Alhamisi, 09 Rajab 1446 | 2025/01/09
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Mgogoro wa Dolari ya Kimarekani Tanzania na Pengine ni Kielelezo cha Ubwana wa Mabavu ya Marekani Kiuchumi

(Imetafsiriwa)

Habari:

Tanzania kama nchi nyingine nyingi inakabiliwa na mgogoro wa uhaba wa fedha ya dolari ya kimarekani. Ripoti zinasema akiba ya fedha za kigeni mwishoni mwa mwezi wa Aprili 2023 ni dolari bilioni 4.9, na ndani ya mwezi wa Julai 2023 ni bilioni 5.55. Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hifadhi hiyo inaweza kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa kwa takriban miezi mitano.

Maoni:

Uhaba wa dolari ni ile hali inayojitokeza wakati nchi inapokuwa ina usambazaji na mzunguko mdogo sana wa dolari za Kimarekani katika akiba yake inayohitajika kufanya biashara ya kimataifa kwa ufanisi.

Hali ya sasa ya uhaba wa dolari ya Marekani imekuwa ikishuhudiwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu katika baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo Kenya, Misri, Zimbabwe, Nigeria, Ghana, Zambia nk, kiasi kwamba ndani ya mwezi Machi 2023 Rais wa Kenya William Ruto alitoa agizo la kufufua masoko ya fedha za kigeni miongoni mwa mabenki.

Kwa muktadha wa Tanzania, pamoja na ukweli kwamba Benki Kuu ya Tanzania iliwahakikishia raia kuwa hifadhi iliyopo sasa inaweza kutumika hadi miezi mitano, hali inaonekana kuwa kinyume, homa ya uhaba wa fedha hiyo iko juu zaidi sokoni.

Kunapokuwa na uhaba wa dolari za Marekani, hupelekea fedha ya ndani kudhoofika dhidi ya dolari ya Marekani. Hivyo, bei za ndani hupanda, kiasi ambacho watu wananunua bidhaa, ikiwa ni pamoja na bidhaa muhimu kama nishati na bidhaa za viwandani kwa sababu zinaagizwa kutoka nje.

Hali hiyo imeonekana wazi katika kikao cha hivi karibuni baina ya Waziri wa Nishati, January Makamba na viongozi wa Chama cha Makampuni ya Uagizaji wa Mafuta Tanzania (Taomac) kilichofanyika tarehe 04/08/2023 wakijadili mgogoro wa nishati ya mafuta, na kuthibitishwa kuwa uhaba wa dolari ya Marekani nchini kuwa ndiyo kikwazo katika uagizaji wa mafuta kutoka nje.

Uhaba wa dolari ya Marekani katika nchi husika huibuka kutokana na kuzorota kwa uwiano wa malipo, ikimaanisha miamala ya kifedha ya nchi na mataifa mengine duniani. Katika upeo mpana, mgogoro wa uhaba wa dolari katika nchi za ulimwengu wa tatu ni zao la ajenda ya unyonyaji na ukoloni wa Marekani tangu mwaka 1944 kupitia Makubaliano ya Bretton Woods. Makubaliano haya yalileta athari kuu mbaya mbili: Kwanza, ni kukomeshwa matumizi ya sarafu kwa kufungamanishwa na dhahabu kwa mbadala wa sarafu za karatasi ambazo hubadilikabadilika na kukosa uimara katika thamani yake kama katika hali ilivyo sasa. Pili, makubaliano hayo yaliimarisha nafasi ya Marekani kwa kupewa mamlaka ya kushikilia na kudhibiti uchumi wa kiulimwengu kupitia sarafu yake (ya dolari) ikiwa ndio sarafu ya juu na kuu katika uwanja wa kimataifa.

Kwa kuwa Marekani kwa sasa ndiyo taifa kinara la ubepari ulimwenguni, linafanya bidii kwa nguvu zote kuendelea kushikilia maslahi haya ya kiuchumi kama msingi wa itikadi yake, kwa kuwanyonya wengine kupitia mabavu ya sarafu yake kwa ukoloni na kuharibu uchumi wa dunia kwa maslahi yake binafsi.

Tanzania, kama nchi nyingine zinazoendelea, haina namna ila kujisalimisha katika minyororo ya Marekani na ubwana wake ikifungamanisha uchumi wake na dolari ya Marekani. Chini ya uchumi huu wa fedha za karatasi za dolari ya Marekani nchi zinalazimishwa kukusanya dolari kutokana na mauzo ya nje na fedha zinazotumwa kutoka nje ya nchi ili kulipia uagizaji wa bidhaa na ulipaji wa madeni.

Hatua na maagizo yote yanayolenga kudhibiti hifadhi ya kigeni kama vile udhibiti wa soko la ubadilishanaji fedha za kigeni, kuboresha mauzo ya bidhaa nje na kuhimiza uwekezaji wa kigeni, yote hulenga katika jambo moja tu, nalo ni kukusanya zaidi dolari ya Marekani kutoka Marekani ambapo kufanya hivyo ni kuipa Marekani ubwana ziada juu ya uchumi wa ulimwengu wa tatu.

Chini ya mfumo wa uchumi wa kibepari, ambao Marekani ndio yenye ubwana, kamwe hakutakuwa na suluhisho la maana lenye matokeo chanya kwa mataifa yanayoendelea isipokuwa unyonyaji zaidi.

Suluhisho la jambo hili lipo ndani ya mfumo wa Uislamu katika nidhamu yake ya kiuchumi. Mfumo ambao haupo kuutumikia ubwana wa kibepari wa Kimagharibi, au kuzinyonya nchi maskini kwa kuzifanya wasambazaji bidhaa kwa bei ya kutupa.

Chini ya dola yake ya Khilafah, viwango vya dhahabu na fedha vitarejeshwa tena katika sarafu na kuurudisha uchumi wa dunia kwenye utulivu na uimara na kuondoa kabisa mabavu ya sarafu ya dolari ya Kimarekani.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mjumbe wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu