- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Je! Utawala wa Kifalme Utaweza Kubakia Hai?
(Imetafsiriwa)
Kifo cha Malkia Elizabeth II kimeifanya Uingereza kuingia katika kipindi cha maombolezi ya pamoja. Upeperushaji mpana wa mazishi na utawala wa malkia wa miongo saba umeshughulisha watu. Kumekuwa na mihemko na rambirambi kutoka kote ulimwenguni huku wengi wakimuona Malkia Elizabeth II kama mtu thabiti katika siasa za Uingereza. Nyumba ya Kifalme ya Windsor leo ndio familia ya kifalme iliyohudumu kwa muda mrefu zaidi na Malkia Elizabeth II alikuwa mfalme aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi, utawala wake ulihusisha mawaziri wakuu 15, kuanzia Winston Churchill na kumalizia na Liz Truss, ambaye Elizabeth alimteua kuwa waziri mkuu mnamo Septemba 6. Huku enzi ya Elizabeth inapofika mwisho, enzi ya Mfalme Charles III inaanza; changamoto kubwa kwa Nyumba ya Kifalme, kando na aibu zake nyingi za mara kwa mara, sio tu kuhifadhi uhalali wake, bali jinsi taasisi ya zamani ya zama za kati inabaki kuwa muhimu katika ulimwengu wa kisasa.
Malkia Elizabeth amepokea sifa nyingi kwa kujitolea kwake katika kazi na kwa kuwa kipengee maarufu cha maisha ya kisiasa ya Uingereza. Amekuwa mtu ambaye anaonekana kutoa utulivu wakati maisha ya kisiasa ya Uingereza yanasuasua sana. Lakini je, kazi ya Familia ya Kifalme ni nini? Kwa baadhi, kazi ya Familia ya Kifalme ni kuunga mkono mfumo wa kidhalimu ili kuwazubaisha watu kutokana na hali halisi za maisha yao kwa gwaride na ibada. Kwa wengine, ufalme ni ishara Waingereza wanaweza kuungana karibu ambao pia hutoa utulivu na ni mwongozo kwa serikali. Ilhali kwa baadhi ya wengine, ufalme wa kisasa ni aina ya nguvu laini, inayotoa taswira ya kitaifa kwa ulimwengu na kuwavutia wageni, kutembelea kama watalii. Wanafamilia wa hivi karibuni zaidi, kama vile Kate Middleton na Meghan Markle (ambaye alikuwa Binti Mfalme wa Sussex hadi alipokiacha cheo chake cha kifalme) kuingia ndani ya Familia ya Kifalme wameonekana na wengi kama ushindi wa nguvu laini kwa Uingereza. Kazi ya Ufalme wa Uingereza sio kama ilivyokuwa zamani licha ya mamia ya miaka ya historia. Familia ya kifalme ya Uingereza imeweza kubakia hai katika eneo na enzi ambapo fadhila za urithi ni jambo lililopitwa na wakati.
Historia ya Ulaya ya Zama za Kati inajumuisha wafalme wenye kutawala sehemu kubwa za bara hilo wakiwa wameungana na Kanisa la Kikristo baada ya kuporomoka kwa Himaya ya Kirumi katika karne ya 5. Kufuatia uvamizi na makaazi ya Viking katika karne ya 9, Ufalme wa Anglo-Saxon wa Wessex uliibuka kama ufalme mkuu wa Kiingereza. Alfred Mtukufu aliipata Wessex, akapata mamlaka juu ya Mercia magharibi na kujitwika cheo ‘Mfalme wa Waingereza.’ Mjukuu wake alikuwa mfalme wa kwanza kutawala juu ya ufalme wa muungano uliokaribiana na mipaka ya sasa ya Uingereza. Hawa wafalme wa Anglo-Saxon waliingia katika Ukristo na Askofu Mkuu wa Canterbury angempaka mfalme mafuta matakatifu, akimuinua mfalme juu ya kila mtu mwengine. Kuanzia wakati huu hadi katikati ya karne ya 17 Wafalme wa Uingereza walitawala.
Kufikia mwisho wa karne ya 18 kutelekezwa kwa ufalme wa Uingereza nchini Amerika na mapinduzi ya umwagaji damu nchini Ufaransa mnamo 1789 yalikuwa yamezipa falme jina baya. Demokrasia, utawala wa uwakilishi na dola za kitaifa yalikuwa ndio mlipuko. Ulimwengu ulikuwa unabadilika na utawala wa kifalme ulionekana kama kitu cha zama katili zilizopita.
Mwanzoni mwa karne ya 20, falme na himaya nyingi kuu za ulimwenguni zilipinduliwa. Qajar nchini Iran, Qing nchini China, Habsburgs nchini Austria na Hohenzollerns nchini Ujerumani zote zilifikia mwisho. Ufalme wa Uingereza ulibadilika na kujirekebisha. Malkia Victoria alitoka katika Nyumba ya Kifalme ya Kijerumani ya Saxe-Coburg na Gotha na mwanawe mkubwa, Mfalme Edward VII, alichukua jina la makaazi ya kila mara ya familia ya majira ya kiangazi katika vitongoji vya magharibi mwa London - Windsor, mnamo 1917, kwa sababu ya chuki dhidi ya Wajerumani wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia (WW1).
Kuporomoka kwa Uingereza kama dola ya kiulimwengu baada ya Vita vya Pili vya Dunia (WW2) kuliipa Familia ya Kifalme sababu mpya ya kuendelea kuwepo. Maafisa wa Uingereza walitumia maonyesho yote yaliyozunguka Familia ya Kifalme kama njia ya kuitangaza Uingereza kote ulimwenguni na kwa nadharia Malkia alikuwa mkuu wa nchi kwa mataifa na maeneo kadhaa. Familia ya kifalme ilikuja kuunda nguvu laini ya Uingereza katika enzi ambayo nguvu ngumu ya Uingereza ilikuwa ikipungua. Dori ya wanaufalme ilihusisha kusafiri mara kwa mara kwa Jumuiya ya Madola na zaidi ya kutoa medali, vyeo vya Himaya ya Uingereza na kuhudhuria sherehe na hafla za michezo kama ishara ya mamlaka ya Uingereza. Huku enzi ya baada ya WW2 ikiwavaa wale waliohusisha nembo ya kitaifa na ufalme walikuwa wakizidiwa na kizazi kipya ambacho kiliuona ufalme kama taasisi ya zama za kati.
Serikali mtawalia za Uingereza zimeitumia Familia ya Kifalme kama nembo ya taifa, rai jumla imekuwa ikiongezeka ya kuondolewa kwa ufalme. Hii ni kwa sababu utawala wa kifalme unakwenda kinyume na mambo mengi ya maisha ya kisasa. Ufalme kutokana na uzawa una nafasi ya upendeleo nchini, kamwe hawakuchaguliwa. Huku wengi wakiiona familia ya kifalme kama chanzo cha kiburi, kashfa za mara kwa mara zimeharibu sifa zao. Talaka, mahusiano ya pembeni, kukwepa kodi, kuondoka kwa Meghan Markle na Mwanamfalme Harry kama wanafamilia ya kifalme wanaofanya kazi na tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji dhidi ya Mwanamfalme Andrew: yote yameharibu vibaya sana sifa ya Familia ya Kifalme. Ingawa uungaji mkono wa umma kwa Malkia Elizabeth ulikuwa wa juu kama 60%, maoni kwa wanafamilia wengine wa kifalme yamekuwa ya chini na yanaendelea kupungua na hii inaiweka Nyumba ya Windsor katika hali mbaya baada ya kufariki Malkia Elizabeth II.
Malkia Elizabeth aliweza kuuweka ufalme kuwa muhimu kwa kutabanni na kuweka dori ya wanafamilia ya kifalme kwani falme zingine ziliondolewa au kupinduliwa kwa nguvu. Wanasiasa wa Uingereza pamoja na tabaka tawala la Uingereza wanaiona Familia ya Kifalme kupitia macho ya kiuchumi na nguvu laini ambayo huleta uaminifu na watalii nchini Uingereza. Malkia Elizabeth aliweza kuendeleza utamaduni wa enzi za kati kutoa taswira ya ufahari, umoja na kitambulisho cha kitaifa kwa Uingereza. Lakini kwa kufariki Malkia na huku Mfalme Charles akichukua dori la ubwana, ufalme wa Uingereza unakabiliwa na kazi kubwa sana ya kuweka taasisi ya zamani za kati na ya kiurithi kuwa muhimu.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Adnan Khan