Alhamisi, 02 Ramadan 1444 | 2023/03/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Hotuba ya Tano Katika Kongamano: ‘Vijana Waislamu …Waanzilishi wa Mabadiliko Msingi’

Kukabiliana na mgogoro wa kitambulisho cha vijana wa kiislamu

Assalamu alaikum wa Rahmatullah wa Barakatahu

(1) Utangulizi:

Dada zangu wapendwa na wageni waheshimiwa, mgogoro wa utambulisho unaoathiri wengi wa vijana wetu wa Kiislamu ni mojawapo ya kadhia sugu mno zenye kuathiri Ummah huu. Na kama ulivyo mgogoro wowote, kukabiliana nao vilivyo na kwa haraka ni wajib. Ni wajib kwani ndiyo itakayoamua mafanikio ya watoto wetu na sisi wenyewe katika maisha haya na maisha ya kesho. Na ni wajib kwani ndio kitovu cha mafanikio ya mustakbali wa Ummah huu na hadhi ya Dini yetu hapa ulimwenguni.

Dada zangu, mwanachuoni mkubwa wa Kiislamu, Imam Ghazali (RH) wakati mmoja alisema, “Mtoto ni amana mikononi mwa wazazi wake. Na moyo wake msafi ni kito cha thamani kisichokuwa dosari, kisichokuwa na mchongo au umbile lolote. Hukubali kuchongwa na kufinyangwa katika mwelekeo wowote. Endapo atalelewa na kufunzwa uzuri, atakulia juu ya hili. Mtoto aina hii atafanikiwa hapa duniani na kesho Akhera na wazazi, walimu na wakufunzi wake wote watashirikiana katika malipo haya. Lakini endapo mtoto huyu atalelewa katika uovu na utepetevu, atageuka kuwa msiba na kutumbukia katika maangamivu, na wanao husika na ulezi wake watashirikiana katika dhambi lake. Endapo atakulia katika uovu na kuachwa bila ya kukanywa, atageuka kuwa msiba na ataangamia.”      

Dada zangu, kwa kweli nyoyo za watoto wetu wanapokuwa wadogo huwa ni safi, zisizo chakachuliwa, mithili ya kito cha thamani. Endapo watazamishwa ndani ya Dini kwa njia sahihi, na kuitambua Haki na kheri inayo tiririka kutokana nayo basi insha Allah watakuwa vijana ambao nyoyo zao ziko imara juu ya haki, wenye yakini na Imani zao za Kiislamu, wenye kujitolea juu ya majukumu yao ya Kiislamu, mashujaa katika kuzungumza Dini yao na dhidi ya batili na dhulma na wenye mapenzi kwa uongofu na kuchukia yale ambayo Mola wao (swt) ameyataja kuwa ufisadi, uchafu, na dhulma. Watakuwa ndio chimbuko la kheri kwa familia zao, jamii zao, mujtama zao, na Ummah huu. Na watakuwa ndio wenye kudhihirisha sifa za kuleta mageuzi ya kweli hapa ulimwenguni, wakibeba majukumu mabegani mwao na kuwezeshwa kwa suluhisho sahihi la Kiislamu la kuuinua Ummah huu na kihakika ulimwengu huu kutokana na matatizo yasiyo idadi na dhulma inayo ukabili leo.   

Lakini lengo hili tutalifikiaje? Vipi tutajenga na kuhifadhi utambulisho wa Kiislamu katika vijana wetu na kuwatayarisha kupambana na changamoto kuu wanazo zikabili katika kushikamana na Dini yao, kuzungumza Dini yao, na kung’ang’ana kwa ajili ya Dini yao?

Leo, ningependa kuzungumzia baadhi ya nukta muhimu na baadhi ya fahamu msingi ambazo zahitaji kujengwa ndani ya vijana wetu ambazo bila shaka ni muhimu mno katika kukabiliana na mgogoro huu wa utambulisho, na kuwawezesha ili kuzishinda changamoto wanazo kumbana nazo barabara insha Allah.

Lakini dada zangu, kwanza kuna swali ambalo ni lazima tulijibu wenyewe – kama wazazi, jamii, na kama Ummah – ikiwa tunataka kukabiliana barabara na mgogoro huu wa utambulisho wa vijana wetu. Nalo ni –tunataka nini haswa kwa watoto wetu? Je, tunauona Uislamu na Uislamu pekee katika nyanja zake zote – kiroho, kiakhlaqi, kijamii, na kisiasa kama njia pekee ya kuwaokoa watoto wetu kutokana na matatizo yanayo umiza roho ambayo vijana wengi wanakumbana nayo leo; njia pekee ya kuwawezesha kutoa mchango wenye natija ya kikweli kwa maendeleo ya wanadamu na hali bora ya ulimwengu huu, pamoja na kuwadhamini mafanikio msingi katika maisha haya na maisha yajayo?

• AU kuna maadili, fikra, tamaduni nyingine ambazo hazikujengwa juu ya Uislamu ambazo tunaunda kwazo mitazamo, matendo, misimamo juu ya mafanikio na matarajio yetu na ya watoto wetu ambazo zinatusababishia kulegeza msimamo kwa Dini yetu, tukisababisha mchanganyiko wa jumbe na mkanganyiko machoni mwa vijana wetu, na hata chuki akilini mwao dhidi ya Uislamu?  

• Vipi kwa mfano, tunaweza kutarajia watoto wetu kuepukana na mahusiano nje ya ndoa, ikiwa tunaruhusu tamthilia, filamu na muziki zinazo pigia debe, kuvutia na kuhamasisha kuhusu uchafu wa mahusiano hayo kuingia ndani ya sebule zetu, au ikiwa tunaruhusu mchanganyiko huru wa wanaume na wanawake katika mijumuiko yetu ya kijamii na harusi kinyume na Uislamu?

• Vipi tutaweza kujenga uhahamu (aqliyya) katika vijana wetu kuwa mafanikio makuu ni kupata Radhi za Mola wetu na kuingia mabustani ya Pepo, ikiwa tunawaruhusu kulegeza msimamo katika swala zao, vazi lao la Kiislamu na majukumu mengineyo ili wafaulu katika elimu au kutafuta ajira au kazi ya kiwango cha juu, ikiwapelekea wao kuamini kuwa kilicho muhimu ni cheo, utajiri na kupata vitu vya kidunia?

• Vipi tutaweza kuwalea vijana wetu kushikamana na matarajio ya Mwenyezi Mungu (swt), ikiwa matarajio yetu ya namna wanavyo vaa, namna ya tabia zao, nani wanaye oana, utiifu wao, mitazamo yao ya kisiasa yamejengwa juu ya maadili yasiyo ya Kiislamu, mila, utaifa, nidhamu ya kidemokrasia iliyotungwa na mwanadamu au matarajio yaliyosemwa na familia au jamii, badala ya lile analo amuru Mwenyezi Mungu (swt)?

• Na vipi tutawapa motisha vijana wetu kuwa mashujaa na kusimama kwa ajili ya Uislamu ikiwa tuna hofu ya kuwashajiisha kuzungumza kwa ajili ya Ummah wao nchini Palestina, Syria na kote ulimwenguni, au dhidi ya mashambulizi juu ya kipenzi chetu Mtume (saw) na Dini, au dhidi ya vita na madhalimu wa Kimagharibi katika ulimwengu wa Waislamu, au katika kuunga mkono Shari’ah au Nidhamu ya Mwenyezi Mungu – Khilafah – kwa kuogopa kuwa watatazamwa kama wenye misimamo mikali na kuwekwa chini ya rada za serikali dhalimu.

• Dada zangu wapendwa, endapo tutawasilisha jumbe za mkanganyiko na kuwa na misimamo miwili miwili kwa vijana wetu kupitia mitazamo, maneno na matendo yetu wenyewe, kamwe hatutaweza kukabiliana barabara na mgogoro wa utambulisho wanaokumbana nao. Hivyo basi, hatua ya kwanza ya kuwaokoa watoto wetu ni kutathmini upya utambulisho wetu wenyewe na kudumu kwetu katika kushikamana na Dini yetu.

(2) Kujenga Itikadi (Aqeedah) kwa Kukinai:

• Baada ya kuelezea nukta hii muhimu ya mwanzo, dada zangu, ni hatua gani muhimu nyenginezo ambazo twahitaji kuchukua ili kukabiliana na mgogoro wa utambulisho katika vijana wetu?

• Kwanza dada zangu, mojawapo ya zawadi za thamani mno ambazo twaweza kuwapa watoto wetu ni uwezo wao wa kutafakari wenyewe kuhusu maisha na ulimwengu, kwa njia ambayo wataweza kutofautisha haki kutokana na batili. Hii yamaanisha kwanza, kuwawezesha kujenga ukweli wa Itikadi ya Kiislamu kwa kukinai kuliko katikiwa kupitia kuwapa dalili nzito za kiakili zinazo jenga yakini ya kuwepo kwa Muumba na kwamba Qur’an ni maneno Yake kwa asilimia 100 – kama alivyo sema Mwenyezi Mungu (swt), 

[إِنَّمَا ٱلۡمُؤۡمِنُونَ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ بِٱللَّهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمۡ يَرۡتَابُو]

“Hakika Waumini ni wale walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake tena wasitie shaka kabisa...” [Al-Hujraat: 15].

• Katika ulimwengu wa leo dada zangu, ambamo vijana wetu wanashambuliwa kwa hotuba katika vyombo vya habari au mitandaoni za kuupinga Uislamu, kushambulia Imani zake, kujenga hofu katika utekelezaji Uislamu, na lile dai kuwa Imani kwa Mungu na dini haingii akilini, iliyopitwa na wakati, ni ya watu wenye akili finyo pekee – kujenga Aqeedah ya Kiislamu kwa kukinai kiakili kuliko katikiwa ni nyeti mno. Ni hili ndilo litakalo badilisha Uislamu kutoka kuwa ni kitu ambacho vijana wengi wanakitazama kama walicho rithi tu kutoka kwa wazazi wao, hadi kuwa ni kitu walicho kikinai kiakili kuwa na majibu sahihi ya maisha na hivyo kinapaswa kupangilia fikra na matendo yao.    

• Ni yakini hii katika Imani ndiyo itakayo fanya Pepo (Jannah) na Moto (Jahannam) kuwa uhalisia usio badilika machoni mwa vijana wetu inshaAllah, na kuhisabiwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni fahamu nzito akilini mwao, ikiwapelekea kuishi maisha yao kwa mujibu wa Sheria na Mipaka yake (swt) inshaAllah. NA ni yakini hii katika Imani ambayo pia itajenga ufahamu safi inshaAllah kuwa lengo maishani na mtazamo sahihi wa mafanikio sio kutafuta vyeo vikubwa na starehe fupi za maisha haya, au kukubaliwa na kupata umaarufu miongoni mwa marafiki na mujtama bali ni kupata Radhi za Mwenyezi Mungu (swt) na thawabu zisizo kifani kesho Akhera.

• Hakika dada zangu, katika ulimwengu ulio pagawa na matumizi ya kimada unaojaribu kuwaundia vijana wetu Pepo duniani kwa matamanio na starehe nyingi za kuvutia zinazo kwenda kinyume na Dini yao, au ambapo utafutaji wa mali za dunia hii – simu, kifaa, ala, nguo za kisasa – zimetawala wakati na umakinifu wao – ni muhimu mno tujenge ndani ya vijana wetu hamu ya Pepo inayo wanyanyua juu ya starere fupi za dunia hii na kuwawezesha kuzikubali hukmu za Kiislamu zilizo wekwa juu ya maisha yao – kupitia kudumu kuwakumbusha kuwa zote hizi si chochote isipokuwa ni tone ndani ya bahari ikilinganishwa na starehe zisizo kifani zinazomsubiri kijana mwema Peponi – kama Mtume (saw) alivyosema,

«وَاللَّهِ مَا الدُّنْيَا فِي الآخِرَةِ إِلاَّ مِثْلُ مَا يَجْعَلُ أَحَدُكُمْ إِصْبَعَهُ هَذِهِ - وَأَشَارَ يَحْيَى بِالسَّبَّابَةِ - فِي الْيَمِّ فَلْيَنْظُرْ بِمَ يَرْجِعُ»

“Naapa kwa Mwenyezi Mungu, haikuwa dunia kwa Akhera isipokuwa ni mithili ya mmoja wenu kutia kidole chake hiki – na akaashiria kwa kidole cha shahada – ndani ya bahari kisha aangalie atakacho baki nacho kidoleni hicho.”

• Dada zangu wapendwa, ni kukinai huku katika Aqeedah na kuwa na hamu ya Pepo ndio yaliyo mpelekea kijana mchungaji dhaifu Abdullah ibn Masud (ra) kuwasomea Qur’an Maquraysh, akijua kwamba watampiga; ndiko kuliko mpelekea kijana Jafar ibn Abi Twalib (ra) kuzungumza kwa niaba ya Waislamu katika mahakama ya Mfalme wa Habasha, bila ya kutishwa na uwepo wa watu walio na ufasaha zaidi katika Maquraysh walio tumwa kuzungumza dhidi ya waumini. Na dada zangu, ni kukinai huku ndiko ambako inshaAllah kutawajaza vijana wetu ushujaa wa kushikamana na Imani zao za Kiislamu katika hali yoyote ile; kusimama dhidi ya shinikizo la wandani wao, hawahofii kubandikwa majina au kuwa tofauti na marafiki zao au hata kubaguliwa kutokana na vazi lao, matendo yao au rai zao za Kiislamu, na kuzungumza kwa ajili ya Uislamu pindi unapo shambuliwa.

 (3) Kuvunja Kivutio cha Mfumo Huru wa Kisekula wa Kimaisha:

• Hatua ya pili ya kukabiliana na mgogoro huu wa utambulisho katika vijana wetu, dada zangu, ni kujenga njia ya kutafakari kwa kudadisi ndani yao inayo wawezesha kutenganisha uongo kutokana na ukweli kuhusiana na fikra zilizo tawala na simulizi zinazo washambulia kutoka katika vyombo vya habari au mujtama na kupambana nazo kwa hekima. Kuwawezesha kupuuzilia mbali uongo dhidi ya Uislamu na kuvunja kivutio cha mfumo huru wa kisekula wa kimaisha ni muhimu mno katika wakati ambao vijana wetu wanafanywa wahisi kuwa Uislamu ndio chanzo cha matatizo yao mengi na ghasia duniani, na kwamba mfumo huru wa kimaisha wa Kimagharibi ndio njia ya furaha na mafanikio, na ustawi na ufanisi katika hii dunia.

• Twahitaji kuwaonyesha – kuwa Uislamu sio uliosababisha janga la mihadarati, ulevi, usumbufu, magenge, uhalifu wa bunduki na tabia nyingine za kiuhalifu zilizo waathiri vijana leo bali ni maadili huria yanayo pigia debe muondoko wa kimaisha wa starehe za kibinafsi na kufuata matamanio ya mtu bila ya kujali matokeo. Uislamu sio uliovunja haiba na Imani ya wasichana wengi wadogo kwa sababu hawawezi kujilinganisha na muonekano wa wasanii na viigizo wengine bali ni muundo wa urembo wa Kimagharibi usio wa kihakika ambao umenasibishwa na mafanikio. Uislamu sio unao wafanya vijana wengi kuhisi kufeli au kuchukuliwa kama walio laaniwa wanapo shindwa kudumu katika fesheni za simu au bidhaa bali ni thaqafa ya kimada ya kirasilimali inayo sawazisha thamani ya mtu bi