Jumanne, 03 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/05
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Hata Watoto Wetu Wadogo Hawapo Salama Chini ya Ubepari

(Imetafsiriwa)

Habari:

Wizara ya Mambo ya Ndani Tanzania imetoa takwimu mpya kuhusu ukatili kwa watoto nchini kuanzia Januari mpaka Septemba 2021. Kwa mujibu wa wizara, jumla ya watoto 6,168 walifanyiwa ukatili na miongoni mwao 3,524 walibakwa.

Maoni:

Takwimu hizo juu ni zile rasmi pekee, kuna uwezekano mkubwa kuwa uhalisia ukawa mbaya zaidi. Kwa mujibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mwaka 2017 watoto 12 walibakwa katika mwaka huo. Hali iliongezeka kwa kasi ambapo mwaka 2018 watoto 533 waliripotiwa kubakwa, kisha miaka mitatu tu baadaye yaani 2021 jumla ya watoto 3,523 wamebakwa kwa mujibu wa takwimu za sasa za Wizara ya Mambo ya Ndani.

Takwimu hizi zinazotoa ishara mbaya na zinazoumiza nyoyo na pia zinaonesha kushindwa kwa mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia katika kutoa masuluhisho thabiti kuhusu matatizo ya kijamii ikiwemo ubakaji. Hii inatokea kutokana na ukweli mchungu wa fikra ya kibepari ya “uhuru binafsi” ambao huhamasisha ushibishwaji wa kimapenzi kwa njia yoyote bila ya kujali madhara kwa wengine.

Nidhamu ya kijamii ya kibepari (capitalist social system) imeubwaga chini ubinadamu kwa kushindwa kutoa suluhisho madhubuti kuhusu jinsi ya kushibisha mahitaji ya kimwili (organic needs) na mahitaji ya ghariza za kimaumbile (instinctual needs) ambavyo vitu viwili hivi ni muhimu katika maisha.

Mahitajio ya kimwili ni kama chakula, maji na mengine ambayo ni muhimu katika kuwezesha binadamu kuishi, yanahitaji mfumo sahihi wa kiuchumi na sera bora ili kudhamini usambazaji wake kwa uadilifu ili kuepusha mashaka kwa binadamu.

Mahitaji ya kighariza za kimaumbile ambayo yanajumuisha  ghariza ya kuendeleza kizazi inayosukuma uhitaji wa kufanya mapenzi, pia inahitaji kushibishwa vyema ili kuepusha kutokuridhika na wasiwasi, lakini iwe chini ya nidhamu ya kijamii iliyo bora ambapo haitasababisha madhara kwa wengine ikiwa na kinga madhubuti ya kijamii hususan kwa  makundi dhaifu kama watoto wadogo.

Asili ya ghariza ya kuendeleza kizazi huibuka pale tu mtu anapokabiliwa na vichochezi vya ngono hata kama itakuwa ni kupitia kujenga fikra akilini. Kwa hiyo, kushindwa kwa  mfumo wa ubepari kuzuia kuenea kwa vitu vinavyochochea hisia za kimapenzi katika jamii kama vile picha utupu (pornographic materials), muziki, na filamu zenye vivutio vya mapenzi, nk na kisha kutambua uchafu huo kuwa ni uhuru binafsi wa haki za binadamu, daima itapelekea kuibuka matamanio ya kimapenzi yasiodhibitika ambayo huathiri vibaya jamii na kupelekea kuongezeka kwa matukio ya unyanyasaji wa mtoto.

Kwa maneno mengine, haiwezekani kuepuka ubakaji na udhalilishaji wa kimapenzi katika jamii ambayo wanawake wanatembea uchi au nusu uchi kwa uhuru, umalaya na kujiuza unaruhusiwa na kuenea kupita mipaka kwa matangazo ya bidhaa yenye mvuto wa kimapenzi.

Zaidi, mfumo fisidifu wa kibepari hautafanikiwa kamwe kuwashibisha watu na mahitajio hayo tuliyoyaeleza hapo awali bila kusababisha madhara kwa wengine ndiyo maana takwimu za ukatili kwa watoto na udhalilishaji wa kimapenzi unazidi kukua kwa kasi siku hadi siku kwa vile mfumo huu umejengwa juu ya msingi wa maslahi na faida bila kujali madhara kwa jamii na kubwa zaidi hauna thamani ya kiroho.

Kwa upande mwingine, mfumo wa kisheria wa kibepari na usimamizi wake wa haki una mapungufu mengi hususan uwepo wa mianya ya kisheria na kuota mizizi utamaduni wa rushwa, hali inayopelekea wabakaji, watendaji wa udhalilishaji wa kimapenzi  na wahalifu wengine kupenya kiurahisi katika mkono wa sheria bila ya kuadhibiwa, baadhi wakishikiliwa kwa muda mfupi kisha kuachiwa. Udhaifu huu imewakatisha tamaa baadhi ya wahanga kuacha kutoa taarifa.

Nidhamu ya kijamii ya Kiislamu (Islamic social system) chini ya serikali yake ya kilimwengu ya Khilafah ina uwezo wa kutatua aina zote za unyanyasaji wa mtoto sawa sawa kama itakuwa ni ubakaji au unyanyasaji mwingine. Uislamu umejikita katika kujenga mapenzi na adabu kati ya watoto, wazazi na jamii kupitia mafundisho yake ambayo daima yanaunganisha matendo ya mtu na maisha ya akhera. Hali hii daima imepelekea uchaMungu miongoni mwa Waislamu na kufanya matendo ya unyanyasaji wa mtoto kutoweka katika jamii ya Kiislamu au kutokea kwa kiwango kidogo sana sana, ambapo hata hivyo muhalifu huadhibiwa vikali adhabu stahiki inayotokana na Wahyi chini ya mfumo wa kimahakama wa Kiislamu

Pia Uislamu umejikita katika kuzuia vishawishi vya wazi vinavyoibua hisia za kimapenzi. Uislamu katu hauruhusu picha za utupu, mabango ya utupu, kuwaweka watoto wakiwa nusu utupu katika matukio, majukwaa au hafla mbalimbali.

Mfumo wa kielimu na vyombo vya habari katika jamii ya Kiislamu hutumika kupandikiza ufahamu sahihi kuhusiana na mahitajio ya kighariza na kimwili. Kwa hiyo katika jamii ya Kiislamu mtoto hutizamwa kama mtu wa kuheshimiwa na kulindwa, na jambo hili huwa ni jambo la kufa na kupona.  Pia Uislamu unapunguza fursa na uwezekano wa mtu muovu kumghilibu mtoto, ukasisitiza kutenganisha vitanda na vyumba vya kulala baina ya watu wazima na hata baina ya watoto kwa watoto wengine.

Kwa kukhitimisha, licha ya kuwa ni jukumu letu kuwalinda watoto na kila aina ya unyanyasaji na udhalilishaji, kuwafundisha jinsi ya kujilinda na kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa au kujaribu kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji, ni muda muwafaka sasa kufanya kazi kwa bidii kutafuta suluhisho la kudumu na madhubuti kwa kuung’oa mfumo wa kishetani, muovu na ulioshindwa wa kibepari na badala yake kurejesha utawala wa Kiislamu wa Khilafah Rashidah ukianzia katika mataifa makubwa ya Waislamu na kisha kuenea mashariki na magharibi kuuokoa ulimwengu kutokana na majanga na mabalaa yote ukiwemo udhalilishaji wa mtoto.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu