Alhamisi, 09 Rajab 1446 | 2025/01/09
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

“Ni Nani Atakaye Komesha Mauaji ya Halaiki Dhidi ya Waislamu wa Rohingya?”

Hotuba ya Dkt. Nazreen Nawaz, Mkurugenzi wa Kitengo Cha Wanawake Katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

(Iliyotolewa nje ya Ubalozi wa Bangladesh, Jijini London Mnamo Tarehe 9 Septemba 2017)

Kaka na Dada zangu wapendwa,

Kama mujuavyo, Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar kwa sasa wanakabiliwa na kampeni katili ya mauaji ya halaiki mikononi mwa serikali katili ya Myanmar, wanaandamwa kwa kisingizio cha urongo cha kupambana na ugaidi. Jinamizi hili ambalo ndugu na dada zetu wa Rohingya wanateseka nalo halielezeki. Kwa muda wa wiki mbili sasa, wanajeshi wa Myanmar na wakaazi walio jihami kwa silaha wa dhehebu la Budha wamekuwa wakitekeleza mauaji ya kinyama dhidi ya Waislamu wa Rohingya – wamekuwa wakiwamiminia risasi kiholela wanaume, wanawake na watoto, kuteketeza nyumba zao na vijiji vyao, wakiwakata kwa visu na mapanga raia wasiokuwa na hatia hadi kufa – yote kwa sababu tu wanasema “La-ilaha illallah...Mungu wangu si mwengine isipokuwa Allah!”.

Mamia ya ndugu zetu na dada zetu na watoto wao wameuwawa. Video za kuogofya za wanawake na watoto wakiuliwa kinyama na wauwaji hawa wa kibudha zimekuwa zikizunguka katika mitandao ya kijamii. Misikiti na Madrassa zimechomwa mpaka kuwa jivu. Na kwa uchache Waislamu wa Rohingya wapatao 270,000 wamekimbia Myanmar na kuelekea Bangladesh kutafuta hifadhi (kwa kukisia hii ni thuluthi moja ya Waislamu wote wa Rohingya wanaoishi Myanmar) – asilimia 80 yao wakiwa ni wanawake na watoto kulingana na shirika la UNICEF, huku maelfu wakiwa wamekwama bila ya chakula wala makao. Madazeni ya wanawake na watoto wa Rohingya wamekufa maji wakijaribu kukimbilia Bangladesh kwa mashua. Mlinzi wa mpakani wa Bangladesh alituma picha kwa shirika la CNN zinazo onyesha maiti za watoto wadogo zikitapakaa katika fuo za Mto Naf. La hawla wala quwatta illah billah!

Majeshi ya usalama ya Myanmar yamekuwa yakiwarushia maguruneti na risasi raia wanao kimbia na kujaribu kuvuka mpaka kuingia Bangladesh kutafuta hifadhi, na hivi majuzi kumekuwa na ripoti kuwa jeshi la Myanmar linatega mabomu ya ardhini katika mpaka wa Bangladesh kuwazuia wakimbizi wa Rohingya kutorudi, ambayo yamesababisha majeruhi mabaya kwa baadhi ya watoto wa Rohingya. Hasbunallah wa ni’mal wakeel!

Ripoti hizi zilizo ibuka kutoka Myanmar za mauaji haya ya halaiki dhidi ya ndugu zetu na dada zetu wa Rohingya na magaidi hawa wa kibudha kwa kweli ni za kuchukiza. Watoto wa Kiislamu kuchinjwa na wengine shingo zao kunyofolewa au kutupwa ndani ya maziwa, akiwemo mtoto mchanga wa miezi sita. Wanaume wa Kiislamu wakikusanywa na kutiwa ndani ya nyumba ya miti ya bamboo kisha kuwashwa moto na kuteketezwa hadi kufa.

Na yote haya ni miongoni tu mwa matukio mapya ya mauaji ya halaiki ambayo Waislamu wa Rohingya wanakumbana nayo katika miongo kadhaa ya mateso nchini Myanmar, ambapo dada zetu wamenajisiwa na magengi na kutazama watoto wao wakichinjwa mbele ya macho yao. Miongo ya kuishi katika uovu wa ubaguzi na umasikini uliokithiri, wakinyimwa haki msingi za elimu, huduma za afya na ajira, wakilazimishwa katika ndoa na sheria za kiimla za uzazi ili kudhibiti idadi yao, na kunyimwa uraia na serikali katili ya Myanmar, kuwapelekea kutokuwa raia wa serikali yoyote katika ardhi ambayo wameishi kwa vizazi na vizazi.

Hivyo basi nawauliza ndugu zangu na dada zangu, ni nani atakaye komesha mauaji haya ya halaiki dhidi ya Waislamu wa Rohingya? Ni serikali ipi iliyoko leo duniani itakayo jitokeza na kumaliza umwagaji damu huu? Ni serikali ipi iliyoko leo duniani yenye hisia ya maadili mema kusimama dhidi ya serikali ya Myanmar na kuwatetea Waislamu wa Rohingya, kuweka maisha ya wanadamu juu ya maslahi ya kisiasa au ya kiuchumi? Ni serikali ipi iliyoko leo duniani inayowakilisha kweli maslahi ya Waislamu ambayo itatia hofu ndani ya nyoyo za jeshi la Myanmar na makatili wa kibudha kiasi ya kuwa hawata subutu kumdhuru hata Muislamu mmoja wa Rohingya mwanamume, mwanamke au mtoto?

Tunajua wazi kuwa HAKUNA serikali aina hiyo, hakuna mfumo aina hiyo, hakuna taasisi yoyote ya kimataifa ulimwenguni leo itakayo weza kufanya haya kwa sababu tumeshuhudia mauaji ya halaiki nchini Syria…na ulimwengu haukufanya lolote; mauaji ya halaiki ya Waislamu nchini Afrika ya Kati… ulimwengu haukufanya lolote; mauaji ya halaiki ya Waislamu wa Kashmir, Somalia, Afghanistan, na kwengineko… ulimwengu pia haukufanya lolote!

Kaka na dada zangu, leo, kila serikali ulimwenguni inayaona mauaji haya ya halaiki, inasikia vilio vya wanawake na watoto wasio kuwa na hatia, inashuhudia udhalimu mbaya na mateso ya viwango visivyo elezeka…lakini inageuza macho yake, na kuosha mikono yake kutokana na jukumu lolote la kulinda maisha ya wasiokuwa na hatia… kwani kwa maoni yao… na kulingana na mfumo wao wa kinyama wa KIRASILIMALI… kuyaokoa maisha haya hakuna pato la kisiasa wala la kiuchumi ndani yake. Kisha eti wanadai kuwa DEMOKRASIA ni ustaarabu huku Sheria ya Kiislamu inayo wajibisha serikali inayo tawala kwayo kulinda wanadamu kutokana na unyama na udhalimu wa madhalimu, ni ya kikatili! Subhaanallah!

Kunyamaza kimya, na hata kukana kwa Aung San Suu Kyi, kiongozi wa kiimla wa Myanmar, na shabiki mkuu wa demokrasia, kuwepo na umwagaji damu huu na kampeni ya kinyama ya kikabila dhidi ya Waislamu na jeshi la nchi hiyo…na kwamba hali ni kama kawaida kwa serikali za kidemokrasia ulimwengu mzima katika mahusiano yao na serikali katili ya Myanmar… inafichua wazi kwa mara nyengine tena sura halisi ya nidhamu ya kibinadamu ya kidemokrasia ambapo dhulma na uchinjaji wa wasiokuwa na hatia hupuuzwa endapo maslahi yataamua.

Na kaka na dada zangu, kuhusu muitiko wa serikali na watawala katika ulimwengu wa Kiislamu juu ya mauaji haya ya halaiki dhidi ya Waislamu…muitikio wao umekuwa upi? Hali hii ni ya kuchukiza mno! Serikali ya Hasina nchini Bangladesh, badala ya kuwakaribisha Waislamu hawa wanaoteseka katika fuo zake na kuwapa hifadhi, bali imewaamuru walinzi wake wa mipakani kuwafurusha kutoka mipakani mwake…na kuwaacha wakifa maji katika mashua zao mbovu au kurudi katika ardhi ya mauaji ya Myanmar, au imewachukuwa na kuwaweka katika kambi duni zisizo kuwa na mahitaji msingi, na kukataa kuwatambua kama wakimbizi.

Maelfu ya Waislamu wa Rohingya wamekwama katika ardhi isiyomilikiwa na serikali yoyote katikati ya mpaka baina ya Myanmar na Bangladesh. Mapema mwaka huu, serikali ya Hasina ilifikiria hata kuwaondoa wakimbizi wa Rohingya na kuwapeleka katika kisiwa kilichoko sehemu ya chini eneo la Bengal ambacho hukumbwa na mafuriko ya mara kwa mara ambacho kimepewa lakabu ya 'kisiwa kisicho kaliwa' na mashirika ya kutetea haki. Subhaanallah! Lakini khiana ya Hasina imeongezeka zaidi, kwa kuwa serikali yake inapendekeza oparesheni ya pamoja na serikali katili ya Myanmar kusaidia ile inayoitwa oparesheni 'dhidi ya ugaidi', kwa jina jengine, kampeni ya mauaji ya halaiki dhidi ya Rohingya. La hawla wala quwatta illah billah!

Serikali khaini ya Pakistan pia haina uchungu wowote kuhusu kuongezwa nguvu zaidi jeshi katili la Myanmar na kudhulumu kwa kuwachinja kaka zao na dada zao wa Kiislamu. Mnamo 2015, ilitia saini mkataba wa kupeleka ndege kumi na sita za kivita aina ya JF-17 kwa jeshi la Myanmar, licha ya mauaji ya halaiki ya Rohingya yaliyotokea mnamo 2012. Ndege hizi zinatarajiwa kuanza kutumika kwa mara ya kwanza na jeshi la anga la Myanmar mwaka huu.

Na vipi kuhusu serikali ya Saudi Arabia, serikali za ghuba, Misri, na Jordan? Ziko tayari kutumia nguvu zao za kijeshi kuuwa na kuwanyima chakula watoto wa Yemen kwa kutii maagizo ya mabwana zao wa kimagharibi kuliko kutumia majeshi yao kuwaokoa watoto wa Kiislamu wa Myanmar!

Na vipi kuhusu Uturuki? Uturuki ambayo ni nchi ya saba kwa ukubwa wa jeshi ulimwenguni na ya pili kwa nchi za NATO… ni upi muitikio wa uongozi wake katika mgogoro huu? Raisi wake, Erdogan alichagua tu kujihusisha na hatua nyepesi ya kidiplomasia na kiongozi Suu Kyi, ikiwemo kumuomba ruhusa ya kupeleka misaada kwa Rohingya iliyo athirika na ghasia hizi. Subhaanallah! Kiongozi wa ardhi ambayo mwanzoni ilikuwa makao makuu ya dola kuu ya Khilafa, dola iliyokuwa na nguvu zaidi duniani iliyo wafanya maadui wa Uislamu kutetemeka kwa hofu… leo anaona haja ya kuomba ruhusa serikali inayo wauwa Waislamu kuwapelekea misaada wale wanao kimbia kichinjo cha serikali hiyo hiyo?! Subhaanallah! Hii inadhihirisha kiwango kikubwa cha idhlali ambayo viongozi wa Waislamu wamefikia leo!

Wakati huo huo Waziri wa Kigeni wa Uturuki alitoa wito kwa Bangladesh kufungua milango yake kwa wakimbizi wa Rohingya wanaokimbia ghasia, huku akisema kuwa Uturuki italipia gharama zote za mahitaji yao…akijaribu kujionyesha shujaa katika mkasa huu kwa njia ya kejeli. Tuna mwambia Erdogan na serikali yake…vipi kuhusu kuyaachilia huru majeshi yako kutokana na kuyatumikia maslahi ya serikali za kimagharibi na NATO na kuyashajiisha katika lengo lao halisi… kulinda damu ya Waislamu nchini Myanmar na ulimwengu mzima, kusimama dhidi ya wanao watesa Waumini, kuwaokoa kutokana na wauwaji wao…na kulipia GHARAMA ZOTE YA HAYA?! Erdogan alisema, "Wale wanao yafungia macho mauaji haya ya halaiki na kuendelea kufanya hivyo chini ya pazia ya demokrasia wote ni washirika kwa hili" – sisi tunasema – ndio Erdogan – hili ni kweli – linalo kufanya wewe na biladi zote za Kiislamu pia kuwa washirika katika uhalifu huu mkubwa…kwani nyote mumekaa kimya ilhali munaweza kusitisha umwagaji huu wa damu kupitia majeshi yenu!

Ni tofauti kubwa ilioje kati ya serikali hizi ovu za watawala Waislamu na vijana na mabinti watiifu wa Ummah huu waliojitokeza barabarani kwa wingi katika kila nchi ulimwenguni, (kutoka Indonesia mpaka Pakistan. Bangladesh mpaka Malaysia, na kwengineko, ikiwemo hapa Uingereza ambapo leo kutakuweko na maandamano nje ya Ubalozi wa Bangladesh jijini London yatakayo hudhuriwa na Waislamu kutoka kila pembe ya Uingereza). Wamejitokeza kudhihirisha uungaji mkono wao kwa kaka zao na dada zao Waislamu wa Rohingya na kuzitaka serikali za Waislamu kukata mahusiano na serikali katili ya Myanmar na kukomesha umwagaji damu huu. Serikali hizi zisizo na chembe ya uchungu hazistahili kutawala juu ya Ummah huu mtukufu hata kwa sekunde moja… zinahitaji kung'olewa…kwani Ummah huu unastahili uongozi utakao dhihirisha mapenzi kwa kaka na dada zake Waislamu kwa ajili ya dini yake.

Kaka na dada zangu wapendwa, hakuna serikali leo itakayo komesha umwagaji damu huu dhidi ya kaka na dada zetu Waislamu wa Rohingya…kwa hivyo ni juu yetu sisi, Ummah wa Rasulillah (saw) KUKOMESHA mauaji haya ya halaiki. Ili kufanya hivyo…haitoshi tu kuhisi uchungu na kumwaga machozi tunapoona yale yanayo endelea kwa kaka na dada zetu, au hata kuonyesha hasira, au hata kuwaombea dua tu. Ni lazima tuunganishe uchungu na hasira zetu kwa SULUHISHO lilio fafanuliwa na dini yetu litakalo komesha jinamizi hili kwao!

Na SULUHISHO hili ni kufanya kazi kusimamisha serikali iliyo na hisia ya maadili mema kusimama dhidi ya uhalifu huu muovu kwa wanadamu; serikali itakayo wakilisha kweli maslahi ya Waislamu na dini yetu; serikali ambayo kiongozi wake ame wajibishwa kuwa mlinzi wa Ummah huu na damu yake; serikali ambayo jeshi lake litakumbatia dori yake halisi ya kuwa mtetezi kwa Waislamu;  NA serikali ambayo NIDHAMU YAKE YA KIISLAMU itatoa himaya, maisha yenye hadhi na haki kamilifu za Uislamu kwa uraia kwa Waumini walio dhulumiwa bila ya kujali wanakotoka.

Serikali hii kaka na dada zangu, si nyengine isipo kuwa ni KHILAFAH katika njia ya utume, nidhamu ya Allah (swt), kwani, hakika Mtume (saw) amesema,     

إِنَّمَا الْإِمَامُ جُنَّةٌ يُقَاتَلُ مِنْ وَرَائِهِ وَيُتَّقَى بِهِ

Hakika Kiongozi (Imam) ni ngao, watu wanapigana nyuma yake na wanajihifadhi kwake.

Kwa hivyo, tunawalinganieni enyi kaka na dada zetu kutoa juhudi zenu zote katika ubebaji wa da'wah hii ya kusimamisha serikali ya Khilafa Rashidah ili tukomeshe uchinjaji huu wa Ummah wetu nchini Myanmar na ulimwengu mzima na kurudisha izza kwa Waumini na kwa dini yetu. Fanyeni kazi na sisi kama Hizb ut Tahrir kusimamisha serikali hii tukufu ambayo haitapumzika mpaka kila serikali dhalimu ibadilike kuwa historia na haki itawale katika dunia hii.

Na kwa maafisa wa kijeshi Waislamu katika ulimwengu wa Kiislamu, tuna walingania kuitikia vilio vya kaka zenu, dada zenu na watoto wenu Waislamu wa Rohingya wanao waomba kuja kuwahifadhi. Ukombozi wao uko mikononi mwenu. Musifuate njia ya watawala wenu walio andaliwa makaazi yao Jahannam kwani wame wakhini Waislamu na dini hii. Toeni nusra (nguvu za kijeshi) yenu haraka iwezekanavyo kwa uongozi shujaa wa Hizb ut Tahrir kusimamisha serikali ya Khilafa itakayo wahamasisha mara moja kuhifadhi damu ya Ummah wenu, na kuufanya urithi wenu ule unao fanana na wa mashujaa wakubwa katika dini hii mfano wa Salahuddin Ayubi na Muhammad ibn Qasim…na kuwaletea heshima katika maisha haya ya duniani na ujira mkubwa kesho Akhera.

Na Allah (swt) asema,

وَمَا لَكُمۡ لَا تُقَـٰتِلُونَ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ وَٱلۡمُسۡتَضۡعَفِينَ مِنَ ٱلرِّجَالِ وَٱلنِّسَآءِ وَٱلۡوِلۡدَٲنِ ٱلَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَآ أَخۡرِجۡنَا مِنۡ هَـٰذِهِ ٱلۡقَرۡيَةِ ٱلظَّالِمِ أَهۡلُهَا وَٱجۡعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ وَلِيًّ۬ا وَٱجۡعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ نَصِيرًا

Na muna nini musipigane katika njia ya Allah na ya wale wanao onewa, miongoni mwa wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola wetu! Tutoe katika kijiji hiki ambacho watu wake ni madhalimu, na tujaaliye tuwe na mlinzi anaye toka kwako, na tujaaliye tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako. [An-Nisa: 75]

Dkt. Nazreen Nawaz
Mkurugenzi wa Kitengo Cha Wanawake Katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 07:27

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu