Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Enyi Waislamu Mlioko India! Acheni “Hisia za Uchache” Mlizopachikwa

Jivunieni kuwa Waislamu!

India hivi karibuni imepitisha sheria inayoitwa Sheria ya Mabadiliko ya Uraia mnamo Disemba 2019, itakayowapa uraia watu wa dini zilizo na watu wachache isipokuwa Waislamu kutoka nchi jirani. Sheria hii mpya ni marekebisho ya sheria ya 1955 na inayowapa uraia wa India kwa walio wachache “wanaoteswa” - Wahindu, Mabaniani, Mabudha, Jains, Parsis na Wakristo – kutoka Bangladesh, Afghanistan na Pakistan, lakini haiwatambui Waislamu. Sheria imesukumwa kupitia Bunge la India na chama cha kitaifa cha Kihindu Bharatiya Janata Party (BJP) na kuidhinishwa na Rais Ram Nath Kovind Disemba 12. Sheria hii, inayounganishwa na Usajili wa Kitaifa wa Raia (NRC), itatoa uraia kwa wasiokuwa Waislamu na kuwafanya Waislamu kuwa wasio na taifa. Vyama vya upinzani vinasema kuwa sheria hii ni ya kibaguzi kwani inawatengua rasmi Waislamu wachache katika taifa ambalo ni rasmi la kisekula lenye watu bilioni 1.3. Waislamu wanajumuisha takribani asilimia 15 ya watu wote wa India. Wakosoaji wanadokeza kuwa hatua hii ni sehemu ya ajenda ya Wahindu ya kuwa juu kuwafanya Waislamu ndio kiegemeo cha kuwachochea wasiokuwa Waislamu kwa ajili ya hifadhi ya kura zao, ambayo serikali hii ya Waziri Mkuu Narendra Modi inaisukuma tokea iingie madarakani miaka sita iliyopita. Upingaji umefanyika mara nyingi dhidi ya sheria hii ikiwemo ile ya chama cha wanafunzi kuchukua hatua na zaidi katika Chuo Kikuu cha Jamia Millia Islamia (JMI). Mitandao ya kijamii imesheheni video za virungu walivyoshika maofisa wa polisi pamoja na watu wao wa karibu wakiwapiga kwa nguvu wanaume, wanawake na watoto. Kwa kutumia fursa ya hali hii na hofu iliyozuka miongoni mwa Waislamu katika aina hizi za sheria za kuwafanya kutokuwa na nchi, vyama vya mrengo wa kushoto na vya kati (UPA) vimejionyesha kuwa ndio walinzi wa haki za Waislamu kama ni njia ya kupata uungwaji mkono wa jamii ya Waislamu kushinda uchaguzi ujao. Kutokana na muono wa Waislamu, utaratibu huu umekuwa ni ule ule tokea India ipate uhuru 1947. Kila wakati, Waislamu huonekana ni kama akiba tu ya kura. Siasa za akiba ya kura ni utaratibu wa kawaida wa Demokrasia ya India kama ilivyo kwa Demokrasia zote Ulimwenguni.

Katikati ya mchezo na matatizo yanayoonekana kutokwisha, ni muhimu sana kwa Waislamu kuwa imara kufanya jitihada katika kubainisha njia sahihi ya kusonga mbele kama suluhisho kamili. Katika kubainisha njia, Waislamu wanahitaji kutafuta majibu kwa masuali kama: Je Waislamu wajiweke mbali na malalamiko yanayotokea chini ya bendera ya utaifa, usekula na katika kuhifadhi katiba ya kidemokrasia na kujiweka kando na siasa na kujitenga? Au waonyeshe ushiriki zaidi na kujiingiza ndani ya nidhamu ya kidemokrasia kwa kutafuta njia ya kutokea? Au kutafuta mbadala kutatua tatizo liliopo?

Uhalisia wa Demokrasia:

Nidhamu ya Demokrasia, ambayo inatafsiriwa kuwa ni “Utawala wa Watu”, ni nadharia ya miaka 2500 nyuma iliyoanzia Ugiriki katika karne ya 6 B.C. Ni nidhamu ya kisiasa inayotokana na akili ya mwanaadamu, na pia inategemea akili ya mwanadamu katika sheria zake. Lakini, uhakika wa akili ya mwanadamu ni kuwa yenye kikomo; haiwezi kutambua lengo la uwepo wa maisha, nini kilicho nyuma ya maisha haya, nini kitafuata baada ya maisha haya, na nini uzuri halisi na nini ubaya halisi. Kwa hivyo, kwa Waislamu, Ummah bora ulioletwa kwa watu kuwa ni mashahidi juu ya mambo ya Waislamu, ni muhimu kuelewa ima wanahitaji kujiunga au kuepukana na uongo wa nidhamu iliyoundwa na binadamu au kutafuta mbadala huku wakibainisha njia ya kusonga mbele, muongozo, mpango makini au mchoro wa vitendo kusuluhisha matatizo yaliyopo.

Mtazamo wa Kiislamu:

Demokrasia ni nidhamu ya utawala inayotokana na Aqeedah ya kikafiri inayoitwa Usekula. Usekula unahimiza kuwa dini na Mwenyezi Mungu hazina dori yoyote katika masuala ya kisiasa ya mujtama na kuwawezesha watu katika mujtama kutunga sheria zinazoendana na akili zao. Hivyo, watu huchagua wawakilishi wao kuunda serikali ili kutekeleza sheria kwa jamii kwa ajili yao. Kwa hivyo, ubwana na mamlaka wamepatiwa wanadamu na sio Mwenyezi Mungu. Wakati Mwenyezi Mungu (swt) ametaja wazi katika Qur’an [ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّه ]   “Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu” [Al-An’am 6:57]

Katika Demokrasia, mwanadamu hutunga sheria na, kwa hiyo, hubeba jukumu ambalo hakuna awezaye kulibeba isipokuwa Mwenyezi Mungu (swt). Kwa mtazamo huu juu ya maisha na itikadi (Aqeedah) ya kisekula, Ruboobiyyah (Ubwana) wa Mwenyezi Mungu umefungika tu kwa masuala ya kibinafsi na kuyatenga yale ya kijamii kwa kuwa wanadamu na akili zao zenye mipaka zimefanywa zenye kuweka sheria na kuamua juu ya Halali na Haramu kwa ajili ya mujtama. Katika tendo hili hasa, ambalo Mtume (saw) amelikataza kama ilivyopokewa katika hadith ya Adi bin Hatim.

Adi bin Hatim (ra) amesema: “Nimemsikia (saw) akisoma aya katika Sura at-Taubah,

[اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِنْ دُونِ اللَّهِ]

 “Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi badala ya Mwenyezi Mungu.” [9:31]

Mtume (saw) amesema, «بَلَى إِنَّهُمْ حَرَّمُوا عَلَيْهِمُ الْحَلَالَ وَأَحَلُّوا لَهُمُ الْحَرَامَ فَاتَّبَعُوهُمْ فَذَلِكَ عِبَادَتُهُمْ إِيَّاهُم» “Ama wao, hawawaabudu, bali wanapofanya jambo kuwa halali kwao, hulihalalisha, na wanapo lifanya haramu kwao, huliharamisha.” (Sunan at-Tirmidhi)

Kutokana na hili, inafahamika kuwa kutoa mamlaka ya kutunga sheria kwa mikono ya wengine isiyokuwa Shari’ah ya Mwenyezi Mungu (swt) ni sawa na kuwafanya wengine mabwana kando na Mwenyezi Mungu (swt). Hii ni hukmu ya Mtungaji Shari’ah juu ya Demokrasia. Aqeedah ya Kiislamu, kwa upande mwingine, inaagiza kuwa Mwenyezi Mungu (swt) afanywe Yeye pekee kuwa ni Mtungaji Shari’ah katika mambo yote ya maisha kuanzia ya kijamii hadi ya kibinafsi. Katika Uislamu, Ubwana na haki ya kutunga sheria iko kwa Mwenyezi Mungu (swt) peke yake, na mamlaka ya kuchagua mtawala (yaani Khalifah) yako kwa watu. Hii ni tofauti ya msingi baina ya Demokrasia ambayo imejengwa juu ya Aqeedah ya Usekula na Khilafah ambayo imejengwa juu ya Aqeedah ya Uislamu.

Waislamu waonyeshe hisia za namna gani?

La muhimu zaidi, Waislamu India lazima waachane na hisia za udhalili zitokanazo na “hisia ya uchache” iliyopachikwa kwao baada ya kile kinachoitwa Uhuru wa India wa 1947. Chini ya nembo hii, Waislamu wamekuwa wakiishi katika hali ya udhalili na kutojiamini na hofu ya kinafsi isio ya lazima. Lazima waachane na hisia hizi za udhalili za kubandikiziwa kuwa ni wachache na wajivunie kuonyesha utambulisho wao kuwa ni Waislamu pekee na watambue nafasi yao ya kuwa ni viongozi wa wanadamu – viongozi wanaoongoza katika njia inayomulikwa kwa muangaza kutoka kwa Muumba wa walimwengu na vyote vilivyomo. Hawapaswi kusahau kuwa kusimama kwa India hii ya leo kumetokana na mchango mkubwa wa Waislamu waliotawala ardhi hii kwa Uislamu kwa zaidi ya karne 10 na kutekeleza mfumo adilifu wa Uislamu juu ya watu wake.

Waislamu wakati wote wachukue uoni kwa Rabii’ ibn Amir (ra) aliyekuja kwa Rustum, kamanda wa jeshi la Waajemi, alipomuuliza Rabii’ ni nini lengo lao na kwa nini wamekuja Uajemi? Rabii’ alisema, “Mwenyezi Mungu Azzawajal ametuleta kukutoeni kutoka kuwaabudu viumbe na kukupelekeni kumuabudu Muumba wa viumbe na kukutoeni kutoka kwenye ufinyu wa dunia hii kuelekea kwenye ukubwa wa dunia hii na maisha baada ya kufa, na kutoka kwenye ukandamizaji wa dini kwenda kwenye uadilifu wa Uislamu. Mwenyezi Mungu Azzawajal ametuleta kukuokoeni kutokana na kuabudiana nyinyi kwa nyinyi.”

Ni jukumu la Waislamu kuwaita na kuwalingania watu kwenye Aqeedah ya Kiislamu na njia ya maisha ya Kiislamu. Waweke wazi uongo na udhaifu wa nidhamu mbovu iliyoundwa na mwanadamu inayoitwa Demokrasia na kuweka njia ya maisha kuwa ni chaguo pekee la maisha haya na yanayokuja. Waziweke nafsi zao katika udhibiti na kutawala matamanio yao kukubali ukweli huu mgumu kuwa Demokrasia ni nidhamu ya Kikafiri na suluhisho pekee kwa walimwengu ni Uislamu. Bila shaka, Uislamu, pamoja na Aqeedah yake na njia yake ya maisha, ni suluhisho pekee kwa matatizo yote ambayo wanadamu wanakabiliana nayo hivi leo. Uislamu ni nidhamu ya Wahyi iliyofunuliwa na Bwana wa Walimwengu, Mwenyezi Mungu (swt). Hivyo, badala ya kutafuta suluhisho kutoka kwenye nidhamu dhaifu, iliyo na upungufu, iliyoundwa na mwanadamu ya Demokrasia, Waislamu ambao ni Ummah bora ulioletwa kwa watu wachukue nafasi ya uongozi kuanzisha hatua za kumkomboa mwanadamu kutoka katika giza la nidhamu ya mwanadamu kama Demokrasia na Urasilimali kwenda kwenye nuru ya nidhamu ya Kiislamu ambayo itasimamisha uadilifu kwa wote bila kubagua jamii, dini, cheo, utaifa au ukabila. Wafanye hivi kwa kufuata njia ya Mtume Muhammad (saw). Ni lazima waachane na Demokrasia na kujishughulisha na kusimamisha nidhamu ya kisiasa ya Kiislamu, Khilafah, kuendeleza njia ya maisha ya Kiislamu kuwa ni suala la kufa na kupona na kuunganisha juhudi zao katika upande huu kwa msukumo kamili.

[وَمَنْ يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَنْ يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِين]

“Na anaye tafuta dini isiyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri.” [Al-Imran 3:85]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Hizb ut Tahrir na

Hameed Bin Ahmad

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 06:43

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu