Watoto kumi na tano wasio na makao, wengi wao wakiwa wachanga, wamekufa nchini Syria kutokana na baridi kali na ukosefu wa matibabu, kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF mnamo Jumanne 15/1/2019. Watoto, 13 kati yao walio chini ya umri wa mwaka mmoja, walifariki katika kambi ya Al-Rukban kusini mashariki mwa Syria, karibu na mpaka wa Jordan. Al-Rukban na kambi nyenginezo zinakumbwa na uhaba mkubwa sana wa misaada ya kibinadamu, pindi wakimbizi wanapowasili baada ya safari nzito baada ya kukimbia ngome ya mwisho ya ISIS mashariki mwa nchi hiyo. Geert Cappelaere, mkurugenzi wa UNICEF wa eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, alisema “Baridi kali zaidi na hali mbaya za maisha katika Al-Rukban zimesababisha maisha ya watoto kuongezeka kuwa hatarini,” aliongeza, “Kwa mwezi mmoja tu, kwa uchache watoto wanane wamekufa – wengi wao wakiwa chini ya umri wa miezi minne, na mdogo wao zaidi akiwa umri wa saa moja.”