Jumatatu, 21 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Kifo cha Dolari

(Imetafsiriwa)

Kumekuwa na mazungumzo mengi juu ya kifo cha dolari na katika muongo mmoja uliopita, idadi kadhaa ya wenye kushindana imeibuka kudai nafasi ya ubwana wa dolari. Kutokana na kuibuka kwa China, wengi wanaizingatia China kuwa katika nafasi ya mhimili wa kuichukua nafasi ya dolari ya Amerika. Dolari imecheza dori kuu katika kuidhibiti nafasi ya kiulimwengu ya Amerika; imeitumia fursa hii kuzuia mataifa na kuyatenga na biashara ya kiulimwengu na pia kuyalazimisha mataifa kuunga mkono malengo ya sera za kigeni za Amerika.

China imekuwa ikizungumzia juu ya kuchukua nafasi ya dolari kwa kipindi sasa. Maendeleo ya China yametabiriwa juu ya mauzo yake makubwa ya bidhaa kwa Amerika, kupelekea kurundika akiba ya dolari zaidi ya trilioni 3. Mnamo Julai 2020, Benki ya taifa ya China ilichapisha ripoti ikisema kuwa kutokana na kitisho cha vikwazo kutoka Amerika, China inapaswa kufanya malipo zaidi ya kimataifa kupitia miundo mbinu yake yenyewe ya kifedha.

Majaribio ya China kujiweka mbali na dolari inajumuisha kuunda kambi ya BRICS. Inajaribu kuanzisha hatua za kuweka mfumo wake wenyewe wa malipo uitwao CIPS ambao utakuwa ni mbadala wa mfumo wa SWIFT. China pia imeanzisha Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB), kuwa ni mbadala wa IMF na Benki ya Dunia mnamo 2014. Maraisi wa Amerika mtawalia waliweka vikwazo kwa Iran na vikwazo hivi vilimuadhibu kila aliyetumia dolari kununua mafuta ya Iran. Donald Trump, wakati wa uraisi wake, alimuonya kila aliyefanya biashara kwa dolari na Iran kuwa atakabiliana na vikwazo vikali. Kwa kweli aliitumia dolari kama silaha na hili liliichochea China kuchukua hatua za kusitisha utumiaji wa dolari. Mnamo 2018, Soko la Ubadilishanaji wa bidhaa la Shanghai lilizindua mkataba wake wa mwanzo wa uuzaji na ununuzi wa bidhaa na ambao ulikaribisha wawekezaji wa kigeni. Mkataba huu, Yuan mustakbali mkuu wa mafuta, una uwezo wa kuwa mshindani wa mikataba iliyotawaliwa na dolari ya Brent na WTI ambayo inahudumu kama alama teule ya sasa.

Lakini huku sarafu ya Yuan ya China ikipata nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari, ukweli ni kuwa haikaribii kabisa kuwa sarafu ya kimataifa. Katika matumizi ya kimataifa, Yuan inatumika kwa malipo ya asilimia 1.22 tu, wakati dolari za Canada na Australia zinatumika zaidi katika biashara. Muundo wa kiuchumi wa China kwa muda mrefu umedhibiti kiwango cha chini cha ubadilishanaji wa fedha, na matokeo yake, China inachapa kiwango kidogo tu cha Yuan na kuweka ukomo wa kuenea kwake ili kudhibiti kiwango chake cha chini cha ubadilishanaji ambacho kinasaidia mauzo yake ya nje ya bidhaa. China ina vizuizi vingi juu ya kubadilisha sarafu yake. Ina udhibiti wa mitaji na sarafu yake haipatikani kwa wepesi duniani. Wakati China ilipoifanya Yuan iweze kubadilishwa kwa uwazi mnamo 2010, utokaji nje wa fedha na mitaji ulikuwa mkubwa na ubadilishaji kamili ulizuiwa. Matokeo yake ni kuwa, hadi vizuizi hivi viondolewa, Yuan haiwezi kuwa sarafu ya akiba ya kilimwengu na kuipiku dolari.

Changamoto halisi katika kuipiku dolari ni kuwa hakuna mbadala halisi hivi sasa. Matamko ya kawaida ya Urusi ya kuwepo sarafu nyengine za kitaifa kuchukua nafasi ya dolari na kufanya malipo ya mafuta yawe kwa sarafu isiyokuwa dolari ni kutokana na vikwazo vya US kwa Urusi baada ya uvamizi wake kwa Crimea na Ukraine ya Mashariki mwaka 2015. Urusi ikaamua kutokana na hili kuwa lazima ipunguze utegemeaji wake juu ya dolari na imechukua baadhi ya hatua kufanikisha hili, lakini licha ya kujaribu kupunguza matumizi yake ya dolari, nchi nyingi duniani hazitaki kununua roubles (sarafu ya Urusi), ambayo inayumba sana katika soko la fedha.

Euro ni sarafu ya pili ya akiba baada ya dolari. Wakati ukanda wa ulaya ulipoundwa mnamo 1999, wengi walitabiri kuwa euro itaipiku dolari. Tokea kipindi hicho, mgawanyiko miongoni mwa nchi za Ulaya umekuwa mbaya zaidi. Wawekezaji wamekuwa wakisita kuaminisha juu ya euro kwa hofu ya kuwa jumuiya ya sarafu hiyo inaweza kuvunjika wakati wowote. Japokuwa euro inatumika kibiashara kwa kiasi kikubwa, lakini inatumika zaidi miongoni mwa nchi za Ulaya na kwa hivyo imekuwa ni sarafu ya kieneo zaidi, na sio ya kiulimwengu.

Kama dolari ya Canada, Australia, na ya New Zealand, pamoja na Pauni ya Sterling, Krona ya Uswisi na ya Denmark zikijumuika na kuwa sarafu za kiulimwengu zinazoachwa zibadilike bila kizuizi, zitaweza kufikia kiwango cha robo tu ya miamala ya kiulimwengu. Sarafu ya akiba ya kiulimwengu inahitaji kurahisisha biashara ya kimataifa, lakini mjumuiko wa sarafu hizi hauwezi kutosheleza hitajio hili.

Huku sarafu za kitaifa zikiwa zimetumika kama akiba ya rasilimali za dunia, baadhi wameona kuwa mbadala unaofaa zaidi wa dolari ni sarafu ya aina nyengine kabisa. Mielekeo miwili inayojiri, haswa, ina uwezo wa kutoa sarafu za kimataifa zisizo za kitaifa: Hundi ya Akiba kwa wanachama wa IMF (Special Drawing Right), na sarafu za kidijitali (cryptocurrencies) kama bitcoin.

SDR inafanya kazi kama fedha ya ndani ya IMF. Thamani yake inatokana na kikapu cha sarafu tano kubwa: dolari, yuan, euro, yen na pauni ya sterling. Nchi zina akaunti za SDR katika IMF, na zinaweza kukopesha na kukopa baina yao kwa kutumia SDR pindi zinapotaka. Hazina hii inafanya maamuzi kwenye kapu, kama kwa mfano sarafu gani ziingizwe na vipimo gani vitumike kukokotoa thamani yake. Katika miaka ya karibuni, liliibuka pendekezo kuiendeleza SDR kuwa sarafu itakayoweza kutumika na watu binafsi na makampuni, kwa kuwa hivi sasa ni nchi tu zinazoweza kuitumia.

Bitcon ilikuwa ni moja ya waanzilishi katika sarafu za kidijitali. Sarafu hizi zinatumia mfumo mgumu – namna pana ya buku la mahesabu au teknolojia ya mnyororo ambapo watumiaji wanagawanya mzigo wa utendaji wa sarafu kwa kutoa nguvu zao za kompyuta, kubuni sarafu ya ‘kidemokrasia’ ambayo haihitajii benki kuu kuisimamia.

Ripoti ya 2015 ilionyesha kuwa wajuzi wa mambo ya bitcoin waliitegemea kuwa ni sarafu ya sita kubwa zaidi ya akiba ifikapo 2030. Lakini tokea kipindi hicho thamani ya sarafu za Bitcoin zimekuwa zikiyumba sana kutokana na wepesi wake wa kubadilika badilika na kwamba El Salvador ambayo ni nchi pekee iliyokubali kuitumia Bitcoin haijathibitika kunufaika kwa kuifanya sarafu yake ya taifa, imani katika sarafu ya kidijitali kuchukua nafasi ya sarafu zilizopo iko mbali sana. SDR na bitcoin zote zinakabiliana na suala moja: kukosekana kwa nguvu. Zote zimeiondoa mamlaka kuu kusimamia utoaji wa sarafu bali pia zinaukosesha mwega unaoweza kutolewa na mataifa makuu ya ulimwengu.

Dolari itaendelea kuwa katika nafasi yake ya kiulimwengu hadi taifa jengine liweze kuifanya sarafu yake kuwa ya kimataifa na kuifanya ni mbadala. Huku hili likionekana kuwa liko mbali sana, hali ya uchumi wa Amerika ni ya mashaka, ikiwa na deni linalotanuka, nakisi ya akaunti hivi sasa na ufungaji wa mara kwa mara wa serikali wa shughuli. Fursa inaweza kupatikana hasa wakati Amerika ikizidiwa na kukabiliwa na mgawanyiko mkubwa wa ndani utakaoshtukizwa na taifa jengine kwa haraka litaloongeza dori yake ya kimataifa na kuiweka sarafu yake katika nafasi kuu ndani ya uchumi wa kimataifa. Kwa hivyo kuipiku dolari inakuwa ni suala la kisiasa zaidi kuliko kuwa ni la kiuchumi.

Imeandikwa Kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb Ut Tahrir na

Adnan Khan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu