogo kubadilisha njia yake kuelekea kuwa ya makabiliano dhidi ya India katika muda wa karibuni.

Hatimaye, suala nyeti zaidi ni ulimwengu wa Kiarabu, ambapo nchi tano za mapinduzi ya Kiarabu zinategemea zaidi uagizaji ngano kutoka Urusi na Ukraine; hivyo, vita nchini Ukraine vimekuwa na athari kubwa kwa ulimwengu wa Kiarabu kupelekea kuongezeka kwa uwezekano wa mapinduzi ya pili ya Kiarabu. Misri ya Al-Sisi hivi sasa inaelekea kutembea juu ya barafu nyembamba. Al-Sisi tayari ametayarisha mpango wa kukaribisha mikopo ya IMF kwa Misri kwa vile wawekezaji wa kigeni wamejitoa nchini kutokana na mzozo wa Ukraine, ambao pia umepelekea dolari kuondoka nchini Misri. Hivyo, Al-Sisi lazima atafute njia ya kupata tena dolari ili aweze kununua bidhaa za kimataifa na pia kulipia deni lililopo la IMF, ambalo pia ni kwa dolari. Mwezi uliopita, kutokana na ugumu wa kiuchumi unaowakabili watu, utawala umeamua kuweka bei elekezi ya mkate, sekta ya uchumi ambayo hata haifidiwi na serikali, ni suluhisho la muda, ambalo bila shaka hatimaye litapelekea kukuza lawama zaidi kwa umma.

Wananchi nchini Misri wameanza kuona hitilafu na ujinga wa utawala wa Al-Sisi ambapo wengi wameonyesha kutoridhika kabisa na utawala wa Al-Sisi. Taarifa za karibuni zimeangazia kwa uwazi mbinyo mkubwa dhidi ya utawala, ambapo matokeo yake yamesababisha utawala kupiga marufuku mikusanyiko ya wazi ili kuzuia maasi. “Serikali ya Misri imepata wazimu juu ya mikusanyiko yoyote, ikiwemo ya kidini,” amesema Essam Teleima, mchunguzi wa masuala ya kidini wa Misri na aliyekuwa imamu mteule wa serikali. “Vizuizi vimekusudiwa zaidi kwa lengo la kuzuia machafuko dhidi ya serikali,” ameliambia Middle East Eye.

Katika kuhitimisha, siasa za ndani za Amerika zina athari kubwa juu ya sera yake ya nje. Pia, Amerika haikuchukua mazingatio kwa hadhari zote za kisiasa. Kama Amerika itashinda dhidi ya Urusi au kutoshinda, kwa namna yoyote heshima ya kisiasa ya Amerika ndani na nje itahasirika. Kama Amerika itashindwa, basi itapelekea kupunguza kabisa ubwana wa Amerika barani Ulaya; na kama itashinda, itazusha changamoto za baadaye kufichua sura halisi ya Amerika na uaminifu wake kama mshirika.

Zaidi ya hayo, katika muda ujao, Biden na Chama cha Democrat wataendelea kukabiliana na wanaharakati wa republican licha ya matokeo utakayoyapata utawala wa sasa nchini Ukraine. Mgawanyiko wa siasa za ndani za Amerika zimezusha vizuizi vingi kwa utawala wa Biden kuweza kutekeleza siasa zake kuelekea Ukraine na Urusi; badala yake, imezalisha mkusanyiko mpya wa lawama. Migawanyiko miongoni mwa Waamerika unaweza kupelekea kwenye mkwamo wa sera za kigeni za Amerika katika kusonga mbele, au pia kuchochea matukio ya maafa kama Mapinduzi ya Kiarabu 2.0, ambayo yataweza kuondoa utulivu wa usanifu wa Amerika katika Mashariki ya Kati. Utulivu ambao hawataweza kuuregesha tena.

Migongano ndani ya Amerika ni kutokana na imani ya kujali manufaa ya kisekula ambapo watu wachache wenye nguvu na makundi machache ndani ya serikali wanacheza na siasa baina yao inayoegemea juu ya kile kinachotamaniwa na kisichotamaniwa badala ya kigezo cha kipi ni sawa na kipi sio sawa. Hiyo ndio sababu msingi ya kufifia kwa nguvu za Amerika na kuongezeka uangamivu wa maisha ya watu wasio na hatia kote duniani. Ni kwa kuuregesha mfumo sahihi wa kisiasa pekee - Khilafah kwa njia ya Mtume (saw) - ndio utakaowezesha kueneza haki, amani, na kuwatosheleza watu mahitaji yao ya viungo na ghariza katika namna sahihi, kama ilivyofunzwa na Muumba, Mwenyezi Mungu (swt).

Mwenyezi Mungu (swt) anasema katika Quran:

(وَقُلْ جَاء الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقًا)  “Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka. Hakika uwongo lazima utoweke!” [17:81].

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Mohammed Mustafa

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu