Jumatano, 23 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Udhaifu wa Mataifa na Nguvu za Mwenyezi Mungu (swt)

Kuna baadhi ya Waislamu wanahoji kuwa kuurejesha tena mfumo wa Mwenyezi Mungu (swt), Khilafah kupitia njia ya Utume kuwa ni jambo lisilowezekana, kama wanavyodai kuwa mataifa yenye nguvu ya dunia kama Marekani, dola za Ulaya, Urusi, China na mengineyo yataungana kuivunja itakaporegea. Wengine hudai kuwa ili majeshi ya ulimwengu wa Kiislamu, kama katika Pakistan, Uturuki, Misri na kwengineko yaweze kuhamasishwa kukomboa Waislamu katika ardhi ambapo wao wametawaliwa, wamedhulumiwa na kuuliwa, kama nchini Palestina, Syria na Kashmir, itakuwa ni kujiua kisiasa na kijeshi kwa mataifa makubwa ya Kiislamu. Wanadai kuwa matokeo ya makabiliano ya kijeshi yatakuwa ni ya uhakika wa kushindwa kwa Waislamu, kwa kuwa sio tu watakabiliana na majeshi ya adui ambayo ni makubwa zaidi na huenda yamejiandaa zaidi kisilaha kuliko yao, lakini pia na waungaji mkono na washirika wao wa Magharibi na Mashariki. Madai yanayo onyeshwa ni kuwa mataifa yenye nguvu ya leo hayashindiki, hayaingiliki, hayapigiki na hayaharibiki na yamejaaliwa kutawala dunia milele – yakiakisi maoni ya viongozi wa sasa wenye kushika hatamu za utawala wa ulimwengu, akiwemo raisi wa Marekani, Donald Trump, ambaye mnamo Agosti 2017, wakati akijadili makombora ya nuklia ya Marekani, alisema: “Itarajiwe kuwa hatutotumia kabisa nguvu hizi, lakini hakutakuwa na kipindi ambacho hatutakuwa taifa lenye nguvu zaidi duniani.”

Kwa Muislamu kushika imani kama hiyo huleta fikra ya kushindwa na kusalim amri (na kubakia kwenye) hali kama ilivyo na kuruhusu unyanyasaji, uovu na maafa kuendelea katika dunia bila kupingwa. Wanaamini kuwa mabadiliko huweza tu kuja kupitia Umoja wa Mataifa au diplomasia ya pamoja baina ya mataifa adui na vyama, ambayo pia huendeleza uhalisia wa dhulma. Hii ni kwa sababu taasisi kama hizo na matendo hayo zimeonyesha muda baada ya muda kuwa zimeshindwa katika hali ya kuhuzunisha katika kuhifadhi damu isio na hatia na kuwadhibiti viongozi jeuri, serikali au taasisi. Bali, ni njia inayotumiwa na mataifa yenye nguvu ya dunia kudhibiti muendelezo wa hali ya sasa kuhusiana na eneo lao la ushawishi na mamlaka kote duniani.

Hukumu kama hizi za kukata tamaa huchipuka kutokana na mahesabu finyu kuhusiana na matokeo ya matendo kwa kutumia uhalisia wa dunia hii tu. Hivyo, huchukuliwa kuwa nchi ilio na nguvu kubwa zaidi kijeshi itaishinda ile ilio na nafasi ya chini, kana kwamba kumiliki matokeo ya masuala ya kisiasa na kijeshi ni kama kumiliki vipande vya sataranji (chess bodi). Fikra kama hiyo inapuuza ukweli kwamba kuna sababu nje ya ulimwengu huu ambayo ndio yenye kuamua ushindi, nguvu na urefu wa muda wa mataifa: Muumba, Mwenyezi Mungu (swt), Mtukufu, Mwenye nguvu zote. Kwa hakika, namna ambayo virusi vya korona, vinavyo tegemea darubini, visivyo onekana kwa macho, vimelemaza uchumi wa mataifa yenye nguvu duniani kwa sasa – vinapasa kihakika vifungue macho ya wale wenye akili kuona udhaifu wa kimaumbile wa mataifa na Nguvu kubwa ya Mwenyezi Mungu (swt). 

Somo kama hili huwasilishwa mara kwa mara katika Quran, ya kuwa mataifa yenye nguvu na himaya kubwa zinazo dhaniwa kuwa hazivunjiki na hazishindiki na ambazo zinapuuza utiifu kwa Mwenyezi Mungu (swt) na zikawa na kiburi na kuwa madhalimu ziliondolewa kutoka ardhini na Yule Ambaye huamua nani wa kupewa nguvu: Mwenyezi Mungu (swt). Habari hizi za Quran zinatoa ukumbusho wenye kamili kwa waumini kwamba kutokushindwa ni kwa Mwenyezi Mungu (swt) pekee.

Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

         (أَلَمْ يَرَوْاْ كَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَبْلِهِم مِّن قَرْنٍ مَّكَّنَّاهُمْ فِي الأَرْضِ مَا لَمْ نُمَكِّن لَّكُمْ وَأَرْسَلْنَا السَّمَاء عَلَيْهِم مِّدْرَارًا وَجَعَلْنَا الأَنْهَارَ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمْ فَأَهْلَكْنَاهُم بِذُنُوبِهِمْ وَأَنْشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قَرْنًا آخَرِينَ)

“Jee, hawaoni vizazi vingapi tulivyo viangamiza kabla yao? Tuliwaweka katika nchi tusivyo kuwekeni nyinyi; tukawapelekea mvua nyingi na tukaifanya mito inapita chini yao. Mwishowe tukawaangamiza kwa madhambi yao; na tukaanzisha baada yao kizazi kingine.” [Al-An’am: 6].

   Na amesema (swt):

قُلْ سِيرُواْ فِي الأَرْضِ ثُمَّ انظُرُواْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ

“Sema: Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha.”                    [Al-An’am: 11].

Na amesema (swt):

(أَلَمْ يَأْتِهِمْ نَبَأُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ قَوْمِ نُوحٍ وَعَادٍ وَثَمُودَ وَقَوْمِ إِبْرَاهِيمَ وِأَصْحَابِ مَدْيَنَ وَالْمُؤْتَفِكَاتِ أَتَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانَ اللّهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَـكِن كَانُواْ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ)

“Je, hazikuwafikia khabari za walio kuwa kabla yao - kaumu ya Nuhu, na A'ad, na Thamud, na kaumu ya Ibrahim, na watu wa Madyana, na miji iliyo pinduliwa chini juu? Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo wazi. Basi Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, walakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe.” [At-Taubah: 70].

Kwa hakika, kisa cha watu wa ‘Aad katika Quran kinabeba uhusiano mkubwa wa uhalisia wa mataifa makuu ya leo na Imani yao kuwa hayashindiki. Taifa la ‘Aad lilikuwa ndio la mwanzo kuianzisha upya ibada ya masanamu baada ya taifa la Mtume Nuh (AS) lililoibuka kufuatia gharika kuu alioipeleka Mwenyezi Mungu (swt). Katika Surah al-Fajr, Mwenyezi Mungu (swt) amewaelezea watu wa ‘Aad kama ifuatavyo:

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِعَادٍ * إِرَمَ ذَاتِ الْعِمَادِ * الَّتِي لَمْ يُخْلَقْ مِثْلُهَا فِي الْبِلَادِ

“Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo wafanya kina A'di? Wa Iram, wenye majumba marefu? Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi?” [Al-Fajr: 6-8]. Watu wa ‘Aad hawakuwa na mshindani katika mataifa mengine katika kiwango cha uwezo na nguvu ambazo Mwenyezi Mungu (swt) amewapa. Hakika, nguvu za mataifa yanayo ongoza ya sasa, zimekuwa si zenye athari kubwa kulinganisha na nguvu na ushawishi ambao taifa la ‘Aad lilikuwa nao. lilitawala ardhi zote pambizoni mwake na sheria yoyote walioitunga – ilikuwa ndio sheria – isiopingwa na mtu mwengine. Kiuchumi, wakiogelea ndani ya utajiri na anasa, na walikuwa na chemichemi na mabustani mazuri zaidi. Kwa hakika, walikuwa na utajiri mkubwa kiasi kwamba wakijenga makasri marefu sana katika milima ambapo hakuna mtu anayeishi; wakijenga kwa ajili ya starehe na mikogo kuonyesha hadhi yao kubwa. Mwenyezi Mungu (swt) pia aliwapatia idadi kubwa ya vizazi kiasi kwamba taifa lilikuwa na watu wengi, na miili ya watu ilikuwa mikubwa na yenye nguvu. Na Mwenyezi Mungu (swt) aliwapatia utaalamu na akili ya kujenga ustaarabu wa hali ya juu.

Hata hivyo, pamoja na nguvu zote hizo, walikuwa ni wenye kiburi na kumkataa Mwenyezi Mungu (swt) na ujumbe wa Mtume Hud aliepelekwa kuwaongoza katika kumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja. walidai kuwa wao ni taifa kubwa katika ardhi ambao hawakuhitaji uongozi kutoka kwa yeyote. Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

  (فَأَمَّا عَادٌ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَقَالُوا مَنْ أَشَدُّ مِنَّا قُوَّةً أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّهَ الَّذِي خَلَقَهُمْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ)

“Ama kina 'Adi walijivuna katika nchi bila ya haki, na wakasema: Nani aliye kuwa na nguvu kushinda sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawa wanazikataa Ishara zetu!” [Fussilat: 15]. Na badala ya kutumia nguvu zao kwa namna nzuri, walijiingiza katika uharibifu na kuwa makatili. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu (swt) alipeleka upepo mkali kuwaangamiza kuwaonyesha kizazi kijacho – Yule Mwenye nguvu zote, Mwenye Enzi, Ambaye pekee ndiye asiyeshindwa, na Anayeamua kuibuka na kuanguka kwa mataifa.

Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

(وَأَمَّا عَادٌ فَأُهْلِكُوا بِرِيحٍ صَرْصَرٍ عَاتِيَةٍ * سَخَّرَهَا عَلَيْهِمْ سَبْعَ لَيَالٍ وَثَمَانِيَةَ أَيَّامٍ حُسُومًا فَتَرَى الْقَوْمَ فِيهَا صَرْعَى كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ خَاوِيَةٍ * فَهَلْ تَرَى لَهُم مِّن بَاقِيَةٍ)

“Na ama A'di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika. Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi ndani. Basi je! Unamwona mmoja wao aliye baki?” [Al-Haqqa: 6-8]

Hata hivyo, hili taifa kubwa lenye nguvu lilifutwa kabisa kutoka katika uso wa dunia katika muda wa masiku machache na Mwenyezi Mungu (swt), kana kwamba halikuwepo; liliangamizwa na kile ambacho hakionekani kwa jicho la mwanaadamu: upepo – kwani kuwepo kwake huhisika tu kwa athari inayoileta. Subhaanallah!

Bila shaka, Mwenyezi Mungu (swt) ameapa katika Surah Al-Fajr, akitilia nguvu uzito wa ujumbe wa kufuatwa, ambao ni majaaliwa ya mwisho ya waovu na madhalimu wa dunia hii wanaomkataa Yeye ni kuangamizwa, kwa kuwa Haruhusu dhulma na kutotii kuendelea kutamalaki ardhi hii. Yeye (swt) anasema: 

(فَأَكْثَرُوا فِيهَا الْفَسَادَ * فَصَبَّ عَلَيْهِمْ رَبُّكَ سَوْطَ عَذَابٍ * إِنَّ رَبَّكَ لَبِالْمِرْصَادِ)

“Wakakithirisha humo ufisadi? Basi Mola wako Mlezi aliwapiga mjeledi wa adhabu. Hakika Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia.” [Al-Fajr: 12-14]. Na Yeye (swt) anasema:

(وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللّهُ النَّاسَ بِظُلْمِهِم مَّا تَرَكَ عَلَيْهَا مِن دَآبَّةٍ وَلَكِن يُؤَخِّرُهُمْ إلَى أَجَلٍ مُّسَمًّى فَإِذَا جَاء أَجَلُهُمْ لاَ يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً وَلاَ يَسْتَقْدِمُونَ)

“Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu kwa mujibu wa dhulma zao, basi asingeli mwacha hapa hata mnyama mmoja. Lakini anawaakhirisha mpaka muda ulio wekwa. Na unapo fika muda wao hawatakawilia hata saa moja wala hawatatangulia.” [An-Nahl: 61]

Kwa hivyo, hii ndio Sunnah ya Mwenyezi Mungu (swt) katika namna anavyo shughulikia watawala wenye kiburi na madhalimu na mataifa katika muda wote wanapo pingana na Haki, kueneza uovu, na ambao huwapinga na kuwatesa waumini. Tunaona namna Mwenyezi Mungu (swt) alivyo muangamiza mfalme Namrudh aliye na kiburi aliye amini kuwa yeye ni Mungu, kwa kitu kilicho kidogo kama mbu aliye ingia puani na kufika kwenye ubongo wake. Tunaona namna Mtume Dawud (AS) alivyo muangamiza kiongozi mkubwa aliye na nguvu wa jeshi la Philistine – Jalut – aliye kuwa ni adui wa Mwenyezi Mungu (swt), kwa mrusho mmoja wa kijiwe. Tumeona namna Firauni aliye tawala himaya kubwa alivyo zamishwa baharini pamoja na jeshi lake.

Na tumeona namna Mtume wetu mpendwa (saw) alivyo washinda maQuraish katika vita vya Badr na namna Waislamu walivyoishinda himaya kubwa ya Uajemi (Fursi) katika vita vya Al-Qadisiyyah wakati wa Khilafah ya Umar bin Al Khattab (ra), licha ya Waislamu kuzidiwa kwa idadi kubwa ya maadui katika mapambano haya. Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

(وَكَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّن قَرْنٍ هَلْ تُحِسُّ مِنْهُم مِّنْ أَحَدٍ أَوْ تَسْمَعُ لَهُمْ رِكْزًا)

“Na kaumu ngapi tumezihiliki kabla yao. Je! Unawaona hata mmoja katika wao au unasikia hata mchakato wao?” [Maryam: 98]. Bila shaka, nguvu za kisiasa, kiuchumi na kijeshi za mataifa haya na himaya hizo ambazo Mwenyezi Mungu (swt) aliziangamiza zinazidi kwa kiasi kikubwa hizi nguvu za mataifa yanayo ongoza hivi leo. Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

(أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَكَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيُعْجِزَهُ مِن شَيْءٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ إِنَّهُ كَانَ عَلِيمًا قَدِيرًا)

“Je! Hawakusafiri katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Na hao walikuwa wana nguvu zaidi kuliko wao. Na hapana kitu kinacho weza kumshinda Mwenyezi Mungu mbinguni wala katika ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye uweza.” [Fatir: 44]. Lote hili ni somo kuwaonyesha wanaadamu kuwa Ubwana wote uko kwa Mwenyezi Mungu (swt) pekee, na kwamba licha ya namna ya maendeleo, usasa na nguvu ambazo ustaarabu unazo, pindi Mwenyezi Mungu (swt) anapo amua mwisho wake, hutokea kwa ghafla. Huu pia ni ukumbusho wa wazi pindi Mwenyezi Mungu (swt) anapo amua kutoa ushindi kwa waumini dhidi ya maadui zao, hakuna kiwango cha nguvu za kisiasa, kiuchumi, kijeshi au kiteknolojia kinachoweza kuzuia ushindi huo.

Hata hivyo, kuna baadhi ya Waislamu wanaodai kuwa habari kama hizi za ushindi mkubwa kwa Waislamu dhidi ya maadui zao ni hadithi zilizopita, zilizo husiana na uwepo wa Mitume au Masahaba miongoni mwa waumini wa nyakati hizo, na haiwezi kuchukuliwa kama ni mifano ya namna Waislamu wanaweza kushughulikia uhalisia wa kisiasa wa leo.

Hata hivyo, madai kama haya yanapingana na ushindi mwingi mnono dhidi ya mataifa yenye nguvu ambao Mwenyezi Mungu amewapatia Ummah huu ukiwa chini ya utawala wa Kiislamu kwa karne nyingi kufuatia kipindi cha Masahaba na Khilafah Rashida. Chukuwa kwa mfano, ushindi mkubwa wa Waislamu dhidi ya Makruseda wakiwa chini ya uongozi wa Kamanda Muislamu, Salahuddin Ayubi, wakati wa Khilafah ya Abbasiyah, uliopelekea ukombozi wa ardhi tukufu ya Palestina na maeneo yaliozunguka kutoka katika mikono ya wavamizi madhalimu wa Kikristo. Katika vita vya tatu vya msalaba vilivyo fuatia Vita vya Hattin na kukombolewa kwa Jerusalem, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza waliunda umoja uliokusanya jeshi kubwa, likiongozwa na wafalme wao, ili kujaribu kuuchukuwa tena mji huu mtakatifu. Baadhi wanakisia jeshi la Ujerumani pekee likiwa na idadi ya askari 300,000 – ni idadi kubwa wakati huo.

Hata hivyo, licha ya kuwa jeshi la Salahuddin likiwa na idadi ya wastani kulinganisha na muungano wa Makruseda, aliamua kuihami Al-Quds kwa namna yoyote, kwa kuwa hiyo ni ardhi tukufu ya Uislamu, na hii ilikuwa ni Amri ya Mwenyezi Mungu (swt). Inaelezwa kuwa wakati kundi la Makruseda la Ujerumani likielekea Ash-Sham, mfalme wao – Frederick Barbarossa – alifariki, kisha maradhi na mtengano ulienea miongoni mwa askari wake kiasi cha kuwa muda ambao jeshi lake linafika Ash-Sham kumkabili Salahuddin, walikuwa ni idadi ya mamia kidogo tu, na walikuwa dhaifu na wameparaganyika. Wakati huo, mfalme wa Ufaransa, Phillip Wapili alipata ugonjwa baada ya kuizingira Acre, mji katika Palestina, na kurudi na jeshi lake Ufaransa, akimuacha mfalme Richard wa Uingereza kukabiliana na Salahuddin peke yake. Hata hivyo, askari wa Richard pia walitaabishwa sana na joto na kukosa maji safi, na wakati wa usiku walitaabishwa na mabuibui wakubwa ambao kuuma kwake kuna sumu na kunaumiza… hivyo wakati wakijitayarisha kuishambulia Jerusalem walibakia askari walio na siha kiasi cha 2,000 tu na hawakuweza kuuchukua mji, Allahu akbar! Kwa hakika ni somo kubwa kwa Waumini kuwa Mwenyezi Mungu (swt) ni msaidizi wa wale ambao matendo yao yameegemea juu ya Uislamu na KWA AJILI YA UISLAM!

Tumeona ushindi mkubwa kama huo kwa Waislamu katika historia ya Uislamu, wakiwa wanapigana kwa ajili ya Dini na kwa kuitikia Amri za Mwenyezi Mungu (swt) kuuhami Uislamu na waumini, licha ya uchache wa idadi yao au nguvu za kijeshi kulinganisha na za maadui wao, katika karne ya 13 kwa mfano, waTatari, waliokuwa wakali na taifa lenye nguvu, waliivamia Khilafah, wakamuua Khalifah na wakahodhi kiasi ya robo tatu ya ulimwengu wa Kiislamu kwa mujibu wa baadhi ya makadirio. Wakielekea Misri, ngome ya mwisho ya Waislamu, waTatari walipeleka barua kwa Wali wa Misri, Mahmoud Saifudiin Qutuz, inayosema, “Tumebomoa ardhi, tumeacha watoto wakiwa mayatima, tumetesa watu na kuwauwa, tumefanya watukufu wao kudharaulika na kiongozi wao mateka. Unafikiri unaweza kutuepuka sisi?” Qutz aliomba msaada kwa Mawali wengine na wanachuoni kutoka katika ardhi za Khilafah, akiwataka kuungana na kusimama kwa ajili ya kuulinda Uislamu na kuwaelekeza Waislamu kuzikomboa ardhi za Waislamu. Katika vita vya Ain Jalut chini ya uongozi wake, na katika mwezi kama huu wa Ramadhan, Waislamu walipata ushindi mkubwa dhidi ya waTatari uliomsaidia Qutuz kukomboa ardhi nyingi za Khilafah zilizotekwa.

Kwa kweli, mifano ni mingi sana kuitaja juu ya ushindi ambao Mwenyezi Mungu (swt) ameubariki Ummah huu wakati ukipigana ‘Katika Njia ya Mwenyezi Mungu’ na kuitikia Maamrisho Yake. Hivyo, sharti kwa ajili ya ushindi kwa Waumini dhidi ya nchi na mataifa adui, na viongozi dhalimu na tawala, sio uwepo wa Mitume na Masahaba, wala sio sharti juu ya uzani wa idadi, kwani Mwenyezi Mungu (swt) amesema:

قَالَ الَّذِينَ يَظُنُّونَ أَنَّهُم مُّلاَقُو اللّهِ كَم مِّن فِئَةٍ قَلِيلَةٍ غَلَبَتْ فِئَةً كَثِيرَةً بِإِذْنِ اللّهِ وَاللّهُ مَعَ الصَّابِرِينَ

“Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mwenyezi Mungu: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.” [Al-Baqara: 249]. Makafiri hutumia mantiki ya uzani wa idadi, nguvu za kisiasa na nguvu za kijeshi kuamua matokeo ya vita na mapambano ya kisiasa ya duniani. Hata hivyo, hii isiwe ni imani kwa Muislamu, kwani tunajua kuwa Mwenyezi Mungu (swt) hatendi kwa mujibu wa mantiki dhaifu ya mwanaadamu.

Bali, Yeye (swt) ana msingi wake wa nini huleta ushindi: utiifu kwa Maamrisho Yake, Tawakkul katika Msaada Wake, na kujitahidi kutoa ushindi kwa Dini Yake – Uislamu! Mwenyezi Mungu (swt) amesema:

 (يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ)

“Enyi mlio amini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu.” [Muhammad: 7]

Tunaona kwa mfano, namna Mwenyezi Mungu (swt) alivyotoa ushindi kwa Waislamu katika vita vya Badri, japokuwa walikuwa ni thuluthi moja ya idadi ya jeshi la maQuraysh, kwa kuwa wakipigana si kwa chengine isipokuwa kwa ajili ya Radhi za Mwenyezi Mungu (swt) kuendeleza mamlaka ya Dini Yake. Hata hivyo, Yeye (swt) ameruhusu Waislamu kuonja kushindwa dhidi ya maadui zao katika vita vya Uhud, japokuwa walikuwa wamejiandaa vizuri zaidi kijeshi na kiidadi kuwakabili maQuraish.

Hii ni kwa sababu katika Uhud, walenga shabaha waliokuwa juu ya jabali walipinga maagizo ya Mtume (saw) ya kubakia katika sehemu zao kutokana na kukimbilia ngawira za vita, na kwa hiyo, wamepinga Amri ya Mwenyezi Mungu (swt). Tunaona pia katika Khilafah, wakati utekelezaji wa sheria za Uislamu uko imara, na umoja baina ya ardhi zake ukiwa wenye nguvu kama ilivyo agizwa na Mwenyezi Mungu (swt), basi dola ilikuwa yenye nguvu kisiasa, kiuchumi na kijeshi ambapo iliweza kumiliki ulimwengu, ikiogopwa na maadui zake, na ilibarikiwa kwa ushindi baada ya ushindi ambapo ilipanua mipaka ya utawala wa Uislamu  katika eneo kubwa la ardhi – kutoka Uhispania hadi Asia ya Kati. Hata hivyo, wakati Waislamu waliporidhika mno katika masomo yao, ufahamu na utekelezaji wa Uislamu ndani ya Khilafah, na kuanza kuchukua fikra kutoka kwenye mifumo mengine, na wakawa wenye kuvutiwa na ming'aro ya dunia hii, basi dola ikawa dhaifu. Hii ikaipelekea kwenye ajenda na njama za mataifa ya kikoloni, ikaidhoofisha, na kufungua milango ya kushindwa kijeshi, migawanyiko, ukoloni na hatimaye kuvunjika.

Hivyo, Quran, Serah na historia yetu ya Uislamu kama Waislamu zinatupatia mafunzo mengi ambayo yatatujengea sisi uoni wa wazi usio na shaka kuwa Nidhamu ya Mwenyezi Mungu (swt), Khilafah, inaweza kusimama kwa msaada wa Mwenyezi Mungu (swt) licha ya nguvu na maendeleo ya dola za sasa zilizo na nguvu ambazo zinazuia kuregea kwake, kama tutafanya kazi kwa ajili yake kwa namna iliyo elekezwa na Dini yetu, kwa kuwa na utiifu kwa Bwana wetu (swt). Na kama tunaamini katika Ukubwa wa Mwenyezi Mungu (swt) na ukweli wa Dini yetu, basi tutakuwa na yakini kuwa majeshi ya Waislamu ya leo yanaweza kukomboa ndugu zetu na dada zetu wanaodhulumiwa nchini Syria, Palestina, Kashmir, China, Myanmar na kwengineko, bila kujali idadi ya majeshi ya mataifa mengine, kwani yanaitikia Wito wa Mwenyezi Mungu (swt) pekee: (nao ni) kuyahami maisha au ardhi za Waislamu. Hakika, ukweli na uhakika huu umejengeka katika maneno ambayo mara nyingi huyatamka lakini hushindwa kuyazingatia – La hawla wala quwwata illa billah – Hakuna hila wala nguvu isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu tu! Na bila shaka ni kuwa Mwenyezi Mungu (swt) atatoa ushindi kwa wale wanaotoa ushindi Kwake (swt) na Dini Yake. Mwenyezi Mungu (swt) anasema,

(فَهَزَمُوهُم بِإِذْنِ اللَّـهِ وَقَتَلَ دَاوُودُ جَالُوتَ وَآتَاهُ اللَّـهُ الْمُلْكَ وَالْحِكْمَةَ وَعَلَّمَهُ مِمَّا يَشَاءُ وَلَوْلاَ دَفْعُ اللّهِ النَّاسَ بَعْضَهُمْ بِبَعْضٍ لَّفَسَدَتِ الأَرْضُ وَلَـكِنَّ اللّهَ ذُو فَضْلٍ عَلَى الْعَالَمِينَ * تِلْكَ آيَاتُ اللّهِ نَتْلُوهَا عَلَيْكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّكَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ)

“Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu waliwatimua, na Daudi akamuuwa Jaluti, na Mwenyezi Mungu akampa Daudi ufalme na hikima, na akamfundisha aliyo yapenda. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawapambanishi watu kwa watu basi dunia ingeli haribika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya walimwengu wote. Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki. Na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.” [Al-Baqara: 251-252]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Dkt. Nazreen Nawaz
Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake Katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

#FromAffliction2Success      #MihnettenKurtuluşa    محن_ومنح#   

#KutokaMatatizoHadiMafanikio

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu