Jumatano, 11 Rabi' al-awwal 1447 | 2025/09/03
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Mauaji ya Halaiki ya Sudan: Dori ya Omar al-Bashir

(Imetafsiriwa)

Ingawa mengi yanajulikana kuhusu mauaji ya halaiki yanayowakumba ndugu na dada zetu nchini Palestina, machache sana yanajulikana—au yanasambazwa—kuhusu wale walio nchini Sudan, ambao kwa muda wa miezi 18 iliyopita wamevumilia mauaji ya halaiki ya kimya kimya. Ukatili huo umeua zaidi ya watu 15,000, zaidi ya milioni 10 wamekimbia makazi yao, na kuacha nusu ya watu—watu milioni 25—wakikabili uhaba wa chakula na njaa.

Kinachojulikana kidogo ni kwamba mauaji haya ya halaiki yanatokana na mzozo unaoendelea kati ya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Wanajeshi wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF). Walakini, matatizo ya Sudan hayakuanza mnamo 2023, lakini mnamo 1956, wakati nchi hii ilipopata uhuru kutoka kwa utawala wa Waingereza na Misri. Tangu wakati huo, Sudan imekumbwa na mapinduzi saba ya kijeshi, moja ya mapinduzi makubwa zaidi yaliyotokea mwaka 1989, ambayo yalimuweka Omar al-Bashir madarakani—mtu ambaye alitawala kama dikteta kwa miongo mitatu.

Baada ya kuvumilia miaka 30 ya ukandamizaji, watu wa Sudan hatimaye walifanikiwa kumuondoa al-Bashir na kusherehekea uhuru wao mpya—uhuru ambao ulinyang’anywa punde na Abdel Fattah al-Burhan, mkuu wa SAF, na Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti, kiongozi wa RSF. Wanaume wote wawili walikuwa wamepata mamlaka na utajiri mkubwa chini ya utawala wa al-Bashir.

Kuinuka kwa Omar al-Bashir

Kabla ya mapinduzi ya 1989 yaliyomfanya Omar al-Bashir kuwa mtawala wa Sudan, nchi hiyo ilikuwa imezama katika Vita vyake vya Pili vya wenyewe kwa wenyewe huku Sudan People's Liberation Army (SPLA), iliyoongozwa na John Garang mara nyingi akituhumiwa kuwa wakala wa Marekani, akifuatilia maslahi ya Marekani ili kuivunja Sudan kwa manufaa ya kimkakati na kiuchumi. Juhudi hizi ziliishia katika Mkataba wa Naivasha wa 2005, uliotiwa saini na al-Bashir na Garang, ambao ulifungua njia ya uhuru wa Sudan Kusini.

Ni muhimu kufahamu kuwa Sudan Kusini ina akiba kubwa ya mafuta, na hivyo kuifanya Marekani kuwekeza zaidi ya dolari bilioni 1.2 katika nchi hiyo changa, chini ya bendera ya “uwekaji amani” na “utawala”, huku pia ikishindana na China kwa ajili ya udhibiti wa kikanda.

Wakati huo huo, uchumi wa Sudan ulikuwa ukiporomoka. Waziri Mkuu wa zamani Sadiq al-Mahdi alipoteza uungwaji mkono wa wananchi huku wananchi wakikabiliwa na njaa, ukosefu wa makaazi, mgogoro wa deni la taifa, na mfumko mkubwa wa bei unaozidi 70%, yote yakichochewa na kuporomoka kwa sarafu iliyosababisha watu kushindwa kumudu mahitaji ya kimsingi.

Masharti haya yalitengeneza mazingira mazuri kwa al-Bashir—akiungwa mkono na National Islamic Front (NIF), ambayo iliungana na Saudi Arabia na Marekani dhidi ya Muungano wa Kisovieti—kufanya mapinduzi yasiyo na umwagaji damu mnamo Juni 30, 1989. Alipochukua mamlaka, al-Bashir alivunja bunge, akajitangaza kuwa Mkuu wa Nchi, Waziri Mkuu, na Waziri wa Ulinzi, na akaweka sura kali ya “Sharia”.

Utawala wake

Akiwa kiongozi mpya, al-Bashir alijizungusha haraka na walinzi waaminifu, hasa Wanajeshi wa Sudan (SAF), ambamo Abdel Fattah al-Burhan alinyanyuka na kuwa Inspekta Jenerali. Dori ya Burhan lilikuwa kuhakikisha usalama wa al-Bashir na kukandamiza upinzani wowote.

Licha ya kuahidi ustawi, serikali ya al-Bashir ilianza haraka kuwakandamiza walio wachache. Miaka ya 1990, ambayo mara nyingi huitwa “miaka ya ugaidi”, ilishuhudia kuanzishwa kwa nyumba za shetani – vituo vya uzuizini vya siri ambapo wapinzani, wakiwemo wasomi, wakomunisti na maafisa wa kijeshi waliteswa. Kupigwa viboko na kunyongwa hadharani pia kulianza, ikiwemo kunyongwa kwa wanaume watatu kwa kuwa na dolari za Kimarekani, na kusababisha wimbi la hofu kwa watu.

Al-Bashir pia alitekeleza tafsiri kali ya Sharia, kama vile kukatwa viungo kwa ajili ya wizi, hata wakati wizi huo ulisababishwa na njaa au umasikini. Hata hivyo, chini ya fiqh halisi ya Kiislamu, adhabu kama hizo husitishwa wakati wa njaa au shida, kama ilivyoonyeshwa na Khalifa Umar ibn al-Khattab, ambaye alikataa kutekeleza adhabu hii wakati wa njaa. Wakati huo huo, al-Bashir na serikali yake waliiba mabilioni, huku dolari milioni 90 zikipatikana nyumbani kwake baada ya kuondolewa kwake mnamo 2019 – ikiangazia utekelezaji wake wa kuchagua wa sheria za dini.

Vita na Mauaji ya Halaiki

Licha ya mbinu zake za kikatili, vita vya wenyewe kwa wenyewe na uasi yalizuka. Kusini mwa Sudan, Vita vya Pili vya wenyewe kwa wenyewe viliendelea kati ya serikali ya Sudan na SPLA, na kugharimu maisha ya zaidi ya milioni 2, wengi wao wakiwa raia. Vita hivi vilipiganwa kwa kiasi kikubwa na SAF, huku Burhan akicheza dori muhimu katika operesheni za kijeshi.

Wakati huo huo, Magharibi mwa Sudan, eneo la Darfur—lililopuuzwa kwa muda mrefu na Khartoum—liliibuka kwa uasi. Badala ya kupeleka SAF, al-Bashir aliajiri wanamgambo wa Janjaweed, akiwemo Hemedti, kukandamiza uasi huo kikatili. Huu ulikuwa mwanzo wa Mauaji ya Halaiki ya Darfur.

Janjaweed, maarufu kwa ukatili wao, waliendesha kampeni ya mauaji ya kikabila. Zaidi ya watu 300,000 waliuawa, milioni 2.5 walikimbia makaazi yao, wanawake kubakwa, wanaume kunyongwa, na watoto kudhulumiwa. Hemedti na vikosi vyake walilipwa fidia kupitia migodi ya dhahabu huko Darfur, na kufanya uhamishaji wa wakaazi wa eneo hilo sio tu lengo la kijeshi, lakini la kiuchumi. “Zawadi” yao kwa mauaji haya ya halaiki ilikuwa kutambuliwa rasmi na serikali ya Sudan na kubadilishwa jina kama Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Al-Bashir alipojitajirisha na kusherehekea, idadi ya watu iliendelea kufa kwa njaa, na uchumi ukasambaratika. Kutokana na uhuru wa Sudan Kusini, Sudan ilipoteza sehemu kubwa ya utajiri wake wa mafuta. Mapitio ya bajeti ya kitaifa yalionyesha kuwa 70% ya matumizi yalikwenda kwa jeshi, na kuacha kidogo kwa huduma za afya, elimu, au usalama wa chakula.

Changanya haya na miongo kadhaa ya ufisadi, mali iliyoibiwa, deni la lililoongeza, na mfumko wa bei uliokithiri, na watu wa Sudan walioachwa kuvumilia jinamizi la miongo mitatu. Lakini wakati tu walipofikiri kwamba yalikuwa yamekwisha, na matumaini yaliibuka baada ya al-Bashir kuondolewa, wanafunzi wake waliingia ndani ili kujaza ombwe—Burhan na Hemedti, wanaume waliopewa mamlaka na utawala wake, sasa wanapigana vita wao kwa wao huku Sudan ikivuja damu.

أزمة_السودان#   #SudanCrisis

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Amatullah Hechmi

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu