Ijumaa, 10 Rajab 1446 | 2025/01/10
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Mgogoro wa Umeme Tanzania

(Imetafsiriwa)

Habari:

Tanzania kwa sasa inakabiliwa na tatizo kubwa la umeme ambalo lilisababisha mgao wa umeme. Kwa mujibu wa serikali, sababu kubwa inayopelekea matatizo ya umeme ni kupungua kwa kina cha maji katika mabwawa ya kufulia umeme pamoja na ukarabati wa miundombinu ya umeme.

Maoni:

Kufuatia tatizo hili la umeme, Rais Samia Suluhu Hassan Jumamosi, tarehe 23/09/2023, alimteua Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuchukua nafasi ya Maharage Chande aliyetumikia wadhifa huo kwa muda wa miaka miwili. Rais Samia amempa kazi Mkurugenzi huyo mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bwana Gissima Nyamo-Hanga kumaliza mgogoro huo ndani ya miezi sita.

Kwa mujibu wa Mkakati wa Maboresho ya Sekta ya Ugavi wa Umeme 2014 – 2025, ikiwa Tanzania inalenga kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, kama ilivyo katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025, itahitaji kuzalisha MW10,000 mpaka kufikia mwaka 2025, kutoka uzalishaji wa sasa wa MW1,872.04 ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.5 kutoka MW1,694.55 mwaka 2022. Mgogoro wa sasa wa umeme unathibitisha kwa uwazi kwamba mipango ya serikali si ya uhalisia na isiyo na matumaini.

Ni aibu kuwa kila mradi mpya wa umeme unapoibuka, wanasiasa huhadaa Umma kwamba mradi huo utaondoa tatizo la umeme na kuuza ziada nje ya nchi. Kwa mfano, wakati wa kuendeleza mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi mwaka 2013, aliyekuwa Waziri wa Nishati wa wakati huo, Sospeter Muhongo alisema: “Mipango yetu ni kwamba ifikapo mwaka 2014 tayari tutakuwa na umeme wa ziada kiasi cha megawati 500 ambao tutauuza nje ya nchi” (Mwananchi, Julai 17, 2013).

Ahadi kama hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipofungua rasmi Kongamano la Tano la Nishati na Maonesho kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Dar es Salaam Jumatano, Septemba 20, 2023.

Tangu miaka ya 1990 wakati Tanzania iliporuhusu uwekezaji binafsi katika sekta ya uzalishaji wa umeme, kumekuwa na matatizo ya umeme kwa miaka mingi yanayoathiri mfumo wa umeme. Kwa mfano, mikataba ya baadhi ya wawekezaji binafsi kama vile IPTL, Richmond na Dowans iligubikwa na tuhuma za ufisadi zilizosababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa mwanzoni mwa mwaka 2008, na kupelekea serikali kupata deni la Tsh bilioni 426 na kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 18, ambapo wananchi maskini ndio wanapaswa kulipa. Baadaye ikaja kujulikana kuwa wawekezaji hao wa kibinafsi katika uzalishaji wa umeme hawakuwahi hata kuwepo, yaani walikuwa wawekezaji “hewa”.

Huu ndio uhalisia wa mfumo wa kibepari unavyofanya kazi ukilenga manufaa ya kibinafsi pekee ukiwa na mipango isiyo ya uhalisia kwa watu na kuwapa watu hao matumaini hewa.

Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya nishati vikiwemo umeme wa maji, jotoardhi na hata upepo. Mikoa mingi kama mkoa wa Singida (katikati mwa Tanzania) inafaa kwa nishati ya upepo, nchi nzima inafaa kwa uzalishaji wa nishati ya jua. Pia Tanzania ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa gesi, kwa kuwa ina hifadhi ya gesi zaidi ya futi za ujazo trilioni 60. Uwepo wa madini ya urani katika mikoa ya Ruvuma, Dodoma, Singida, Manyara na Arusha kunatoa fursa ya kuzalisha umeme wa nyuklia.

Kwa ufupi, Tanzania haingepaswa kuwa na matatizo ya umeme, lakini rasilimali zote hizi zinazoweza kutumika kuzalisha umeme hazinufaishi Umma au kutumika ipasavyo katika uzalishaji wa umeme kutokana na mfumo wa kibepari wa kinyonyaji ambapo rasilimali huwanufaisha wachache hususan makampuni ya kikoloni ya kigeni.

Katika Uislamu, tofauti na ubepari, umeme na mitambo ya kuzalisha umeme, migodi ya madini na mali nyingine zinazofanana nazo haziruhusiwi kubinafsishwa (umiliki binafsi), kutaifishwa (kufanywa mali ya serikali) bali ni mali ya Umma, na ziko chini ya umiliki wa Umma.

Huu ndio mtazamo wa Kiislamu chini ya dola yake (Khilafah) utasimamia na kuzuia wachache kumiliki suala zima la uzalishaji wa umeme kama biashara ya kutengeneza pesa, ili kuifanya huduma hii muhimu ipatikane bure au kwa bei nafuu kwa wote.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mjumbe wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu