Ijumaa, 10 Rajab 1446 | 2025/01/10
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Je, Erdogan Anajitayarisha Kutangaza Khilafah Nchini Uturuki?
(Imetafsiriwa)

Waislamu kweli wanasubiri kwa hamu Khilafah. Miongoni mwa idhlali na maangamivu yanayoukumba ulimwengu wa Kiislamu, leo Waislamu wanasubiri tetemeko la ardhi, siku ambayo Waislamu nchini Uturuki, biladi za Kiarabu na biladi nyenginezo za Kiislamu watakapochukua msimamo walioupoteza, na kutupilia mbali utiifu wowote mwengine isipokuwa utiifu kwa Mola wao, na kutokana na nidhamu yoyote nyengine isipokuwa kwa Dini yao tukufu ya Uislamu. Uislamu uliwageuza Waarabu kutoka kuwa ni taifa duni thamani miongoni mwa mataifa na kufikia kilele cha uongozi baada ya kumakinisha hali yao ya kindani kwa hukmu za Kiislamu, na kujenga nguvu yao kwa muda mfupi mno, ambapo bado ingali ni mada inayofanyiwa utafiti na wanafikra wa kisiasa, walioanza kuvamia na kueneza utukufu wa Uislamu. Na makabila ya Kiarabu katika kisiwa hicho yalikubali Dini hii mpya, kuupa nguvu Uislamu kabla ya mwisho wa muongo wa kwanza wa Dola ya Muhammad (saw), na kisha kuanza kuvamia nchi kubwa kubwa pambizoni mwake.

Na swali kuu ambalo Waislamu hulijibu kwa urahisi ni: ikiwa tutalirudia tena hili, na kusimamisha dola ya Khilafah ya pili, je, itaweza kuwa kama dola ya kwanza ya Kiislamu?

Bila shaka Waislamu watajibu “Ndio”, na wasomi wa dola za kikafiri pia wanalijua hili vizuri mno, na wanasiasa katika nchi kuu wanahofia kurudi kwa Uislamu. Wanahofia kwamba kurudi kwa Uislamu kutatokea katika dola imara mithili ya Uturuki, ambao watu wake wanawaza kusimamisha tena Izza ya Uislamu, iliyomakinika katika historia ya Kiuthmani, wakati Istanbul ilipokuwa ndio kitovu cha dola ya Kiislamu na Ummah mzima, au kutokea katika biladi imara mithili ya Pakistan, au Misri, inayo miliki jeshi kubwa na imepakana na bahari ya Mediterrania na bahari nyekundu, na mkondo wa Suez ambao ni njia ya biashara za kimataifa. Wasiwasi huu unawakosesha usingizi wanasiasa wa nchi kuu, hususan Amerika. 

Ili kutambua hofu za Amerika na Ulaya kutokana na tetemeko kubwa la Khilafah, Wamagharibi wanaiona hali ya upinzani katika Ummah wa Kiislamu. Hii ni kwa sababu Wamagharibi walikuwa wakidhibiti kila kadhia ndogo au kubwa katika biladi za Kiislamu. Walikuwa wakidhibiti kila kitu. Lakini, mwanzoni mwa karne hii, hali mpya ya upinzani iliibuka katika Ummah wa Kiislamu. Mandhari kuu ya kwanza ya hali hii kuonekana ni mnamo 2001 ambapo Taliban – Afghanistan ilikataa kuiacha mkono Al-Qaeda, ambayo Amerika iliituhumu kwa matukio ya Septemba 11 na Taliban ilikhiari kuingia katika vita, na kupoteza mamlaka kutokana na uvamizi wa Amerika nchini Afghanistan, lakini ilikataa kusalimu amri. 

Hiyo ilikuwa ni mwanzoni, kisha ukaja uvamizi wa Amerika nchini Iraq mnamo 2003. Baada ya Amerika kutangaza ushindi juu ya jeshi la Iraq, ilijipata ikikabiliana na upinzani mkali ambao haukuliogopa jeshi la Amerika. Upinzani huu uliisikuma Amerika ndani ya migogoro ya Iraq na ilikaribia kuishinda. 

Kisha, mnamo 2011 kulitokea mapinduzi ya Kiarabu yaliolingania kupinduliwa kwa serikali; yaani, serikali vibaraka wa Amerika na Ulaya, ambazo umaarufu wake ulioza na kumomonyoka kufikia nukta ambapo zilifikia ukingo wa kuporomoka. Mapinduzi haya hayakutarajiwa na huduma za kijasusi za Kiamerika na Ulaya. Hili lilizua taharuki ya hali ya hatari ya upinzani ambayo ilianza kulipuka. Mapinduzi ya Syria, ambayo yamekuwa yakiendelea tangu 2011, yana msimamo maalumu. Mwito wa kupindua serikali ulifuatiwa na mwito mwengine wa kusimamishwa Khilafah Rashida, na ulikuwa ni mwito hatari mno. Hivyo basi, Amerika ilipambana nao kwa nguvu sana kupitia kuzisaidia serikali na Wairani na Warusi na wengineo katika jaribio la kuzima mapinduzi haya. Amerika ilijionesha kupinga serikali ya Syria na washirika wake wa Kirusi na wa Kiirani, na sera hii ya Kiamerika ni muhimu ili kudhibiti hatari hii, vyenginevyo mambo yangezidi kuwa mabaya na kulipuka na kutoka nje ya mikono yao na mikono ya wafuasi wao. Kiujumla, mapinduzi ya Syria yameifanya Amerika kutetemeka kwa sababu yalikuwa kizingitini mwa tetemeko la Khilafah kwa njia ya Utume.   

Mambo mawili yaliibuka katika mandhari hii kama natija yake: Kwanza:

Uturuki imeongeza pakubwa ushirikiano na Amerika ili kuyadhibiti mapinduzi ya Syria. Manufaa makubwa ya Uturuki ni kuwa chama chake tawala kilisifiwa kuwa cha “Kiislamu” na raisi wake, Erdogan, alikuwa maarufu sana kwa harakati zilizosifiwa kuwa harakati za “Uislamu poa”. Pili ni tangazo la Khilafah bandia katika mji wa Mosul. Kutokana na kadhia mbili hizi, mtazamo mpya umeibuka nchini Amerika, unaoitwa “Uturuki ya Kiuthmani”, ambao huenda ukawa ndio njia ya mafanikio katika kuondoa hali ya upinzani katika ulimwengu wa Kiislamu. Na kuthibitisha hatari ya mtazamo huu wa Kiamerika, ilinukuliwa katika shirika la habari la CNN Arabic mnamo 12/6/2014:  

“kwa miaka, wajuzi walitabiri mambo, baadhi yao kutokana na historia, ambayo baadhi yanahusishwa na maamuzi muhimu ya hivi majuzi, huenda yakachochea zaidi moto katika eneo lenye uhasama.” Wanafikra katika “Baraza la Atlantiki” walionya kuwa ghasia eneo la bara Arabu huenda zikapelekea wazo kuwa “msingi wake ni kusimamisha dola ya Khilafah katika eneo kubwa”. Wajuzi wa Kiamerika walionya mnamo 2016 kutokea kwa mkurupuko wa vita viwili vikuu dhidi ya Amerika, moja ni katika ulimwengu wa Kiislamu, na vyengine nchini China. Ikimaanisha kuwa Amerika, ili kudumisha ushawishi wake na msimamo wake wa kimataifa, haina budi kuangalia kwa makini sana uwezekano kuwa huenda isitarajie, yaani, tetemeko la Khilafah kulipuka usoni mwake; hivyo basi, ikaanza kujitayarisha.  Ili kuweka wazi, mtu hana budi kutizama uhakika wa utawala nchini Uturuki na utiifu wa Erdogan, na kule kuwa yale makundi yanayoitwa “yenye Uislamu poa” yanavutiwa na Istanbul na Ankara, na kurudi ili kujionea umakinifu wa Amerika katika kuitazama “Uturuki ya Kiuthmani”, na kisha kuviangalia viashiria vya kiuthmani, ambavyo Erdogan anavionesha, na kufanya maamuzi kutokana na yote haya juu ya uhalisia wa hatari ya fikra hii, ili Waislamu wasianguke ndani ya mtego huu mkubwa wa kisiasa.

Uhakika wa Utawala Nchini Uturuki

Ama kuhusu uhakika wa utawala nchini Uturuki, ni utawala wa kisekula kikamilifu. Nidhamu ya kisekula iliyojengwa na Mustafa Kamal juu ya magofu ya Khilafah ya Kiuthmani bado angali mtawala nchini Uturuki leo. Muundo wa dola hii, ima wa kiraisi kama alioutaka Erdogan kwa kuufanyia kura ya maamuzi mnamo 2017, au muundo wa kibunge ambao dola huongozwa na waziri mkuu, yote haya ni maelekezo ya nidhamu ya kirasilimali ambayo hayana uhusiano wowote na Dini yetu tukufu, na hayana mafungamano na Uislamu; ni nidhamu isiyokuwa ya Kiislamu kutokana na muundo wake wa utawala. Ama kuhusu siasa iliyotabanniwa upande wake wa ndani, ni sera ya kirasilimali isiyokuwa ya Kiislamu. Leo, sheria za Uturuki ni sheria zinazotungwa na bunge, na hakuna hata moja wapo inayotokana na sheria za Kiislamu isipokuwa baadhi tu ya sheria zinazohusu mambo ya mtu binafsi ambazo ni chache. Hata kadhia ya kuowa zaidi ya mwanamke mmoja inaruhusiwa na Uislamu, lakini imeharamishwa na kutoruhusiwa kwa mujibu wa sheria ya Uturuki na hata kumruhusu mwanamke wa Kiislamu kuolewa na mwanamume kafiri. Sheria za mahakama zimetungwa na mwanadamu na wala hazikujengwa juu ya Shariah. 

Licha ya chama cha Uadilifu na Maendeleo (AKP) cha Erdogan, chama tawala, kusifiwa kama chama cha Kiislamu, ni sura tu ambacho hakijabadilisha chochote katika sheria za kibinadamu na wala hakifanyi majarabio ya kuzibadilisha. Baadhi ya makundi, yanayosifiwa kuwa ya Kiislamu, yameweka wazo la “kutenda hatua kwa hatua”, katika utabikishaji wa hukmu za kisheria, na ufahamu mwepesi wa “kutenda hatua kwa hatua” pasi na kuzingatia hukmu ya kisheria juu yake, ni dola iliyojengwa juu ya utekelezaji Uislamu “hatua kwa hatua” inatekeleza baadhi na kuakhirisha sehemu nyengine, na kila mwaka inaongezea sheria mpya juu ya hukmu ambazo kiasili zilikuwepo. Huu ndio ufahamu mwepesi. Lakini, Raisi wa Uturuki Erdogan na chama chake cha “Kiislamu” hatabikishi hukmu yoyote ya kisheria (isipokuwa kwa yale tuliosema yanatokana na sheria chache za mambo ya kibinafsi ambazo kiasili zilikuweko kabla ya Erdogan) licha ya utawala wake nchini Uturuki tangu 2002.

Lakini, utabikishaji wa hukmu za sheria katika dola haujaongezeka, na yeye (Raisi Erdogan) habebi fikra ya «kutenda hatua kwa hatua» kamwe; haipigii debe, na katika mipango yake ya uchaguzi hakuna mahali popote hukmu za sheria zilipotajwa; yeye ni msekula wazi wazi, na wala haoni aibu kwa usekula wake. Aliitaka hata pia Ikhwan al-Muslimina nchini Misri kulingania usekula (Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan aliwasihi Wamisri kufanya kazi kujenga dola ya kisekula, akisisitiza kuwa dola ya kisekula haimaanishi dola iso Dini. Erdogan alitoa mwito wakati wa mkutano wake na kituo cha runinga nchini Misri cha “Dream” kuunda katiba juu ya misingi wa kisekula, ikizingatia Uturuki kuwa kiigizo cha dola hiyo ya kisekula. Alitaja kuwa yeye ni Muislamu, licha ya kukalia wadhifa wa Waziri Mkuu katika dola ya kisekula). (DWA German Agency 13/9/201) 

Erdogan na chama chake hata ni wakali zaidi katika kupigana dhidi ya Sharia (Chama tawala cha Uadilifu na Maendeleo (AKP) nchini Uturuki kimeamua kutuma manaibu wake wawili katika mji ulio katika Bahari Nyeusi wa Riza kufungua uchunguzi rasmi kwa mwanachama wa chama hicho na Meya wa mji huo, Khalil Bakrji, kutokana na taarifa za vyombo vya habari ambapo alitoa mwito wa kuruhusu ndoa za wake wengi nchini Uturuki, kinyume na katiba. (dot Misr 14/1/2014) 

Zaidi ya hayo, mtazamo wa uaswabia wa Kituruki ndio kitovu cha serikali ya Uturuki. Waislamu Wakurdi pamoja na Waarabu ni wachache waliochini ya dola ya Uturuki, na hawaonekani katika vyeo serikalini kama wanavyoonekana Waturki. Dola hii haifichi umbile lake la kitaifa lisilokuwa la Kiislamu, kana kwamba Muhammad (saw) hakusema:

«دَعُوهَا فَإِنَّهَا مُنْتِنَةٌ» "Uacheni (uaswabia) hakika huo ni uvundo." Uislamu unapinga na kuharamisha kila uaswabia unaoganya Umma mmoja wa Kiislamu.

Sera ya kigeni ya Uturuki haikujengwa juu ya Uislamu. Hakujawahi kuwa na matendo yoyote kutoka kwa dola ya Uturuki ya kulingania Uislamu ng’ambo. Kila mmoja anapenda kujenga msikiti nchini Amerika au kufungua kituo cha Kiislamu eneo la Magharibi na serikali zote katika ulimwengu wa Kiislamu zinafanya hili, mithili ya Dola za Ghuba, Misri na nyenginezo, na wala hili si maalumu kwa Uturuki pekee. Jamii za Waislamu ng’ambo zinajenga misikiti kwa usaidizi au pasi usaidizi wa biladi za ulimwengu wa Kiislamu. Uturuki haipigii debe kadhia za Waislamu katika sera yake ya kigeni kama Waislamu; inadumisha mahusiano yake ya kidiplomasia na umbile la Kiyahudi, na kushirikiana nayo kijeshi licha ya uhalifu wake wa kila siku kwa watu wa Palestina, ambao Erdogan anajigamba kuwasaidia, lakini usaidizi wa Kituruki kwa watu wa Palestina haukufikia hata ushuri moja ya usaidizi wa nchi yoyote ya Ulaya.

Usaidizi huu kiasili ni sehemu ya mkakati wa Kimagharibi wa amani kwa umbile la Kiyahudi. Nchini Syria, Bashar ameuwa maelfu ya watu. Amerika, washirika wake wa Ulaya na Urusi zimejitumbukiza nchini Syria. Lakini kujitosa kwa Uturuki, kulikotokea baada ya miaka ya mauwaji, kulikuwa kwa kumpendelea mhalifu Bashar. Uturuki inayashinikiza makundi yaliyo nyuma yake kujadiliana na Bashar jijini Ankara, Astana na Geneva, na inayatoa kutoka katika viwanja vya vita na Bashar na kuyapeleka katika viwanja vyengine vya kupigana kwa ushirikiano “Ngao ya Furaat” kupigana dhidi ya makundi ya Kikurdi katika “Tawi la Olive”, na kuingilia kati kote kwa Uturuki kunapelekea katika ushindi wa Bashar juu ya mabaki ya mapinduzi ya kiikhlasi. Wakati wa mgogoro wa Rohingya, ulioufanya ulimwengu kulia, Uturuki ililiwakilisha jeshi katili la Myanmar kwa msaada ilioutangaza kuwapelekea watu wa rohingya.

Hivyo basi, ni wazi kuwa Uturuki ni dola ya kisekula katika utawala wake na katika sera yake ya kindani na ya kigeni, na wala hakuna mwelekeo wa Sharia ya Kiislamu hata kwa dhana ya “utendaji wa hatua kwa hatua” hii ni licha ya sharia kujiweka mbali na fikra hii. Na ikiwa mambo yako wazi namna hii, wale watakaodanganywa na Uislamu wa Erdogan wa Uturuki wanajidanganya nafsi zao. Uturuki si kama biladi nyenginezo katika ulimwengu wa Kiislamu.  

Inawaandama wabebaji Da’wah ya Kiislamu na kuwafunga magerezani. Dola hii haihimili ulinganizi wa kutabikishwa kwa Uislamu nchini Uturuki na inawabandika majina walinganizi wake kuwa wenye misimamo mikali na magaidi, kama vile wafanyavyo Wamagharibi.

Utiifu wa Raisi Erdogan wa Uturuki

Utiifu wa Erdogan katika sera yake ya kigeni hauhitaji tafakari ya kina. Uturuki, nyuma ya Erdogan na pamoja naye, ni dola ya NATO, yaani, rasmi iko chini ya taasisi ya Amerika ya utoaji amri za kijeshi, na ni mwenyeji wa kambi kubwa zaidi ya kijeshi ya NATO, kambi ya Incirlik. Kutokana na kambi hii, ndege za kijeshi za Kiamerika huanzisha mashambulizi ya mauwaji ya Waislamu nchini Syria na Iraq. Huu ni upande mmoja, na upande mwengine, Uturuki imejaribu kwa miaka mingi kuingia katika Muungano wa Ulaya na inajiita kuwa ni nchi ya Ulaya, na imejisalimisha kwa masharti ya Muungano huo ili kujiunga nao. Na licha ya kukataa kwa nchi za Ulaya kutokana na idadi yake kubwa ya Waislamu, ambao ndio uhakika, haikuachana na ombi lake la kutaka kujiunga; hivyo basi, dola ya Uturuki ni dola ya Kimagharibi katika matamanio yake na mwelekeo wake.    

Raisi Erdogan hajabadili mtindo huo. Ama kuhusu kuimarisha mahusiano yake na ulimwengu wa Kiislamu, anajibu hisia zake za kukataliwa kwake kujiunga na Muungano wa Ulaya upande mmoja, na upande mwengine, ana mahusiano na serikali za kibinadamu ndani ya nidhamu ya kibinadamu iliyoko sasa, na si sehemu ya jaribio la kubadilisha hilo. Hili ni wazi, wala halihitaji tochi.

Wanasiasa wanaochunguza kwa makini sera za nchi huona bila ya ugumu wowote fungamano baina ya dola ya Uturuki na Amerika. Amerika ndio iliyomsaidia Erdogan na chama chake kudhibiti Uturuki kupitia mbinu nyingi za kisiasa na uwezo wa kifedha na kadhalika. Amerika ilitaka kuwadhibiti majenerali wa jeshi la Uturuki wenye utiifu kwa Ulaya; hili lilitimia baada ya kutibuka kwa mapinduzi ya mnamo 2016, licha ya mchezo uliopangwa kumbwagia lawama “Gulen”, na mchezo wa kuilaumu Amerika kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi lililofeli. Pengine matukio ya Syria ndio mifano iliyo wazi zaidi ya ushirikiano kati ya Erdogan wa Uturuki na Amerika. Huduma za kijasusi za Uturuki pamoja na za Amerika zilikawaribisha wazi wazi waasi kutoka katika maafisa wa jeshi la Syria katika majaribio ya kuunda kundi pinzani la kisilaha kama yale ya “Majenerali wa Kijeshi” na “Amri Kuu ya Majeshi” ili kuyapoteza dira mapinduzi ya Syria na makundi yake ya kijeshi kutoka katika njia ya kuing’oa serikali na kuunda dola ya Uislamu.   

Uturuki na Amerika zilikuwa zikifanya kazi pamoja na wazi wazi, na hii ndio iliyokuwa hali ya makongamano ya upinzani ya Syria ambayo yalisimamiwa na Balozi wa Amerika nchini Syria, Ford, jijini Istanbul na Ankara. Pindi Amerika ilipoamua kujiondoa kutoka katika majadiliano na Urusi juu ya Syria baada ya kuwasili kwa Trump, iliifanya (Amerika) Uturuki kuwa naibu wake katika majadiliano ya Astana, ambayo yalizalisha ndoto ya Amerika ya kusitisha vita nchini Syria na kupunguza joto la uhasama huo na wazo la dola mdhamini. Uturuki ni moja ya nchi zilizodhamini kusitisha vita, lakini serikali za Bashar na Warusi hazikusitisha vita hivyo, na Uturuki haikudhamini chochote. Na kama ilivyo Amerika katika Baraza la Usalama, inaonesha wasiwasi wake, huku serikali ya mhalifu nchini Syria ikizitia mkononi tena Barada eneo la Magharibi mwa Ghouta na Chifonia na mengineo eneo Mashariki mwa Ghouta, na kabla ya hapo vita mjini Idlib, yote ni maeneo yanayokusudiwa kupunguzwa joto la kivita ambapo Uturuki ni mdhamini wake. Sera za Uturuki ni mmuliko wa sera za Amerika: “Iwache serikali ishinde”. Hivyo basi, utiifu wa Raisi wa Uturuki Erdogan ni kwa Amerika pekee, na anashirikiana nayo kikamilifu katika sera ya kigeni ya Uturuki.

Kuyavutia Makundi ya “Uislamu Poa” kwa Uturuki

Matendo ya Uturuki ya kuyavutia makundi ya “Uislamu Poa” yamejitokeza wazi wazi kwa mujibu wa sera ya Kimagharibi ya “gawanya utawale”. Uturuki dola kubwa ya “Kisunni” ina uwezo wa kuyavutia makundi ya Kiislamu ya Kisunni kama vile Iran ina uwezo wa kuyavutia makundi ya Kiislamu ya Kishia kwa mujibu wa sera ya Kimagharibi. Chama tawala cha Uturuki kimesifiwa kuwa chama cha “Kiislamu”, hili likirahisisha mchakato wa kutia mvuto. Hivyo basi, makundi ya Kiarabu yakawa changamfu nchini Uturuki, ambayo yanasifiwa kuwa ya “Uislamu Poa”. Istanbul imekuwa “qibla” cha Ikhwan al-Muslimina, hususan wale wanaokimbia serikali ya Sisi nchini Misri baada ya mapinduzi ya 2013 dhidi ya Raisi Morsi; kwa hivyo tunayaona makongamano na ruzuku na usaidizi kwa vyama vya “Uislamu Poa”, kana kwamba ni sera mpya iliyotabanni na Erdogan nchini Uturuki, kinyume na mtangulizi wake mamlakani tangu enzi nyeusi ya Mustafa Kamal. Kutokana na usaidizi na uharakishaji huo, umaarufu wa Erdogan umejitokeza katika makundi ya Kiarabu, yanayosifiwa kuwa ya “Uislamu Poa”. Amepewa lakabu ya “Kiongozi adhimu wa Kiislamu” na kinara wa Chama cha An-Nahdha cha Tunisia, Rached Gannouchi alimsifu, na hata Qardhawi kumsifu kama “Sultan”. Uturuki imekuwa pepo kwa viongozi wengi wa Hamas ambao wamekwama, hususan baada ya Saudi Arabia na Misri kuikata Qatar, baada ya Qatar kuwaomba kuondoka.

Tunapo tazama kwa ndani zaidi, tunaona kuwa nchi zote zilizo na mamlaka ya eneo hilo zinajaribu kuishawishi hali ya kindani ya nchi dhaifu zinazozizunguka kupitia vyama, upinzani na makundi ya kisilaha katika maeneo muhimu. Ikiwa ushawishi wa Dola kuu ni muhimu kwa dola ndogo, basi ushawishi wa dola ndogo ni muhimu katika kiwango cha vyama na makundi katika nchi jirani. Uturuki, na Amerika nyuma yake, inataka kuyavuta makundi haya upande wake, kupitia njia fiche. Na kwa hivyo si kizingiti dhidi ya sera za Amerika, na inatarajia kwamba vyama hivi vitakuwa ni sehemu ya ala zake tofauti tofauti za sera yake. Kwa mfano, usaidizi wa kifedha na wa kisiasa na kutoa majukwaa ya vyombo vya habari na uharakishaji kama kutoa hifadhi na usalama kwa viongozi wanaoandamwa na serikali zao, ambayo yatafanikisha yafuatayo:  

1- Nchini Palestina, Amerika inataka kuweka ushawishi wa Uturuki juu ya Hamas kama hasimu kwa ushawishi wa Qatar, ili isiiruhusu Qatar, ambayo nyuma yake ni Ulaya, kuzuia miradi ya Amerika ya kutatua kadhia ya Palestina.

2- Nchini Syria, Uturuki imefaulu kupitia usaidizi wa kifedha, pamoja na “hadhi” yake ya “Uislamu poa”, kuyavuta makundi mengi ya kijeshi ya Syria yaliyo katika vuguvugu la “Uislamu poa” kuingia katika majadiliano ya kusitisha vita na kuyavuta katika majadiliano ya Astana pamoja na Warusi na serikali (ya Syria). Imeyadanganya kuwa inayaunga mkono kama “dola mdhamini”, na ikayasukuma katika vita haramu kama kupigana na Wakurdi badala ya kupigana na kuing’oa serikali ya kihalifu. Hii ndio mojawapo ya siri za kurefuka kwa uhai wa serikali ya Syria ambao Amerika inautoa kupitia Uturuki na wengineo.

Baada ya mapinduzi ya 2013 nchini Misri, viongozi wengi wa Ikhwan al-Muslimina walielekea Uturuki kwa sababu chama chake tawala ni cha “Kiislamu”. Hili ni muhimu mno kwa sera ya Kiamerika inayotaka kudhibiti harakati za Ikhwan al-Muslimina baada ya mapinduzi dhidi ya Morsi, na kuzuia hatari yoyote kuu kwa serikali ya Sisi. Pindi matendo yao yatakapokuwa wazi, upande wa pili utaweza kuyakabili na kuyatibua. Amerika pia inataka Dola ya Qatar kutokuwa mshawishi pekee juu ya harakati za Ikhwan al-Muslimina.

Katika nchi za maghrib, harakati za “Uislamu poa”, kama vile Chama cha An-Nahdha cha Tunisia na Vuguvugu la Uadilifu la Morocco na nyenginezo, zimevutiwa sana na mafanikio ya Uturuki ya Erdogan na zinataka kujifunza kutokana na ujuzi huu wa utawala na zinataka kujenga mahusiano thabiti na Uturuki. Huu ndio mwanzo wa ushawishi wa Uturuki na Amerika nyuma yake pamoja na ala nyenginezo katika nchi za Maghrib na jaribio la kuingiza ushawishi wa Kiamerika ndani yake kama badali ya ushawishi wa Kiingereza na Kifaransa. Huu ni mchezo hatari; pindi harakati hizi za “Uislamu poa” zitakapojipata katika uwanja wa mizozo ya kimataifa na kieneo ambayo haina uhusiano wowote na Dini yao na mfumo wao zilioutangaza, na kugeuka kuwa kama harakati nyenginezo za kisekula, kuni za moto wa mizozo ambayo kamwe haifaidishi Ummah. Kiasili, kubadilisha nidhamu ya kisekula kwa nidhamu nyengine ya kisekula sio mabadiliko kwa mujibu wa sharia, lakini ni muhimu sana katika mizozo ya kimataifa, hususan kwa kuwa Amerika inataka kuzing’oa serikali tiifu kwa Uingereza na Ufaransa kwa njia yoyote ile, ima kupitia chaguzi au kupitia matumizi ya silaha.

Uturuki inawavutia wapinzani wa “Kiislamu” kutoka katika nchi nyengine nyingi, hususan kama inavyo tangaza mara kwa mara, kama ilivyokuwa wakati wa vita vya Mosul, kama kitovu cha «Masunni», ndani ya msingi wa miradi ya Kiamerika ya mgawanyiko wa kimadhehebu katika eneo hilo. 

Hatari ya Mradi wa “Uturuki ya Kiuthmani” na Pondo ya Kiamerika Kwao

Baada ya Uturuki kuwa ya kisekula kufuatia Mustafa Kamal kutenganisha mshikamano wake na Uthmani, imeonekana katika miaka michache iliyopita kuwa Erdogan amekuwa “akiichafua” sera hii ya Uturuki, na wakati mwengine inaonekana kuwa huenda anajaribu kuivunja. Majaribio ya Erdogan yanagongana na mawimbi ya Kikamali ya upande wa kulia nchini Uturuki; anazitilia maanani sana rai zao katika hesabu zake. Mawimbi haya yalikashifu namna mke wa raisi, Abdullah Gul, alivyokuwa akijitokeza, kwa kufinika kichwa chake; yalihisi kuwa “mke wa raisi”, nchini Uturuki hapaswi “kuchafua” fikra ya dola ya usekula, kwa kuwa hijab inatoa sura ya Uislamu.  Lakini katika miaka michache iliyopita, Erdogan amesubutu kuvuka mpaka. Baadhi ya nembo za Kiuthmani zimeibuka nchini Uturuki, kama vile walinzi wa Erdogan, na sare zao za Kiuthmani na kufufuliwa kwa turathi za Kiuthmani. Hii ni ikiwemo kile kilichonukuliwa na shirika la habari la Anadolu mnamo 10/2/2018 M: (Raisi wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mnamo Jumamosi alikashifu uadui kwa baadhi ya historia ya Sultan Abdul Hamid II, ambayo imejaa mafanikio … alionya dhidi ya kuchukua kwa ubaguzi inaposomwa historia. Erdogan alitaja kuwa “kuna wale wanaofanya kazi kwa kudumu kurudisha mwanzo historia ya Uturuki kuanzia 1923 (Tarehe iliyobuniwa Jamhuri ya Uturuki), na kuna wale wanaofanya bidii ya mchwa kutung’oa kutoka katika asili zetu na katika maadili yetu ya jadi.” Aliongeza: “Kundi ambalo kiongozi wa upinzani pia yumo ndani (Raisi wa chama cha Watu cha Kijamhuri (KDP), Kamal Klegodaroglu) kimeweka kiwango cha utiifu kwa jamhuri, kwa msingi wa uadui kwa babu (zetu).” Aliendelea: “Kwao wao, Jamhuri ya Uturuki ni ya kileo, na wala haiwakilishi fungamano na Maseljuk na Mauthmani walioongoza mfumo wa kiulimwengu kwa karne sita.”       

Hili ni jambo la kindani la Uturuki, ama kuhusu pondo inayotiwa na Amerika kuangazia sura ya leo ya “Kiuthmani” ya Erdogan wa Uturuki yaweza kuonekana ifuatavyo:

Amerika imetoa uwezo mkubwa kwa Uturuki kujenga kambi za kijeshi ng’ambo, na hii ni kuionesha Uturuki kama nchi kubwa. Kadhia hii ilianza pindi Uturuki ilipotuma vikosi vyake mnamo 2014 kutoa mafunzo kwa Peshmerga katika kambi ya Baasheqa nchini Iraq.

Kisha, katikati mwa mzozo wa Qatar, Uturuki ilituma wanajeshi wake katika kambi mpya ya Uturuki nchini Qatar, na inashangaza kuwa wanajeshi wa Uturuki mnamo 2017 walikuwa wakitua katika kambi ya Al-Udeid nchini Qatar, ambako kambi kubwa ya Amerika iko, na hili halingewezekani bila ridhaa ya Waamerika. Amerika, inakusudia kuwa inapopanga kupeleka thuluthi mbili ya majeshi yake katika mipaka ya China, inapanga nchi yenye kuiamini kama Uturuki kuchukua nafasi ya baadhi ya kambi zake au kuwa sehemu yake kama Al-Udeib nchini Qatar na pia kambi ya kijeshi ya Uturuki nchini Somalia.  

Nchi ndogo hazina kambi za kijeshi ng’ambo. Hili ni dhihirisho la ukubwa, lakini kudhani kuwa Uturuki ni dola kuu yenye nguvu ni makosa katika tafakari ya kisiasa. Uturuki haiwezi kutatua matatizo yaliyo karibu au muhimu kwake, kama vile Amerika kuwahami kisilaha Wakurdi wa Kisyria, kwa mujibu wa maslahi ya Kiamerika. Haiwezi kujitosa barabara ndani ya jirani yake Syria, kama Iran, Urusi na nchi zilizo katika muungano wa kimataifa na Amerika. Ikiwa haiwezi kutatua matatizo yake msingi na ya dharura, hivyo basi itapata ugumu katika kujenga maslahi yake nchini Qatar, Dola za Ghuba na Somalia. Na yanayoweza kueleweka pekee kupitia kambi zake za kijeshi katika nchi hizo ni kuwa ziko kuhudumia maslahi ya Kiamerika.

Wakati wa ziara yake nchini Sudan mnamo 24/12/2017, Raisi wa Uturuki Erdogan alizuru kisiwa cha Sudan cha Swakin na kutangaza mradi wa kufufua turathi za Kiuthmani. Kisiwa hicho kilikuwa ni kitovu cha hifadhi ya jeshi la wanamaji la Kiuthmani la Bahari Nyekundu. Kulikuwa na ripoti za faili za siri za kongamano la Swakin kukigeuza kuwa kambi ya kijeshi ya Uturuki. Wakati wa mkutano wake naye, Raisi wa Sudan, Bashir, alisema kuwa anamuona Erdogan kama “mabaki ya utawala wa Kiuthmani”. Kwa maana nyengine, Erdogan anazizunguka nchi zilizotiifu kwa Amerika kama Sudan kupigia upatu sura mpya ya Uturuki ya Kiuthmani. Hii ni pondo kubwa ambayo haiwezi kutokea pasi na usaidizi kutoka kwa Amerika.

Wale wanaodhani kuwa watawala wa Kiarabu wako huru katika maamuzi yao kupokea kambi za kijeshi za Uturuki au nyenginezo wanajidanganya. Kila mmoja wao anafuata sera ya bwana wake, na Bashir anafuata sera ya Amerika. Hivyo basi, uwezo wa Bashir kwa Erdogan umo ndani ya sera ya Amerika, ambayo leo inaiunda sura ya Uturuki.

Wakati wa ziara yake nchini Chad, Erdogan alitaja kuwa “mahusiano baina ya nchi mbili hizi ni ya jadi tangu karne ya kumi na sita ambapo utawala wa Kiuthmani ulikuwa ukipanua ushawishi wake katika eneo hili.” Raisi wa Chad, Idriss Deby, alijibu: “Uturuki ni nchi kubwa. Kuna historia ndefu … ni nchi inayojulikana na maarufu duniani.

Uturuki ni nchi muhimu iliyocheza dori kubwa kwa jina la ubinadamu na jamii ya Kiislamu katika historia yote”. (Shirika la habari la Kituruki la Anadolu 26/12/2017). Hii yadhihirisha mkondo mpya wa Kituruki kupitia kuangazia “Uturuki ya Kiuthmani”, ambayo haikuweko miaka ya mwanzoni ya utawala wa Erdogan, lakini hatimaye imeibuka.

Kuna swali limebakia, linalohusiana na umakinifu wa Amerika katika fikra na mradi wa “Uturuki ya Kiuthmani”. Ikiwa tunatambua hofu ya Amerika kwa tetemeko la Khilafah ni ya kihakika, na ndio sababu inatabanni sera ambazo zinatabikishwa na maafisa. Hofu hii haikuibuka tu kutokana na fikra ndani ya vituo vya elimu na benki nchini Amerika. Amerika ilinufaika pakubwa kutokana na tangazo la Khilafah la Baghdadi mjini Mosul; manufaa haya yalikuwa katika muundo wa kumakinisha hali nchini Syria ambayo ilikuwa inanadi Khilafah. Khilafah ya Baghdadi ilizuka kama mchanganyiko wa umwagikaji damu, starehe za wanawake “wake wenza” na utawala wa mizimu, makaburi na panga, hivyo basi ikiwasilisha sura mbaya ya Dola kuu ya Khilafah. 

Hii ni kwa upande mmoja, na kwa upande mwengine, sera za Kiamerika na Kimagharibi kwa jumla zimefeli kulipa utawala vuguvugu la “Uislamu poa”. Utawala wa mwamko nusu wa chama cha An-Nahdha cha Tunisia umefeli, na utawala nusu wa Yemen umefeli. Yaliyoifika Gaza sio makubwa, na yaliyoifika Ikhwan al-Muslimina nchini Misri yamefeli. Kufeli kukubwa kwa Amerika ni kuwa kuwasili kwa makundi haya hayakuweza kukomesha yale yanayolinganiwa na Amerika “Uislamu wa misimamo mikali” – ambalo ndio lengo la kuruhusu makundi haya ya “Uislamu poa” kupata utawala. Hivyo basi Amerika ilitupilia mbali fikra ya kuruhusu makundi ya “Uislamu poa” kuchukua utawala.  

Kwa upande mwengine, hali ya upinzani katika Ummah wa Kiislamu inakuwa katika njia inayoiogopesha Amerika kutokana na matukio ya ghafla kama mapinduzi ya Kiarabu, na Amerika ni dola kuu yenye nguvu ambayo inafanya majaribio ya miradi tofauti tofauti ambayo inaitabikisha moja kwa moja au kupitia wafuasi wake, ili maslahi yake ya kimataifa yawe salama. Hivyo basi utafutaji wa Amerika wa mradi mpya bila shaka ni kwa lengo la kutatua hali ya upinzani katika ulimwengu wa Kiislamu, na wala sio kuyaacha matukio kutokea kwa ghafla ambayo huenda yakasababisha tetemeko kubwa, Khilafah ya kweli katika njia ya Utume.

Ama kuhusu kunufaika pakubwa kwa Amerika kutokana na tangazo la Khilafah la Baghdadi mjini Mosul, haikubaliki kuiacha nje fikra inayorudiwa rudiwa ya “Khilafah bandia” iliyodhaminiwa na Amerika. Lakini, kumekuwa na viashiria vya kutosha vya Raisi wa Uturuki Erdogan kuinasibisha na dola ya Kituruki ya leo na yale yaliyokuwa kabla ya tangazo la kuvunjwa Khilafah Uthmaniya mnamo 1923, pamoja na uwezo uliotolewa na Amerika kwa Uturuki nchini Sudan na nchi nyenginezo washirika wake.

Mradi huu wa Amerika huenda ukawa uko matayarishoni na kwamba Raisi wa Uturuki Erdogan anatambulisha hili kupima uwezekano wake. Hili pia linaashiriwa na mgongano wa Uturuki na nchi za Ulaya kana kwamba inataka kujifananisha na dola ya Kiuthmani. Erdogan aliisifu Ujerumani na Uholanzi kama “mabaki ya Unazi” kana kwamba anazipa mgongo kwa njia isiyo ya kawaida. 

Kutamatisha, si busara kupuuza viashirio vyote vya mradi hatari mno wa Amerika wa kuigeuza Uturuki kuwa dola ya “Khilafah bandia” ili kusimama dhidi ya Khilafah ya kikweli. Tangazo lake litautingisha ulimwengu mzima. Mradi kama huo bandia wa Khilafah huenda ukawakanganya Waislamu, hususan wafuasi wa lile wimbi la “Uislamu poa” ambao viongozi wake wanajenga imani kwa Erdogan, na baadhi kumsifu kama Sultan, ingawa hafichi mahusiano yake na makafiri, ikiwemo umbile la Kiyahudi. Miradi kama hiyo haiwezi kutabikishwa kwa miezi, bali yahitaji kazi kubwa ya kindani pamoja na vyama vya Kikamali na kinje.

Lakini kitu muhimu zaidi kinachohitajika kutoka kwa Waislamu wenye ikhlasi, waliounganisha njia yao juu ya Uislamu safi na mtukufu kwa mujibu wa dalili za Kisheria, na wale wanaotaka kazi yao iwe kwa ajili ya Allah pekee, ni lazima waendelee kwa umakinifu katika kujenga dola ya Uislamu, Khilafah Rashida ya pili kwa njia ya Utume, ambayo utiifu wake ni kwa Mola na sheria zake ni zile zitokazo katika Dini imara. Itaitingisha Amerika na Wamagharibi, na moja kwa moja itaanza kuondoa ushawishi wao na kambi zao za kijeshi kutoka katika ulimwengu wa Kiislamu, na kufagia vibaraka wao kutoka katika mwili wa Ummah wa Kiislamu, kama vile najisi anavyoondolewa nguoni. Na itatabikisha sheria tukufu za Uislamu.  Na watu watafurahia na Baraka zitateremka kutoka mbinguni, na hali ya Ummah leo itaimarika, na utakuwa kama ulivyokuwa jana. Itakusanya nishati yake na kujenga nguvu zake na kuhofisha adui yake, adui wa Allah, na hili haliko mbali, na kwa kila amri ina muda wake. Twamuomba Allah kwamba jambo hili liwe karibuni katika siku zinazokuja, na siku hiyo watafurahi waumini kwa ushindi wa Allah na izza ya Uislamu mtukufu.

Na: Essam Al Sheikh Ghanim

Chanzo:

Al Waie Magazine - Issues 378-379-380 - 33rd year, Rajab-Sha'ban-Ramadan 1439 AH, April-May-June 2018 CE

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 07:23

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu