- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Nyuma ya Kongamano la Wanazuoni wa Dunia la 2024
(Imetafsiriwa)
Habari:
Afisi ya Waziri katika Idara ya Waziri Mkuu (Mambo ya Kidini), kwa kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya Kiislamu ya Malaysia (JAKIM) na Jumuiya ya Waislamu Ulimwenguni (MWL) kutoka Saudi Arabia, hivi karibuni iliandaa Kongamano la Viongozi wa Kidini Ulimwenguni la 2024 na Baraza la Wasomi wa Asia la 2024 jijini Kuala Lumpur. Kongamano hili lililenga kukuza ruwaza ya hadhara ya pamoja inayounganisha maadili ya wastani na umoja, kushughulikia tishio la fikra ya msimamo mkali, na kubadilisha mizozo kuwa maelewano, ushirikiano, na umoja.
Maoni:
Mnamo Mei 2016, kamati iliundwa jijini Washington ili kupanga ushirikiano na Saudi Arabia kama kituo cha kushughulikia itikadi kali. Baadaye, Mei 2017, Kituo cha Kimataifa cha Kupambana na Mfumo wenye Misimamo Mikali (GCCEI) kilianzishwa na kuzinduliwa wakati wa ziara ya Rais Donald Trump jijini Riyadh, Saudi Arabia. MWL ilicheza dori muhimu katika kuwezesha ajenda hii ya "Uislamu wa wastani". Kupitia uongozi wa Muhammad bin Abdulkarim Al-Issa, MWL ilianzisha "Mkataba wa Makka" mnamo Mei 2019, ambao uliungwa mkono na kikundi cha wasomi mashuhuri wa Kiislamu waliokusanyika katika Jiji hilo Takatifu ili kukuza simulizi ya Uislamu wenye msimamo wa wastani. Uislamu wa wastani ni dhehebu la kifikra linalofadhiliwa na nchi za Magharibi ambalo linaunganisha mafundisho ya Kiislamu na kanuni za kisekula na uwazi, likihimiza tafsiri zenye kunyumbuka aghlabu zinazokengeuka kutoka kwa unyoofu na haki ya Uislamu. Kwa ajili hiyo, Saudi Arabia na MWL wanawajibika kama majukwaa ya kueneza ajenda hii kwa nchi nyingine za Kiislamu kupitia makongamano na mabaraza mbalimbali ya wanazuoni, yakilenga kujenga kizazi kipya cha Kiislamu ambacho fikra zao zimeegemezwa kwenye mawazo ya Mkataba wa Makka. Tunachoweza kusoma kutokana na hili ni kwamba nchi za Magharibi zinasisitiza kwamba Uislamu lazima ubadilishwe kulingana na dhurufu, badala ya dhurufu kubadilishwa kwa Uislamu. Na dhurufu tunazoishi leo zimetawaliwa na fikra na thaqafa ya Magharibi. Kwa Waislamu wanaotamani utabikishwaji kamili na sahihi wa Uislamu, aghlabu huitwa Waislamu wenye siasa kali, na sio mara chache, kama watu wenye msimamo mkali na wenye itikadi kali!
Kwa uhalisia, Umma wa Kiislamu hauhitaji fahamu ya Uislamu wa wastani na njia ya uvumilivu inayonadiwa na kuanzishwa na Marekani. Kwa miaka 1400, Waislamu wameishi kwa amani na watu na dini mbalimbali chini ya Uislamu. Hili limeandikwa vyema katika kumbukumbu za kihistoria na vitabu vingi - hata wanahistoria wasio Waislamu wanakiri ukweli huu. Kwa mfano, kitabu "Pambo la Dunia" (The Ornament of the World) kilichoandikwa na msomi wa Kimarekani, kiliwasilisha utajiri mkubwa wa thaqafa mbalimbali wakati Waislamu walipotawala Al-Andalus (Uhispania) chini ya sheria za Kiislamu. Wakati huo, Waislamu, Mayahudi, na Wakristo hawakuishi pamoja tu bali pia walikuza utamaduni wa hali ya juu wa kuvumiliana. Inajulikana hata kuwa ni zama za dhahabu kwa Mayahudi! Kwa upande mwingine, kuenea kwa fikra mbalimbali za Kimagharibi kumeleta maafa mengi katika maelewano na ustawi wa maisha ya mwanadamu. Na ni mawazo haya ambayo nchi za Magharibi zinawataka Waislamu kuyakubali kwa jina la Uislamu wa wastani.
Inasikitisha kwamba wakati huu, wanazuoni walipaswa kuelekeza juhudi zao zote katika kujenga umoja na nguvu katika ulimwengu wa Kiislamu ili kuikomboa Palestina na maeneo yote yanayokandamizwa, na wala sio kujitia mtegoni katika mchezo huu wa utawala wa Magharibi. Kwa kweli, nchi za Magharibi hazistahiki wala hazijawahi kuwa na msimamo wa kimaadili kufundisha au kuongoza jamii ya kiulimwengu kuhusu maana ya maisha na amani.
Badala yake, leo, waliohitimu zaidi kufundisha ulimwengu kuhusu ubinadamu ni Waislamu nchini Palestina. Tumeona mateso na dhulma za kutosha zinazowapata Waislamu huko na khiyana zinazofanywa na viongozi wa ulimwengu wa Kiislamu. Wanazuoni lazima wakatae wito huu unaofadhiliwa na Magharibi wa Uislamu wa wastani na waanze kuelekeza juhudi katika kuunganisha Ummah chini ya bendera ya Khilafah.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Dkt. Mohammad – Malaysia