Jumatatu, 03 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/04
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Faini ya Mamilioni ya Rupia Imetozwa kwa Maafisa wa Serikali Kutokana na Kesi za Watu Waliopotea

Sauti ya Amerika Urdu

Januari 06, 2021

Asim Ali Rana

(Imefasiriwa Kutoka Lugha ya Kiurdu)

Islamabad –

“Imepita miaka minane, tukizunguka kutoka mahakama moja kwenda nyengine na nyengine, lakini hakuna aliyeweza kumtoa mume wangu. Mtoto wangu alikuwa na miaka miwili wakati mume wangu alipotekwa nyara. Hakuwa mwenye kumtambua vyema baba yake wakati huo.”

Haya ni maneno ya wakili Sadia Rahat, mke wa Naveed Butt, aliyepotelea kutokea Lahore. Mume wa Sadia, Naveed Butt, aliyekuwa msemaji wa Hizb ut Tahrir, alitekwa nyara mnamo mwaka 2012, na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake. 

Sadia Rahat anasema, “Tokea wakati huo tumekuwa tukienda mahakama moja hadi nyengine, lakini bila ya kupata afueni ya mahakama. Tume ya watu waliopotea ilitoa amri ya kutolewa nyaraka za mashtaka (production order) kwa watekelezaji wa sheria, lakini kwa mume wangu haikufanyika.”

Aliongeza kusema, “Wanasema kuwa idara za kiusalama zote zinakanusha kumzuilia mume wangu, lakini nina uhakika kwamba wanae wao,” aliongeza.

Katika siku za karibuni, Mahakama Kuu ya Islamabad ilitoza faini ya mamilioni ya rupia kwa maafisa wa juu wa serikali katika kesi za watu waliopotea.

Mahakama ilitoza faini ya Rs milioni 10 kwa polisi, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Ulinzi katika kesi ya Ghulam Qadir, aliyepotea kutokea Islamabad kwa miaka sita.

Katika hili, serikali kuu imekata rufaa kwa ajili ya uhakiki wa Mahakama Kuu, ambapo imesikilizwa kwa mara ya kwanza hapo jana, na mahakama ikasema kuwa faini ingalipo, lakini ukweli ni kwamba ikiwa mtu atapotea, nini kitafanyika kwa hilo. Hakimu Athar Minallah alisema kuwa mahakama inatoza fidia kwa sababu dola hushindwa kumpata aliyepotea.

Kaimu Mwanasheria Mkuu jijini Islamabad, Syed Tayyab Shah, amesema kuhusu hili kuwa kesi aina hizi haziwezi kuzungumziwa sana, kwa kuwa rufaa katika kesi hizi huachwa mahakamani. Alisema dola ina haki kukata rufaa, kama haijakinaika na maamuzi ya mahakama.

Amri kali zimetolewa na mahakama nchini Pakistan katika siku za karibuni juu ya kutopatikana kwa watu waliopotea. Hii sio mara ya kwanza kutozwa faini ya Rs milioni 10. Maafisa wa serikali wametozwa faini katika kesi tatu tofauti na mahakama hapo awali.

Kesi mojawapo ni ile ya mhandisi wa mawasiliano ya Tehama (IT) Sajid Mehmood. Mke wake Mahira Sajid alifungua mashtaka mahakamani juu ya gharama za matumizi ya nyumbani, ambapo mahakama alimpatia milioni 4.5 kwa kutoonekana Sajid Mehmood hadi sasa pamoja na kupatiwa rupia laki moja na alfu tano kila mwezi.

Katika kesi hii, wakili wa Mahra Sajid, Omar Gilani alisema, “Serikali ina jukumu kwa usalama wa kila mtu. Kama mtu amepotea, basi kupatikana kwake ni jukumu la serikali. Katika kesi hii vile vile tumezungumzia kuhusu suala sawa, na mahakama imetoa maamuzi ya mwisho kuhusiana na nayo, ambapo serikali pia imekubali. Utekelezaji wake unatakiwa kuonekana. Ni mategemeo kwamba serikali itafanya malipo haya karibuni.”

Kuhusiana na suala hili, Raisi wa Baraza la Wanasheria wa Pakistan Abid Saqi amesema kuwa chini ya katiba na sheria, uhuru wa kila mtu, pamoja na usalama wao, ni jukumu la serikali. Mahakama ni walinzi wa katiba hii na maamuzi ya Mahakama Kuu ya Islamabad ni dhihirisho la hasira juu ya kutotekelezwa kwa amri za mahakama katika suala hili.

Abid Saqi amesema kuwa katika kesi za waliopotea, amri za wazi hutolewa na mahakama, lakini hazitekelezwi. Mahakama za Pakistan zina jukumu kwa uhuru na usalama wa kila mtu na zinatekeleza wajibu wao.

Sadia Rahat anasema amekuwa katika matatizo makubwa, tokea mume wake atekwe nyara. Wana watoto watatu wa kiume na wa kike mmoja, na watoto bado wako katika huzuni ya kumpoteza baba yao.

Sadia amesema kuwa katika ombi lake linalo subiri katika Mahakama Kuu, alitaka pia fidia kutoka serikalini kwa kuwa kutokuwepo kwa mume wake kumemsababishia matatizo makubwa ya kifedha.

Kwa mujibu wa tume ya watu waliopotea ya Pakistan, idadi ya watu waliopotea ni zaidi ya alfu mbili na mia tano. Japokuwa amri kali zimetolewa na mahakama juu ya kadhia hii, watu wengi bado hawaonekani, ambapo taasisi za serikali ndio zenye kubeba jukumu. Hata hivyo, taasisi za dola na serikali yenyewe zimekuwa muda wote zikikanusha madai haya.

[Chanzo: Urdu OVA]

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu