Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Tamko la Mwenyezi Mungu (swt) Kuhusiana na Dalili Zote Zinazotuzunguka katika Tendo la Uumbaji 

(Imetafsiriwa)

Mwenyezi Mungu (swt) ameteremsha Aya nyingi zinazoelekeza wanaadamu kuzingatia vyote vinavyowazunguka, kufikiria na kuzingatia maumbile yao, kuwa ni tendo la Uumbaji. Nyingi ya Aya hizo ziliteremshwa ndani ya miaka mitatu ya mwanzo tokea kushuka Wahyi. Ilikuwa kwa Aya hizi ndio Mtume wa Mwenyezi Mungu (swt) aliwathaqafisha Masahaba wakubwa (ra) ndani ya Halaqaat (darsa duara) zilizofanyika katika Dar ul Arqam. Ilikuwa ni Aya hizi zinazohusiana na tendo la Uumbaji ambazo zilisimamisha imani iliokita mizizi ya Masahaba (ra), kiasi kwamba waliwazidi vizazi vyote hadi mwishoni mwake, na kuwa kizazi bora zaidi kuliko vyote.

Kwa kuwa usomaji makini wa Wahyi ulikuwa ndio msingi wa sera ya elimu ya Khilafah, Waislamu walikuwa na uelewa wa maelezo ya Quran juu ya Uumbaji. Ilikuwa ni Aya hizi ambazo ndizo zilizokuwa msingi wa kuimarisha ushindi. Zilitumika kwa kutoa thaqafa kwa kundi la watu na kuwashawishi kuufuata Uislamu. Ilikuwa ni kwa kiwango ambacho raia wa kawaida waliweza kuwashawishi wasio Waislamu. Kwa mfano, Indonesia ni ardhi ya U’shri kwa kuwa Uislamu uliingia kupitia Da’wah ya Waislamu waliokuwa wakifanya biashara na watu wake.

Ni muhimu kuchunguza kwa makini Aya kama hizi, kunufaika na busara zake nyingi, katika wakati ambao kuna wengi katika dunia wanaopotoshwa na makafiri. Lakini bado kuna wengi wanaotafuta ukweli na majibu ya ushawishi kuhusiana na yote yaliowazunguka wanayoyaona katika Uuumbaji. Ni fursa kwa Waislamu wanaoishi nchi za Magharibi pamoja na wasio Waislamu. Na pia ni fursa kwa Waislamu katika Ulimwengu wa Waislamu kwa kuwa mitandao ya kijamii imeyafanya mawasiliano kuwezekana katika maeneo makubwa. Haya yote ni kabla ya kurejea kwa Khilafah, ambapo harakati njema kama hizi za kibinafsi zitaungwa mkono na Da’wah ya Dola kwenye Uislamu.

Katika Quran Tukufu, Mwenyezi Mungu (swt) amesema,

[إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاخْتِلاَفِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَالْفُلْكِ الَّتِي تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِمَا يَنفَعُ النَّاسَ وَمَا أَنزَلَ اللّهُ مِنَ السَّمَاءِ مِن مَّاء فَأَحْيَا بِهِ الأرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَآبَّةٍ وَتَصْرِيفِ الرِّيَاحِ وَالسَّحَابِ الْمُسَخِّرِ بَيْنَ السَّمَاء وَالأَرْضِ لآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ]

“Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana, na merikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayo amrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo ishara  kwa watu wanao zingatia.” [TMQ Baqarah: 164].

Mama wa Waumini, Aisha (ra), amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) wakati aliposoma aya hii, alisema, «وَيْلٌ لِمَنْ قَرَأَهَا وَلَمْ يَتَفَكَّرْ فِيهَا» “Hasara yake kwa yule anayeisoma aya hii na akawa hakuizingatia” [ad-Dar al-Manthur]. Hivyo, Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume Wake (saw) wamewataka wanaadamu kuzingatia yote yanayowazunguka. Wakati wanaadamu wanazingatia Uumbaji, nini wanakigundua? Wanagundua mfumo madhubuti (Nidham) unaotawala mambo yote tunayoyahisi. Mambo yote tunayoyahisi yaliyotuzunguka, makubwa na madogo, mepesi na mazito, yana ukomo maalum (Huduud) unaoyatawala. Kuna sheria zinazoyatawala ambazo haziyakiuki na sunnah (mwenendo) ambao umejifunga nayo. Kwa hakika, ni vyenye mipaka na hii ni wazi kwa vitu vyote na sio baadhi.

Zingatia mwenendo wa nyota na sayari. Kuna mbingu na ardhi, ikiwemo nyota na sayari ambazo kila moja ipo katika mzingo katika mfumo maalum. Licha ya ukubwa wao na mzunguko, hazikengeuki kutoka njia yake. Je hii sio nidhamu maalum, yenye mahusiano yaliopangwa na ubora? Zingatia usiku na mchana. Kuna usiku na mchana, mfuatano wao na tofauti katika urefu wao, hali, kiza, mwangaza na nuru, athari yao juu ya kulala na shughuli za kimaisha. Je hakuna nidhamu maalum inayotawala usiku na mchana? Zingatia meli na bahari, Imam Qurtubi amesherehesha katika tafsiri yake:  والفلك التي تجري في البحر الفلك: السفن  ‘Fulk’ (meli) ni zile zinazosafiri baharini: vyombo vya majini (kiujumla). Ameongeza kuwa, تجري على وجه الماء ووقوفها فوقه مع ثقلها  “vinakwenda juu ya maji na kuelea licha ya uzito wake.” Kwa hakika, kuna mpangilio makini kuhusiana na maji na meli, ambapo aina ya chombo cha baharini huelea wakati kitu chenye uzito sawa nacho huzama.

Kisha kuna maji yanayoanguka kama mvua kutoka mawinguni kuja ardhini, kuihuisha ardhi ambapo huhuika baada ya kuwa kame na kuwa imefunikwa kwa ustawi wenye rangi kijani baada ya kuwa imenyauka, ya rangi manjano. Kisha kuna wanyama wanaoenea ardhini, wanaoongezeka, kuzaliana na kutegemea maisha yao kwa kile ambacho ardhi inakitoa, kupitia maji yanayomwagika juu yake. Kisha kuna upepo unaoyaendesha mawingu, kutoa mvua hapa au pale kulingana na nidhamu maalum na mpango usiobatilishwa. Imam Qurtubi amesema, فسأله ابن عباس: هل سمعت كعب الأحبار يقول في السحاب شيئا؟ قال: نعم، قال: السحاب غربال المطر، لولا السحاب حين ينزل الماء من السماء لأفسد ما يقع عليه من الأرض “(Tubay) alimuuliza Ibn Abbas: Je ulimsikia Ka’ab al-Akhbar akisema chochote kuhusu mawingu? Akasema ndio, akasema: Mawingu ni kama chungio la mvua. Lau sio mawingu wakati mvua inanyesha kutoka mawinguni, ingeliiharibu ardhi pale inaponyeshea.”

Tunapohisi na kutambua vyote vilivyotuzunguka, ni wazi kuwa kuna mfumo (nidham). Ndani ya mfumo huo, hakuna fujo wala mvurugano, wala kutoka nje ya mzingo, wala kijani kibichi bila maji, wala bahari katika mahala sipo, wala upepo katika muda usio wake. Ni mfumo uliothabiti na makini. Mwenyezi Mungu (swt) amesema,

 [مَا تَرَى فِي خَلْقِ الرَّحْمَنِ مِنْ تَفَاوُتٍ]

“Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa mwingi wa Rehema.” [Surah al-Mulk 67:3]. Ibn Kathir ameielezea, أي: بل هو مصطحب مستو، ليس فيه اختلاف، ولا تنافر، ولا مخالفة، ولا نقص، ولا عيب، ولا خلل “Yaani, hufanyika bila kuwa na dosari, huenda sambamba kwa uzani wa usawa, bila kutengana, wala kugongana, wala kuhitalifiana, wala kuwepo upungufu, wala kasoro au ila.”

Hivyo tunaona kuwa mambo yote yaliotuzunguka yamefungika kwenye ukamilifu, nidhamu isiyo na dosari. Vitu vinawajibika ndani ya nidhamu changamano katika uwiyano wa kimaumbile (takayyuf), na ukadiriaji (taqdiir). Kuhusiana na uwiyano wa kimaumbile (takayyuf), kila kimoja kinakitegemea chengine au vyengine. Hivyo kijani kibichi kinategemea (muhtaaj) maji na mwangaza wa jua ili kipatikane. Kijani kibichi chenyewe ni dhaifu kwa kuwa kinahitaji maji na mwangaza wa jua. Namna ya utegemezi (ihtiyaaj) sio wa kiasi chochote tu, bali ni kwa kiwango maalum (qadar) na kiasi (nasbah). Kiwango (taqdir) kiko wazi katika hali zote tunazozihisi. Kama mwangaza wa jua ni wa kiwango maalum, mmea utastawi. Kama utakuwa mdogo utakunyaa. Zaidi ya hivyo, kama utakuzwa kupitia lenzi au kifaa chengine, unaweza kuudhuru mmea, na kupelekea mmea kuchomeka na kuunguza misitu. Kuhusiana na maji, tunaona kuwa baadhi ya mazao hustawi vizuri na kupea, kiasi kwamba mbubujiko wa ghafla wa maji huyafaa zaidi, ambapo kwa baadhi ya mazao kiwango kama hicho kitakuwa ni mafuriko yenye kudhuru mavuno yote. Katika zao moja, katika kipindi kimoja mvua huwa na manufaa, hupelekea kuyapevusha, wakati katika kipindi chengine, mvua husababisha mazao yaliopevuka kuharibika. Kuhusiana na maji, muundo wake ni kuwa kuchemka kwake hutegemea juu ya joto. Hata hivyo, utegemezi ni kuwa maji huchemka tu kwa mujibu wa kiwango cha joto. Hivyo nidhamu ina uundwaji maalum na viwango maalum.

Ni wazi kuwa vitu vyenyewe ni vyenye kutegemea nidhamu iliyowekwa juu yao na vyenyewe sio waanzilishi au waendeshaji wa nidhamu. Kama vingelikuwa hivyo, vingeweza kubadilisha nidhamu vinapotaka, ambapo hali sivyo ilivyo. Zingatia kuwa maji huchemka katika mbinyo maalum kwa kiwango maalum cha joto. Sio kanuni inayoendesha, wala kiwango kuwa ni vyenye kutawala maji au joto. Maji hayawezi kuanzisha uchemkaji wenyewe bila joto, au joto lolote tu, na kiwango maalum cha joto hakibadiliki, kwa kuwa zinaongozwa kwa namna maalum. Kwa hakika, kwa kutafakari juu ya vitu vyote tunavyovihisi tunapambanukiwa kwa uhakika kuwa havianzishi na kuongoza nidhamu ambayo imewajibishwa juu yavyo. Hivyo, bila shaka kuna Mmoja ambaye hahisiwi nasi moja kwa moja, Ambaye anaongoza na kuanzisha nidhamu kwa ajili ya vyote hivyo. Mwenyezi Mungu (swt) amesema,

[وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافُ أَلْسِنَتِكُمْ وَأَلْوَانِكُمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّلْعَالِمِينَ]

“Na katika ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wajuzi.” [Ar-Rum: 22].

Al-Qurtubi katika Tafsiri yake amesema, فهذا من أدل دليل على المدبر البارئ “Basi hizi ni katika dalili kuu alizoziweka al-Mudabbir, al-Baarii.” Katika lugha, Al-Mudabbir (Mpangaji) ni moja ya majina ya Mwenyezi Mungu (swt) na lina maana,    الذي يُجري الأمور بحكمته ويصرّفها على وفق مشيئته وعلى ما يوجب حُسْنَ عواقبها “ambaye huyapeleka mambo kwa hikma yake na anayasarifu kwa kuwafikiana na kutaka kwake na kwa mujibu wa kile kinachowajibisha uzuri wa matokeo yake.” Katika lugha, Al-Baarii (Muanzilishi) pia ni katika majina ya Mwenyezi Mungu (swt) na linamaanisha, واهب الحياة للأحياء، والسَّالم الخالي من أيِّ عيب “Yule anayetoa uhai kwa wanaoishi na Aliyesalimika (as-Saalim) kutokana kila aibu.”

Imam Abu Hanifa (rh) ameelezea kuhusiana na Tadbiir (Upangaji Mambo) ya dunia. Ibn Abi al-‘izz ameripoti kuwa: وَيُحْكَى عَنْ أَبِي حَنِيفَةَ رَحِمَهُ اللَّهُ أَنَّ قَوْمًا مِنْ أَهْلِ الْكَلَامِ أَرَادُوا الْبَحْثَ مَعَهُ فِي تَقْرِيرِ تَوْحِيدِ الرُّبُوبِيَّةِ فَقَالَ لَهُمْ أَخْبِرُونِي قَبْلَ أَنْ نَتَكَلَّمَ فِي هَذِهِ الْمَسْأَلَةِ عَنْ سَفِينَةٍ فِي دِجْلَةَ تَذْهَبُ فَتَمْتَلِئُ مِنَ الطَّعَامِ وَالْمَتَاعِ وَغَيْرِهِ بِنَفْسِهَا وَتَعُودُ بِنَفْسِهَا فَتُرْسِي بِنَفْسِهَا وَتَتَفَرَّغُ وَتَرْجِعُ كُلُّ ذَلِكَ مِنْ غَيْرِ أَنْ يُدَبِّرَهَا أَحَدٌ فَقَالُوا هَذَا مُحَالٌ لَا يُمْكِنُ أَبَدًا فَقَالَ لَهُمْ إِذَا كَانَ هَذَا مُحَالًا فِي سَفِينَةٍ فَكَيْفَ فِي هَذَا الْعَالَمِ كُلِّهِ عُلْوِهِ وَسُفْلِهِ (شرح العقيدة الطحاوية) ‘Imepokewa kutoka kwa Abu Hanifa Mwenyezi Mungu amrehemu kuwa watu katika wanafalsafa walitaka mjadala pamoja naye kuzungumzia upweke wa Mwenyezi Mungu. Abu Hanifa akasema, “Kabla ya kujadili mas-ala haya nielezeni mnafikiria nini kuhusu boti katika mto Furaat inayokwenda ufukweni, imebeba chakula na bidhaa nyengine, kisha inarejea, inafunga nanga na kushusha bidhaa zote yenyewe bila ya yeyote kuiongoza? Wakasema, “Hayo ni muhali na haiwezekani kabisa.” Abu Hanifa akawaambia, “Kama hilo haliwezekani kwa boti basi vipi kwa ulimwengu huu wote, ukubwa wake na ueneaji wake?” [Chanzo: Sharh al-Aqidah al-Tahawiyah 1/35]

Imam bin Hanbal (rh) alizungumzia kuhusu As-Saania (Mbunifu), ambapo As-Saania imekuja kutoka kwa neno la kiarabu kwa maana ya kubuni au kuunda. Mwenyezi Mungu (swt) amesema,

[صُنْعَ اللَّهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ]

“Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliyetengeneza vilivyo kila kitu” [Surah an Naml 27:88]. Ibn Kathir amesema, عَنِ الْإِمَامِ أَحْمَدَ بْنِ حَنْبَلٍ رحمه الله أَنَّهُ سُئِلَ وُجُودِ الصَّانِعِ فَقَالَ هَاهُنَا حِصْنٌ حَصِينٌ أَمْلَسُ لَيْسَ لَهُ بَابٌ وَلَا مَنْفَذٌ ظَاهِرُهُ كَالْفِضَّةِ الْبَيْضَاءِ وَبَاطِنُهُ كَالذَّهَبِ الْإِبْرِيزِ فَبَيْنَا هُوَ كَذَلِكَ إِذِ انْصَدَعَ جِدَارُهُ فَخَرَجَ مِنْهُ حَيَوَانٌ سَمِيعٌ بَصِيرٌ ذُو شَكْلٍ حَسَنٍ وَصَوْتٍ مَلِيحٍ يَعْنِي بِذَلِكَ الْبَيْضَةَ إِذَا خَرَجَ مِنْهَا الدَّجَاجَةُ “Imam Ahmad ibn Hanbal, Mwenyezi Mungu amrehemu, aliulizwa kuhusu uwepo wa Asswaani’ (Muundaji) akasema, “Zingatia ngome isiyopenyeka isio na milango wala eneo la kutoka. Nje yake ni kama fedha nyeupe, na ndani yake ni kama dhahabu inayomeremeta. Imejengwa namna hii hadi kuta zake zinapasuka na hutoka humo mnyama msikivu mwenye kuona mwenye umbo zuri na sauti nzuri.” Ahmad alikusudia kwa hilo, ni yai linapotoa kifaranga” [Chanzo: Tafsir ibn Kathir 2:21]

Imam Shafi (rh) amesema juu ya Uwepo wa Asswani’ (swt), kama ilivyopokewa na Ibn Kathir, هَذَا وَرَق التُّوت طَعْمه وَاحِد تَأْكُلهُ الدُّود فَيَخْرُج مِنْهُ الْإِبْرَيْسَم وَتَأْكُلهُ النَّحْل فَيَخْرُج مِنْهُ الْعَسَل وَتَأْكُلهُ الشَّاة وَالْبَقَر وَالْأَنْعَام فَتُلْقِيه بَعْرًا وَرَوْثًا وَتَأْكُلهُ الظِّبَاء فَيَخْرُج مِنْهَا الْمِسْك وَهُوَ شَيْء وَاحِد “Hili ni jani la mforosadi, ladha yake ni moja. Linapoliwa na nondo wa hariri, hariri hutokea. Linapoliwa na nyuki asali hutokea. Linapoliwa na mbuzi, ngombe na wanyama kinyesi na mbolea hupatikana. Linapoliwa na kulungu maski hutokea. Na hali ya kuwa ni kitu kimoja.” [Chimbuko: Tafsir ya Ibn Kathir]

Ama kwa wale wanaohusishwa na uundaji na uendeshaji wa maumbile yenyewe, Ibn al-Qayyim amesisitiza, اخبريني عَن هَذِه الطبيعة اهي ذَات قَائِمَة بِنَفسِهَا لَهَا علم وقدرة على هَذِه الافعال العجيبة ام لَيست كَذَلِك بل عرض وَصفَة قَائِمَة بالمطبوع تَابِعَة لَهُ مَحْمُولَة فِيهِ فَإِن قَالَت لَك بل هِيَ ذَات قَائِمَة بِنَفسِهَا لَهَا الْعلم التَّام وَالْقُدْرَة والارادة وَالْحكمَة فَقل لَهَا هَذَا هُوَ الْخَالِق البارئ المصور فَلم تسمينه طبيعية “Nielezeni kuhusu maumbile haya: Je dhati yake inajisimamia yenyewe? Je yana elimu na nguvu juu ya matendo haya ya kushangaza? Au sio hivyo bali hujitokeza na sifa za asili zinazojisimamia zenyewe? Kama watasema kuwa zinajisimamia zenyewe na zina elimu kamili, nguvu, utashi, na hikma, basi waambie huyu ni Muumbaji, Muundaji, Mtengenezaji, basi kwa nini mnaita maumbile?” [Chanzo: Miftah Dar al-Sa’adah 1/261]

Kile ambacho kina taswira ya uundwaji lazima kiwe na muundaji. Ibn al-Qayyim amesema, وَإِن قَالَت تِلْكَ بل الطبيعة عرض مَحْمُول مفتقر الى حَامِل وَهَذَا كُله فعلهَا بِغَيْر علم مِنْهَا وَلَا إِرَادَة وَلَا قدرَة وَلَا شُعُور اصلا وَقد شوهد من آثارها مَا شوهد فَقل لَهَا هَذَا مَالا يصدقهُ ذُو عقل سليم كَيفَ تصدر هَذِه الافعال العجيبة وَالْحكم الدقيقة الَّتِي تعجز عقول الْعُقَلَاء عَن مَعْرفَتهَا وَعَن الْقُدْرَة عَلَيْهَا مِمَّن لَا عقل لَهُ وَلَا قدرَة وَلَا حِكْمَة وَلَا شُعُور “Kama wakisema sio, bali maumbile ni sifa iliokosa uwakala na matendo yake yote yamekosa elimu, utashi, nguvu, au utambuzi kutokea kwenye chanzo chake na athari zake tu ndio zinashuhudiwa, basi waambie haya hayaaminiwi na mwenye akili iliosalimika. Basi vipi matendo haya ya kushangaza na ya kistadi, ambayo hayawezekani kutambuliwa au kupimwa na akili zilizopevuka, na kushindwa juu yake kwa wale wasio na busara, nguvu, hikma au ufahamu? [Chanzo: Miftah Dar al-Sa’adah 1/261]

Kwa kweli mambo yote na nidhamu inayoyatawala ni yenye kutokea na kuasisiwa na chengine kisichohisiwa. Basi vipi hao wanaodai kuwa ni hoja za kiakili katika fikra ya uyakinifu wanasema hayo?

Zaidi ya hivyo, Mwenyezi Mungu (swt) asema,

 [أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ]

“Au hao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji?” [TMQ At-Tur 52: 35].

Ibn Kathir ameelezea, أي: أوجدوا من غير موجد؟ أم هم أوجدوا أنفسهم؟ أي: لا هذا ولا هذا، بل الله هو الذي خلقهم وأنشأهم بعد أن لم يكونوا شيئا مذكورا “yaani, wamepatikana kutokana na kisichokuwepo (ghayri mawjuud)? Au walijileta wenyewe? Yote sio sawa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliyewaumba na kuwaleta baada ya kuwa hawakuwa chochote.” Hivyo katika lugha, husemwa, خَلَقَ اللهُ الإِنْسَانَ: أَوْجَدَهُ مِنَ العَدَمِ، أَنْشَأَهُ، صَوَّرَهُ “Mwenyezi Mungu (swt) amemuumba mwanaadamu: Amemleta kutokana na kisichokuwepo, amemuanzisha na kumpa umbo”.

Mwenyezi Mungu (swt) ameumba viumbe na viumbe sio sawa Naye. Yeye (swt) ni mkubwa zaidi ya ulimwengu na sio mtegemezi juu ya chochote cha kumsimamia. Mwenyezi Mungu (swt) ni Azzalii, Asiyeumbwa. Katika lugha, inasemwa kuhusu Azzalii, الأَزَلِيُّ ما لا أَوّل له “Kisicho na mwanzo ni kile kisicho na mtangulizi.” Hivyo, hakuna muendeshaji au muanzilishi kwa Azzalii. Pia inasemwa kuhusu Azzalii, الخَالِدُ الدَّائِمُ الوُجُودِ لاَ بَدْءَ لَهُ “Azzalii, muda wote yupo, hakuna mtangulizi kwake Yeye” Wakati Mwenyezi Mungu (swt) akiwa ni Azzalii, yupo bila kuwa ameumbwa, vyote vyenye kuhisiwa vimeumbwa, viko chini ya nidhamu. Tendo la uumbaji (khalq) ni kukileta kitu bila kutokana na chochote. Vyote ambavyo vinapatikana duniani havina uwezo wa kuumba au kukitoa chengine bila kutokana na chengine  (إبداع من عدم), ima kupitia kimoja kimoja au kwa pamoja. Hakuna kitu kimoja kimoja chenye uwezo wa kuumba au kuanzisha chengine bila kuwepo kwa chengine. Hata kwa vile vinavyojikamilisha kwa pamoja, vyote havina uwezo wa kuumba au kuanzisha chengine bila kuwepo chochote. Basi kwa vipi wale wanaodai kuwa ulimwengu wenyewe ni wa milele husema hivyo?

Kwa hakika, Ushahidi wa uwepo wa Mwenyezi Mungu (swt) unajionyesha katika kila chenye kuhisiwa. Vyote ni vitegemezi (muhtaaj) kwa vyengine, mbali ya vyenyewe. Utegemezi wao ni wa namna halisi (takayyuf) ambao umelazimishwa kwao. Utegemezi wao pia unaonekana kuwa wa kadiri maalum (taqdiir), kwa kiwango na ukubwa maalum. Hivyo uumbaji wa vile tunavyovihisi ni hakika, kwa sababu kuwa kwao katika utegemezi humaanisha kuwa vimeumbwa na mwengine, na sio vyenyewe. Hivyo, wingi wote wa vile tunavyovihisi ni dalili ya wazi ya uwepo wa Mwenyezi Mungu (swt), bila ya Yeye visingekuwepo, wakati Yeye (swt) hafanani na vyote ambavyo Yeye (swt) ameviumba.

Mwenyezi Mungu (swt) asema,

 [قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ * اللَّهُ الصَّمَدُ * لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ * وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ]

“Sema, Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee (1). Mwenyezi Mungu Mkusudiwa (2). Hakuzaa wala hakuzaliwa (3). Wala hana anaye fanana naye hata mmoja (4).” [Surah al-Ikhlaas 112:1-4]

 Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Musab Umair – Wilayah Pakistan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu