- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Vichwa vya Habari: 13/07/2022
Vichwa vya Habari:
• Ongezeko la Idadi ya Watu Lagonga Kiwango cha Chini Zaidi
• Urusi Yakatiza Gesi Ulaya
• Kitengo cha SAS Kiliwaua Mara kwa Mara Wafungwa wa Afghanistan, BBC Yagundua
Maelezo:
Ongezeko la Idadi ya Watu Lagonga Kiwango cha Chini Zaidi
Ongezeko la idadi ya watu duniani limefikia kiwango cha chini zaidi tangu 1950, ripoti moja ya Umoja wa Mataifa imegundua. Idadi ya watu ulimwenguni iliongezeka kwa chini ya 1% kwa mwaka kwa mara ya kwanza tangu baada ya Vita vya pili vya Dunia mnamo 2020 na 2021 huku jumla ya idadi ya watu barani Ulaya ikipungua wakati wa janga la virusi vya Korona. Idadi ya watu wa nchi 61 - haswa nchi zilizoendelea inatabiriwa kupungua kwa angalau 1% kati ya 2022 na 2050, na viwango vya chini vya uzazi vinavyohusishwa pia vitaunganishwa na huduma bora za afya ili kuharakisha kuzeeka kwa jamii. Hata hivyo, idadi inayoongezeka ya wazee katika nchi nyingi inatabiriwa kuathiri ukuaji wa uchumi na fedha za umma na tayari inaleta changamoto zinazoongezeka za kisiasa. Idadi ya watu barani Ulaya ilipungua kwa 744,000 mwaka wa 2020 na kufikia milioni 1.4 mwaka jana - punguo kubwa zaidi ya bara lolote tangu rekodi zianze mnamo 1950. Lakini, janga hilo "sio sababu kuu", alisema John Wilmoth, mkurugenzi wa kitengo cha idadi ya watu na idara ya kiuchumi na masuala ya kijamii cha UN. Kiwango cha uzazi "kimekuwa cha chini sana katika takriban nchi zote za Ulaya kwa miongo mingi na hiyo inamaanisha kuwa hakuna vijana wengi", alisema.
Urusi Yakatiza Gesi Ulaya
Urusi iliacha kusukuma gesi kupitia bomba la Nord Stream 1 hadi Ujerumani ili kufanya ukarabati ulioratibiwa, ambao umepangwa kudumu hadi Julai 21. Urusi ilikuwa tayari imepunguza kwa kiasi kikubwa usafirishaji, ikidai kuwa ni kwa sababu ya kuchelewa kurudi kwa banka kutoka Canada. Ukraine tayari imefunga mfumo wa mabomba kutokana na mashambulizi ya Urusi, hivyo bomba la Ujerumani la Nord Stream linasalia kuwa bomba pekee linaloweza kupeleka nishati Ulaya. Pia lilikuwa bomba pekee la kuleta nishati kwa Ujerumani, ambayo inaitegemea Urusi kwa nishati. Huku bei za nishati zikizidi kupamba moto na usafirishaji kudorora, utekelezaji ukarabati katika wakati kama huo mgumu ungeashiria kwamba Urusi inajaribu kuilaghai Ujerumani kujitoa katika muungano wa Magharibi ulioanzishwa dhidi yake kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.
Kitengo cha SAS Kiliwaua Mara kwa Mara Wafungwa wa Afghanistan, BBC Yagundua
Wahudumu wa SAS (kitengo cha vikosi maalum vya Jeshi la Uingereza) nchini Afghanistan waliwaua wafungwa na watu wasiokuwa na silaha mara kwa mara katika hali ya kutiliwa shaka, kulingana na uchunguzi wa BBC. Ripoti mpya za kijeshi zilizopatikana zinaonyesha kuwa kitengo kimoja huenda kimewaua watu 54 kinyume cha sheria katika ziara moja ya miezi sita. BBC ilipata ushahidi unaoonyesha kwamba mkuu huyo wa zamani wa kikosi maalum alishindwa kuwasilisha ushahidi kwenye uchunguzi wa mauaji. Wizara ya Ulinzi ilisema wanajeshi wa Uingereza "walihudumu kwa ujasiri na weledi nchini Afghanistan". BBC inafahamu kwamba Jenerali Sir Mark Carleton-Smith, mkuu wa zamani wa Kikosi Maalum cha Uingereza, alifahamishwa kuhusu madai ya mauaji hayo kinyume cha sheria lakini hakuwasilisha ushahidi huo kwa Polisi wa Kijeshi wa Kifalme, hata baada ya RMP kuanza uchunguzi wa mauaji katika kikosi cha SAS. BBC Panorama ilichanganua mamia ya kurasa za akaunti zinazoendeshwa za SAS, zikiwemo ripoti zinazohusu zaidi ya dazeni za uvamizi wa "kuua au kukamata" uliofanywa na kikosi kimoja cha SAS huko Helmand mnamo 2010/11. Watu waliohudumu katika kikosi cha SAS katika upelekwaji huo waliiambia BBC kuwa walishuhudia maafisa wa SAS wakiwaua watu wasiokuwa na silaha wakati wa mashambulizi ya usiku. Pia walisema waliona wahudumu hao wakitumia kile kinachoitwa "silaha za kuanguka" - AK-47 zilizopandikizwa kwenye eneo la tukio ili kuhalalisha mauaji ya mtu asiye na silaha.