Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali
Kongamano la Maraisi Baina ya Amerika na Korea Kaskazini
(Imetafsiriwa)

Swali:

Kongamano la maraisi baina ya Amerika Kaskazini na Korea Kaskazini lilifanywa kupitia mkutano wa Maraisi wawili, Trump na Kim mnamo 12/6/2018 nchini Singapore. Walitia saini waraka kwa pamoja mwishoni mwa kongamano hilo. Makubaliano hayo yalifanywa kwa haraka, ikizingatiwa kuwa mzozo kati yao ulifikia kilele mwaka jana ambapo kila mmoja wao alitishia kumpiga mwengine kwa silaha za kinuklia. Ni vipi makubaliano haya yalifanyika kwa haraka? Ni yapi yaliyomo ndani yake na ni zipi natija zake?

Jibu:

Ili kuweza kufahamu ukweli wa jambo hili, twapiga darubini yafuatayo:

1- Amerika imejaribu mara kwa mara pamoja na vitisho kuifanya Korea Kaskazini kuachana na silaha zake za kinuklia, lakini vitisho hivi vimeambulia patupu, na Korea Kaskazini haikusalimu amri na wala haikuachana na mradi wake na silaha za kinuklia. Amerika ikaamua kutumia mbinu nyengine, ikiwemo mbinu ya kisiasa na ya kidiplomasia na shinikizo za kiuchumi. Mojawapo ya mbinu hizo ilikuwa ni Amerika kutia juhudi kuifanya China iishinikize Korea Kaskazini. Tulitaja katika Jibu la Swali la tarehe 23/4/2017: Kwa sasabu ya yote yaliyo juu, Amerika kwa sasa haiko tayari kwa vita nchini Korea Kaskazini, na hana masuluhisho mengine muwafaka. Inasubiri China kuishinikiza Korea Kaskazini, na inajaribu kuliharakisha hili, na taarifa zake kwamba Amerika iko tayari kusuluhisha tatizo hilo kipeke yake (yaani, bila ya China) zinaongezeka, kana kwamba inaitishia China kutii Amerika na kuishinikiza Pyongyang kuachana na silaha zake za kinuklia. Amerika imetangaza kupitia Naibu wa Waziri wa Kigeni wa Maswala ya Asia Mashariki na Pacific, Susan Thornton, aliyesema nchi yake haitafuti mzozo na Korea Kaskazini au kuibadilisha serikali yake: “Amerika imeeleza wazi wazi kuwa inataka kutatua tatizo hili na Korea Kaskazini kupitia kuachana na silaha za kinuklia kwa amani katika bara la Korea, kwa yakini hatulengi mzozo au kubadilisha serikali.” (Chanzo: Russia Today, 17/4/2017). Mawasiliano ya kidiplomasia baina ya pande mbili hizi yalianza kupitia China. Shinikizo zimewekwa kupitia kulazimisha vikwazo vya kiuchumi na kugomewa kisiasa kwa ili kuitenga kimataifa na kunyanyua propaganda dhidi yake ili kuwalazimisha kujisalimisha na kujitayarisha kuachana na silaha hizo. Iliongeza pia vivutio na ahadi za kukua kwa uchumi moja kwa moja na kupitia Korea Kusini, ambayo imeanza kuungana na Korea Kaskazini na kimataifa wazi wazi kwa ajili yake.

2- Mawasiliano ya siri ya kidiplomasia yalianza kupitia China, ambapo aliyekuwa Waziri wa Kigeni Tillerson aliwasiliana na watu wa Korea Kaskazini kupitia China mnamo Julai 2017. Alielezea upinzani wake kwa mbinu ovyo ya Trump, iliyohatarisha kuiangamiza Korea Kaskazini kutoka katika uso wa dunia, huku Tillerson akifanya maongezi ya kisiri na watu wa Korea Kaskazini nchini China! Wenyeji wa Korea Kaskazini waliposikia vitisho vya Trump walijiondoa kutoka katika mazungumzo hayo na kuondoka nchini China kurudi nchini kwao… Tillerson alikasirika na kumwita Raisi wake bwege mnamo 20/7/2017 kama ilivyo fichuliwa baadaye na shirika la habari la Amerika la NBC mnamo 4/10/2017 lilipowanukuu maafisa wa tatu wa Amerika. Trump aliandika katika mtandao wake wa Twitter siku moja baada ya Tillerson kutangaza kuwa Amerika ina njia za moja kwa moja za mawasiliano na Korea Kaskazini: “Nilimwambia Rex Tillerson, Waziri wetu adhimu wa Kigeni, kuwa anapoteza muda wake kujaribu kujadiliana na mtu mwenye kombora dogo”. Hayo hayo ndiyo yaliyotokea, yaani matumizi ya vitisho wakati wa mazungumzo pindi Makamu wa Raisi wa Amerika Mike Pence alipo jaribu kukutana na watu wa Korea Kaskazini nchini Korea Kusini alipoizuru kwa kisingizio cha kushiriki katika michezo ya Olimpiki ya Msimu wa Baridi. Alikuwa akijitayarisha kwa hilo pindi aliposema mnamo 7/2/2018, alipokuwa akiyahutubua majeshi ya Amerika yaliyoko katika kambi ya wanahewa ya Yokota nchini Japan “Daima tutatafuta amani. Daima tutajikakamua kwa ajili ya mustakbali bora…” (Chanzo: Reuters, 7/2/2018). Alisema haya wakati alipokuwa akijitayarisha kwenda Korea Kusini katika jaribio la kukutana na maafisa wa Korea Kaskazini chini ya kisingizio cha kuhudhuria ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi mjini Pyeong Chang, ulio na umbali wa takriban 80 Km kutoka mpaka wa Korea Kaskazini… Lakini Pence siku tatu baadaye mnamo 10/2/2018 alisema: “Hakuna mwangaza kati ya Amerika, Jamhuri ya Korea na Japan juu ya haja ya kuendelea kuitenga Korea Kaskazini kiuchumi na kidiplomasia hadi iachane na mradi wao wa kinuklia na mizinga aina ya ballistic,” (Chanzo: Al Arabiya, 10/2/2018). Hii ilipelekea Korea Kaskazini kufutilia mbali mkutano wake na Pence, yote haya yakiashiria kuwa mbinu ya kisiasa ya Kiamerika iliyo tabanniwa na Trump ni kutumia vitisho kumshinikiza mpinzani huyu wakati wa mazungumzo na mawasiliano ya kidiplomasia ili kumfanya mpinzani huyu ajisalimishe kwa yale Amerika iyatakayo. Haya pia yanathibitishwa na Mike Pompeo wakati wa kipindi chake kama mkuu ya shirika la ujasusi la Kiamerika la CIA: “Raisi ana nia ya kutoa suluhisho kupitia mbinu za kidiplomasia… Sisi pia, wakati huo huo, tunahakikisha kuwa tukitamatisha hilo halitawezekana, kwamba tunawasilisha kwa Raisi machaguo kadha wa kadha yanayoweza kufikia nia aliyoitaja”, (Chanzo: Reuters, 23/1/2018), na hivyo basi suluhisho la kidiplomasia linajumuisha machaguo mengine yanayoashiria vitisho. Inaonekana kuwa mbinu hii, vitisho wakati wa mazungumzo ya kidiplomasia, haikumfurahisha Tillerson kwa sababu ilimfedhehesha kama Waziri wa Kigeni, na hivyo basi Trump akamtimua…

3- Kwa hiyo mbinu hii haikufanya kazi kwa Korea Kaskazini, na wangesitisha majadiliano kulipokuwa na vitisho vya aina yoyote. Lau kama China haingeingilia kati, kongamano hilo lisingefanyika, hii ndio sababu Trump kufuatia kongamano na Kim wakati wa mkutano wake na waandishi habari nchini Singapore alisema, “Anamshukuru Raisi wa China Xi Jinping, kwa juhudi zake za miezi ya hivi karibuni kuwezesha kufanyika kwa kongamano hili la kihistoria” (Chanzo: AFP, 12/6/2018). China imeishinikiza Korea Kaskazini kulegeza msimamo. “Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un alifanya ziara isiyokuwa rasmi nchini China kuanzia Jumapili (25/3/2018) hadi Jumatano (28/3/2018)”, shirika rasmi la habari la Xinhua liliripoti mnamo Machi 28, ambapo lilijadili kwa kina hali ulimwenguni na bara la Korea, na Raisi wa China Xi Jinping aliwambia mwenzake wa Korea Kaskazini kwamba China imejitolea katika lengo la kuachana na silaha za kinuklia katika bara la Korea na kuhakikisha kuwepo kwa amani na utulivu pamoja na kulitatua tatizo hili kupitia mazungumzo na majadiliano. Shirika hili la habari la Korea Kaskazini liliripoti “kiongozi wake Kim Jong-un alizuru China kumpongeza kibinafsi Xi Jinping kwa tukio la kuchaguliwa tena kama raisi wa China kwa kuambatana na tamaduni za kirafiki baina ya nchi mbili hizi…” na “alionesha matumaini kuwa ziara yake nchini China itachangia kumakinika kwa amani na utulivu katika bara la Korea, akitangaza kuwa yuko tayari kwa mazungumzo na Amerika na Korea Kusini pamoja na kufanya mikutano na viongozi wao”, na akaongeza: “Kuachana na silaha za kinuklia nchini Korea kunawezekana ikiwa Washington na Seoul zitachukua hatua imara na za pamoja za kufikia amani”. Hii ndio maana Trump alitangaza katika mtandao wake wa Twitter mnamo 28/3/2018 furaha yake ya kile kilicho patikana kutokana na ziara hiyo: “Nilipokea ujumbe usiku wa jana kutoka kwa XI JINPING wa China kwamba mkutano wake na KIM JONG UN ulikwenda vizuri sana na kwamba KIM anasubiri kwa hamu kukutana nami. China iliikabidhi Amerika Korea Kaskazini kama kafara kwa maslahi yake, ikiishinikiza Korea Kaskazini hadi kumfanya raisi wake kuwa tayari kulegeza msimamo na kukutana na majivuno Trump. Hususan kwa kuwa China tayari ishawahi kuhusika katika shinikizo la kisiasa, na katika kuchukua maamuzi katika Baraza la Usalama kuweka vikwazo kwa Korea Kaskazini. Hili limekuwa jambo muhimu katika kuifanya Korea Kaskazini kuwa tayari kulegeza msimamo juu ya mradi wake wa nuklia. Inaamini kuwa endapo itakosa uungwaji mkono na usaidizi wa China na China itafanya kazi kuidhibiti na kuizuia, hapo Korea Kaskazini itateseka! Hivyo basi Korea Kaskazini imelegeza msimamo! Wizara ya Kigeni ya China imefichua kuhusu dori yake ya ushawishi katika uamuzi wa Korea Kaskazini, ikitangaza hilo “Beijing imecheza dori murua juu ya bara la Korea” (Chanzo: Reuters, AFP, 23/5/ 2018). China imeonesha kuwa iko makini katika kupata maslahi yake ya kibiashara kwa Amerika zaidi ya washirika wake ambao haipati faida za kibiashara kutoka kwao, na huenda ikadhurika kibiashara kwa sababu ya hili, hata kama ni mwandani wa kikomunisti. Wasiwasi mkubwa wa dola ya kikomunisti umegeuka kuwa biashara na sio kulinda nchi nyenginezo za kikomunisti washirika wake! Kana kwamba China haitambui kuwa Amerika, huku ikitafuta kuinyang’anya silaha Korea Kaskazini, inatumia kadhia hii kuizunguka China na kuzuia udhibiti wake wa bahari ya China Mashariki na Kusini!

4-Hili linathibitishwa na tangazo la China la kulikaribisha kongamano hili na kutangaza kuwa mshirika wake Korea Kaskazini imeachana na silaha zake za kinuklia kwa ajili ya Amerika. Balozi mkuu wa China na mshauri wa serikali, Wang Yi, alisema baada ya kongamano hilo: “Tunakaribisha na kuunga mkono matokeo yaliyo patikana katika kongamano hilo… Tunatarajia kuwa DPRK na Amerika zitafuatilia juu ya maafikiano ya pamoja yaliyoafikiwa na viongozi wao… katika kufikia kumaliza nuklia katika bara la Korea”, aliongeza, “wakati huo huo, ipo haja ya kuweko mpangilio wa amani kwa bara la Korea kutuliza hofu ya kiusalama inayohisiwa na Korea Kaskazini.” (Chanzo: Reuters, 12/6/201). Ikiwa China ilikuwa na utambuzi wa kutosha kisiasa na azma imara ya kisiasa, haingeishinikiza Korea Kaskazini, mshirika wake kwa njia hii! Lakini inathibitisha kuwa upeo wake na utambuzi wake wa kisiasa wa siasa za kimataifa bado ungali mwembamba na azma yake ya kisiasa ni dhaifu, kwa hivyo imefanya tu kwa kuchunga na kuhakikisha kuwa mahusiano yao ya kibiashara na Amerika ni mazuri kwa badali ya kuisalimisha Korea Kaskazini kwa Amerika, na wala haikuangalia mbele zaidi kwa lile ambalo hili litapelekea. Haitarajiwi kuwa Amerika inafanya kazi kuiteka Korea Kaskazini, kuileta karibu kwa ajili ya Amerika kuliko China, na kwamba Amerika inatafuta kupata umoja au muungano kati ya Korea mbili ili Korea mpya iwe nguvu ilio nje ya ushawishi wa China. Vietnam ni mfano usiokuwa wa mbali, ambayo ilikuwa hasimu kwa China baada ya Amerika kuziunganisha Vietnam Kusini na Kaskazini katika kongamano la Paris mnamo 1975!    

5- China imecheza dori muhimu katika kuifanya Korea Kaskazini kukubali mkutano wa kongamano hilo kuiweka kadhia ya kuachana na silaha za kinuklia mezani pasi na kujadili pia Amerika kuachana na silaha za kinuklia. Amerika ni nchi pekee iliyozitumia na kueneza ufisadi ardhini, lakini shinikizo la China lilikuwa na athari ya kihakika! Kwa hivyo kongamano lilifanywa… Kongamano hilo lilitarajiwa kuchukua siku mbili lakini likafupishwa kuwa siku moja na muundo mpana ukakubaliwa, unaoashiria kasi ambayo Korea Kaskazini itaitikia yale Amerika inayoyataka. Korea kaskazini iliharibu kiwanda cha majaribio ya nuklia kuthibitisha azma yake ya kuachana na mradi wake wa nuklia, pamoja na kuwaacha huru Waamerika waliokuwa gerezeni mwake. Trump alieleza furaha yake kwa kile alichofaulu: “Ni mkutano murua sana. Maendeleo ni mengi mno”. Huku Kim akilikadiria tukio hili la kihistoria alisema: “Ulimwengu utayaona mabadiliko makubwa”. (Chanzo: Reuters, 12/6/2018). Wametia saini taarifa ya pamoja iliyo na nukta nne: Kwanza: pande mbili hizi zimejitolea kuasisi mahusiano mazuri kwa mujibu wa matarajio ya watu wao ya amani na ufanisi; pili: pande mbili hizi zitafanya kazi kuasisi na kuimarisha amani ya kudumu na utulivu kwa bara la Korea. Tatu: Korea Kaskazini ni lazima ijitolee kuchukua hatua za kuachana na silaha hizo kikamilifu katika bara la Korea. Nukta ya nne ilihusishwa na upande wa kibinadamu, kuahidi kurudisha mabaki ya Waamerika waliopotea na wafungwa tangu vita vya Korea na Amerika (1950-1953). Trump aliyasifu makubaliano hayo kuwa “mapana na muhimu mno” na Kim akaahidi katika taarifa “kuachana kikamilifu na silaha hizo katika bara la Korea”. (Chanzo BBC, 12/6/2018). Taarifa hii yaashiria kuwa kuna muundo wa makubaliano, wala sio tu makubaliano juu ya nukta zinazofafanua yale yaliyoafikiwa juu yake, jinsi ya kutekeleza mpango wa kuachana na silaha hizo, mipangilio yake na muda na usimamizi wa utekelezwaji huo, na mambo mengine yanayohitajika na makubaliano hayo ambayo yaweza kutekelezwa mara moja kama ilivyokuwa katika makubaliano ya nuklia na Iran, ambayo maelezo yote haya yaliandikwa…   

6- Hivyo basi, inatarajiwa kwamba Amerika itafanya majadiliano na mazungumzo marefu na Korea Kaskazini ambayo huenda yakachukua miaka mingi. Inaonekana kana kwamba Trump alitaka kukamilisha makubaliano ya mwanzo kwa haraka na kutatua tatizo hili na Korea Kaskazini, kwa kuwa tayari alikuwa ashafanya vitisho na hangeweza kurudi nyuma isipokuwa kufaulisha kitu kitakachoonesha amefaulu katika kuidhalilisha Korea Kaskazini. Kama tulivyo sema juu, lau si shinikizo la China, vitisho vya Trump havingepelekea kufanyika kwa kongamano hili na kutiwa saini kwa tangazo la Korea Kaskazini la azma yake ya kuachana na silaha za nuklia. Hivyo basi Trump ameweka rekodi ya ushindi wa kihistoria ambao huenda ukamfanya kufaulu katika raundi ya pili ya uchaguzi wa Uraisi wa Amerika utakapofanyika miaka miwili tu ijayo na kuziba sakata zote zilizojitokeza dhidi yake ambazo mpaka sasa bado hazijamalizika, na tuhuma za kufeli na kukashifiwa na wengine kwa kiburi chake na ubwege. Hili ni dhahiri kutokana na maneno ya Trump mwenyewe: “Usiniambie kuwa nchi yake tayari inaharibu kiwanda cha majaribio ya makombora … Tutaondoa vikwazo pindi tu tutakapopiga hatua muhimu katika kadhia ya kupunguza silaha za kinuklia… Bado hatujakata tamaa na chochote katika majadiliano haya… Tutakomesha mazoezi ya kijeshi tukiilenga Korea Kaskazini. Nitaitisha mkutano ikululini White House muda muwafaka utakapo wadia”, pia alisema: “Alitia saini makubaliano ya kuachana na silaha za nuklia na UM kwa ajili ya kupunguza silaha hizo, nadhani tunao muundo wa kutayarisha upunguzaji silaha za nuklia kwa Korea Kaskazini”. (Chanzo: Al-Jazeera, 12/6/2018). Hivyo basi Trump alitaka kumaliza faili ya mzozo na Korea Kaskazini, kuonesha kuwa amepata ushindi mkubwa.  

7- Kumaliza faili ya mzozo na Korea Kaskazini au kuutuliza kunamsaidia Trump kujitolea katika vita vyake vya kibiashara na washirika wake na maadui zake! Anamahusiano tata na washirika wake pindi alipotangaza kuwa ametoza ushuru mkubwa wa forodha katika biashara zao za madini ya Steel na Aluminium kutoka nje kuingia nchini mwake, ikizingatiwa kuwa makubaliano yao ya kibiashara yaliyotangulia yalikuwa na ubaguzi, aliandika katika mtandao wa Twitter mnamo 8/6/2018 alipokuwa akielekea katika kongamano la nchi kuu saba zenye uwezo mkubwa duniani (G7) jijini Quebec, Canada: “Akitarajia kuimarisha mikataba ya kibaguzi ya kibiashara na nchi hizo za G-7. Ikiwa hilo halitatokea, tutajitokeza vizuri zaidi!” Raisi wa Ufaransa Macron, na Waziri Mkuu Justin Trudeau, walizungumza katika mkutano wa pamoja wa waandishi habari wakikataa hatua hizi. “Hawako tayari kukubali kila kitu ili kutoa taarifa ya pamoja na Amerika”, (Chanzo: AFP, 6/6/2018) Trump aliituhumu Ufaransa na Canada kutoza ushuru mkubwa kwa bidhaa za Amerika na kumtuhumu Waziri Mkuu wa Canada Trudeau kuwa “msumbufu”.  

“Kutakuweko na tofauti kubwa juu ya kadhia nyingi”, afisa wa Canada aliwaambia maripota jioni ya Juni 7, 2018 (Chanzo: Reuters, 8/6/2018). Hata Raisi wa Ufaransa Macron, aliyefanya kazi juu ya maridhiano ya Kifaransa na Kiamerika, hakuweza kujimudu na kuendelea kutembea na Amerika na kuficha upinzani wake halisi, ambapo Ufaransa haikubobea kama Uingereza. Macron alisema: “Wanachama wengine sita wa G7 huenda wakaunda kundi lao wenyewe ikiwa kutakuwa na umuhimu”, aliongeza kumkashifu Trump “Hakuna kiongozi anayedumu milele”. (Chanzo: Reuters, 8/6/2018) Ujanja wa Uingereza ulijitokeza pindi Uingereza ilipotaka kuonesha kuwa haikubaliani na hisia hizi ili kudumisha mahusiano yake na Amerika huku ikichochea wengine dhidi yake. Waziri Mkuu May aliwaambia maripota: “Anataka Muungano wa Ulaya kujizuia kutokana na hisia zake dhidi ya ushuru wa Kiamerika na kwamba hisia hizi zapaswa kuwa za kisawa na halali” (Chanzo: Reuters, 8/6/2018). Chansela wa Ujerumani alisema katika mahojiano na runinga ya Ujerumani ya ARD mnamo 10/6/2018 juu ya uamuzi wa Trump wa kuondoa saini yake: “Kwa kweli, kuondoa huko, kupitia kuandika katika mtandao wa Twitter ni kwa kihakika na kwa kiasi fulani kuna vunja moyo, lakini huo sio mwisho”. Waziri wa Kigeni wa Ujerumani Haiku Maas aliandika katika mtandao wa Twitter katika kujibu ufidhuli wa Trump, “kunaangamiza kiwango kikubwa sana cha imani”. Uhasama huu unaolizunguka kongamano la G7 nchini Canada ulimazikia kwa kushambuliwa Trump na viongozi wa nchi nyenginezo zinazoshiriki kongamano hilo. Trump aliondoa saini yake katika taarifa ya pamoja ya kongamano la G7 na kumtuhumu Waziri Mkuu wa Canada aliyeongoza kongamano hilo kuwa “tapeli na dhaifu” (Chanzo: AFP, 10/6/2018). Trump aliwasili kwa kuchelewa katika kongamano hilo na kuondoka kabla ya kumalizika kwa kongamano hilo. Hivyo basi inaonekana kana kwamba vita vya kibiashara vimeanza, na vilitangazwa na Trump mnamo 2/3/2018 alipoandika katika mtandao wa Twitter: “Pindi nchi (Amerika) inapopoteza mabilioni ya dolari katika biashara na karibu kila nchi inayofanya nayo biashara, vita vya kibiashara ndio huwa bora, na rahisi kushinda”. Yote haya yaonesha kuwa faili la vita hivi vya kibiashara ni muhimo mno kwa Amerika, huku ikiendelea kuteseka kutokana na matunda ya mgogoro wa kifedha uliolipuka mnamo 2008 huku madeni yakifikia zaidi ya dola trilioni 20, na Raisi Trump ambaye akili yake imetawaliwa na biashara anafanya kazi kuuokoa uchumi wa Amerika, akinyanyua mwito wa “Amerika kwanza”. Hili linatishia kuvunjika kwa taasisi za kimataifa zilizotumiwa na Amerika tangu jadi kulazimisha ushawishi wake wa kiulimwengu na hivyo pasi kuvunjika kwa mfumo wa kiulimwengu na kuibuka kwa msimamo mpya wa kimataifa, ambapo Amerika haijitolei tena muhanga ili kubakia kuwa dola inayoongoza duniani, kwa usaidizi wa nchi nyenginezo na uvumilivu kupitia kuifanya mizani ya kibiashara kuwa upande wake, lakini inajali ubwana pekee pamoja na faida ya kibiashara pasi na usaidizi kutoka kwa washirika wake ili kuwaweka chini ya mwavuli wake na kutembea nyuma yake.  

8- Amerika haijifungi na makubaliano yoyote na upesi hujiondoa au kuyatupilia mbali pindi inapo amini kuwa maslahi yake yanahitaji kujiondoa na kuvunja makubaliano hayo. Ilifanya hivyo kwa Korea Kaskazini mnamo 2003 chini ya George W. Bush, mwana, na kujiondoa kutoka katika makubaliano ya 1994 yaliyotiwa saini na Bill Clinton. Raisi wake wa sasa, Trump, alitia saini taarifa ya pamoja na washirika wake katika kongamano la G7 nchini Canada na kisha kuvunja makubaliano yake na kuondoa saini yake siku moja baadaye. Alivunja mkataba wa nuklia wa Iran uliotiwa saini na nchi yake chini ya Obama mnamo 2015. Makubaliano haya na Korea Kaskazini hayana dhamana na itatishia kuyavunja ili kuishinikiza Korea Kaskazini kuyatekeleza pindi majadiliano juu yake yanapoanza, kila inapopinga au kukataa kipengee chochote chake!

Uvunjaji mikataba na kiburi na kujiona tofauti na wengine na kuwatenza nguvu wengine yamekuwa ndio sifa ya kudumu ya Amerika, na yote haya ni nukta za kuporomoka, hivi karibuni… dola ya Khilafah Rashida itarudi kuwa ndio dola ya kwanza inayoongoza, kwa idhini ya Allah, kusimamisha uadilifu na kudumisha ahadi na kueneza uongofu na kutekeleza haki na kuondoa batili ikileta kheri kwa wanadamu na watu kuishi kwa usalama na amani katika nyanja zote. Mtume wa Allah (saw) ametoa bishara njema ya kurudi kwake baada ya utawala wa kiimla:

«ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ»“kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume”, imesimuliwa na Ahmad kutoka kwa Hudhayfah (ra), na hili ni jepesi kwa Allah kulitimiza.

2 Shawwal 1439 H

Jumamosi, 16/6/2018 M

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 02 Aprili 2020 21:16

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu