- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Vita vya Karne ya 21 Vimeanza
“Mzozo wa kibiashara kihakika ni vita dhidi ya kuinuka kwa China, ili kuona ni nani aliye na nishati kubwa zaidi. Huu kamwe sio wakati wa ulegevu na kunyamaza kimya.”
Hivi ndivyo namna mamlaka za China, katika toleo lililovujishwa, zilivyoelezea vyombo vya habari vya dola kwa mukhtasari namna watakavyoziba mzozo wake wa kibiashara na Amerika. Vita vya kiuchumi vya karne hii sasa vimeanza. Baada ya miezi kadhaa ya vitisho vya ushuru, mnamo 6 Julai Amerika ilitoza ushuru wa asilimia 25 juu ya bidhaa kutoka China zenye gharama ya dolari bilioni 34. Katika hatua ya kujibisha hilo China ilitoza ushuru juu ya bidhaa za ukulima zenye athari ya kisiasa kutoka Amerika. Katika kujibisha hatua hii ya China, mnamo Julai 10, wawakilishi wa kibiashara wa Amerika walianzisha mchakato wa miezi miwili wa utozaji ushuru juu ya bidhaa nyengine zaidi kutoka China zenye thamani ya dolari bilioni 200. Huku majadiliano yakiendelea kati ya Amerika na China ili kupata muwafaka wa pamoja, mashindano ya chini kwa chini kati ya dola mbili hizi zenye uwezo mkubwa wa kiuchumi duniani kihakika yanahusiana na bwana anayeshikilia uongozi wa kiulimwengu akijaribu kukabiliana na nguvu mpya inayoibuka. Kikweli huu ndio mwanzo wa ubwana wa kiuchumi na wa kisiasa wa karne ya 21.
Kwa miongo kadhaa Amerika imeitazama China kama simba marara bandia, taifa lenye uwezo kochokocho lakini lililozama katika mzoroto, umasikini na ukomunisti. Amerika yenye tajriba ya kisiasa iliweza kuitongoza China kutoka katika Muungano wa Kisovieti mwanzoni mwa miaka ya sabini, ambayo China daima ilikuwa na mahusiano tete nayo na kuigawanya kambi ya Mashariki. Kufikia miaka ya sabini viongozi wengi wa kikomunisti walitambua kuwa Ukomunisti umeshindwa kuimarisha China na kwa hakika ulilisababishia taifa hilo matatizo makubwa ya kiuchumi. Huku wakiigeukia Amerika wakati wa Vita Baridi viongozi wa China walitaraji wangepata mwanya wa kufikia teknolojia ya kisasa, tajriba na ujuzi.
Katika miaka ya tisini na baada ya kuporomoka kwa Muungano wa Kisovieti mnamo 1991 Amerika haikuizingatia China kama tishio na kuyachukulia matarajio yake kuwa finyo. Utawala wa Clinton (1991-2001) uliitazama China kama mshirika wa kiulimwengu baada ya kumalizika kwa Usovieti, hususan nguvu kazi yake rahisi, ambayo mashirika ya Amerika yalikuwa yanataka kuipatiliza.
Lakini yote haya yalibadilika pindi George W. Bush alipoingia mamlakani mnamo 2001 akizungukwa na wanaharakati wapya wenye kudumisha tamaduni za kale za kisiasa (neocons) waliokuwa wakitaka kuifanya karne ya 21 kuwa karne ya Amerika. Condoleezza Rice aliandika katika Makala ya Jarida la Wizara ya Kigeni mnamo 2000: “China inachukia dori ya Amerika katika eneo la Asia-Pasifiki. Hii yamaanisha kuwa China si dola “inayoendana na hali halisi” bali ni dola inayopenda kugeuza mizani ya utawala ya Bara Asia kwa manufaa yake. Hilo pekee linaifanya kuwa mshindani wa kistratejia, wala sio “mshirika wa kistratejia” kama ilivyowahi kuitwa na utawala wa Clinton”. Watunzi wa sera za Amerika katika enzi ya Clinton waliona kuwa njia bora ya kuidhibiti China ilikuwa ni kupitia kuamiliana nayo na kuipa mwanya wa kufikia baadhi ya teknolojia ya Amerika. Idara ya wanaharakati wa neocon ilikabiliana na China ambayo uchumi wake ulipita kiwango cha dolari trilioni 2 na ambayo inatafuta kawi na rasilimali ulimwenguni. Utajiri mpya iliopata ulisababisha wasiwasi mkubwa katika eneo la Asia Mashariki, hususan pindi China ilipoanza kudai milki ya vyanzo vya maji, visiwa vya kuundwa na miamba. Watunzi wa sera wa Amerika wameona kuidhibiti ndiyo njia bora zaidi kupunguza matarajio ambayo China yaweza kuwa nayo, ilizitumia nchi za pambizoni kama Korea Kusini, Vietnam, Japan, Taiwan na India kwa miamala ya silaha ili kudhibiti kuibuka kwa China kwa namna yoyote.
Lakini leo, kuzuia huku kumefeli wazi wazi. Uchumi wa China umekuwa pakubwa na mnamo 2016 ulizidi uzalishaji jumla (GDP) wa Amerika. Kila mwaka Amerika imekuwa ndio uchumi mkubwa duniani tangu 1881. China leo ni mshirika wa kibiashara nambari moja kwa mataifa 138 duniani kati ya mataifa 200, hii ikiifanya kuwa mfanyi biashara mkubwa zaidi duniani. Ili kuujumuisha ulimwengu ndani ya mpango mkubwa zaidi wa kibiashara mnamo 2013 China ilitangaza mradi wa Ukanda na Barabara (OBOR) utakaopelekea uwekezaji wa hadi dolari trilioni 4 katika miundo mbinu kati ya Ulaya na Asia. China sasa imeanzisha badali ya Shirika la Fedha Duniani na Benki ya Dunia zinazodhibitiwa na Amerika – Benki ya Asian Infrastructure Investment (AIIB). Utajiri huu na miradi kadha wa kadha yamaanisha kuwa China na Amerika ziko katika mgongano.
Raisi Trump katika Mkakati wake mpya wa Usalama wa Taifa mnamo Disemba aliangazia ukuaji wa uwezo wa kiteknolojia wa China kama tishio kwa nguvu za kiuchumi na za kijeshi za Amerika. Amerika inatafuta kuudhibiti uwekezaji na umilikaji wa China katika sekta za kistratejia kama teknolojia. Zaidi ya hayo, Amerika inafanya msako juu ya kampuni za kiteknolojia za China. Mnamo Aprili 16 2018, Kitengo cha Biashara cha Amerika kilirudisha upya agizo la kupiga marufuku kampuni za Kiamerika – zikiwemo kampuni kuu za kiteknolojia kama vile Google, Qualcomm na Intel – kuuza vipuri, barnamiji na vifaa kwa shirika kubwa la mawasiliano lililoko Shenzhen la ZTE Corp. ZTE in mojawapo ya makampuni muhimu zaidi katika mkakati wa uvumbuzi wa kiteknolojia unaoendelea kwa sasa nchini China. Inakadiriwa asilimia 25 hadi 30 ya mahitaji na vipuri vyake hutoka katika kampuni za Amerika.
Amerika inazilenga sekta za kiuchumi na teknolojia ambazo ukuaji wa China unazitegemea. Tofauti na uchumi nyenginezo kubwa, asilimia 20 ya uchumi wa China umejengwa juu ya usafirishaji bidhaa ng’ambo. Amerika ndicho kituo kikubwa zaidi cha bidhaa kutoka China – mnamo 2016, asilimia 23 ya bidhaa za kutoka China, zenye thamani ya takriban dolari bilioni 481, zilielekea nchini Amerika. Uzalishaji jumla (GDP) wa Amerika ni dolari trilioni 18.5, usafirishaji bidhaa ng’ambo ni dolari trilioni 1.4 – chini ya asilimia 12. Uagizaji bidhaa wa Amerika kutoka ng’ambo, au idadi kubwa ya usafirishaji bidhaa wa China kwenda Amerika ni bidhaa za matumizi ya kila siku. Amerika yaweza kupata bidhaa hizi kutoka katika maeneo mengine, ikiwa itahitajika. China kwa upande mwengine haitaweza kupata soko jengine litakalotumia bidhaa hizi kama vile Amerika itumiavyo.
Mdadisi mkongwe wa siasa za maeneo na mwandani wa maraisi waliotawala wa Amerika, Henry Kissinger amesema katika dhifa tofauti tofauti kuwa anaona kuimarisha mahusiano na Urusi kama jambo muhimu kutokana na ongezeko la nguvu za China. Hivyo basi si ajabu kwa Putin na Trump, licha ya balagha yao kukutana katika kongamano nchini Finland mnamo Julai 16. Miongoni mwa kadhia nyingi za kiulimwengu, Amerika na Urusi ni lazima zijadiliane kuhusu mahusiano ya Urusi na China. Amerika inataka kuitumia Urusi dhidi ya China, sawa na dori iliyocheza China dhidi ya Muungano wa Kisovieti siku za nyuma. Ushuru na vikwazo vya kibiashara pamoja na kuunda mgawanyiko baina ya Urusi na China ndio mkakati wa Amerika wa kukabiliana na kukua kwa mpinzani imara wa siku za usoni kwa hadhi yake kama dola kuu inayoongoza duniani.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Adnan Khan