Jumapili, 20 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Sakata ya Imran Khan

(Imetafsiriwa)

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan, Imran Khan alikamatwa kwa kasi na maafisa wa kutuliza ghasia alipokuwa mahakamani kujibu mashtaka ya ufisadi na uchochezi. Wafuasi wa Khan waliingia mabarabarani, wakiteketeza magari, kushambulia kambi za jeshi pamoja na nyumba za baadhi ya makamanda. Kukamatwa na kufungwa kwa Mawaziri Wakuu wa zamani sio jambo la kawaida nchini Pakistan, hatua dhidi ya jeshi hata hivyo ni kawaida. Imran Khan na jeshi kwa muda mrefu walikuwa na mahusiano mazuri lakini haya yote yamefikia mwisho mkubwa kwani mahusiano yamezorota.

Jeshi la Pakistan tangu muongo wa kwanza baada ya kugawanywa Pakistan liliweza kuchukua madaraka kwani kizazi cha kwanza cha viongozi wa Pakistan hakikuweza kukabiliana na changamoto za Pakistan. Jeshi liliimarisha dori yake wakati Vita Baridi vilipokuwa vikianza na Pakistan ilijiunga na mkakati wa udhibiti wa Amerika dhidi ya USSR. Vifaa vya kijeshi pamoja na misaada ya kijeshi na kiuchumi ilimiminika nchini Pakistan na kuwafanya wanajeshi kuwa watawala halisi wa Pakistan. Jeshi kwa wakati huo lingepanua mamlaka yake na kujenga maslahi yake ya kiuchumi kutoka kwa biashara hadi ardhi na mali. Leo jeshi la Pakistan ni kampuni kama ambavyo pia ni jeshi. Kutokana na hili, jeshi limekuwa na mamlaka ya moja kwa moja, likiendesha serikali kwa miaka 31 kati ya miaka 76 ya uwepo wa Pakistan. Lakini linapokuwa haliko serikalini jeshi limekuwa likiunda wanasiasa, kuwahamisha, kuwatumia kusawazisha dhidi ya wengine. Pindi mwanasiasa wa kiraia anapokuwa na tamaa kubwa au anapinga nafasi ya jeshi nchini Pakistan anaweza kuondolewa au hata kunyongwa kama Zulfiqar Ali Bhutto alivyo nyongwa mwaka 1979.

Jeshi lilimgeukia Imran Khan katika miaka ya 2010 huku mienendo ya Pakistan ikibadilika na kutishia hali halisi ilivyo. Uungaji mkono wa Jenerali Musharraf kwa vita vya Marekani dhidi ya ugaidi na kupiga marufuku kwake makundi yaliyokuwa yakijaribu kuikomboa Kashmir haukupata tu jina la 'Busharraf,' lakini pia ulitilia shaka uaminifu wa jeshi. Jeshi lilianza mazungumzo katikati ya miaka ya 2000 pamoja na Benazir Bhutto, na hatimaye kupelekea mumewe Asif Ali Zardari kuwa Rais kutoka 2008 - 2013 na kisha Nawaz Sharif kuregea madarakani kutoka 2013. Kizazi kizima cha Wapakistani kilikulia katika vita dhidi ya ugaidi na Uvamizi wa Marekani kwa Afghanistan na kuwaona Musharraf, Zardari na Sharif kuwa wasioguswa na hisia zao. Uchumi pia ulidorora sana kwani viongozi kama vile Zardari walikuwa na hamu zaidi ya kukaa katika ikulu ya rais badala ya kufanyia kazi sera ya kitaifa. Wakati Nawaz Sharif alipochukua nafasi ya Zardari mnamo 2013 mambo yalizidi kuwa mabaya. Viongozi wa juu wa kijeshi walikuwa na wasiwasi kwamba kizazi hiki kipya kilikuwa kinazidi kuwa na msimamo mkali zaidi kwani serikali, uchumi na watawala walikuwa kinyume kabisa na hisia zao. Ilikuwa katika muktadha huu uongozi wa juu wa jeshi ulimgeukia Imran Khan.

Imran Khan alikuwa na taaluma ya kriketi yenye mafanikio ambayo ilimpelekea kuwa nahodha wa timu ya taifa hadi Kombe la Dunia mwaka wa 1992. Khan, shujaa wa kitaifa, alistaafu baada ya hili na kulenga kujenga hospitali ya kwanza ya saratani ya Pakistan. Mnamo 1996 Khan alianzisha Pakistan Tahreeq-i-insaf (PTI) - harakati ya kupigania haki, na akaingia kwa mara ya kwanza katika siasa za kitaifa. Lakini kwa miongo miwili iliyofuata Khan angesalia nyikani huku chama chake kikijitahidi kushinda viti vyovyote katika bunge la kitaifa, isipokuwa Khan mwenyewe. Khan alifanikiwa kushinda bunge la jimbo la Khyber Pakhtunkhwa mwaka wa 2013 na hapa ndipo alipojenga wasifu wake kwa kauli mbiu zake dhidi ya Wamarekani na dhidi ya ufisadi. Katika enzi ya siasa za umaarufu Khan alipitisha kauli mbiu za Dola ya Madina, dola ya ustawi, haki na kung'oa ufisadi. Wakati huo Pakistan ilikuwa katika machafuko ya kiuchumi huku wanasiasa wakipora nchi. Lakini kulikuwa na mambo mawili muhimu ambayo yalibadilisha bahati ya Khan, baada ya kuwa katika jangwa la kisiasa kwa muda mrefu. Kwanza jeshi lilikuwa linatafuta mtu ambaye angeweza kurudisha imani kwenye mfumo. Kwa vile chama cha Khan kilibuniwa pambizoni mwake mwenyewe na haiba yake jeshi lilifanya kama lilivyokuwa likifanya siku zote, lilipata idadi kadha ya wanasiasa kuvihama vyama vyao na kujiunga na cha Imran Khan. Mambo haya mawili ndiyo yaliyopelekea Imran Khan kuwa Waziri Mkuu mwaka 2018.

Kuanzia 2018 hadi mwisho wa 2021, Imran Khan alikuwa na uhusiano mzuri sana na jeshi. Khan hakuacha kulisifu jeshi, akiliita nguzo ya nchi. Lakini mnamo Oktoba 2021, Imran Khan alifunga hatima yake.

Jenerali Bajwa aliripotiwa kutuma barua kwa Waziri Mkuu kutangaza mabadiliko kadhaa ya wafanyikazi katika jeshi. Hili ni jambo ambalo daima limefanyika; mkuu wa jeshi huamua upandishaji vyeo, kustaafu, uhamisho, kisha serikali ya kiraia inatangaza haya kutoa picha ya demokrasia. Khan hata hivyo angeburuza miguu yake wakati mhudumu wake Luteni Jenerali Faiz Hameed, ambaye alipanga kupanda kwake madarakani alipokuwa akihamishwa kutoka kuwa mkuu wa shirika la kijasusi la ISI - Pakistan, hadi kuwa Kamanda wa Jeshi. Kwa Jenerali Bajwa huu ulikuwa mstari mwekundu ambao hakuna raia anayepaswa kufikiria kuuvuka. Jenerali Bajwa alifika kwa Masharif nchini Uingereza ambao wangetoa chachu kwa Pakistan Democratic Movement (PDM) ambayo ilikuwa muungano wa wanasiasa wanaompinga Imran Khan waliokuwa wakitafuta madaraka. Hii iliishia kwa kura ya kutokuwa na imani mnamo Aprili 2022 wakati wanasiasa wengi waliojiunga na Imran Khan na kumsaidia kutawala, waliachana naye.

Imran Khan alikataa kushuka chini kimya kimya. Khan alianza kampeni ya hotuba, matembezi na maandamano kwamba kuondolewa kwake ni njama ya kigeni, iliyopangwa na Marekani kwa ushirikiano na Jenerali Bajwa. Khan pia aliendeleza wazo kwamba wezi wa zamani walikuwa wamerudi madarakani, ambao walikuwa wamepora nchi kwa muda mrefu.

Khan amepiga hesabu ya rai jumla kuwa upande wake, huku serikali iliyochukua nafasi yake ikihangaika na uchumi na jenerali mpya wa jeshi bado hajajithibitisha kuwa yuko katika nafasi ya nguvu badala ya udhaifu. Jenerali Bajwa na inaonekana kana kwamba Jenerali Munir wote wamekosea hesabu za msaada ambao Imran Khan anao na kudhani wangeweza, kama vile jeshi linavyofanya siku zote, kucheza mchezo wa chesi wapendavyo wao. Jeshi linajaribu kutumia taasisi tofauti nchini Pakistan kuanzia idara ya mahakama hadi vyombo vya habari kumhujumu Imran Khan. Lakini Imran Khan amefanikiwa kujenga rai jumla dhidi ya jeshi, ambalo Khan analishutumu kuunga mkono serikali ambayo imejaa wezi. Hili ni eneo lisilojulikana la jeshi ambalo kila wakati rai jumla ilikuwa upande wake. Jeshi sasa linakabiliwa na uundaji wa miundo yake wenyewe ambayo inakataa kwenda chini bila ya mapambano.

Imran Khan sasa anaitisha maandamano kadhaa ya uhuru huku akikabiliwa na kesi mbalimbali mahakamani. Uamuzi wa Mahakama ya Upeo kwamba ni kinyume cha sheria kwa vikosi vya kijeshi kumkamata Khan unaimarisha zaidi msimamo wa Khan. Inasalia kuonekana iwapo makubaliano yanaweza kufanywa kati ya pande mbili zinazo zozana ambazo zinataka kukaa juu ya kiti cha enzi cha Pakistan.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Adnan Khan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu