Jumapili, 05 Rajab 1446 | 2025/01/05
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 “Usasa wa Kiislamu (الحداثة الإسلامية)”:
Shambulizi kwa Sunnah ya Mtume

(Imetafsiriwa)

Usasa wa Kiislamu (الحداثة الإسلامية) unakusudia fikra inayotaka kutafsiri upya Uislamu ili kuwiana na maadili na miundo ya mfumo wa kilimwengu wa kiliberali wa Kimagharibi. Ikiibuka katika karne ya 19, wimbi hili la mageuzi lilisukumwa na watu mashuhuri kama vile Jamal ud Din Afghani, Muhammad Abduh, Rashid Rida, na Syed Ahmed Khan. Juhudi zao zililenga kufanya maridhiano ya Uislamu na mifumo ya kisasa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Ufafanuzi huu upya, hata hivyo, mara nyingi ulihusisha upotoshaji wa kanuni za Kiislamu ili kuendana na desturi zinazobadilika za ulimwengu wa kisasa, ikiwa ni pamoja na fahamu za Kimagharibi kama vile utaifa, urasilimali, sheria za binadamu, haki za binadamu, usawa wa kijinsia, na maelewano ya dini mbalimbali.

Moja ya changamoto kuu zinazoletwa na usasa ni jaribio la kuunda upya Uislamu ili kuhalalisha fikra za Kimagharibi kama vile uvamizi wa ardhi za Waislamu, ubinafsishaji wa rasilimali za umma, uchumi unaotegemea Riba, na uanzishwaji wa dola za kitaifa, ambazo ni ngeni kwa fikra ya Kiislamu. Ajenda ya usasa, kwa hiyo, inahusisha kukarabati mafundisho ya Kiislamu ili kuyafanya yaonekane yanaendana na mifumo na nidhamu za Kimagharibi.

Usasa unalenga kupata nafasi ndani ya Quran Tukufu na Sunnah za Mtume kwa maadili ya mfumo wa kilimwengu wa Magharibi. Mchakato huu unajumuisha kupinda tafsiri ya nususi za Kiislamu ili kuzipa nafasi fikra kama vile ukaliaji kimabavu, unyonyaji wa kiuchumi, na kukuza uhuru wa mtu binafsi, ambayo yote yanapingana na misingi ya Kiislamu. Wafuasi wa usasa wanahoji kwamba Uislamu unapaswa kuendana na ulimwengu wa kisasa, lakini mara nyingi wanapuuza ukweli kwamba mahitaji ya kimsingi ya mwanadamu hayajabadilika. Wanadamu wangali wanahitaji kufanya biashara, kumiliki mali, kuteua watawala, na kudhibiti mahusiano ya kijamii, nk. Kilichobadilika, hata hivyo, ni mbinu na mitindo ambazo kwazo mahitaji haya yanatimizwa, kutokana na maendeleo ya kiteknolojia.

Moja ya hoja muhimu zinazotolewa na wanausasa ni madai kwamba Uislamu hautoi mwongozo wa kina kwa mifumo mbalimbali, kama vile utawala, uchumi, au mfumo wa kisheria wa jamii. Madai haya, hata hivyo, yanashindwa kutambua mapokeo tajiri ya kifikra ndani ya Uislamu, ambayo yanatoa ufafanuzi wa kina juu ya mambo haya.

Kwa mfano, wanazuoni wa Kiislamu wa zamani kama vile Al-Mawardi, Ibn Taymiyah, na Abu Yousaf waliandika kazi za kina kuhusu utawala, uchumi, na mpangilio wa kijamii. Ahkaam Sultaniya iliyoandikwa na Al-Mawardi inazungumzia undani wa utawala, ikiwa ni pamoja na sifa za watawala na hukmu za uongozi katika dola ya Kiislamu. Al-Siyasah al-Shariyah cha Ibn Taymiyah inatoa ufahamu juu ya dori ya serikali na uhusiano wake na watawaliwa. Kitab Al-Khiraj cha Abu Yousaf, mwanafunzi wa mwanachuoni mashuhuri Abu Hanifa, anatoa uchunguzi wa kina wa matendo ya kiuchumi, hasa kuhusu kodi ya ardhi na fedha za umma.

Zaidi ya hayo, fasihi ya Hadith, kumbukumbu za maneno, matendo, na ridhaa ya kipenzi chetu Mtume Muhammad (saw), zinatoa mwongozo wa kina juu ya utawala, uchumi, mahusiano ya kijamii, na hata mwenendo wa mtu binafsi. Kwa hiyo zipo Hadith zinazotoa maagizo mahususi juu ya mambo ya utawala, kama vile kuweka sifa ya kuwa mwanamume kwa watawala katika Hadith «لن يُفْلِحَ قومٌ ولَّوْا أمرَهَمُ امرأَةً» “Watu wanaomweka mwanamke kuwa mchungaji (mtawala) wa mambo yao kamwe hawatafanikiwa”, umoja wa utawala katika hadith, «إذا بُويِعَ لِخَلِيفَتَيْنِ، فاقْتُلُوا الآخِرَ منهما» “Pindi wanapopewa ahadi ya utiifu (bay’ah) Makhalifa wawili,, muuweni yule wa pili”, na kwa kukabidhi mamlaka juu ya mambo ya dola kama ilivyo katika Hadith بَعَث رسول اللہ ﷺ عمر علی الصدقۃ “Mwenyezi Mungu (saw) alimteua Umar (ra) katika Zaka”. Vile vile, tunapata maelezo kuhusu masuala ya uchumi, jinsi ardhi inavyopaswa kumilikiwa na kugawanywa, na jinsi masoko na biashara zinapaswa kudhibitiwa. Kwa mfano, Mtume Muhammad (saw) alisema,

«الناس شرکاء فی الثلاث: الماء والکلا والنار» “Watu ni washirika katika vitu vitatu: maji, malisho na moto.” Taarifa hii inabainisha fahamu ya rasilimali za umma za pamoja, kipengee muhimu cha utawala na sera ya kiuchumi katika Uislamu.

Sunnah pia inazungumzia mambo kama vile kukataza ukiritimba kama katika Hadith,

« مَنِ احْتَكَرَ فَهو خاطِئٌ » “Mwenye kufanya ukiritimba yu juu ya upotovu”, ikionyesha kwamba vitendo vya ukiritimba vimeharamishwa katika Uislamu, kuhusu suala la kupanga bei, kama ilivyo katika Hadith «بل اللہ یخفِض ویرفع», “Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kupunguza na kupandisha bei”, kuhusu suala la sarafu kama katika Hadith, «الوزنُ وزنُ أَهْلِ مَكَّةَ والمِكْيالُ مِكْيالُ أَهْلِ المدينة» “Uzito ni uzito wa watu wa Makka na kipimo ni kipimo cha watu wa Madina”, ambapo inaweka kiwango cha sarafu ya kiwango cha madini mawili ya 2.975g Dirham ya Fedha na Dinari ya Dhahabu ya 4.25g. Vile vile aliatoa maagizo kwa umma juu ya masuala kama vile umiliki wa ardhi kama katika Hadith «من أحيا أرضًا مَيتةً فهي له» “Mwenye kufufua ardhi iliyokufa ni yake”, na ushuru wa dhulma kama katika Hadith «لا یدخل الجنۃ صاحب المکس» “Anayechukua ushuru (haramu) hataingia Peponi”, ikionyesha zaidi muongozo wa kina ambao Uislamu unatoa juu ya mifumo ya kisiasa ya maisha.

Changamoto kubwa kwa tafsiri mpya ya usasa kwa Uislamu ni ushughulikiaji wake wa Hadith. Baadhi ya wanausasa wanahoji kwamba ingawa Quran inalindwa na Mwenyezi Mungu, Hadith haiwezi kuwekwa katika kundi moja, kwani ni mkusanyiko tu wa riwaya za wanadamu. Hata hivyo, mtazamo huu unapuuza dori kuu ya Hadith katika kueleza na kufafanua maandishi ya Qur'an.

Quran tukufu yenyewe inathibitisha Sunnah. Imethibitika kwa njia ya kukatikiwa kuwa Sunnah ni Wahyi, thabiti katika maandishi (thabit) na thabiti katika maana (dalaalah). Mwenyezi Mungu amesema,

 وَمَا يَنْطِقُ عَنِ الْهَوَى  “Wala hatamki kwa matamanio.” [Surah An-Najm 53:3]. Katika Tafsiri yake, Ibn Kathir alisema kuhusiana na ayah hii, ما يقول قولا عن هوى وغرض “hakuna chochote anachosema Mtume kuhusu mazungumzo ni kwa matakwa yake au matakwa yake.” Imam Qurtubi amesema katika Tafsiri yake, ما يخرج نطقه عن رأيه، إنما هو یوحي من الله عز وجل “hakuna chochote katika anachozungumza ni kwa maoni yake mwenyewe. Ni yale tu aliyoteremsha Mwenyezi Mungu Mtukufu.” Amesema Mwenyezi Mungu (swt): [إِنْ هُوَ إِلاَّ وَحْىٌ يُوحَى] “Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa.” [Surah An-Najm 53:4]. Ibn Kathir amesema, إنما يقول ما أمر به ، يبلغه إلى الناس كاملا موفرا من غير زيادة ولا نقصان “Yeye (saw) anafikisha tu kwa watu kile alichoamrishwa kufikisha, bila ya kuongeza wala kupunguza kabisa.” Bila ya Sunnah, maelezo mengi ya kivitendo ya hukmu za Kiislamu ikiwemo Ibadaat, kama vile njia ya swala, saumu, na hukmu nyenginezo, zingebakia kuwa hazieleweki.

Fauka ya hayo, kuhifadhiwa kwa Hadith kulifuata mbinu sawa na ile ya aya za Quran Tukufu. Zote mbili zilipitishwa kwa mdomo na kisha kurekodiwa. Ukusanyaji wa Hadith ulihusisha taratibu kali za uthibitishaji ili kuhakikisha uhalisi wao. Wanazuoni wa Hadith (Muhadithun), kama vile Imam Bukhari, Imam Muslim na wengineo, walitengeneza mbinu za kina za kuthibitisha kutegemewa kwa wapokezi na usahihi wa yaliyomo. Mfumo huu wa uthibitishaji ulihakikisha kwamba simulizi za kuaminika tu ndiyo zilizohifadhiwa.

Licha ya hoja ya wanausasa kwamba Hadith hazijahifadhiwa kwa uthabiti kama vile Quran Tukufu, ushahidi wa kihistoria unaonyesha kwamba ukusanyaji na uhifadhi wa Hadith ulichukuliwa kwa uangalifu wa hali ya juu. Mchakato huo haukuhusisha tu uwasilishaji wa simulizi bali pia uchunguzi wa kina wa tabia, kumbukumbu, na kutegemewa kwa wasimulizi. Kwa mfano, Hadithi kuhusu Abu Musa kuulizwa na Umar ibn al-Khattab inaonyesha uangalifu ambao Hadith zilichunguzwa, hata wakati wa Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).

Al-Jariri amesimulia kutoka kwa Abu Nadra ambaye amesimulia kutoka kwa Abu Sa'iyd kwamba Abu Musa alimsalimia Umar kwa Salamu mara tatu kutoka nyuma ya mlango lakini hakupewa ruhusa ya kuingia. Basi akarudi. Umar (ra) alimtuma mtu kwa ajili yake na akamuuliza kwa nini umerudi? Akasema: Nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema:

«إذا سلم أحدكم ثلاثاً فلم يُجب فليرجع» “Mmoja wenu akitoa salamu mara tatu na asijibiwe, basi na arudi nyuma” [Ahmad]. Umar akajibu, لتأتيني على ذلك ببينة أو لأفعلن بك “Lazima uniletee ushahidi juu ya jambo hili vyenginevyo nitakuadhibu.” Abu Musa akatujia tukiwa tumekaa huku uso wake ukitoka jasho. Tukasema: “Una shida gani?” Basi akatufahamisha na akauliza: “Je, kuna yeyote kati yenu aliyeisikia Hadith hii?” Tukajibu: “Ndio, sote tumesikia (Hadith hii).” Basi tukamtuma mtu miongoni mwetu mpaka akafika kwa Umar (ra) na kumwambia.

Vile vile Ali (r.a) amesema, كنت إذا سمعت من رسول الله حديثاً نفعني الله بما شاء منه، وإذا حدثني عنه محدث استحلفته فإن حلف لي صدقته “Ilikuwa pindi ninaposikia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw)  hadith ambayo Mwenyezi Mungu (swt) ameninufaisha nayo, na pindi mtu yeyote anaponihadithia kuihusu, humuapisha kiapo, na akiniapia basi humwamini.”

Zaidi ya hayo, juhudi za kuhifadhi Hadith zinaweza kuonekana katika matendo ya Maswahaba (ra) wa Mtume Muhammad (saw). Kwa mfano, Abu Huraira (ra), mmoja wa wapokezi mahiri wa Hadith, alisema kauli mashuhuri, ما من أحد من أصحاب النبي أكثر حديثاً منّي إلا ما كان من عبد الله بن عمر فإنه كان يكتب ولا أكتب “Hakuna yeyote katika Mswahaba wa Mtume (saw) ambaye amesimulia Hadith nyingi kuliko mimi isipokuwa Abdullah ibn Umar, kwani alikuwa akiziandika, na mimi sikuziandika.” Hili linaangazia juhudi za uangalifu wa nyaraka ambazo zilifanywa kuhifadhi mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Juhudi za wanausasa za kuhujumu mamlaka ya Hadith zinapuuza ukweli kwamba Hadith ni chimbuko la kisheria la kiasili ndani ya Uislamu, sambamba na Quran yenyewe. Aya nyingi za Quran zinasisitiza umuhimu wa kumtii Mtume Muhammad (saw) na kufuata mafundisho yake. Kwa mfano, Mwenyezi Mungu asema, [وَمَا آَتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا] “Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho.” (Al-Hashr: 7). Vile vile Mwenyezi Mungu (swt) amesema katika Aya nyingine:

[وَمَا يَنْطِقُ عَنِ الْهَوَى * إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَى] “Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa.” [Al-Najam 3-4]. Aya hizi zinathibitisha kwamba matendo na maneno ya Mtume sio mwongozo tu, bali ni Wahyi wa Mwenyezi Mungu.

Sunnah pia inazungumzia masuala muhimu ya kisheria na kijamii ambayo ni ya lazima kama maamrisho ya Qur'an. Kwa mfano, sheria zinazohusu uharamu wa mchanganyiko huru wa jinsia, udhibiti wa miamala ya kiuchumi, na uendeshaji sahihi wa mikataba ya ndoa zote zimetokana na Sunnah. Vile vile Sunnah inatoa hukmu za kina za uteuzi wa watawala, uendeshaji wa vita, na usimamizi wa mambo ya umma. Haya yote ni muhimu katika utendaji kazi wa dola ya Kiislamu yenye haki na yenye ufanisi.

Harakati za wanausasa mara nyingi hutafuta kudhoofisha mamlaka ya Hadith, kwa hoja kwamba mafundisho ya jadi ya Kiislamu yamepitwa na wakati na hayaendani na maisha ya kisasa. Hoja hii inadhihirishwa na ripoti ya Uislamu wa Kidemokrasia ya Kiraia iliyochapishwa na Shirika la RAND mwaka 2004, ambayo inasema kwa uwazi katika kiambatanisho-A chenye kichwa “Vita vya Hadith”, kwamba kikundi cha “hadith za kupinga” kinapaswa kuundwa ili kuunga mkono uliberali zaidi, usawa, na tafsiri za kidemokrasia za Uislamu. Juhudi hizi zinaonyesha hamu ya Magharibi ya kuunda Uislamu kwa njia ambayo inalingana na maadili na mifumo yake, haswa kujitolea kwake kwa demokrasia ya kiliberali na usekula.

Hata hivyo, juhudi kama hizo zinashindwa kutambua kwamba Uislamu ni mfumo kamili wa muongozo, wenye uwezo wa kushughulikia mahitaji ya mwanadamu, katika zama zilizopita na za sasa. Mahitaji ya kimsingi ya wanadamu—kama vile hitaji la uadilifu, uthabiti wa kiuchumi, utawala, afya, usalama, elimu na mshikamano wa kijamii—hayabadiliki. Kipengele pekee ambacho kimebadilika ni njia na mitindo ambayo mahitaji haya yanashughulikiwa. Iwe kupitia mifumo ya kisasa ya benki, teknolojia ya hali ya juu ya mawasiliano, au vita vya kisasa, Uislamu unabaki kuwa na uwezo wa kutabanni mbinu na zana mpya za zama hizi. Mfumo wa kijadi wa Kiislamu, unaoegemea juu ya Quran na Hadith, unaendelea kutoa masuluhisho yanayofaa na ya kina kwa jamii ya kisasa.

Jaribio la “Usasa wa Kiislamu” la kutafsiri upya Uislamu kwa kuzingatia uliberali wa Magharibi linaleta changamoto ya moja kwa moja kwa usahihi na mamlaka ya Hadith. Kwa kuhujumu umuhimu wa Sunnah, wanausasa wanatafuta kuuondolea Uislamu mwongozo wake wa kina katika nyanja zote za maisha. Hata hivyo, mfumo wa kimapokeo wa Kiislamu, uliokita mizizi katika Qur'an Tukufu na Sunnah za Mtume, unasalia kuwa mfumo kamili na unaofaa wa kushughulikia mahitaji ya binadamu. Kutafsiri upya Uislamu ili kuendana na maadili ya kisasa ya Magharibi sio tu kwamba ni potofu bali pia kunashindwa kutambua umuhimu usiofungika na zama wa mafundisho ya Kiislamu. Kupitia mchakato mkali wa uhifadhi na uthibitisho, Hadith inabaki kuwa halali, muhimu na yenye mamlaka leo kama ilivyokuwa wakati wa Mtume Muhammad (saw), ikitoa ufumbuzi usiofungika na zama kwa changamoto za ulimwengu wa kisasa.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Idrees Pasha – Wilayah Pakistan

Yaliyomo ndani ya kifungu hichi: « Uhadaifu wa Utaifa

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu