Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Vipi Khilafah Itakavyo Hifadhi Haki za Kisiasa za Wanawake

  • Uislamu huwawajibisha wanawake kuwa na dori changamfu katika siasa za mujtama wao: kuchunga mambo ya Ummah wao, kuzungumza dhidi ya ukandamizaji na ufisadi, kuamrisha mema (Ma’ruf) na kukataza maovu (Munkar), na kuwahisabu watawala wao. Dalili za Kiislamu zinazo waamrisha Waislamu kuwa wachangamfu katika siasa zinawahusu wanaume na hali kadhalika wanawake.

(وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ)

“Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi …” [At-Taubah: 71]

Mtume (saw) amesema,

كَلاَّ وَاللَّهِ لَتَأْمُرُنَّ بِالْمَعْرُوفِ وَلَتَنْهَوُنَّ عَنِ الْمُنْكَرِ وَلَتَأْخُذُنَّ عَلَى يَدَىِ الظَّالِمِ وَلَتَأْطُرُنَّهُ عَلَى الْحَقِّ أَطْرًا وَلَتَقْصُرُنَّهُ عَلَى الْحَقِّ قَصْرًا

“Hapana, Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, hamutaacha kuamrisha mema na hamutaacha kukataza maovu, na wala hamutaacha kuzuia mikono ya dhalimu, na wala hamutaacha kumlazimisha juu ya haki na kumfunga sawa sawa na haki, isipokuwa Mwenyezi Mungu atazigonganisha nyoyo za baadhi yenu dhidi ya wengine, na atawalaani kama alivyo walaani wao.” [Abu Dawud]

  • Wanawake wana haki sawa za kisiasa kama wanaume chini ya Khilafah.

 “Raia wote wa Dola watatendewa usawa bila ya kujali dini, jinsia, rangi au jambo jengine lolote. Dola imeharamishwa kubagua miongoni mwa raia wake katika mambo yote …” (Kifungu cha 6, Kielelezo cha Katiba ya Al Khilafah cha Hizb ut Tahrir)

  • Kuhisabu na uwazi ni nguzo msingi za utawala wa Kiislamu. Hivyo basi Khilafah itawapa wanawake njia kadha wa kadha ili kutoa malalamishi dhidi ya dola au kumhisabu mtawala. Itawarahisishia na kuwashajiisha katika kudhihirisha rai zao za kisiasa. 

 “Kuwataka watawala kuhisabiwa kwa vitendo vyao ni haki kwa Waislamu pamoja na faradhi ya kutoshelezana (fardh kifaayah) juu yao.” (Kifungu cha 20, Kielelezo cha Katiba ya Al Khilafah cha Hizb ut Tahrir)

  • Nidhamu ya Kiislamu inawapa wanawake haki ya kuchagua wawakilishi wao na Khalifah. Hakika, Uislamu ndio nidhamu ya kwanza ulimwenguni kuwapa wanawake wake haki ya kuchagua kiongozi wao.

Wanawake wawili – Nusaybah bint Ka’ab Umm ‘Amarah na Asma bint Amr ibn Adi – walikuwa ni miongoni mwa ujumbe wa Waislamu wa Yathrib katika Bay’ah ya Pili ya Al-Aqaba. Hii ilikuwa ahadi ya usaidizi wa kisiasa na ulinzi wa kijeshi aliopewa Mtume (saw), wakimkubali kama kiongozi wa dola yao.

Pindi Amr bin Al-‘As (ra) alipokuwa akishauriana na raia wa Khilafah juu ya ni nani wanayempendelea kuwa kiongozi wao baada ya kifo cha Khalifah Umar bin Al-Khattab (ra), alitafuta maoni ya wanawake na wanaume vile vile.

“Mwanamke anaweza kuwachagua wanachama wa baraza la Ummah, na yeye mwenyewe kuwa mwanachama wake, na anaweza kushiriki katika uchaguzi wa Kiongozi wa Dola na kumpa ahadi ya utiifu (bay’ah).” (Kifungu cha 115, Kielelezo cha Katiba ya Al Khilafah cha Hizb ut Tahrir)

  • Chini ya Khilafah wanawake wanaweza kuwa wanachama wa vyama vya kisiasa, kutoa maoni yao katika vyombo huru vya habari, kuwa waandishi habari au kuasisi vyombo vya habari pasi na haja ya leseni.  
  • Wanawake watakuwa na haki ya kuchagua wawakilishi wa Baraza la Wilaya (Majlis Al-Wilayah) au Baraza la Ummah (Majlis Al-Ummah) yanayo shauri na kuhisabu mawali na Khalifah katika mambo yote ya dola.

“Kila raia wa Dola ana haki ya kuwa mwanachama wa Baraza la Ummah (Majlis al-Ummah), au Baraza la Wilaya … Hii ni kwa Muislamu na asiyekuwa Muislamu.” (Kifungu cha 107 Kielelezo cha Katiba ya Al Khilafah cha Hizb ut Tahrir)

  • Katika Uislamu, maoni ya kisiasa ya wanawake huthaminiwa.

Mtume (saw) alitafuta ushauri na kuchukua ushauri wa mkewe Umm Salamah (ra) alipokabiliwa na mgogoro mbaya wa kisiasa katika Mkataba wa Hudaibiyah.

Umar bin Al-Khattab (ra), Khalifah wa pili wa Uislamu alikuwa akiwakusanya wanaume na wanawake msikitini na kutafuta rai zao juu ya mambo kadha wa kadha. Pia angetafuta ushauri wa mwanamke anayeitwa Al-Shifa bint Abdullah juu ya mambo kadha wa kadha ya kisiasa kutokana na maarifa yake na upeo wake wa ufahamu, aghlabu akifadhilisha rai zake juu ya wengine.

Katika jumuiko moja la umma wakati wa utawala wa Umar bin Al-Khattab (ra) alipokuwa akiwaamrisha watu kutoweka viwango vya juu vya mahari katika ndoa, mwanamke mmoja ajuza alipambana na Khalifah wazi wazi katika rai zake, akipaaza sauti, “Umar! Huna haki ya kuingilia katika jambo ambalo Mwenyezi Mungu (swt) tayari ashalipitisha katika Qur’an”, akisoma ayah katika Surah An-Nisa, ayah ya 20 ili kuthibitisha hoja yake. Khalifah huyo akajibu, “Mwanamke huyu yuko sahihi na Umar amekosea”, na akaondoa amri yake.

Nafisa Bint Hasan alikuwa mwanachuoni maarufu wa karne ya 9 nchini Misri chini ya Khilafah ya Abbasiya. Alihusika pakubwa katika siasa za mujtama wake kiasi ya kuwa pindi watu walipokuwa na mizozo na wali wa Misri wangemtaka kutatua hali hiyo na kuhakikisha kupatikana kwa haki zao.

  • Khilafah itawawezesha wanawake kuchukua malalamishi dhidi ya watawala au maafisa wa dola hadi Mahakama ya madhalim (Mahkamat ul-Madhalim), mahakama maalumu inayo chunguza utepetevu au dhulma katika utawala, ikiwaruhusu wanawake kuwahisabu waziwazi watawala wao bila ya hofu.

“Kadhi wa Mahakama ya Madhalim huteuliwa ili kuondoa vitendo vyote vya dhulma, vinavyofanywa na Khalifah, (ma)wali au afisa yeyote wa Dola, ambavyo vimetendewa yeyote …” (Kifungu cha 87, Kielelezo cha Katiba ya Al Khilafah cha Hizb ut Tahrir)

Ma’moon Ar-Rashid, mmoja wa Makhalifah wa Abbasiya, alikuwa akitenga siku za Jumapili kwa ajili ya hadhara ya umma ili kusikiza malalamishi yao. kuanzia asubuhi mapema hadi mchana, kila mmoja – wanaume na wanawake – walikuwa huru kuwasilisha malalamishi yao kwa Khalifah ambayo yalishughulikiwa mara moja.  Siku moja mwanamke mmoja ajuza masikini alilalamika kuwa mtu mmoja dhalimu amempokonya mali yake. “Mtu huyo ni nani?” Khalifah aliuliza. “Ameketi ubavuni mwako,” mwanamke huyo ajuza akajibu, akimulekezea mtoto wa Khalifah, Abbas. Abbas akajaribu kutetea kitendo chake kwa sauti ya kusitasita huku mwanamke huyo ajuza akiendelea kupaza sauti katika manung’uniko yake. Khalifah akataja kuwa ni kutokana na ukweli wa kesi yake uliomfanya (mwanamke huyo) kuwa mkakamavu na kutoa uamuzi kwa manufaa yake.

  • Kwa mujibu wa nass za Kiislamu, mwanamke hawezi kuwa mtawala katika Khilafah lakini hili kwa vyovyote vile kamwe haliingilii uwezo wake wa kujihusisha kikamilifu katika siasa za mujtama wake. Fauka ya hayo, Uislamu hautazami kuwa mtawala kama haki ya au fadhila bali jukumu kubwa lililofungamana na hisabu nzito kesho Akhera. Lakini mwanamke anaweza kuwa afisa au mwakilishi wa dola katika wadhifa usio wa kiutawala, kama vile mkuu wa kitengo au msemaji.

لَمَّا هَلَكَ كِسْرَى سَأَلَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ‏«مَنِ اسْتَخْلَفُوا؟»‏ قَالُوا: بِنْتَهُ.قَالَ: «لَنْ يُفْلِحَ قَوْمٌ وَلَّوْا أَمْرَهُمُ امْرَأَةً

Pindi Kisra alipokufa, Mtume (saw) aliuliza: “Ni nani aliyechukua wadhifa wake?” wakasema: binti yake. Akasema: “Watu wanaomtawalisha mwanamke mambo yao kamwe hawatafaulu.”

“Raia yeyote wa dola, mwanamume au mwanamke, Muislamu au asiyekuwa Muislamu, aliye na uwezo stahiki aweza kuteuliwa kama mkuu au mtumishi wa umma wa idara, halmashauri au kitengo chochote.” (Kifungu cha 98, Kielelezo cha Katiba ya Al Khilafah cha Hizb ut Tahrir)

“Inaruhusiwa kwa mwanamke kuteuliwa katika nyadhifa za utumishi wa umma na mahakama isipokuwa Mahakama ya Madhalim.” (Kifungu cha 115, Kielelezo cha Katiba ya Al Khilafah cha Hizb ut Tahrir)

  • Hivyo basi Khilafah inasimama kama mwakilishi wa kweli wa haki za kisiasa za wanawake. Itawawezesha kujihusisha kisiasa kikamilifu katika mujtama, ambapo wamenyimwa hilo kwa muda mrefu chini ya tawala za kiimla na nidhamu zilizotungwa na binadamu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Dkt. Nazreen Nawaz

Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 26 Aprili 2020 10:46

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu