Jumapili, 20 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Je, Sio Muda Sasa wa Kusema ‘Ndiyo’ kwa Mabadiliko?

(Imetafsiriwa)

Urasilimali unashindwa – muda wote umekuwa ni mfumo mbovu; ukiwanufaisha matajiri kwa gharama ya masikini au, kwa maana nyengine, kuwaweka wachache katika afya njema na wenye mafanikio kupitia kuwanyonya waliobakia katika dunia. Hali hii haijabadilika – wala haitobadilika. Inaendelea kuwa mbaya. Lakini hiyo pia sio sababu ya kuwa nimesema kwamba Urasilimali unashindwa.

Kushindwa kwake ni kwa maana ya kuwa umeanikwa wazi – watu wanatambua juu ya kasoro na hila zake. Dunia yote inaweza kuona madhara inayoyaleta. Mwanzoni, ulistawi kutokana na mafanikio yake katika kuhadaa umma na dunia. Lakini hivi sasa, kutokana na suala la Gaza, umeshindwa kutudanganya na kutuhadaa.

Tunaweza kuona uovu ambao mfumo umeuruhusu. Tunaona msaada ambao umepatiwa ‘Israel’; namna Marekani isivyowajibishwa kwa msaada wao kwa ‘Israel’, namna watawala kote duniani wanavyoiruhusu ‘Israel’ kuendeleza mauaji ya halaiki – licha ya kuwa sheria zao wenyewe za kimataifa zinasema wazuiwe. Tunaona namna taasisi zote za kimataifa ambazo dunia inazitetea zinavyosaidia uovu ndani ya mfumo. Tumeona namna vyombo vya habari vilivyo kuwa ni taasisi za serikali, zinazosaidia watawala katika majaribio yao kuficha ukweli na kuwalenga kwenye safu za masuala mengine – chochote kitakachowapa umbile la Kiyahudi na Marekani muda wanaohitaji kutekeleza malengo waliyonayo katika eneo.

Tunapokaa na kufikiri kuhusu kile kilichotokea miezi michache iliyopita – sio tu Gaza bali duniani kote, tunahisi kutokuwa na matumaini, wenye hasira na wagonjwa. Tunaweza kuona kufeli kwa Urasilimali. Tunaweza kuona kuwa hauwezi, na hautoweza kuleta haki kwa watu au kuwalinda wakati maslahi ya Urasilimali hayaendi sambamba na malengo hayo ya udhanifu.

Na bado, wakati tunapofikiri kuhusu namna mbadala tunaamini kuwa haiwezekani kuleta mabadiliko.

Tunasema, kwa vipi tuupe mgongo Urasilimali? Dunia haitoweza kwenda bila ya mfumo huo.

Lakini tunahitaji muda kidogo kufikiria kuhusu hilo – kwa nini hatuwezi kuupa mgongo Urasilimali?

Sisi kama binaadamu, umetukosea sana.

Na tukiwa Waislamu, unatulazimisha kukubali sheria za wanadamu dhidi ya sheria za Mwenyezi Mungu.

Lakini tukiliweka hili pembeni kwa muda. Kwa nini tunaamini kuwa haiwezekani kuuregesha Uislamu duniani?

Hatukuishi na mifumo miwili au zaidi ya Himaya moja zama za nyuma?

Tunapoangalia historia, tunaona mpangilio wa ‘dola kubwa’ na ‘himaya’ zilizotawala kwenye ardhi kwa wakati mmoja. Tumekuwa na Himaya za Rumi na Fursi. Tumekuwa na Himaya za Uingereza, Ufaransa, na safu kamili za Himaya za Ulaya zilizokuwepo kwa pamoja.

Baada ya Kuanguka kwa Himaya, tumekuwa na Vita Baridi ambapo mifumo miwili ilishindania mamlaka, nguvu na ushawishi. Ndio, Ukomunisti ulishindwa. Lakini ulikuwepo muda huo huo pamoja na Urasilimali kwa miongo kadhaa. Na kufeli kwake ilikuwa zaidi ni matokeo ya kasoro katika mfumo wa Kikomunisti na machaguo yaliyofanywa na uongozi wa Umoja wa Kisoveti, kuliko kuwa ni suala la kuwa haimkiniki kuwa na mfumo zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja.

Hivyo, kwa nini tunaangalia hali ya sasa na kusema kuwa haiwezekani kwa Ulimwengu wa Kiislamu kujiweka mbali na Mfumo wa Kirasilimali na kuuelekea uhalisia ambapo Uislamu unatabikishwa kama mfumo?

Sababu kuu ya hilo ni kuwa tumefundishwa fahamu na fikra ambazo zinatufanya tuamini kuwa hilo haliwezekani. Mfumo wetu wa elimu, vyombo vya habari na taasisi za kisiasa vyote vinatilia nguvu fikra ya kuwa sisi tunaishi katika dunia ambayo inategemeana, na njia pekee ya kupiga hatua ya maendeleo ni kubakia katika njia hiyo – vyenginevyo ni kwa namna gani tunaweza kuyafikia manufaa ya vitu ambayo Urasilimali umetuahidi? Tukiwa ni umma, tusilenge juu ya kuhakikisha kuwa sisi tunajitegemea, lazima tufanye biashara ili tuweze kupata manufaa ya kuishi ndani ya ulimwengu wa utandawazi.

Haya yanafanywa kwa lengo maalum, kuwa ni muendelezo wa Urasilimali uwe ni Mfumo wa Kilimwengu unaotegemea juu ya uungwaji mkono na hadaa kwa watu. Pindi tukiwa na ufahamu tutahoji. Tutakapohoji tutafikiri. Na pindi tukifikiri utapoteza uungaji mkono wake na ubwana wake.

Ni kweli kuwa Marekani kwa msaada wa dola za kitaifa duniani kote, imeunda uhalisia ambapo sisi sote tumeunganishwa. Wameunda sheria na kanuni kwa kila taifa kujifunga nazo na kisha kuhakikisha kuwa sisi sote tunaona matokeo ya kutofanya kazi ndani ya mfumo huo. Hivyo, kama hatutoisaidia Marekani katika vita vyake dhidi ya ugaidi, vipi tutapata mikopo ya kutusaidia kustawi? Kama tutazungumza dhidi ya maovu yanayotekelezwa, makampuni ya kibinafsi yatakataa kushirikiana na sisi. Kama tutajaribu kutekeleza sheria za Kiislamu, tutatengwa na kukashifiwa na mataifa mengine.

Lakini haya hayamaanishi kuwa haiwezekani kuachana na Urasilimali – inamaanisha kuwa kuachana na Urasilimali kutabadilisha muundo wa mfumo wa kimataifa. Hivi ndivyo imefanyika kabla, Marekani ilifanya baada ya kuanguka kwa Himaya. Na ukizingatia ukweli kuwa Ukomunisti haukuanguka hadi miaka ya 80 na 90, ubwana pekee wa Urasilimali haujafikia hata miaka 70.

Tena kuna ukweli kuwa muunganiko huu unaweza pia kuwa ni dosari kubwa kabisa ya mfumo. Dolari, ambayo ni moja ya nguzo muhimu ya ubwana wa Urasilimali, inaegemea juu ya uaminifu. Uaminifu kwa dolari na uaminifu kwa Marekani. Kama tutapoteza uaminifu huo na kuachana na Dolari, basi itapoteza thamani yake. Lakini kwa kuweka wazi, kuachana nayo haimaanishi kuchukua badala yake sarafu nyengine ya karatasi isiyo na thamani yake yenyewe, ambayo inafungamana na dolari lakini sio moja kwa moja, bali kuachana nayo ni kuachana na fedha hizo za karatasi moja kwa moja na kuelekea kwenye Mfumo wa sarafu za Dhahabu na Fedha.

Kabla ya kusita na kusema kuwa haiwezekani, zingatia mambo mawili:

1) Ni nani aliyetwambia kuwa haiwezekani - ni watu wale wale wanaonufaika kutokana na kuikubali kwetu?

2) Je, hili haliwezekani tu kama tutataka kubakia ndani ya mfumo huu unaoanguka?

Ukataaji wa Dolari kunaidhoofisha, na udhoofishaji huo utakuwa kwa hasara yao na sio kwetu - hasa inapokuwa nyingi ya nchi duniani zimechoka na ubwana wa Kimagharibi na kutaka mabadiliko.

Huu ni uhalisia tu wa kiuchumi – ubaya wa Mfumo wa Kibepari unaenea zaidi ya hapo, kijeshi, kisheria, kisiasa na maeneo ya kijamii. Lakini hadi sasa, tunasukumwa kupuuza ukweli na kuzingatia hofu. Hofu ya ‘nini itakuwa’ na ‘inaweza kuwa’ ndiyo yanayotusukuma kuendelea kuunga mkono Urasilimali katika utawala wake wa kigaidi. Ni njia ya Urasilimali kujilinda yenyewe, na kuhakikisha kuwa unabakia bila kupingwa. Kwa sababu kama tutakataa sheria na kanuni zake, na kuachana nao, utaanguka.

Hivyo, unatusukuma kupuuza uhalisia mgumu wa ulimwengu wa Kirasilimali, ambapo baadhi ya nchi zipo mbele kiuchumi kwa sababu tu wanawanyonya wengine; kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja wakiwauwa mamilioni ya watu katika mchakato huo.

Kwa kweli wanaogopa. Kwa sababu wanajua kuwa sio tu nchi moja au serikali moja inayoukataa Urasilimali. Utakuwa ni ummah wote wa Kiislamu kwa ujumla. Hii sio kwamba haiwezekani, inahitaji sisi kufikiri nje ya hofu yetu na kukumbuka kuwa tukiwa Waislamu, mara zote tunaweka uaminifu wetu kwa Mwenyezi Mungu (swt).

Je, tunaamini kuwa watu hawako tayari kwa mageuzi?

Hoja inayofuata inayokuja akilini ni hii – hata kama inawezekana kivitendo kutekeleza mfumo wa Kiislamu, (ati) hautofanya kazi kwa sababu watu hawajawa tayari.

Tukiuangalia ulimwengu hivi leo, na suala la kuwa rai amma haiko kwa Urasilimali au kwa ubwana wa Wamagharibi, ndani na nje ya Ulimwengu wa Kiislamu, je tunaweza kusema kuwa hakika hili ni kweli?

Kuna wito wa mabadiliko kote duniani. Kukubalika kunakoendelea kuwa matatizo tunayoyakabili ni ya kupangiliwa yaani ni matokeo ya mfumo wa Kirasilimali. Tatizo ni kuwa bado, kwa kujua au kutokujua, wanajaribu ‘kuimarisha mfumo’, kwa kutumia njia na zana ambazo Urasilimali unazingatiwa kukubalika. Tunapofanya haya, tunaulinda mfumo kwa kunaswa ndani yake. ‘Suluhisho’ letu linatulazimisha kurudia kwenye sheria na kanuni zinazosababisha tatizo mwanzoni kabisa na ‘dawa’ itakuwa kama ni suluhisho lisilo zingatia sababu ya tatizo.

Tunaweza kuona hili katika chaguzi, katika maandamano, katika ususiaji. Wakati haya mawili ya mwisho ni njia nzuri ya kuonyesha hasira zetu kuelekea serikali na sera za kimataifa, hayatopelekea kwenye mabadiliko ya kweli. Tunawauliza wanasiasa na mashirika ya kimataifa, kuwa ni wazi kwamba wana maslahi katika hali ya sasa, kwa mabadiliko. Na hawatofanya maamuzi yatakayodhuru maslahi ya Urasilimali au ubwana kote duniani.

Baadhi husema kuwa njia pekee ya kubadilisha hali ni kujiweka sisi wenyewe kuwa Waislamu na kujikurubisha zaidi na Uislamu. Katika kujibu hayo tunapaswa kuzingatia yafuatayo, ni ipi njia kubwa zaidi ya kujikurubisha kwenye Uislamu kuliko ile ya kuusimamisha ukiwa ni mfumo juu ya Ardhi hii? Na hilo mara litakapofanywa je halitotusaidia sisi katika juhudi zetu binafsi kuwa karibu na Mwenyezi Mungu? Dola ya Kiislamu itakuwepo kutuelimisha, kutusaidia katika ibada, kuhakikisha kuwa kila maamuzi tunayoyafanya ni kuwa Mwenyezi Mungu ameruhusu. Je, tunaweza kusema kuwa hilo linawezekana katika Mfumo wa Kirasilimali, ambapo dhumuni pekee ni kutuweka mbali na dini na sio kutuweka karibu yake?

Watu duniani kote wamechoshwa na hali hii na wako tayari kufanya lolote ili kuleta mageuzi, kwa njia ya kusimamisha vitisho vinavyotokea Gaza na duniani kote. Kile tunachohitaji kukitambua ni kuwa kubadilisha sheria au sura chache haitosimamisha uovu wa Urasilimali – njia pekee ya kusimamisha ni kuuepuka na kisha kupambana nao, na hilo litawezekana tu kama tutakuwa na mfumo mwengine mbadala.

Je, tunaamini kuwa itatuweka sisi katika hali ngumu zaidi kuliko tulionayo hivi sasa?

Kuna hofu ya wazi ambayo inaambatana na wazo la kubadilisha mfumo. Ni suala la kimaumbile – mwanaadamu kawaida anahofia mabadiliko, wanatamani udhibiti na kukaa mbali na kutokuwa na uhakika. Tunaposoma kuhusu Mfumo wa Kiislamu, tunafahamu kuwa kuurudisha Uislamu duniani itakuwa ni mabadiliko magumu.

Lakini je itakuwa ni magumu zaidi ya kile tunachokabiliana nacho wakati huu? Watu wanauliwa katika machafuko ya kichochezi na vita vinavyopiganwa kote duniani. Hali ya sasa ya Gaza ni mfano mmoja tu kati ya mingi, na yataendelea muda wa kwamba yanahitajika kuhifadhi maslahi ya dola za Kibepari.

Katika sehemu za dunia ambapo hakuna vita na machafuko, Urasilimali umetupa hisia ya uongo. Umetufunza kuwa kama tutajifanya tunaepuka hatari, kuendelea kutii sheria zilizopo, na kufanya haki yetu kwa jamii, basi tutakuwa sawa. Lakini kama tutakaa kwa muda na kufikiri kuhusu hili – je tunao kweli umiliki huo?

Katika maisha, kama Waislamu tunafahamu (kupitia fikra ya ‘Qadhaa’) kuwa tunaweza tu kudhibiti matendo yetu. Kile kinachotokea kwetu, kile ambacho watu wengine wanatuchagulia kufanya, hayo yote yapo katika mzunguko tusio na mamlaka nao. Mzunguko ambao unahusisha vifo vyetu (ajal) na riziki zetu; pia kuchagua kutenda haram – kama kuchukua mali ya Riba au kupora benki - havitobadili rizki zetu. Hiyo imeandikwa kwetu na itatufikia.

Kwa hivyo, wakati Urasilimali unatueleza kwamba tutaweza tu kuendesha maisha yetu kama tutatii, ni kuwa wanatucheza shere ili tubaki kuwa watiifu kwao. Watu katika dunia hii hawawezi kubadilisha rizki zetu, hata kama wakijitahidi vipi kutuaminisha. Na wakati tukipitia hatua za maisha ambapo tunakumbana na matatizo ya kiuchumi, hiyo ni mitihani ambayo Mwenyezi Mungu (swt) ametuchagulia ili tuwe karibu naye. Na hakuna tunachoweza kufanya ili kubadilisha. Hakuna ambacho Mfumo wa Kirasilimali unafanya kuweza kubadilisha.

Tukirudia suala la ugumu wa maisha – muda wote tutakumbana na mitihani katika dunia. Hiyo haiepukiki. Lakini tuna chaguo katika namna ya kukabiliana na majaribio hayo. Je, chaguo letu litatupeleka karibu na Mwenyezi Mungui li tuingie Peponi au tutaruhusu Urasilimali kutumia hofu yetu ya mabadiliko na ugumu kwa kutucheza shere?

Lakini vipi Uislamu utafanya kazi katika wakati na zama zetu?

Hili ni jambo linalotuchanganya sisi – na ni shaka ambayo imepandikizwa makusudi kwetu. Urasilimali - katika aina zake zote mbili ukoloni mkongwe na ukoloni mambo leo – unafanya kazi kwa nguvu zote kutuchanganya kuhusu Uislamu. Unatulisha uwongo kama; ‘tumejitenga na dini’, dini haina nafasi katika dunia hii’, ‘Uislami ni dini ilio nyuma, na haina nafasi katika ulimwengu wa sasa.’ Wanatuambia kuwa nchi za Waislamu zipo nyuma na fisadi – hawakiri kuwa ufisadi huo ni matokeo ya fikra na fahamu ambazo wametulisha kwa karne chache za nyuma.

Kwa sababu wanajua kuwa kama tutafahamu na kutaka kujua ukweli, bila shaka itatupelekea mahala ambapo watapahofia – mahala ambapo sisi tukiwa kama Ummah, kusema ‘Imetosha! Uislamu utashamiri tu pindi tukiutekeleza kama mfumo katika ardhi hii’. Wakati ambapo tutatambua kuwa ‘matatizo yote tunayokabiliana nayo hivi leo ni matokeo ya Urasilimali’ na hayatobadilika kamwe.

Kwa sababu Uislamu unapokuja, hautobadilisha kitu kimoja. Hautobadilisha hata kundi la vitu. Bali utabadilisha kila kitu.

- Tutaondoa utegemezi wetu kwenye sarafu zisizojifunga na dhahabu, na mikopo yote inayohusiana nayo.

- Tutahakikisha kuwa kila mtu anapata mahitaji yake yote ya msingi, ili watu wasikabiliane na hali ya ukosefu mkubwa na ugumu wa maisha.

- Tutakataa nidhamu yao ya jamii, na kuichukua ile ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia.

- Tutawafundisha vijana Uislamu, na sayansi, ili waweze kuendelea kama walivyokuwa huko nyuma.

- Tutakataa nidhamu ya utawala inayo tulazimisha, na kuichukua ile ambayo Khalifah atakuwa mwenye kuhisabiwa kwa matendo yake hapa duniani na akhera.

Urasilimali unatambua hili. Unajua kuwa tulifanya haya mwanzoni wakati wa Mtume (saw) wakati Uislamu uliposimamishwa juu ya mfumo katika dunia hii. Ulionyesha (Urasilimali) namna tulivyostawi na ulifanya kazi kikamilifu kwa karne nyingi kutushughulisha na kutuondoshea utiifu wetu kutoka kwenye Uislamu na maadili yake.

Na njia moja muhimu iliyoifanya ni kupitia kutushughulisha ufahamu wetu wa sheria za Kiislamu.

Tulipofundishwa kuwa Uislamu upo nyuma, tumefundishwa kuudharau mwanga wa sheria za Uislamu – ambazo hazikuundwa na akili ya mwanadamu, bali tumepatiwa na Mwenyezi Mungu (swt). Mtume (saw) ametufundisha kuvua hukmu juu ya kila kinachozuka hadi Siku ya Kiyama. Ametufundisha namna ya kuchunguza uhalisia, na kutumia hukmu za Mwenyezi Mungu (swt) juu yake. Pia ametufundisha namna ya kuchunguza uhalisia mpya na kufanya Ijtihadi yaani kuvua hukmu za Uislamu kwa ajili ya mazingira mapya.

Sasa, tunasema hii haitoweza kufanya kazi katika uhalisia huu. Kwa kuwa kuna sheria nyingi ambazo hatuwezi kuzitekeleza katika ulimwengu wetu huu leo – na hiyo ni kweli. Lakini sio kwa sababu dunia ‘imefanya upya’ yale yaliopita hatua ambayo Uislamu unaweza kutumika. Hii ni kwa sababu tunaishi katika ulimwengu wa Kirasilimali, ambapo sheria za Kiislamu zinagongana na sheria za mwanadamu. Kuutekeleza Uislamu katika maisha yetu, kuhakikisha kuwa utiifu kwa Mwenyezi Mungu katika kila nyanja ya maisha yetu ni kuwa lazima tubadili mfumo.

Uislamu sio tatizo. Chaguo letu la kuishi chini ya Urasilimali ndio tatizo.

Tutakapobadilisha mfumo, tutaona namna gani sheria zote za Mwenyezi Mungu zinavyofanya kazi katika upatanifu kutusaidia sisi kupiga hatua katika dunia hii na maisha yajayo.

Je, sio muda wa sasa kusema ‘ndio’ kwa ajili ya mabadiliko?

Hakuna sababu kwetu ya kusema hapana. Tatizo kote duniani ni kuwa kuna ukosefu wa elimu na ufahamu wa ndani juu ya namna ya kuleta mabadiliko. Tunaambiwa kuwa hii ni hali nyepesi, ambapo tunaweza kufanya mabadiliko kama tutafuata njia ambazo tumefundishwa na Mfumo wa Kirasilimali.

Lakini hilo liko mbali na ukweli – ni rahisi kufanya kazi ndani ya mfumo huu, lakini haitopelekea kwenye mabadiliko ya kweli. Tunaweza kuyaona haya, kwa sababu tumejaribu njia zao na matatizo yamebakia. Matatizo hata sio mapya – bali ni maregeo ya yale ya zamani, ambayo yalielezewa kwa msururu wa visingizio.

Kama tunataka dunia ipige hatua mbele, tunahitaji mabadiliko ya mfumo. Tunayo njia ya kutekeleza hili – tunahitaji kuregea kwenye Quran na Sunnah. Ni uongozi pekee ambao tunauhitaji sisi kama Waislamu. Na njia pekee ambayo kwayo tutaweza kuleta mabadiliko – kwa sababu utekelezaji wa mfumo wa Kiislamu ni njia pekee kwetu ili kuuepuka Urasilimali.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Fatima Musab

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu