Jumanne, 08 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/10
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Hata Madrasa zetu Haziko Salama Chini ya Ubepari

(Imetafsiriwa)

Habari:

Mnamo tarehe 02/02/2024 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kuifunga Madrasa ya Al Habash iliyokuwa maeneo ya Sogea Mbele na Nkuhungu, Dodoma katikati mwa Tanzania kwa tuhuma za kutoa huduma ya elimu katika mazingira hatarishi. Madrasa hiyo ilikuwa na jumla ya wanafunzi wa kike takriban 132 wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 20 katika maeneo yote mawili, wanafunzi hao walikuwa wanatoka maeneo tofauti hususan ndani ya mkoa wa Dodoma.

Maoni:

Tunalaani vikali uamuzi huu usiokubalika wa serikali wa kuifunga madrasa ya Al-Habash bila sababu za msingi. Inaonekana kuwa serikali ilichukua hatua kama sehemu ya muendelezo wa kampeni ya kimataifa dhidi ya Uislamu. Sababu zilizotajwa hazina mashiko kwa serikali kufikia uamuzi huo. Wakati hayo yakijiri, siku chache baadaye, tarehe 06/02/2024 serikali iliuvunja msikiti wa wanafunzi katika shule ya sekondari ya Tawalanda iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani.

Kampeni ya Kibepari kimataifa ya chuki dhidi ya Uislamu ambayo inasukumwa hasa na Marekani inatumia visingizio mbalimbali kudhibiti, kuingilia kati na kufunga vyanzo vya elimu ya Kiislamu. Hili linafanyika katika ulimwengu wote wa Kiislamu zikilengwa Madrasa zenye mfumo wa kiasilia, vyuo vya kati au vyuo vikuu vya Kiislamu.

Ndani ya mwaka 2015 takriban wanafunzi 147 katika Wilaya ya Hai, Kaskazini mwa Tanzania waliokuwa wakisoma katika Madrasa ya misikiti mitatu: Masjid Bilal (Kibaoni), Masjid Othman (Uzunguni) na Masjid kwa Kiriwe waliwekwa kizuizini na vyombo vya dola. (Chanzo: Mtanzania 2 Aprili 2015). Pia katika mwaka huo huo mwalimu wa madrasa, Al-Haji Maulana Shiraz (71) wa jumuiya ya Zawiyatul-Qaadiriya katika Wilaya ya Masasi Kusini mwa Tanzania alikamatwa akiwa na wanafunzi 11 tu kwa kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi. (Chanzo: Habari Leo, 3 Aprili 2015).

Mabepari wakoloni wa Kimagharibi walitengeneza propaganda (ya vita dhidi ya ugaidi) zinazosababisha mgawanyiko, kuyumbishwa kwa watu kijamii na kiuchumi, kueneza chuki, na mara nyingi waendesha mashtaka hushindwa kuleta ushahidi mbele ya mahakama dhidi ya madai ya ugaidi, hata baada ya miaka mingi ya kile kinachoitwa "upelelezi".

Kuhusu suala haswa la kufungwa kwa Madrasa ya Al-Habash, serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule mnamo tarehe 05/02/2024 ilitoa sababu kwa madai kuwa eti Madrasa hiyo ina msongamano mkubwa wa wanafunzi, wa takriban wanafunzi 30 au 65 kutumia chumba kimoja kama darasa au bweni.

Hili ni jambo la aibu na kichekesho cha wazi kwani shule za serikali ni duni na zenye msongamano mkubwa zaidi. Kwa mfano, katika Shule ya Msingi ya Tambukareli iliyopo Nyamagana mkoani Mwanza, wanafunzi 300 wanatumia chumba kimoja kama darasa (Chanzo: Jambo FM. 27 Oktoba 2023), katika Shule ya Msingi ya Njiwa iliyopo Malinyi mkoani Morogoro, wanafunzi 172 wanatumia chumba kimoja kama darasa (Chanzo: Jembe FM. 9 Mei 2023), katika Shule ya Sekondari Mlonwena iliyopo Lushoto mkoani Tanga, kulikuwa na upungufu wa mabweni kiasi cha wanafunzi watatu kutumia kitanda kimoja (Chanzo: ITV, 22/04/2019).

Uwiano wa sasa wa wanafunzi kwa walimu ni hadi wanafunzi 100 kwa mwalimu 1 katika shule za serikali, uwiano wa wanafunzi kwa darasa ni hadi wanafunzi 81 kwa darasa 1 (Chanzo: Mwananchi 11, 2023).

Huu ndio uhalisia wa shule za serikali, pamoja na msongamano huo katika shule za serikali, kwa nini serikali haikufunga shule zote hizi kama ilivyofanya kwenye Madrasa yetu? serikali ilipata wapi haki ya kimaadili ya kuzungumzia msongamano katika Madrasa za Waislamu? Ikiwa sio chuki kwa Uislamu, ni kitu gani kingine?

Kuhusiana na kile kinachoitwa hali duni ya usafi kama vile upatikanaji wa maji safi na vyoo. Madrasa ya Al-Habash ilikuwa na vyoo na upatikanaji wa maji, ingawa katika chuo cha Sogeambele wanafunzi walitumia maji kutoka kwenye bwawa dogo la karibu. Lakini katika shule za serikali hali ni mbaya zaidi kuliko hii. Katika manispaa ya mkoa wa Morogoro hakuna vyoo vya kutosha katika shule zake kuna matundu 892 ya vyoo tu, kati ya matundu 2574 yanayohitajika (Chanzo: Mtanzania 21/07/2023)

Pia ni undumilakuwili wa wazi kufunga madrasa ya Al-habash kwa sababu wasichana wananyimwa elimu ya kisekula. Nchini Tanzania kuna takriban watoto wa mtaani 4,383, kati yao wavulana ni 3,508 na wasichana ni 875, kama serikali inataka kutoa elimu kwa wasichana, kwa nini haiwakusanyi watoto wote hawa wa mtaani na kuwapeleka shule.

Tunaitaka serikali kuifungua tena Madrasa ya Al- Habash na kuipa muda kufanya mabadiliko yanayohitajika. Wakati umefika kwa serikali kujiweka mbali na kampeni ya kimataifa ya kibepari dhidi ya Uislamu ambayo inatia doa mahusiano ya serikali na watu wake. Uislamu umetoa mchango mkubwa na wa kipekee kwa Tanzania, na utafanya zaidi mara tu dola ya Khilafah itakaposimamishwa tena katika ulimwengu wa Kiislamu InshaAllah.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu