Jumapili, 26 Rajab 1446 | 2025/01/26
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Mpango Kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Umbile la Kiyahudi
ni Zao la Mfumo wa Kimagharibi Litakalowadhuru Ndugu Zetu wa Palestin

Mnamo tarehe 13 Agosti 2020, ‘Israel’ na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zilikubaliana juu ya Mkataba wa Abraham (Abraham Accord). Inategemewa kuwa nchi mbili hizi zitautia saini mkataba huu wa amani nchini Amerika mwezi huu. Makubaliano hayo yanapongezwa kuwa ni ya mafanikio. Amerika, kama ilivyotarajiwa, inayaunga mkono huku Trump akiandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa ni ‘Mafanikio Makubwa’. Na Kelly Craft, Balozi wa Amerika katika Umoja wa Mataifa ameuita “ushindi mkubwa” kwa Raisi Trump na kwa ulimwengu, akisema kuwa mshikamano wa kisiasa unaonyesha “namna tulivyo na kiu ya amani katika hii dunia”.

Maelezo ya Makubaliano Hayo

Mpanga huu unaifanya Imarati kuwa dola ya tatu ya Kiarabu kulitambua umbile la Kiyahudi baada ya Misri mwaka 1979 na Jordan mwaka 1994. Wakati kuitambua hakupelekei mahusiano ya kidiplomasia baina ya umbile la Kiyahudi na Misri au umbile la Kiyahudi na Jordan, inategemewa hilo kutokea baina ya umbile la Kiyahudi na Imarati. Makubaliano yanaangazia juu ya utalii, biashara, teknolojia, na nyanja  nyengine zisizokuwa za kijeshi.

Yataiwezesha Imarati:

* Kuendeleza mafungamano ya biashara, diplomasia na usalama pamoja na umbile la Kiyahudi huku ikidai kuwa inawasaidia Wapalestina kwa kuifanya Israel kusitisha uunganishaji (sehemu ya Palestina na Israel)

* Kuwepo uwezekano wa kuondoa kizuizi cha kupata silaha za Amerika, kama droni za kisasa na hata ndege za F-35

* Kuweza kukabiliana na hasara ya mauzo ya ndani kutokana na vifungu vya mkataba kwa msaada wa sasa wa Amerika.

Yataliwezesha umbile la Kiyahudi:

* Kupata mshirika “aliye na mfuko ulionona na utawala wa kiimla unaofanya maamuzi ya haraka juu ya ununuaji wa silaha” (Kwa mujibu wa kitengo cha ulinzi cha umbile la Kiyahudi).

* Uwezekano wa kupata mahusiano ya kidiplomasia na mataifa mengine ya Kiarabu (kuyawezesha kuidhibiti Palestina)

Athari juu ya Palestina

Moja ya wasiwasi mkubwa ni athari ya mpango huu juu ya Palestina. Kuna uoni mwingi tofauti katika taarifa zinazohusiana na athari itakazozipata kwa mpango wa umbile la Kiyahudi kuunganisha Ukingo wa Magharibi. Wakosoaji wanahoji kwamba mpango huo unaonyesha namna Imarati ilivyo wasaliti Wapalestina na haki yao juu ya ardhi hiyo. Waungaji mkono wanaashiria kuwa umbile la Kiyahudi limekubali kusitisha majaribio yake ya kuliunganisha na Ukingo wa Magharibi – japokuwa haiko wazi iwapo jambo hili ni la muda au la kudumu. Inapo angaliwa athari na uhalisia wa makubaliano baina ya Imarati na umbile la Kiyahudi, hatuwezi kupuuza athari itakayopata Palestina. Ardhi za Waislamu ambazo zimechukuliwa kwa nguvu na umbile la Kiyahudi, ambapo nguvu zake zinaendelezwa kupitia Umoja wa Mataifa na nchi wanachama.

Amerika imesema kutakuwa na ‘amani’ katika eneo hilo, lakini ni aina gani ya ‘amani’ watakayokuwa nayo Wapalestina kwa makubaliano haya?

Uhalisia wa Watu wa Palestina

“Wakaazi milioni mbili wanaishi wakiwa na umeme kwa masaa manne tu kwa siku baada ya Israel kukata usambazaji wa mafuta, na kupelekea kufungwa kwa kiwanda pekee cha kuzalisha umeme cha Gaza wiki iliopita.” (Ripoti ya Aljazeera ya 2020)

Kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch 2020, serikali ya “Israel imeendelea kuweka vikwazo vikali na vya kibaguzi juu ya watu wa Palestina; kuwazuia watu na mizigo kuingia na kutoka Ukanda wa Gaza. Wana fursa finyu katika elimu, uchumi na mambo mengine, huduma za afya, maji safi na umeme takriban kwa Wapalestina milioni 2 wanaoishi Gaza.” Hii imefanya kiasi cha asilimia themanini ya watu wa Gaza kutegemea misaada ya kibinaadamu.

Wakati Imarati ikitangaza mpango huo, walisema kuwa wamewafikiria Wapalestina kwani umbile la Kiyahudi halitoendelea na mipango yake ya kuunganisha (eneo la Wapalestina). Lakini Waziri Mkuu wa umbile la Kiyahudi, Benjamin Netanyahu, alisema “amechelewesha” mipango ya uunganishaji Ukingo wa Magharibi, lakini mipango hiyo ingali “juu ya meza”.

Je, mpango wa Imarati na umbile la Kiyahudi umebadilisha chochote?

Hapana, umbile la Kiyahudi sasa linajiamini zaidi kushinda lilivyokuwa awali.

Na jeshi la umbile la Kiyahudi linafanya mashambulizi Gaza karibu kila siku tokea Agosti 6, pamoja na kukazanisha vikwazo ambapo limepiga marufuku uingiaji wa mafuta kwa kiwanda pekee cha kuzalisha umeme, na kuitumbukiza mamlaka ya Palestina kwenye kiza.

Lakini kwa nini wasiwe wenye kujiamini? Wakati kile wanachoweza kuhofia ni kauli za kukataa za wale waitwao watawala wa Waislamu.

Waziri wa Kigeni wa Iran ameuita mpango huo “jambia ambalo Imarati inawapiga Wapalestina na Waislamu wote nyuma ya migongo yao kwa dhulma”.

Uturuki imesema kuwa watu wa eneo hilo “hawatosahau na hawatosamehe tabia hii ya kinafiki” ya Imarati.

“Unapozungumzia Israel na Palestina, tunahitaji kufikiri, je tunaweza kumjibu (Mwenyezi Mungu) kama tutawatelekeza watu hao ambao wanakumbana na kila aina ya uonevu na ambao haki zao zimeporwa? Dhamira yangu hainiruhusu kufanya haya, sitoweza kukubali hiki” Khan alisema.

Wanasema hawawezi kusamehe au kusahau, lakini wanalikubali – matendo yao hayatupi sababu ya kuamini vyenginevyo.

Ahadi zinatolewa ili kufikia malengo yao na kutunyamazisha

Tunapoangalia kauli za watawala wa Waislamu, hatuna budi kukumbuka kuwa wana malengo mawili. Wanataka kuwafurahisha watawala wa Kimagharibi, katika suala hili hasa Amerika, na kuendeleza usaidizi wa kura za watu wao.

Kuifurahisha Amerika

Umbile la Kiyahudi na Amerika zimeendeleza mahusiano ya karibu tokea Vita Baridi. Wamekuwa wakipeleka zaidi ya dolari bilioni 3 kama msaada wa kijeshi na kiuchumi kwa umbile la Kiyahudi. Zaidi ya hayo, dola hii ya Kimagharibi inafanya juhudi kubwa dhidi ya Palestina, likitumia msaada wa Kigeni kuyavunja moyo dola na mashirika ya kimataifa katika kuitambua dola ya Palestina.

Kuwafurahisha Waislamu

Waislamu kote duniani wanafungamano imara kwa ardhi ya Palestina. Wale wanaoitwa watawala wa Waislamu hawawezi kupuuza hili – ili kudumisha nguvu zao na uhalali wao, na kufanya kazi kueneza ajenda ya Wamagharibi – wanahitaji msaada wa watu wao.

Namna gani tukabiliane na mpango huu?

Watawala wa sasa wanafuraha kubaki ndani ya mipaka yao, kutangaza kutoridhika kwao juu ya umbile la Kiyahudi wakati kaka zetu na dada zetu wakishinda na njaa, wakiishi katika hali mbaya kabla ya damu zao kumwagwa. 

Baadhi wanaweza kuhoji kuwa katika mfumo wa sasa, mikono ya watawala imefungwa. Baada ya yote, tunaishi katika mfumo ambao tumegawika kimipaka. Hawawezi kuchukua hatua dhidi ya umbile la Kiyahudi, kwa kuwa ni dola tofauti.

Kwa hili lazima tuulize, kwa nini? Kwa nini baada kuuona ukweli wa dhulma na mateso ambayo Waislamu wanakumbana nayo je tukubali hili? Hasa wakati inapomaanisha kumuasi Mwenyezi Mungu na kukubali nidhamu za kisiasa, kijamii na kiuchumi ambazo haziegemei hukmu Zake kwa usafi na ukamilifu wake?

Kukataa kulitambua umbile la Kiyahudi haitoshi – haijalishi kama nchi chache za Waislamu zitatoa taarifa za kusema kuwa wanapinga hilo.

Kuitetea dola ya Palestina haitoshi – haiwezi kutatua matatizo yanayowakumba Wapalestina. Mfumo wa Kimagharibi hauwezi na hautoweza kulinda haki za ndugu zetu na dada zetu Waislamu. Ushahidi wa hili umetuzunguka – tumeona yale yanayowakuta Ummah wa Kiislamu, wale wanaosemekana kuwa na dola inayowalinda.

Kile tunachohitaji kukumbuka ni kuwa kuangazia juu ya suluhisho la kuwa na dola mbili (Israel na Palestina) kunapelekea kuhalalisha mfumo wa sasa – kuwapelekea Ummah wa Kiislamu kuamini kuwa njia pekee ya kukomesha mizozo na dhulma ni ikiwa tutawaunga mkono watawala wetu katika majaribio yao duni ya kidiplomasia ya kupigia debe dola ya Palestina.

Lazima tuchukue msimamo, kushinikiza kusimamisha tena Khilafah kwa njia ya Utume. Historia imetufunza kuwa bila ya kuwa na watawala wenye kumcha Mwenyezi Mungu, wanaotekeleza Uislamu kwa ukamilifu wake, Ummah wa Kiislamu hautokuwa salama na damu ya wanaume, wanawake na watoto itaendelea kumwagwa.

Je, Mtume (saw) hakusema kuwa

"إنَّ دِماءَكُم، وأمْوالَكم وأعْراضَكُم حرامٌ عَلَيْكُم"

“Hakika damu zenu, mali na heshima zenu ni vitakatifu kwenu”? (Muslim)

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Fatima Musab

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumatano, 16 Septemba 2020 11:00

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu