- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Hukmu za Uislamu kuhusiana na Jinsia, Jinsia Isiyofahamika, na Kubadili Jinsia
(Imetafsiriwa)
Utanguliz: Mdahalo juu ya Ulinzi wa Watu Waliobadili Jinsia katika Ulimwengu wa Kiislamu
Mnamo tarehe 5 Septemba 2022, Seneta wa Pakistan Mushtaq Ahmad aliwasilisha mswada wa marekebisho katika Sheria ya Kuwalinda Wanaobadili Jinsia, 2018, kwa Kamati ya Kudumu ya Seneti ya Haki za Kibinadamu. Katika mkutano huo, Seneta Mushtaq Ahmad, alisema kuwa, "Transgender ni neno la Kimarekani, halina nafasi katika Uislamu, na sheria kuhusu jamii ya watu waliobadili jinsia ni kinyume na Qur'an na Sunnah na itakuza ushoga." Mjadala mpana kuhusu ulinzi wa watu waliobadili jinsia, umekuwa mada ya mkanganyiko ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu. Imewaongoza hata wachache kutilia shaka uhalali wa Uislamu katika zama hizi.
Ili Waislamu wazungumze na kutenda kulingana na yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu (swt), ni muhimu kuyaweka mambo yanayohusu jinsia katika mapali pake sahihi. Uislamu unawataka Waislamu wachunguze suala (mas’alah) hilo kisha wachukue hatua kwa mujibu wa hukmu za Shariah kuhusiana na suala hilo. Hivyo basi Waislamu nawachunguze uamuzi wa kijinsia kwa kuzingatia sifa za kibiolojia, za kimwili pamoja na za kihisia, kwa kuzingatia jeni, kazi za jinsia za jinsia isiyoeleweka na mtazamo wa dume jike au jike dume, pamoja na mabadiliko ya homoni na ubadilishaji jinsia kupitia upasuaji.
Ujinsia ni Fahamu ya Kimagharibi ya Kufafanua Jinsia kupitia Mtazamo wa Kibinafsi
Magharibi imetabanni mtazamo mpya kuhusu suala la jinsia katika miongo ya hivi karibuni. Ili kutibu karne nyingi za ubaguzi wa kikatili dhidi ya wanawake, kutokana na Kanisa la Kikristo na itikadi zake za ukandamizaji, Magharibi iligeukia "ujinsia" ili kufafanua jinsia. Magharibi iliipa mgongo fahamu ya jinsia, kwa mujibu wa kipimo cha uwili wa kibaolojia, yaani uume na uke, badala yake wakageukia fahamu ya ujinsia. Chini ya ujinsia, jinsia hufafanuliwa kulingana na muundo wa kithaqafa na kijamii wa mtu binafsi. Chini ya ujinsia, jinsia hupeanwa kupitia fikra za mtu binafsi, kwa mtazamo wa kibinafsi, na si kwa biolojia. Kama mwanafalsafa wa Kifaransa wa filosofia ya uwepo huru wa mtu binafsi, Simone de Beauvoir, alivyosema, "Mtu hazaliwi, lakini badala yake anakuwa, mwanamke (Kifaransa: On ne naît pas femme, on le devient)" katika kitabu chake ‘Jinsia ya Pili’ (Kifaransa: Le Deuxième Sexe).
Ujinsia, asili, uliibuka kama sehemu ya wimbi la pili la utetezi wa haki za wanawake, katika jitihada za kuondoa ubaguzi wa kijinsia, kwa kuzingatia uwili wa uume na uke. Kwa hivyo, ujinsia ulitaka kuondoa uamuzi wa kibaolojia wa jinsia. Kwa kufanya hivyo, ujinsia pia ulitaka kuondoa matokeo yake, unyanyapaa wa kijinsia na dori za kijinsia, ambayo yalionekana kuwa ya kukandamiza.
Ujinsia Umetabanniwa na Vuguvugu la Ushoga
Kiasili, ujinsia ulitabanniwa ili kuzuia ubaguzi dhidi ya wanawake, na wanaume. Hata hivyo, ujinsia ukapanuliwa kutoka kwa uungaji mkono haki za wanawake, hadi uungaji mkono haki za mashoga. Ujinsia iliungwa mkono kwa kiasi kikubwa na watetezi wa ushoga, ili kukomesha ubaguzi, dhidi ya wale wanaojitangaza kuwa mashoga. Kwa hivyo, lengo la ujinsia halikufungika tena tu katika kukomesha ubaguzi dhidi ya wanawake. Ujinsia ulipanuliwa ili kukomesha ubaguzi dhidi ya wale waliojichagulia jinsia, kupitia mtazamo wao wa kibinafsi, bila kujali sifa za kibaolojia.
Kupitia fahamu yake ya uhuru wa kibinafsi, Magharibi iliruhusu watu binafsi kujipachika jinsia, kwa namna wanavyojitazama kibinafsi. Kwa hivyo, kulingana na ujinsia, mwanamume anaweza kuamua kuwa yeye ni mwanamke, licha ya ukweli kwamba ana sifa za kibaolojia za mwanaume. Anaweza kufanyiwa upasuaji na tiba ya homoni ili kubadili jinsia aliyojichagulia. Kwa hivyo mtu aliyebadili jinsia anaweza kuficha sifa za kibaolojia za kiume na kupata sifa za kibaolojia za kike. Watu waliobadili jinsia ambao hutumia usaidizi wa kimatibabu kubadilisha jinsia zao, kwa njia hii, wanaitwa ‘transsexual’. Vile vile, mwanamke anaweza kujiona kuwa yeye ni mwanamume. Kisa maarufu ni cha mwanamke, Ellen Paige, ambaye aligeuka kuwa Elliot Page, baada ya mabadiliko ya upasuaji na homoni. Kwa hiyo, sasa katika mtazamo wa Kimagharibi kuna watu waliobadili jinsia (transgender), ambao wana kitambulisho cha kijinsia, tofauti na jinsia yao ya kibaiolojia wakati wa kuzaliwa.
Kwa upande wa Sheria ya Ulinzi ya Watu Wanaobadili Jinsia ya Pakistan, baada ya kufanyiwa marekebisho, imeegemezwa juu ya fikra ya ujinsia ya Kimagharibi. Inasisitiza, "Mtu aliyebadili jinsia atakuwa na haki ya kutambuliwa kulingana na kitambulisho chake wa kijinsia kupitia anavyojitazama mwenyewe." Kwa hivyo kulingana na watawala wa Pakistan, jinsia inapaswa kuamuliwa kwa kujitazama kibinafsi, kama watetezi wa Magharibi, badala ya kuzingatia baolojia peke yake, kama Uislamu unavyo taka.
Muamala wa Uislamu kwa Jinsia na Dori ya Kijinisa
Mwenyezi Mungu (swt) anasema,
[وَلَيْسَ الذَّكَرُ كَالْأُنثَىٰ]
“Na mwanamume si sawa na mwanamke.” [Surah Aali Imran 3:36]. Katika Uislamu, kiasili kuna jinsia mbili. Jinsia hizi mbili huamuliwa na masuala ya kibiolojia pekee. Jinsia haiamuliwi na uamuzi wa mtu binafsi au mtazamo wa kibinafsi. Jinsia isiyoeleweka inaamuliwa na wataalamu, kama moja ya jinsia mbili. Kisha, dori za kijinsia zinaamuliwa na Sharia iliyoteremshwa kwa wahyi na Mwenyezi Mungu. Katika Uislamu, kuna hukmu za Shariah kwa wanadamu wote, wanaume na wanawake, na pia kuna hukmu za Shariah ambazo ni maalum za kijinsia. Kwa hiyo, Uislamu uliwapa majukumu wanaume pamoja na wanawake kuhusiana na Swalah, Saumu, Hijja na Zaka. Kisha, Uislamu ukatoa hukmu za Shariah kwa mwanamke peke yake, kuhusu hedhi, mimba na uzazi wa mtoto. Uislamu pia ulimpa mwanamke haki ya ulezi wa watoto, kando na mwanamume. Uislamu ulimpa mwanamke haki ya kuchuma, ambapo mume wake hana haki katika mali yake, huku ukimlazimu mwanamume kumpa masrufu mke wake na watoto wake. Kupigana si faradhi kwa wanawake, ilhali ni faradhi kwa wanaume.
Kuepusha kuleta ukandamizaji juu ya mwanamke, au mwanamume, Shariah inahakikisha kwamba wanaume na wanawake wanashirikiana, ili kuzalisha familia imara na jamii yenye utulivu inayoegemezwa kwenye kitengo hicho. Hata bila ya Khilafah ili kuzuia dhulma na ufisadi, maisha ya familia katika Ulimwengu wa Kiislamu yanasalia kuwa mwenge, kwa wale walioko Magharibi, wanaokabiliwa na matokeo mabaya, ya uharibifu wa maisha ya familia.
Uislamu Huipa Jinsia Isiyoeleweka (خُنْثَىKhuntha) Jinsia kutoka katika Jinsia Mbili
Neno ‘khuntha’ linatumika kwa mtu ambaye hawezi kujulikana kwa urahisi, kuwa ni mwanamume au mwanamke, kwa mazingatio ya kibiolojia. Ni mwanadamu ambaye ana maumbile ya kiume na ya kike, au yule ambaye hana yoyote. Katika Uislamu, mtaalamu humpa yule aliye na jinsia isiyoeleweka moja ya jinsia mbili, mwanamume au mwanamke, baada ya kutafiti uhalisia wa kibaolojia. Mwanafaqihi wa kale Ibn Qudamah alisema katika kitabu chake Al-Mughni, kuhusiana na utata: “Haitengwi kuwa ya kiume au ya kike. Amesema Mwenyezi Mungu (swt):
[وَأَنَّهُ خَلَقَ الزَّوْجَيْنِ الذَّكَرَ وَالأُنْثَى]
“Na kwamba Yeye ndiye aliye umba jozi, dume na jike.” [Surah An-Najm 53:45]. Na Yeye (swt) amesema,
[وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالا كَثِيرًا وَنِسَاءً]
“Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi.” [Surah An-Nisaa 4:1] na kwa hivyo hakuna kiumbe cha tatu.”
Kwa hivyo, Uislamu haujaweka jinsia ya tatu. Daktari muaminifu wa Kiislamu ambaye ni mtaalamu wa masuala ya dosari katika uume na uke, maumbile ya kijinsia, jeni na tabia ya kijinsia, huthibitisha jinsia. Kwa hivyo yeye, kwa utulivu na umakini, huchunguza kwa undani tabia za kibaolojia, za kimaumbile, za kimwili, kwanza, ili kuona ni kipi kinachotawala, cha sifa za kiume au za kike. Yeye huchunguza mambo ya kimwili, kama vile sehemu za siri, na pia kuzingatia kromosomu za jinsia za X na Y, zinazounda jinsia. Ikiwa, katika hali nadra sana, kwamba sifa za kimaumbile na za kijeni pekee hazitatui utata, suala la kibaolojia ya kiume na kike, mivutio ya kijinsia na hamu pia huzingatiwa, kabla ya kuamua jinsia. Baada ya hapo, hukmu za Kiislamu hutumika kulingana na jinsia iliyoamuliwa, ikiwemo ndoa, dori na majukumu ya kijinsia.
Mara tu uamuzi wa kijinsia unapokuwa umefanywa, unaidhinishwa na amri ya Khalifah, kama mamlaka ya Waislamu, ambaye ni lazima atiiwe. Baada ya hapo, mtu huyo anaamiliwa na jamii pana, kulingana na jinsia aliyopewa, bila ya ubaguzi. Mwanamume au mwanamke ameunganishwa kama mwanajamii anayethaminiwa wa jamii ya Kiislamu, ili kwamba majukumu yote ya Shariah yaweze kutekelezwa, huku haki zote za Shariah zikitolewa.
Hukmu ya Uislamu Kuhusiana na Mwanamume Mwenye Kujifananisha na Mwanamke (مُخَنَّثMukhannath) na Mwanamke Mwenye Kujifananisha na Mwanamume (مُتَرَجِّلَةُ Mutarajillah)
Ibn Abbas (ra) amesimulia, «لَعَنَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم الْمُتَشَبِّهِينَ مِنَ الرِّجَالِ بِالنِّسَاءِ، وَالْمُتَشَبِّهَاتِ مِنَ النِّسَاءِ بِالرِّجَالِ» “Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake, na wanawake wanaojifananisha na wanaume.” [Bukhari]. Ibn Abbas (ra) amesimulia kwamba, «لعن الله الْمُخَنَّثِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالْمُتَرَجِّلَاتِ مِنَ النِّسَاءِ وَقَالَ أخرجوهم من بُيُوتكُمْ» “Mwenyezi Mungu amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake, na wanawake wanaojifananisha na wanaume, na akasema watoeni majumbani mwenu.” [Bukhari]. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema, «ثَلاَثَةٌ لاَ يَنْظُرُ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ إِلَيْهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ الْعَاقُّ لِوَالِدَيْهِ وَالْمَرْأَةُ الْمُتَرَجِّلَةُ وَالدَّيُّوثُ» “Watu watatu Mwenyezi Mungu Mtukufu hatawatazama Siku ya Kiyama: Mwenye kuwaasi wazazi wake wawili, na mwanamke mwenye kujifananisha na wanaume na Dayuthi.” [An-Nisaa]
Kujifananisha na jinsia huja kwa maana jumla, katika upande wa kitambulisho, tabia, mavazi na suluki. Inakuja kwa maana kamili, bila ya mipaka na tofauti yoyote. Dhambi inaenea hadi kwenye mahusiano ya kimwili, na jinsia moja, na yote yanayopelekea katika hilo. Kwa hivyo, katika Uislamu, matamanio na vivutio sio mwamuzi wa kitendo. Badala yake, hukmu za Shariah ndio huamua mahusiano kati ya wanaume na wanawake, pamoja na mwenendo, tabia na dori zao. Baada ya Uislamu kuamua namna ya mahusiano, kwa undani, mapenzi na mahusiano ya kimwili hutukia ndani ya fungamano la ndoa, kati ya mwanamume na mwanamke. Ni Khilafah ndiyo itakayozalisha mazingira yanayokuuza dori sahihi za kijinsia. Jamii ya Kiislamu ndiyo iliyo mbali sana na mkanganyiko, taabu na mateso haya ambayo hadhara ya Kimagharibi imesababisha kupitia uhuru na dhihirisho lake, ujinsia.
Mtazamo wa Uislamu juu ya Ubadilishaji Jinsia
Jinsia haiamuliwai kwa kujitazama kibinafsi, na kupuuza uhalisia wa kibaolojia wakati wa kuzaliwa. Kubadilisha jinsia ya mtu kutoka kwa mwanamume kwenda kwa mwanamke, au kinyume chake, kunachukuliwa kuwa ni kubadilisha uumbaji wa Mwenyezi Mungu ﷻ ambao umeharamishwa. Hii ni ima mabadiliko hayo yanatokana na tiba ya kihomoni au upasuaji. Amesema Mwenyezi Mungu (swt):
[إِن يَدْعُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا إِنَاثًا وَإِن يَدْعُونَ إِلَّا شَيْطَانًا مَّرِيدًا (117) لَّعَنَهُ اللَّهُ ۘ وَقَالَ لَأَتَّخِذَنَّ مِنْ عِبَادِكَ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا (118) وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الْأَنْعَامِ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّهِ ۚ وَمَن يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِّن دُونِ اللَّهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا (119) يَعِدُهُمْ وَيُمَنِّيهِمْ ۖ وَمَا يَعِدُهُمُ الشَّيْطَانُ إِلَّا غُرُورًا]
“Wao hawawaombi badala yake Yeye ila wanawake, wala hawamuombi ila Shet'ani aliye asi (117) Mwenyezi Mungu amemlaani. Naye Shet'ani alisema: Kwa yakini nitawachukua sehemu maalumu katika waja wako (118) Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha, basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi watabadili aliyo umba Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shet'ani kuwa ni mlinzi wake badala ya Mwenyezi Mungu, basi huyo amekhasiri khasara ya dhaahiri (119) Anawaahidi na anawatia tamaa. Na Shet'ani hawaahidi ila udanganyifu (120)” [Surah An-Nisaa 4:117-120].
Katika suala la mpito wa mwanamume hadi mwanamke, ni kudhihirisha sifa za uke, au kuficha sifa za uume. Hata hivyo, haibadilishi uhalisia wa kibaolojia wa mtu huyo wakati wa kuzaliwa, ambao ndio msingi wa uwekaji wa jinsia katika Uislamu. Kwa hivyo hukmu za asili ya jinsia yake zinabaki kuwa za kiume, kabla ya mabadiliko. Haijuzu kwa mwanamume mwengine kufanya mkataba wa ndoa na mtu wa asili ya kiume, bila ya kujali mabadiliko hayo.
Hitimisho: Kukabiliana na Batili ya Fikra ya Ujinsia
Baada ya kuhakikisha uharibifu wa familia na maadili ya familia katika nchi zao, Magharibi inafanya kazi kupitia watawala wa Waislamu kutangaza vita vya kithaqafa dhidi ya Uislamu na Waislamu. Katika Magharibi, serikali za Kimagharibi zina uwezo wa kuongoza na kudhibiti watu wao kwa urahisi, kutokana na kusambaratika kwa familia na kusababisha ukosefu wa mshikamano, jamii na hatua za pamoja. Watawala wa nchi za Magharibi sasa nao wanataka vivyo hivyo kwa Waislamu, kwa kuwa wameshindwa kukabiliana na Uislamu kifikra na kiitikadi. Sasa hivi inaeneza fikra ya ujinsia miongoni mwa Waislamu ili kuwafisidi, ikitaka kuangamiza mfumo wa kijamii na mafungamano imara ya kifamilia miongoni mwa Waislamu. Hii ni ili Magharibi iweze kuwadhibiti Waislamu, kuzuia, au angalau kuchelewesha, mwamko wa Ummah kupitia Khilafah kwa Njia ya Utume. Ni juu ya Waislamu kukabiliana na wimbi hili la ufisadi kupitia kujijenga imara kithaqafa kutoka kwenye Uislamu, huku wakifanya kazi ya kusimamisha tena ngao yao ya ulinzi, Khilafah.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Musab Umair – Wilayah Pakistan