Alhamisi, 16 Rajab 1446 | 2025/01/16
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Vichwa vya Habari: 06/08/2022

Vichwa vya Habari:

• Gavana wa Benki Kuu ya Uingereza, Bailey, Aonya Uingereza Inakabiliwa na Mshtuko Mkubwa Sana wa Mfumko wa Bei

• Taliban yasema ‘hakuna taarifa yoyote’ kuhusu Mkuu wa Al Qaeda Zawahiri nchini Afghanistan

• China Yasitisha Ushirikiano wa Amerika juu ya Maswala Anuwai baada ya Ziara ya Pelosi Taiwan

Maelezo:

Gavana wa Benki Kuu ya Uingereza, Bailey, Aonya Uingereza Inakabiliwa na Mshtuko Mkubwa Sana wa Mfumko wa Bei

Benki ya Uingereza mnamo Alhamisi ilitetea uamuzi wake wa kuongeza viwango vya riba kwa haraka zaidi katika kipindi cha miaka 27, ikisema kwamba Uingereza inakabiliwa na mshtuko "mkubwa sana" wa mfumko wa bei. Gavana wa BOE Andrew Bailey alisema kuwa hatari za mfumko wa bei kuwa ni wenye kuendelea zimeongezeka tangu mkutano wa awali wa Benki hiyo mwezi Juni, na kuifanya kuchukua "hatua kali zaidi." "Tunakabiliwa na mshtuko mkubwa sana wa mfumko wa bei," Bailey alimwambia Joumanna Bercetche wa CNBC. "Hatua yetu leo ​​ilikuwa wazi sana [kwamba] tunahisi lazima tuchukue hatua kali." BOE mnamo Alhamisi ilipandisha viwango vya riba kwa msingi wa pointi 50, na kupandisha gharama za kukopa hadi 1.75% katika jitihada zinazoendelea za kupunguza mfumko wa bei unaoongezeka. Pia ilitoa mtazamo mbaya kwa ukuaji wa uchumi wa Uingereza, ikitabiri kuwa nchi hiyo itaingia kwenye mdororo kutoka robo ya nne ya 2022, na mdororo unatarajiwa kudumu kwa robo tano. Benki kuu imekabiliwa na ukosoaji kwa kutochukua hatua mapema na kwa ukali zaidi kukabiliana na mfumko wa bei. Lakini Bailey alisisitiza Alhamisi kwamba mishtuko mingi ya mfumko wa bei inayoukabili uchumi wa Uingereza ilikuwa ya nje na isiyotarajiwa - haswa vita vya Urusi nchini Ukraine na athari zake mbaya kwa bei ya nishati. "Hatutengezi sera kwa kutazama nyuma," Bailey alisema. Vita nchini Ukraine “si jambo lililotabiriwa au kusema kweli lingeweza kutabiriwa.” [Chanzo: CNBC].

Kujiondoa kwa Uingereza kutoka kwa EU kumefanya iwe vigumu kwa serikali hiyo kupona katika ulimwengu wa baada ya Uviko, huku nchi hiyo ikielekea kwenye mteremko. Kuna uwezekano mkubwa kwamba Benki Kuu italazimika kuongeza viwango vya riba juu zaidi ili kudhibiti mfumko wa bei, na hii itaambatana na ukuaji duni sana.

Taliban yasema ‘hakuna taarifa yoyote’ kuhusu Mkuu wa Al Qaeda Zawahiri nchini Afghanistan

Taliban ilisema mnamo Alhamisi kuwa hawajui kuhusu uwepo wa Ayman al-Zawahiri nchini Afghanistan, siku chache baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kutangaza mauaji ya mkuu huyo wa Al Qaeda kwa shambulizi la droni jijini Kabul. Mauaji ya Zawahiri ni pigo kubwa zaidi kwa Al Qaeda tangu vikosi maalum vya Marekani kumuua Osama bin Laden mwaka 2011 na kutilia shaka ahadi ya Taliban ya kutohifadhi makundi ya wanamgambo. "Imarati ya Kiislamu ya Afghanistan haina habari kuhusu kuwasili kwa Ayman al-Zawahiri na kukaa jijini Kabul," ilisema taarifa rasmi - utajaji wa mara ya kwanza wa Taliban wa jina lake tangu kutangazwa kwa Biden. Zawahiri aliaminika kuwa ndiye msimamizi wa operesheni za Al Qaeda - ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya 9/11 - na pia kuwa daktari wa kibinafsi wa bin Laden. Afisa mkuu wa utawala wa Marekani alisema Mmisri huyo mwenye umri wa miaka 71 alikuwa kwenye roshani ya nyumba ya ghorofa tatu katika mji mkuu wa Afghanistan alipolengwa kwa makombora mawili aina ya ‘Hellfire’ mapema Jumapili. Taarifa ya Taliban ya Alhamisi iliyo andikwa kwa uangalifu haikuthibitisha kuwepo kwake nchini Afghanistan wala kukiri kifo chake. "Uongozi wa Imarati ya Kiislamu ya Afghanistan umeagiza mashirika ya kijasusi kufanya uchunguzi mpana na wa kina," ilisema. "Ukweli kwamba Amerika ilivamia eneo letu na kukiuka kanuni zote za kimataifa, tunalaani vikali kitendo hicho kwa mara nyingine tena. Ikiwa hatua kama hiyo itarudiwa, jukumu la matokeo yoyote litakuwa kwa Marekani. Taliban ilisisitiza katika taarifa yao kwamba "hakuna tishio" la nchi yoyote kutoka ardhi ya Afghanistan. Walitoa wito kwa Washington kuzingatia mkataba wa Doha uliotiwa saini Februari 2020 ambao ulifungua njia ya kuondolewa kwa vikosi vya kigeni kutoka Afghanistan, na hivyo kuhitimisha miongo miwili ya uingiliaji kijeshi unaoongozwa na Marekani nchini humo. Akitangaza kifo cha Zawahiri mnamo Jumanne, Biden alisema "haki imetolewa" kwa familia za wahasiriwa wa shambulizi la 9/11 dhidi ya Amerika. Shambulizi la Jumapili la droni lilikuwa shambulizi la kwanza kujulikana la juu-juu lililofanywa na Marekani kulenga shabaha nchini Afghanistan tangu Washington ilipoondoa majeshi yake nchini humo Agosti 31 mwaka jana, siku chache baada ya Taliban kuregea madarakani. Nyumba iliyolengwa katika shambulizi hilo iko Sherpur, moja ya vitongoji tajiri zaidi vya Kabul, kikiwa na nyumba kadhaa za kifahari zinazokaliwa na maafisa na makamanda wa ngazi za juu wa Taliban. [Chanzo: Dawn]

Ni vigumu kuamini kwamba Taliban pamoja na Pakistan hawakuhusika katika mauaji ya Zawahiri. Shambulizi la droni huhitaji wafanyakazi wa chinichini kufuatilia na kuthibitisha lengo kabla na baada ya shambulizi la droni. Kwa hili kutokea katika nyumba ya afisa mkuu wa Taliban linasisitiza kwamba Taliban ilihusika katika mauaji hayo. Zaidi ya hayo, droni huhitaji kambi ya kurukia kutoka au ukanda salama wa anga. Inaonekana Pakistan ilitoa hii kama badali ya malipo ya IMF. Siku iliyofuata tu baada ya kuuawa kwa Zawahiri, IMF ilithibitisha kwamba italipa malipo kwa Pakistan.

China Yasitisha Ushirikiano wa Amerika juu ya Maswala Anuwai baada ya Ziara ya Pelosi Taiwan

Uhusiano kati ya nchi hizi mbili zenye uchumi mkubwa zaidi duniani umeporomoka katika hali ya sintofahamu zaidi huku China ikisitisha uhusiano na Marekani juu ya maswala mbalimbali muhimu - kuanzia kwa mazungumzo juu ya mzozo wa hali ya hewa hadi kwa mazungumzo kati ya majeshi yao - kufuatia ziara ya Taiwan mapema wiki hii ya Spika wa Bunge la Amerika, Nancy Pelosi. Tangazo la mfululizo wa "hatua za kukabiliana" lilikuja wakati Beijing kwa siku ya pili ikifanya mazoezi makubwa ya kijeshi kuzunguka kisiwa cha Taiwan na pia kutangaza vikwazo dhidi ya Pelosi na wanafamilia wake wa moja kwa moja kwa kile ilichokiita kwake "vitendo viovu na vya uchochezi". Wizara ya ulinzi ya Taiwan ilisema kuwa inazo ndege za kupinduka punduka kuzionya ndege 49 za China katika zoni yake ya ulinzi wa anga mnamo Ijumaa na jumla ya ndege 68 za kijeshi za China na manuari 13 za jeshi la wanamaji zimefanya misheni. Wizara ya mambo ya nje ya Taipei pia iliripoti kuwa imegundua idadi kubwa ya majaribio ya mashambulizi ya mtandao dhidi ya tovuti yake mnamo Alhamisi na Ijumaa asubuhi. Huku hali ya wasiwasi ikizidi kutanda katika mlango wa bahari wa Taiwan, China mnamo Ijumaa ilisema inafutilia mbali baadhi ya juhudi za kuweka njia za mawasiliano wazi kati ya makamanda wa kijeshi wa China na Marekani. Hizo ni pamoja na majaribio ya kuratibu shughuli za anga na baharini ili kuzuia milipuko isiyokusudiwa, kwa mfano, na manuari zinazofanya operesheni karibu karibu baharini. Mazungumzo na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili kuhusu masuala ya dharura ya hali ya hewa, kuwaregesha makwao wahamiaji haramu, kupambana na dawa za kulevya na usaidizi wa kisheria katika masuala ya uhalifu yalisitishwa. Ikulu ya White House ilisema imemwita balozi wa China jijini Washington kulaani tabia ya "kutowajibika" ya Beijing juu ya Taiwan. Afisa mmoja wa ubalozi wa China jijini Washington alisema njia pekee ya kutoka kwa mgogoro huo ni kwa Amerika "kurekebisha makosa yake na kuondoa athari mbaya ya ziara ya Pelosi." Wachambuzi wanasema kusitishwa kwa baadhi ya shughuli za nchi hizo mbili - hasa zile zinazohusiana na jeshi - kunatishia kuvunja kile Ikulu ya White House inachokiita "vizuizi" kati ya nchi hizo mbili, ambapo inaweza kuzuia hali kutoka nje ya udhibiti. "Hatua hizi zitapunguza nafasi kwa Marekani na China kupata modus vivendi inayohitajika mno," alisema Zeno Leoni, mtaalamu wa ulinzi katika Chuo cha London cha King's College. "Mataifa mawili yenye nguvu zaidi sasa hayawezi kuongea - kwa njia yenye natija." Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken, aliuambia mkutano wa wanadiplomasia wa Asean mnamo Ijumaa kwamba mwitikio wa China ulikuwa "uchochezi wa hali ya juu". “Ukweli ni kwamba, ziara ya spika ilikuwa ya amani. Hakuna uhalali wa mwitikio huu wa kijeshi uliopitiliza, usio na uwiano na unaozidi kuchochea moto," Blinken alisema. Huiyao Wang, mwanzilishi wa Kituo cha China na Utandawazi chenye makao yake jijini Beijing na mshauri wa serikali ya China, alisema China iliiona ziara ya Pelosi kama ushahidi kwamba Washington tayari imevunja "vizuizi". Alisema Beijing inalichukulia suala la Taiwan kama "mstari mwekundu wa mwisho" wa uhusiano wa nchi hizo mbili, na ziara yake itawatia moyo wanasiasa wengine kuzuru Taiwan katika siku zijazo. [Chanzo: The Guardian]

Baada ya kuihusisha Urusi nchini Ukraine, Marekani inataka kufanya vivyo hivyo kwa China dhidi ya Taiwan. Ziara ya Pelosi inaashiria kupamba moto kwa Marekani kuhimiza China kuchukua hatua za kijeshi nchini Taiwan. Wakati huo huo Marekani inazitumia zote mbili Urusi pamoja na China kuidhoofisha Ulaya na kuifanya itegemee zaidi usalama wa Marekani. Kwa mfano, uchumi wa Ujerumani uko ukingoni mwa kuporomoka huku ikihangaika kubadilisha uchukuaji gesi kutoka Urusi na msimamo wake wa kuunga mkono Marekani dhidi ya Taiwan ni lazima ukaribishe ulipizaji kisasi kutoka China—soko kubwa zaidi la mauzo ya nje la Ujerumani. Hatua hizi zote zimekusudiwa kuiwezesha Amerika kusisitiza ubwana wake wa kiulimwengu baada ya miaka ya majanga ya Trump.

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu