Jumanne, 03 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/05
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa

Amiri wa Hizb ut Tahrir

Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah katika Ukurasa Wake wa Kifikra wa Facebook
Jibu la Swali

Hukmu ya Miamala ya Kifedha na Kibiashara kupitia Mtandao wa Intaneti
Kwa: Saed Khatib
(Imetafsiriwa)

Swali:

Assalamu alaikum wa Rahmatullah wa Barakatahu,

Je, ni ipi hukmu ya biashara, kwa mfano, kununua dinari, mafuta, dhahabu nk kwa dolari wakati wa bei nafuu, kisha kuiuza kwa wakati wa bei ya juu ili kupata faida, huku ukijua kwamba yote haya yanapatikana kwenye mtandao, na anaweza kuhamisha pesa benki na kuzitoa wakati wowote anapotaka?

Swali la pili: Je, inahitajika wakati wa kubadilishana sarafu kuzipokea ana kwa ana au inatosha kuzipokea mtandaoni bila mkono?

-Nitaongeza katika swali hili: Je, akinunua mafuta ni lazima apate kuyamiliki na kuyapokea, na je ikiwa atauza bila kumiliki?

Akijua kwamba akinunua mafuta, chuma, dhahabu au pesa hawezi kuzipokea isipokuwa atazibadilisha kuwa dolari na kuzipokea kama dolari. Kwa hivyo ukinunua mafuta, huwezi kuyapokea kama mafuta, lakini yanabadilishwa kuwa dolari.

Imeelezwa pia katika kitabu cha Nidhamu ya Kiuchumi kwamba hairuhusiwi kabisa kuiuzia, na hii ni pamoja na kile anachomiliki lakini hajakipokea, ambacho kinahitaji kumilikiwa kwa ajili ya kukamilisha mauzo, ambayo hukisiwa, kupimwa uzito, na kuhesabiwa. Ama kile kisichohitaji kukitia mkono kwa ajili ya kukamilisha umiliki wake, ambacho hakikisiwi, hakipimwi, wala hakihesabiwi, kama vile mnyama, nyumba, ardhi na mengineyo, basi inajuzu kwa muuzaji kuuza kabla ya kukipokea.

Swali ni: Je, nitawezaje kuhukumu ikiwa kitu kinakisiwa, kupimwa, au kuhesabiwa au la? Alitaja mfano wa kitu ambacho hakikisiwi, kama mnyama au nyumba, lakini mnyama kama kondoo katika nchi yetu tunapomnunua, tunampima na anauzwa kulingana na uzito wake, akionekana kupimika. Kadhalika, nyumba inaitwa ghorofa moja au ghorofa mbili, ikiwa itahesabiwa, je, nitavichukuliaje kuwa ni vitu visivyohesabiwa au kupimwa?

Jibu:

Wa Assalamu alaikum wa Rahmatullah wa Barakatahu,

Kuhusu suala la biashara, hapo awali tumejibu swali kama lako, na nimetoa kutoka kwake kile kinachohusiana na swali lako:

[Kuhusu jibu la swali la kwanza, ambalo ni biashara ya mtandaoni, ni kama ifuatavyo:

1- Kuhusu mafuta, swali haliko wazi:

Je! unataka kujaza gari lako kwenye kituo cha mafuta na kadi ya elektroniki na kumpa afisa wa kituo cha mafuta ambaye atajaza gari lako na petroli? Ikiwa ndivyo, basi inaruhusiwa kwa sababu ikiwa utoaji wa thamani kutoka kwa akaunti yako utachelewa kwa siku moja au mbili, basi inaruhusiwa kununua bidhaa hii kwa mkopo bila riba, na wewe kupokea bidhaa (petroli kwa ajili ya gari lako) na achukua thamani mara moja au baada ya siku moja au mbili. Ikiwa uhalisia ni kama huu, basi hakuna kitu kibaya na hilo.

Hata hivyo, ikiwa lengo lililokusudiwa la biashara ni kununua kiasi kidogo cha mafuta na kisha kuyauza kabla ya kuyapokea, basi hii hairuhusiwi kwa sababu kupokea ni sharti la kuuza bidhaa hizi. Imepokewa kutoka kwa Abu Dawud kutoka kwa Zaid bin Thabit ambaye amesema:

«فَإِنَّ رَسُولَ اللَّهِ ﷺ نَهَى أَنْ تُبَاعَ السِّلَعُ حَيْثُ تُبْتَاعُ حَتَّى يَحُوزَهَا التُّجَّارُ إِلَى رِحَالِهِمْ»

“Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu () amekataza kuuzwa bidhaa zinaponunuliwa, mpaka wafanyibiashara wachukue katika maboma yao”. Yaani bidhaa hizi haziuzwi isipokuwa baada ya kumilikiwa na kupokelewa. Kwa hivyo, kumiliki ni sharti la uhalali wa uuzaji wao isipokuwa kama kuna andiko maalum kuhusiana na bidhaa fulani, basi inaruhusiwa na sio zengine, na hii haikutajwa hapa ... hivyo basi haijuzu kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu.

Lakini ikiwa unamaanisha kuwa mshirika katika kisima cha mafuta kwa kulipa pesa kupitia kadi ya elektroniki kwenye mtandao, basi hii hairuhusiwi kwa sababu visima vya mafuta ni mali ya umma na havina umiliki wa kibinafsi.

Lakini ikiwa unamaanisha kitu chengine, basi fafanua.

2- Biashara ya dhahabu na fedha:

Ama dhahabu na fedha, kuuza na kununua kwa kila moja yao au kwa pesa taslimu lazima kufanyike mkono kwa mkono, kama katika hadith iliyopokelewa na Al-Bukhari na Abu Dawud kutoka kwa Omar: “Dhahabu kwa fedha ni riba isipokuwa ikiwa ni mkono kwa mkono,” ikimaanisha mkono kwa mkono. Kwa hiyo, kununua dhahabu kwa fedha au kwa pesa si halali isipokuwa kwa mkono kwa mkono.

Na kwa sababu baada ya kujifunza jinsi ya kufanya biashara mtandaoni, ubadilishanaji haufanyiki mara moja, lakini badala yake inaweza kuchukua masaa au siku, kwa hivyo hairuhusiwi kununua dhahabu na fedha kwa kadi ya elektroniki kupitia mtandao isipokuwa ikiwa kadi itakatwa kutoka kwa akaunti hapo hapo wakati wa kununua dhahabu au fedha, yaani mkono kwa mkono, hivyo usipokee dhahabu au fedha isipokuwa wakati kiwango cha thamani kitatolewa kutoka kwa akaunti yako. Na kwa kuwa hakuna ubadilishanaji wa hapo hapo katika biashara ya mtandaoni, bali baada ya siku moja au mbili, basi haijuzu.

3-Biashara ya hisa na bondi ni haramu kwa sababu hisa zinatokana na makampuni ya hisa ambayo ni batili kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, na kwa sababu bondi zinahusishwa na riba, na vile vile katika kitabu Msukosuko wa Masoko ya Hisa na vitabu vyengine, tumetaja katika kijitabu, Msukosuko wa Masoko ya Hisa, mukhtasari wa jambo hili kama ifuatavyo:

“Ama hukmu ya Shari ́ah inayohusu kufanya biashara katika hisa hizi na katika dhamana, iwe kununua au kuuza, ni haramu. Hii ni kwa sababu hisa hizi ni za muundo wa kampuni ambayo ni haramu kwa mujibu wa Shari ́ah. Kwa hakika ni vyeti vya bili ambazo zina kiasi mseto kutoka kwa mtaji halali na faida haramu inayotokana na muamala haramu. Kila bili inawakilisha thamani ya hisa, na hisa hii inawakilisha sehemu ya mali ambayo ni ya kampuni haramu. Mali hizi zimechanganywa na muamala wa haramu ambao Shari ́ah imeharamisha. Kwa hivyo, ni pesa haramu, ambayo kununua na kuuza kunakuwa ni haramu, na kuamiliana na pesa hizo pia ni haramu. Hii pia ndio hali kwa dhamana, ambayo fedha imewekezwa kwa riba, na hivyo ndivyo hali ya hisa za benki na mithili yake, kwa kuwa zote zinajumuisha kiasi cha pesa haramu; hivyo kununua na kuuza kwake ni haramu, kwa sababu pesa zilizomo ndani yake ni haramu.” MWISHO WA NUKUU.

4- Uuzaji wa sarafu za karatasi kwenye mtandao, kama vile dolari na euro, ni marufuku kwa sababu hakuna ubadilishanaji wa mkono kwa mkono, ambao ni muhimu katika kubadilishana pesa. Kubadilishana mkono kwa mkono, kama inavyotumika kwa dhahabu na fedha, pia hutumika kwa pesa za karatasi kwa misingi ya sarafu, yaani kuzitumia kama thamani ya bidhaa na mishahara. Tulitaja yafuatayo katika Jibu la Swali la tarehe 11/07/2004:

[Kuamiliana na sarafu za karatasi

Ndiyo, kinachotekelezeka kwa dhahabu na fedha katika suala la riba na hukmu nyengine za fedha kinatekelezeka kwake pia. Hii ni kwa sababu utambuzi wa sababu (pesa taslim, yaani matumizi yake kama bei na mishahara) katika karatasi hizi huzifanya zichukue hukmu za pesa.

Kwa hiyo, kununua vitu vya riba kwa karatasi hizi kunatekelezeka kwa yale yaliyotajwa katika Hadith (mkono kwa mkono), yaani sio deni.

Mada ni kama ifuatavyo:

Mtume (saw) asema:

«الذَّهَبُ بِالذَّهَبِ، وَالْفِضَّةُ بِالْفِضَّةِ، وَالْبُرُّ بِالْبُرِّ، وَالشَّعِيرُ بِالشَّعِيرِ، وَالتَّمْرُ بِالتَّمْرِ، وَالْمِلْحُ بِالْمِلْحِ، مِثْلًا بِمِثْلٍ، سَوَاءً بِسَوَاءٍ، يَداً بِيَدٍ، فَإِذَا اخْتَلَفَتْ هَذِهِ الْأَصْنَافُ فَبِيعُوا كَيْفَ شِئْتُمْ إِذَا كَانَ يَداً بِيَدٍ»

“Dhahabu ilipwe kwa dhahabu, fedha kwa fedha, ngano kwa ngano, shayiri kwa shayiri, tende kwa tende, na chumvi kwa chumvi, mithili kwa mithili sawa kwa sawa, malipo yafanywe mkono kwa mkono. Ikiwa matabaka haya yatatofautiana, uzeni mupendavyo ikiwa malipo yatafanywa mkono kwa mkono.” (Imepokewa na Al-Bukhari na Muslim kutoka kwa Ubada bin Al-Samit, Mwenyezi Mungu awe radhi naye.)

Andiko liko wazi pindi vigawanyo hivi vya riba (riba) zinapotofautiana, kwamba uuzaji ni kama munavyotaka, yaani, sawa kwa sawa sio sharti, lakini ubadilishanaji ni sharti. Neno “vigawanyo” lilitajwa kwa jumla katika vigawanyo vyote vya riba, yaani sita, na hakuna kinachotolewa humo isipokuwa kwa andiko, na pale ambapo hakuna andiko, hukmu ni kwamba ngano inaruhusiwa kwa shayiri au ngano kwa dhahabu, au shayiri kwa fedha, au tende kwa chumvi, au tende kwa dhahabu, au chumvi kwa fedha ... nk. Haijalishi jinsi thamani ya ubadilishanaji na bei ni tofauti kiasi, lakini mkono kwa mkono, yaani sio deni. Na kile kinachotekelezeka kwa dhahabu na fedha kinatekelezeka kwa pesa za karatasi kwa sababu ya lengo kuwa moja (pesa, yaani, matumizi yake kama bei na ujira).] Mwisho.

Kwa kuchunguza jinsi biashara hii ya mtandaoni ya kununua na kuuza dhahabu inavyofanyika, imebainika kuwa ukusanyaji au malipo hucheleweshwa kwa siku moja au mbili ... kuanzia tarehe ya mkataba, na hii ni kinyume na sharti lililokubaliwa la ubadilishanaji, ambalo Mtume (saw) ameliweka katika kauli yake: “Mkono kwa mkono.” Imesimuliwa na Al-Bukhari kutoka kwa Al-Bara’ bin Azib, ambaye amesema: Tulimuuliza Mtume (saw) kuhusu hilo, naye akasema:

«مَا كَانَ يَداً بِيَدٍ فَخُذُوهُ وَمَا كَانَ نَسِيئَةً فَذَرُوهُ»

“Chukueni kile ambacho ni mkono kwa mkono na acheni kile ambapo ni kwa mkopo.” Muslim amepokea kutoka kwa Malik bin Aws bin al-Hadathan kwamba amesema: Nilikuja na kusema: Ni nani anayebadilishana dirham? Talha ibn Ubaydullah akasema alipokuwa na Umar ibn al-Khattab: Tuonyeshe dhahabu yako, kisha uje kwetu atakapokuja mtumishi wetu na tutakupa pesa zako. Umar bin al-Khattab akasema: Hapana, Wallahi ni lazima ima umpe pesa zake au umrudishie dhahabu yake, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «الْوَرِقُ بِالذَّهَبِ رِباءَ وَهَاءَ...» “Dhahabu na fedha ni riba, isipokuwa hii kwa hii...”

Kutokana na hayo, hairuhusiwi kufanya biashara ya euro, dolari na aina nyingine za sarafu kwenye Mtandao kwa sababu hakuna ubadilishanaji wa hapo kwa hapo)] Mwisho wa kunukuu.

Kuhusiana na swali lako kuhusu bidhaa zenye kukisiwa, kuhesabiwa na kupimwa, nyuma tulijibu swali kama hilo kama ifuatavyo:

Jibu la Swali la tarehe 12/02/2006, ambalo lilisema: [Kuhesabiwa, kupimwa na kukisiwa ni kulingana na uhalisia wa uuzaji wa bidhaa.

...Angalia sokoni uone hii bidhaa inauzwaje? Je, inauzwa kwa idadi, maana yake inasemwa sokoni kila nafaka kwa bei hii au kila moja kwa bei hiki? Je, inauzwa kwa uzito, kwa hiyo inasemwa kila kilo kwa bei hii? Au inasemwa kila mita kwa bei hii? Au kila saa’ (aina ya kipimo kikavu) kwa bei hii?...

Ikiwa ni hivyo, maelezo ya kuhesabiwa, uzito au kipimo yanatekelezeka kwake, iwe ni maelezo ya kimoja au zaidi, kumaanisha kuwa bidhaa hiyo inaweza kusifiwa kuwa ni yenye kupimwa na kuhesabiwa...

Mifano: ngano, shayiri ... kwa uzito na kipimo.

Ndizi, machungwa... kwa uzito na kwa idadi (katika baadhi ya nchi huuzwa kwa idadi)...

...na kuamua maelezo yake wakati wa kuvichukua vitu hivi ni muhimu ili kuondoa ujinga. Mtu anaponiambia kuwa nina kilo 100 za ngano, haitoshi kuamua maelezo. Badala yake, aina ya ngano lazima ielezwe ili uzito uondoe ujinga, na vilevile kwa kipimo na kuhesabiwa.

Lakini je, mnyama anauzwa kwa idadi, ili hata itangazwe kila ngamia mmoja kwa elfu, au anauzwa kupitia mnunuzi kumuona na kumtazama na kusema ngamia huyu hana thamani ya elfu moja kisha amchague ngamia wa pili? Je! kila ngamia ni kama mwenzake kiasi kwamba mauzo ni kwa idadi?

Kisha je, nyumba zinauzwa kwa idadi, uzito, au ujazo? Kwa maana nyengine, je, mtu mwenye nyumba kumi hunadi na kusema, “Nyumba moja ni ya elfu moja,” au nyumba yoyote hununuliwa kwa kuiona, na ni tofauti na nyengine...

Kwa hiyo, inasemekana kwamba mnyama na nyumba haziuzwi kwa kipimo, uzito au idadi. Unaweza kusema kwamba baadhi ya watu huuza wanyama wao kwa uzito, lakini sivyo ilivyo kwa kila mnyama. Anaweza kuuza kondoo fulani kwa kutumia uzito, lakini hauzi kila kondoo, wala hauzi kila mnyama, kwa hivyo hauzi ng'ombe kwa uzani ... kwa hivyo haisemwi kwangu, chukua kilo mia za wanyama (bila shaka, kumaanisha wako hai).

Vivyo hivyo, unaweza kusema kwamba baadhi ya watu huuza nyumba kwa mita, lakini hii haitumiki kwa kila nyumba. Badala yake, mita katika nyumba hii ni kumi, na katika nyumba ile ni ishirini, na kadhalika. Kwa hiyo, maelezo sahihi kwake sio kwa kipimo, kwa hivyo haisemwi kwangu, chukua nyumba ya mita mia moja

... Na kadhalika....] Mwisho.

Natumai hili linatosheleza, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na ni Mwingi wa Hekima.

Ndugu Yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

11 Rabi' al-Akhir 1446 H
Sawia na 14/10/2024 M

Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri Facebook.

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu