Jumapili, 12 Rajab 1446 | 2025/01/12
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Unyanyasaji Dhidi ya Wanawake na Watoto

Janga Lililoletwa Kutoka Magharibi ya Kisekula

Kuenea kwa ghasia ndani ya ndoa kumekuwa ndiyo ada kwa kuendelea kuongezeka kwa idadi ya wanawake na watoto katika biladi za Waislamu. Hususan, mbio za kuiga muondoko wa kimaisha na utawala wa Kimagharibi, ghasia za kinyumbani zimesababisha kiza kizito kinacho ongezeka juu ya mujtamaa za Waislamu. 

Kuvunjika kwa kiini cha familia, na hivyo basi hadhi na utulivu wa maisha ya kijamii katika ardhi za Waislamu ni natija ya yakini inayotokana pakubwa na kupigia debe fahamu na maadili ya kisekula ya kibinadamu yaliyoundwa na mfumo wa Kimagharibi wa kirasilimali. Mfumo huu hudai kuwa viwango ambavyo havina budi kutafutwa na mwanadamu ni maadili ya hali ya juu ambayo mwanadamu anajiwekea nafsi yake. Kwa msingi huo, hususan maadili ya Kimagharibi ya usawa wa kijinsia ni mojawapo ya fahamu msingi yaliyo enea katika mujtamaa na familia zetu kwa fitna zile zile za Wamagharibi wasiokuwa Waislamu. Zilifisidi mahusiano katika ndoa na maisha ya kijamii kupitia uhuru usio na mipaka na utafutaji matakwa ya kibinafsi; zilihujumu nukta zote za heshima, hali nzuri, hadhi kwa wanawake, watoto, na wanaume katika jamii. Wakati huo huo shutma kali za kisekula kwa sheria za kijamii za Kiislamu huziacha familia nyingi za Waislamu chini ya kinyongo cha kutapata.

Na ile dhana – kama aghalabu inavyodaiwa na wasomi wa kileo – kuwa muozo uchungu unaoendelea katika mujtamaa zetu ni kutokana tu na natija ya sera dhaifu juu ya wasiokuwa na talanta; ni makosa mno! Bali ni natija isokuwa na budi ya mfumo wa kirasilimali, ambao hauwezi kutatua kadhia nyeti za watu wake wenyewe. Hivyo basi ili kuhakikisha kubakia kwake, hauna chaguo jengine isipokuwa kuziba muozo wake pamoja na kuchafua na kuharibu utamaduni na miondoko ya kimaisha ya itikadi ya nidhamu nyenginezo. Kwa hayo haswa tatizo la ghasia katika mujtamaa zetu, hususan ghasia za kijamii, ni natija ya mradi muovu uliopangwa kabla kwa muda mrefu ili kuzikoloni ardhi zetu, uliomakinika kupitia utekelezaji nidhamu za kiutawala, serikali zao, taasisi rasmi, vyama na mashirika ya kutetea haki za wanawake, ambayo ni vifaa vya dola za kikoloni vinavyo tumiwa kuwatawala Waislamu. Makala haya yatatoa ushahidi wa ukubwa wa ghasia katika familia na dhidi ya wanawake na wasichana zinazoenea katika ardhi zetu za Kiislamu. 

Tunisia ndio nchi ya kwanza katika ulimwengu wa Kiarabu iliyo anzisha Kanuni ya Kileo ya Hadhi (CPS) mnamo 1957 iliyo badilisha sheria nyingi za kijamii na familia kwa zile zilizojengwa juu ya usekula. Dola hii tiifu ya kisekula daima iliwakilishwa na serikali za Kimagharibi, watetezi wa wanawake na taasisi kama muundo wa kutafuta haki za wanawake katika ulimwengu wa Waislamu. Lakini, upigiaji debe na utekelezaji wa maadili huru ya kisekula, sera na kanuni ndani ya mujtamaa wake yamepelekea tu ongezeko la ukandamizaji kwa watu wake na hususan ghasia dhidi ya wanawake. Leo, nchi hii iliyo Kaskazini mwa Afrika kwa sasa ina moja wapo ya viwango vikubwa mno vya ghasia za kifamilia ulimwenguni huku utafiti ukionyesha kuwa karibu nusu ya wanawake wote ni waathiriwa wa uhalifu huu katika kipindi fulani cha maisha yao. Utafiti uliofanywa na Chama cha Kidemokrasia cha Wanawake cha Tunisia (ATFD, ufupisho wake kwa Kifaransa) umefichua kuwa asilimia 84 ya wanawake ambao ni waathiriwa wa ghasia wameolewa, na asilimia 82 ya kesi hizi hutokea katika nyumba zao za ndoa.

Afisi ya Kitaifa ya Familia na Idadi ya Watu imefichua kuwa takriban asilimia 50 ya wanawake wa Tunisia wameteseka kupitia baadhi ya aina za ghasia, na kwamba asilimia 42 yao wamehitimu chuo kikuu. Uchaguzi wa kiwango cha wastani cha wanawake 3000, ulionyesha kuwa asilimia 31 yao wamewahi kuwa waathiriwa wa ghasia za kimwili, asilimia 28 wamepitia ghasia za kijinsia na asilimia 7.1 walikabiliwa na ghasia za kiuchumi (13 Agosti 2014). Mwaka huu, utafiti mwengine, uliochapishwa na Kituo cha Utafiti, Uchunguzi, Unakili na Habari juu ya Wanawake (Kundi la Kitunisia kwa ushirikiano na UN), liligundua kuwa asilimia 70 – 90 ya wanawake wamekuwa ni waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia, wengi wao wakiwa katika usafiri wa umma, kuanzia 2011 hadi 2015.

Chimbuko jengine la wasiwasi kuhusiana na usalama wa wanawake nchini humo ni usafirishaji wa wanawake. Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), Tunisia ni chimbuko, sehemu na nchi ambayo ni njia ya usafirishaji wanawake ambao “wanafanyishwa kazi kwa lazima na kusafirishwa kwa ajili ya ngono”.

Yote haya yanaonyesha kuwa kutabanni kanuni kwa aina yoyote hakujafeli tu kuwalinda wanawake nchini Tunisia, bali kikweli imepelekea ukandamizaji mbaya na ongezeko la ghasia. Na bado, nchi hiyo inahamu ya kutekeleza zaidi maadili na kanuni za kisekula za Kimagharibi, kama kuanzisha usawa kamilifu wa kijinsia katika katiba yake, na “Sheria ya Kuondoa Ghasia dhidi ya Wanawake” ambayo inatarajiwa kutekelezwa mwaka huu.

Uturuki ni biladi nyengine ya Kiislamu iliyopewa misheni ya kuwa kiigizo chema kwa haki za wanawake na kuwa mwanzilishi katika kupigia debe na kutabikisha maadili ya kirasilimali kama usekula, demokrasia na usawa wa kijinsia katika ulimwengu wa Kiislamu. Uturuki imeshiriki kichangamfu takriban katika kila makubaliano ya kimataifa kuhusiana na wanawake. Iliidhinisha mkataba wa kimataifa wa UN, Kongamano juu ya Kuondosha Aina zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) mnamo 1986, na kuasisi Kitengo Jumla juu ya Hadhi ya Wanawake (GDSW) kama mbinu ya kitaifa mnamo 1990 ambayo ilichangia pakubwa kushiriki kichangamfu kwa Uturuki katika Tangazo la Beijing na Jukwaa la Utendakazi juu ya michakato ya haki za wanawake mnamo 1995. Ilikuwa nchi ya kwanza iliyotia saini Kongamano la Kukinga na Kupambana na Ghasia dhidi ya Wanawake na Ghasia za Kinyumbani mnamo Mei 11, 2011 na kuwa nchi ya kwanza kuliidhinisha mnamo Novemba 25, 2011. Kupambana na ghasia dhidi ya wanawake kulitambulika kama sera ya dola hiyo na kukumbatiwa na taasisi nyingi za dola yake tangu 1995.

Ilhali vitendo vyote na juhudi zote hizi na miradi ya kupigia debe na kutekeleza usawa wa kijinsia ndani ya nchi hiyo vilizalisha ongezeko la kasi la viwango vya ghasia dhidi ya mwanamke ulimwenguni. Kwa mujibu wa Wizara ya Haki ya Uturuki, kuanzia 2003 (pindi chama cha APK kilipoingia mamlakani) hadi 2014, kulikuweko na ongezeko la asilimia 1,400 katika idadi ya mauwaji ya wanawake. Na ni muhimu kutaja kuwa mabadiliko makubwa katika kanuni na sheria kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa kama CEDAW na Tangazo la Beijing yalifanywa na serikali ya APK.

Kwa mujibu wa TUIK (Taasisi ya Takwimu ya Uturuki), wanne kati ya wanawake kumi hukumbwa na ghasia za kinyumbani, huku Wizara ya Familia na Sera za Kijamii ya Uturuki ikiripoti kuwa asilimia 86 ya wanawake nchini Uturuki walipitia ghasia za kimwili au kisaikolojia kutoka kwa wapenzi wao au mwanafamilia mwenza. Zaidi ya wanawake 300 walikufa kutokana na ghasia za kinyumbani mnamo 2015 pekee. Mnamo 2014, mamia ya wanawake waliuwawa na wanandoa wenzao katili hata baada ya kuomba hifadhi ya polisi. Kwa sasa Uturuki inasimamia nyumba rasmi takriban 100 zinazowapa makao wanawake chini ya 3,000, huku mashirika yasiyo ya kibiashara yakilemewa na kung’ang’ana kuwachunga wanawake wengine 20,000 zaidi wanao tafuta makao kila mwaka. Ripoti hiyo ya shirika la wanawake (Kadın Cinayetlerini Durduracağız Platformu) lilifichua mauwaji 409 ya wanawake, kesi 387 zilizo rekodiwa za dhulma za kimapenzi kwa watoto, na kesi 332 zilizo rekodiwa za ghasia za kijinsia kwa wanawake mnamo 2017. Idadi inaongezeka kwa kasi kila mwaka. Zaidi ya hayo, la kuogofya zaidi ni habari moja kuhusiana na ghasia dhidi ya watoto. Mtindo mpya unaibuka katika kesi za talaka, ambapo kina baba huwauwa watoto wao wenyewe kama kisasi cha talaka wanayoikataa. Hivyo basi, watoto 20 waliuwawa na baba zao wenyewe mnamo 2017 pekee.

Idadi na ripoti kutoka katika biladi za Kiislamu, zinazo tawaliwa na serikali na nidhamu za kisekula au serikali na nidhamu nyenginezo zisizo kuwa za Kiislamu, zinaashiria sura kama hii: Nchini Afghanistan asilimia 80 ya wanawake wa Afghan wanapitia au washapitia kwa uchache aina mojawapo ya ghasia katika maisha yao (UNFPA 2016). Wizara ya Afya ya Umma ilisajili kesi 8,188 za ghasia za kijinsia ambapo kesi 2,806 zilikuwa za ghasia za kimwili, 3,470 dhulma za kisaikolojia, 1,207 ukosefu wa njia ya kufikia rasilimali, 403 ndoa za lazima, 166 dhulma za kimapenzi na 136 unyanyasaji wa kimapenzi dhidi ya wanawake. Wizara ya Mambo ya Wanawake ya Afghanistan ilitangaza takribani kesi 4,000 zilizo rekodiwa za ghasia dhidi ya wanawake mnamo 2017.  

Karibu wanawake milioni 1.5 nchini Misri wanapitia ghasia za kinyumbani kila mwaka kwa kiwango cha zaidi ya kesi 4,000 kila siku (Baraza la Kitaifa la Wanawake nchini Misri / 2016). Nchini Palestina, takriban asilimia 37 ya wanawake ambao wameolewa washawahi kupitia aina mojawapo ya ghasia kutoka kwa waume zao (Utafiti wa Kitaifa juu ya Ghasia katika Jumuia ya Palestina, 2011). Indonesia takwimu zake ni kama hizi zinazo eleza kwa ufupi kuwa kesi 245,548 za ghasia dhidi ya wake zilitokea mnamo 2016 pekee (Komnas Perempuan, 2016). Malaysia inafuata kuripotiwa kesi 10,282 za ghasia za kinyumbani mnamo Januari 2016 pekee (WAO, 2016). Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC huduma ya Kifursi, asilimia 66.3 ya wanawake nchini Iran wamepitia ghasia maishani mwao (RUDAW, 2014).

Janga hili kubwa la ghasia dhidi ya wanawake na ghasia za kinyumbani ukweli ni kadhia iliyo ingizwa ndani ya ardhi zetu kutoka Magharibi inayoteseka yenyewe kutokana na janga la uhalifu kama huu kutokana na nidhamu yake ya kirasilimali, kisekula na thamani huru. Kwa mfano, nchini Uingereza, wanawake milioni 1.2 waliripoti dhulma za kinyumbani nchini Uingereza na Wales katika mwaka wa 2016, na mwanamke 1 kati ya 4 hupitia ghasia za kinyumbani. (Afisi ya Kitaifa ya Takwimu). Mnamo 2014, utafiti uliofanywa na shirika la Haki Msingi la Muungano wa Ulaya (FRA), lilifichua kuwa thuluthi moja ya wanawake katika Muungano wa Ulaya washapitia ghasia za kimwili au za kimapenzi tangu umri wa miaka 15, sawia na watu milioni 62. Utafiti huo kutoka nchi 28 za Ulaya pia uligundua kuwa 1 kati ya wanawake 10 barani humo ashawahi kuteseka kupitia baadhi ya aina za ghasia za kimapenzi na 1 kati ya 20 amebakwa, asilimia 55 walipitia unyanyasaji wa kimapenzi, aghalabu makazini, huku asilimia 75 ya wanawake waliofuzu taaluma au walio katika vyeo vya juu makazini wamepitia aina hii ya ukiukaji dhidi ya heshima yao, ikivunjilia mbali madai ambayo aghalabu hurudiwa kuwa ajira ni njia ya kuinua hadhi ya wanawake. Cha kuchekesha ni, nchi zilizo na idadi kubwa zaidi ya matukio ya ghasia zilikuwa ni Denmark (asilimia 52), Finland (asilimia 47), na Sweden (asilimia 46) – dola zilizo sifiwa kwa kanuni zake za usawa wa kijinsia na kutajwa kama nchi zilizo na usawa zaidi wa kijinsia kwa mujibu wa jedwali la Usawa wa Kijinsia la UN, ripoti ya Jukwaa la Uchumi wa Dunia ya 2013 na Taasisi ya Ulaya ya Usawa wa Kijinsia. 

Na hizi ni baadhi ya takwimu kuhusu ghasia nchini Amerika, zilizochapishwa katika gazeti la ‘Huffington Post’ mnamo Aprili 5, 2017: Kila siku zaidi ya watu 570 hupitia ghasia za kimapenzi katika nchi hii ambayo imejaa takribani visa vya kila siku vya dhuluma za kimapenzi katika vitivo vya chuo, na kwamba hata inatawaliwa na Raisi ambaye ametuhumiwa hadharani akiwadhulumu kimapenzi zaidi ya wanawake 15. Takribani wanawake milioni 18 wamekuwa waathiriwa wa ubakaji tangu 1998. 1 kati ya wanawake 6 wa Amerika aliokoka na jaribio au ubakaji wa kihakika katika maisha yao. Idadi ya wastani ya waathiriwa wa ubakaji kwa mwaka inafikia hadi 321,500. Zaidi ya hayo, ghasia za kinyumbani ni za kawaida mno nchini Amerika, ambapo karibu wanawake milioni 5 hupitia ghasia za kimwili kutoka kwa mpenzi wake … na kadhalika … Kila aina ya dhuluma ya kimapenzi, ubakaji na aina nyengine za ghasia zaweza kupatikana viwango vya kutisha mno katika nchi hii, huku ikidai kuwa msimamizi wa haki za wanawake na binadamu.

Kiulimwengu wanawake na wasichana ni asilimia 80 ya makadirio ya watu 800,000 wanaosafirishwa kuvuka mipaka ya nchi kila mwaka, huku asilimia 70 yao wakisafirishwa kwa ajili ya kudhulimiwa kimapenzi. Hadi wanawake 7 kati ya 10 kwa mujibu wa ripoti ya dunia wamepitia ghasia za kimwili au za kimapenzi katika kipindi fulani cha maisha yao. Kote duniani hadi asilimia 50 ya dhuluma za kimapenzi hufanywa dhidi ya wasichana chini ya umri wa miaka 16. Zaidi ya wasichana milioni 100 hupotezwa kutokana na kuchaguliwa kwa ngono. Na yote haya yamejitokeza huku mfumo huru wa kisekula wa kirasilimali unaotawala siasa za kimataifa na kitaifa leo na kujionyesha kutokuwa na fununu na kutokuwa na uwezo wa kusitisha wimbi hili la ghasia dhidi ya wanawake na wasichana. Zaidi ya hayo, mjumuiko wa kanuni za usawa wa kijinsia, vifungu na miradi yake pamoja na mipango yake na sheria yake inayopigiwa debe kimataifa na kutekelezwa ndani ya dola za kimagharibi na za Waislamu ili kukabiliana na ghasia dhidi ya wanawake na wasichana imefeli waziwazi hata kupunguza mizani ya tatizo hili.  

Mifano hii ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu yaonyesha kuwa maadili huru ya kisekula ya urasilimali, yanayo shajiisha watu binafsi kutekeleza matamanio na matakwa yao na ambayo sekta za burudani, zimeidunisha hadhi ya wanawake na kupigia debe uhuru wa ngono ambao unaufisidi na kuudhuru uhusiano baina ya jinsia ndani ya mujtamaa na imechochea moja kwa moja kudunishwa, kudhalilishwa na tabia ya ghasia dhidi ya wanawake kote ulimwenguni. Zaidi ya hayo, ukosefu wa hukmu na sheria za kukinaisha na kuridhisha ili kupangilia mambo na maingiliano baina ya wanaume na wanawake pamoja na ukosefu wa adhabu stahiki kwa wakiukaji wowote dhidi ya heshima na hadhi ya wanawake ilipelekea kukolea kusikodhibitika kwa ghasia dhidi ya wanawake. Maadamu maadili haya na mitazamo hii fisidifu itabakia ni yenye kutawala katika jamii zetu, kuunda sera chache au kanuni au kuunda miradi na mashirika ya wanawake daima zitafeli kuzungumzia tatizo hili. Badala yake zitaendeleza tu hali halisi, kuhifadhi utawala na uwepo wa nidhamu ya kiitikadi yenye kudhuru itokayo kwa mkoloni na miundo katika ardhi za Waislamu, ikiongeza zaidi uhalifu unaokiuka heshima na hali nzuri ya wanawake, na kuharakisha uharibifu wa muundo wa kijamii wa jamii za Waislamu. 

Suluhisho pekee la janga hili ni kupinga kwa ujumla nidhamu mbovu za uhuru za kisekula zilizo lazimishwa juu yetu na wakoloni wa Kimagharibi wa kirasilimali na kuunda mustakbali wa ardhi za Waislamu juu ya mfumo wa Kiislamu pekee.

قُلْ أَتُعَلِّمُونَ اللٌّهَ بِدِينِكُمْ وَاللٌّهُ يَعْلَمُ مٌا فِي السَّمٌوٌاتِ وَمٌا فِي الأَرْضِ وَاللٌّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿

“Sema (ewe Muhammad): ‘Je, munamfundisha Allah kuhusu Dini yenu (mfumo kamili wa maisha) na ilhali Allah anajua vilivyomo ndani ya mbingu na vilivyomo ndani ya ardhi; Na hakika Allah ni mjuzi wa kila kitu.” [Al-Hujraat: 16]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Zehra Malik

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 07:11

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu