Jumapili, 26 Rajab 1446 | 2025/01/26
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Kuwa na Pupa katika Kukimbilia Radhi za Mwenyezi Mungu (swt)

Muumini huzingatia suala la kujitahidi kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu (swt) kwa kufanya pupa. Muumini yuko mbali na kutokuwa na ufanisi, uzito wa maisha ya utawa, kujinyima anasa za mwili na ushirikina katika kumuabudu Mwenyezi Mungu (swt). Muumini husifika na mabadiliko ya kusisimua, pupa ilio kubwa, uwajibikaji wa umakini, nidhamu thabit na tija yenye kuongezeka. Sifa hizi pambanuzi ni matokeo ya kukimbilia radhi za Mwenyezi Mungu (swt), kuyapenda yale ambayo Yeye (swt) anayapenda kwa ajili ya wanaadamu, kuchukia yale ambayo Yeye (swt) anachukizwa nayo kwa waja Wake, ufahamu wa ukaribu wa kifo, utambuzi wa kuhisabiwa na Mwenyezi Mungu (swt) na shauku ya hamasa ambayo kila wakati hutolewa katika hali ya utumishi mzuri kwa Mwenyezi Mungu (swt).  Wingi wa waumini kama hao ndio umewezesha Ummah wa Kiislamu kupanda juu ya tamaduni nyengine katika mafanikio kwenye nyanja zisizohesabika, kuzalisha wingi mkubwa wa aina tofauti za hisabati, kuweka misingi kwa kiasi kikubwa ya kile kinachojulikana leo, katika nyanja mchanganyiko kama ushindi wa kijeshi, sheria, madawa, uhandisi, ujenzi na fasihi. Waumini kama hao walifanikisha kumbukumbu muhimu katika maeneo zaidi ya moja, katika umri mdogo, kutokana na kusadikisha kwao Dini tukufu ya Uislamu, wakajifunga nayo kabisa katika chaguo la maisha yao, aina ya maisha, maadili na tabia. Urithi wa Kiislamu umejaa aina hiyo ya waumini walioacha alama yao maridhawa isiosahaulika katika dunia, pamoja na mrundo wa mambo mema walioandikiwa kwa ajili ya Akhera.

Aliye juu zaidi ya wote aliyeishi kwa Uislamu, ni mbora zaidi wa walimwengu wote, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), ambaye kwa kipindi cha miongo miwili tu amebadilisha mkondo wa wanaadamu tokea aipe heshima Dunia hii kwa uwepo wake. Katika kipindi kimoja kifupi cha maisha, ameanzisha misingi ya Ummah mkubwa ambao utaishi hadi Siku ya Hukumu, utakaotawala dunia yote kwa utaratibu wa Dini ambayo Yeye (saw) ameileta na utakuwa ndio Ummah pekee mkubwa zaidi ya Ummah wa Mtume yeyote katika Siku ya Hukumu. Katika thuluthi moja ya kipindi chake cha maisha, Ameweza kufanikisha kile ambacho vizazi vya imani nyengine na mifumo havikuweza kufanikisha, kwani alikuwa ni mfano halisi wa Uongofu, inayomuongoza kuwa Bwana wa Manabii wote (as), Imamu wa Mitume wote (as) na mtukufu zaidi ya wanaadamu wote.

Ni wahyi mtakatifu, Quran na Sunnah, ambavyo pekee ndivyo vyenye kuongoza akili, vyenye kuhuisha moyo na kutia nishati viungo. Mtu anayeulea moyo wake kwa Uislamu anahuika na kustawi, wakati yule anayejitenga na Dini ya Haki hunyauka kama tawi lililo wazi, lisilo na mizizi wala maisha. Wahyi mtakatifu hutakasa moyo kutokana na tabia ya uvivu, kupoteza muda, kutokuwa na lengo, kukwepa taklifu na kuchukia usumbufu, yote haya huzuia muitiko wa wito wa Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume Wake (saw).

Hakika, Muumini hulazimishwa na maneno ya Mwenyezi Mungu (swt) kwa kuwa na pupa katika kukimbilia radhi za Mwenyezi Mungu (swt). Mwenyezi Mungu (swt) amesema,

  [وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ]

“Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyowekwa tayari kwa wachamungu.” [Surah Aali Imran 3:133]. Kwa kufaidika na Tafsiri mashuhuri, imeelezwa kuwa Al-Qurtubi amefasiri, “Kufanya haraka na kuchukua hatua, ambayo ni mjibizo… yaani, wanafanya haraka kwa yale yanayowajibisha msamaha, ambayo ni utiifu (twa’ah). Anas bin Malik na Makhoul wamesema katika Tafsiri ya

[وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ]

“Na yakimbilieni maghfira.” Ina maana ya takbira ya ufunguzi (wa swalah)’ Ali bin Abi Talib (ra) amesema, ‘Kutekeleza mambo ya wajibu (faraa’idh).’ Uthman bin Affan (ra) amesema, ‘Kuwa Mwaminifu.’ Al-Kalbi amesema, ‘Kutubia kutokana na riba.’ Na pia imesemwa, ‘Kuwa imara katika mapigano.’ Na mbali ya haya pia yamesemwa. Na aya yote imekuja kwa ujumla. Maana yake zaidi ni kwenye matendo mema yanayo tangulizwa. Al Baghawi amesema kuwa, ‘Abdullah bin Abbas (ra) amesema, ‘Kwa Uislamu,’ As-Sa’di amefasiri kuwa, “Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaamrisha kufanya pupa kwa ajili ya kutaka msamaha wake na kufanikisha kuipata Pepo Yake, ambayo upana wake ni wa mbingu na ardhi, basi upi urefu wake, ambao Mwenyezi Mungu (swt) ameuandaa kwa waja wema, kwani wao ni watu wake na matendo ya ucha Mungu yamewaelekeza huko.”

Hakika, Muumini ni imara, huyajaza maisha yake kwa matendo mema, hakatai fursa za kutenda mema na kutengeneza mazingira ambayo yatamuwezesha kutenda mema zaidi. Mwenyezi Mungu (swt) amesema,

[فَاسْتَبِقُوا الْخَيْرَاتِ]

“Basi shindanieni mema” [Surah al-Baqarah 2:148]. Katika Tafsiri yake, as-Sa’ad amesema, “Maamrisho ya kutarajia katika kutenda mema yako juu zaidi ya maamrisho ya kutenda mema. Hii ni kwa sababu matarajio kwao yanahusisha kuyatekeleza, kuyakamilisha, kuyatumia kwa hali zote na kuchukua hatua kuhusiana nayo. Yeyote anayetangulia katika dunia hii kwa matendo mema, basi Akhera hutangulia Peponi, hivyo wa kwanza kabisa ndiye wa juu zaidi katika viumbe. Matendo mema yanajumuisha matendo ya Wajibu (faraa’dh) na yanayopendekezwa (Nawaafil), kama Swalah, Funga, Zakat, Hajj, Umrah, Jihad…” At-Tabari ameelezea, “Abu Jaafar amesema, ‘Ina maana Mwenyezi Mungu Mtukufu amemtaja kwa kusema: ‘Hivyo tumainia’ na kwa hivyo wanachukua hatua na kuwa na pupa, ambayo ni ya matumaini, ambayo ni kuchukua hatua (mubaadarah) na haraka.”

Kama Mwenyezi Mungu (swt) alivyoteremsha katika Quran umuhimu wa kuwa na pupa, uchukuaji hatua na kuwa na kasi katika matendo mazuri, Yeye (swt) pia ameteremsha kama hivyo kupitia Sunnah za Mtume (saw). Hivyo katika Sunnah Tukufu, kuwa na pupa kunaeleweka kutokana na tamko la Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), aliyesema,

«بَادِرُوا بِالْأَعْمَالِ فِتَنًا كَقِطَعِ اللَّيْلِ الْمُظْلِمِ يُصْبِحُ الرَّجُلُ مُؤْمِنًا وَيُمْسِي كَافِرًا أَوْ يُمْسِي مُؤْمِنًا وَيُصْبِحُ كَافِرًا يَبِيعُ دِينَهُ بِعَرَضٍ مِنْ الدُّنْيَا»

“Fanyeni haraka katika kufanya amali njema (kabla hamjakumbana) na fitna ambayo ni kama sehemu ya usiku wa kiza. Mtu atapambaukiwa hali ya kuwa muumini na jioni kuwa kafiri, au atakuwa muumini jioni na asubuhi kuwa kafiri, anauza dini yake kwa bidhaa za dunia.” [Muslim]. Katika Sunnah Tukufu, kufanya pupa kumeonekana katika matendo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) mwenyewe. Al-Bukhari amepokea kutoka kwa ‘Uqba kuwa amesema, “Niliswali ‘Asr nyuma ya Mtume (saw) Madina. Alipomaliza na kutoa salamu, alinyanyuka kwa haraka na kukata safu za watu hadi kwenye chumba cha mmoja wa wake zake. Watu walishtuka kwa haraka zake. Mtume (saw) aliporudi na kuwaona watu wamefadhaika kutokana na haraka zake akawambia,

«ذَكَرْتُ شَيْئًا مِنْ تِبْرٍ عِنْدَنَا فَكَرِهْتُ أَنْ يَحْبِسَنِي، فَأَمَرْتُ بِقِسْمَتِهِ»

“Nilikumbuka kipande cha dhahabu tulichokuwa nacho ndani nikachukia kisije kunishughulisha, hivyo nimeagiza kigawanywe (kuwa ni sadaka).” Hii inaonyesha namna Waislamu wanavyotakiwa wakimbilie katika kutekeleza kile ambacho Mwenyezi Mungu (swt) amewajibisha juu yao.

Kutokana na mwangaza wa Sunnah, uharaka umeonekana kutiwa msukumo na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwa Waumini. Muslim amepokea kuwa Anas (ra) ameeleza, ‘Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na Masahaba wake walifika Badr kabla ya makafiri, na walipofika, yeye (saw) aliwaelekeza,

«لَا يُقَدِّمَنَّ أَحَدٌ مِنْكُمْ إِلَى شَيْءٍ حَتَّى أَكُونَ أَنَا دُونَهُ»

“Asinitangulie yeyote kati yenu kwenye jambo.” Makafiri walipokaribia, Mtume (saw) alisema,

«قُومُوا إِلَى جَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَوَاتُ وَالْأَرْضُ»

“Simameni kuielekea Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi.” “Umair bin Al-Humam (ra) aliuliza, “Pepo upana wake ni kama mbingu na ardhi?” Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akajibu,

«نَعَمْ»‏

“Ndio” “Umair akasema, “Vizuri” Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akamuuliza, “Ni lipi limekupelekea wewe useme hivyo,” Akasema, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakuna isipokuwa ni matarajio ya kuwa niwe mmoja wa watu wake.” Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema,

«فَإِنَّكَ مِنْ أَهْلِهَا»

“Hakika wewe utakuwa miongoni mwa watu wa humo.” ‘Umair akatoa tende kutoka kwenye ala (ya kuweka mishale) yake, na akawa anakula, kisha akasema: "iwapo nitakuwa hai mpaka nimalize kula tende zangu hizi itamaanisha maisha marefu." Hivyo akazitupa tende alizokuwanazo mkononi, kisha akapigana na adui mpaka akauwawa”.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ameweka msingi wa kizazi cha makamanda wakubwa wa kijeshi na wanasiasa ambao wamebadilisha mkondo wa ubinaadamu pamoja naye. Baada yake (saw), kizazi hiki kilichobarikiwa kimeendeleza ujumbe wake kwa kuubeba Uislamu kwa wanaadamu wote. Ni kizazi hiki cha mwanzo, kizazi kilicho bora zaidi ambacho ni kiigizo kwa vizazi vyote. Hivyo, mwanasiasa anayetaka kuipeleka Dawah ya Uislamu, kuufanya Uislamu kuwa msingi kwa jamii hivi leo, kuiweka fikra ya Uislamu katika kusafisha mazingira ya Ulimwengu wa Kiislamu, hukumbuka mfano wa Maswahaba (ra) walioingia katika jamii ya Maquraysh kutoka Dar ul Arqam kwa nguvu na juhudi ambazo kwazo, nuru ya uongofu ilihisiwa Bara Arabu yote kwa muda mfupi tu. Hivyo, afisa wa jeshi mwenye shauku ya kukomboa ardhi na kufungua ardhi mpya kwenye Uislamu, humkumbuka Khalid bin Walid (ra), Upanga wa Mwenyezi Mungu (swt). Usiovunjwa na makafiri katika vita vyovyote, ilisemwa kuhusu Khalid (ra) kuwa, “hakulala wala hakuwaacha wengine kulala, na hakuna kilichofichikana kwake.” (at-Tabari: Vol. 2, p.626).

Kwa hakika Muumini anapolelewa kwa utajiri wa thaqafa ya hadhara ya Kiislamu, hulazimika kujitahidi kufanya pupa kwa ajili ya radhi za Mwenyezi Mungu (swt). Huwa mwenye nidhamu na mwenye kuaminika. Hapotezi wakati, hajichoshi katika kufuatilia mambo yasio na maana. Atatekeleza majukumu yake yote, ima iwe Swalah, Zakah au kuingia vitani au kuamrisha mema na kukataza maovu katika namna ilio bora. Hatojiingiza katika mijadala isio na maana, bali kwenye ile yenye faida. Ataiweka nyumba yake kwenye utaratibu, atazipangilia shughuli zake ili kurahisisha uendeshaji wa Dawah kwenye Uislamu. Atajinyima matamanio yake ya kidunia, ili aweze kujitahidi kwa ajili ya matamanio ya Akhera. Atakamilisha matendo yake kwa utimilifu na hatoridhika mambo kuwa kama yalivyo.

Zaidi ya hayo, kile kinachomtafautisha Muumini kutokana na wanaozaliwa na imani nyengine zote na njia za maisha, ni lengo kwa ajili ya jitihada na pupa yake. Kwa hakika, hatopumbazwa na hadhara ya Kimagharibi kwa uzalishaji wake, bali hushtushwa kwa muelekeo wake mzima, kukosekana utiifu na uasi kwa Mwenyezi Mungu (swt). Mwenyezi Mungu (swt) amesema,

     [الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا]

“Ni wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kwamba wanafanya kazi nzuri.” [Surah al-Kahf 18:104]. Hivyo uoni wake hautodumazwa na manufaa ya kimada, majivuno na hadhi katika Dunia hii ya kupita. Uoni wake hutanuka kwa hamu yake ya kutaka Pepo, ambayo mapana yake ni ya mbingu na ardhi, basi ni upi urefu wake. Uoni wake huamuliwa kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu (swt) ameamua kuwa ni kitendo chema na vitu halali. Hutaka radhi za Mwenyezi Mungu (swt) na kuepuka kile ambacho kinaleta Hasira Zake na Adhabu. Moyo wake ni mzito wa kubeba maafa makubwa ya Ummah kutokana na kukosekana kwa Uislamu na kuangazwa kwa imani ya kina kuwa Mwenyezi Mungu (swt) Pekee ndiye Bwana wa Mambo Yake. Hafikirii chengine isipokuwa kuitoa muhanga afya yake, utajiri na muda kwa ajili ya kuiendeleza zaidi Dini katika ardhi. Midomo yake hulainishwa kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu (swt) na macho yake huwa na machozi kwa kilio kwa ajili ya kumkhofu Mwenyzi Mungu (swt). Miguu yake imechoka na yenye maumivu kutokana na kisimamo cha usiku na mchana wenye hatua ndefu za juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (swt). Hivyo, kwa ajili ya mafanikio ya kweli na neema, basi na wajitahidi wenye kuamini! Mwenyezi Mungu (swt) amesema,

  [إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۚ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ وَمَن يُطِعِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَيَخْشَ اللَّهَ وَيَتَّقْهِ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ]

“Haiwi kauli ya Waumini wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumetii. Na hao ndio wenye kufanikiwa.” [Surah An-Nuur 24: 51-52].

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Musab Umair - Pakistan

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 06 Disemba 2020 12:12

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu