Jumanne, 21 Rajab 1446 | 2025/01/21
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Kufahamu Uke na Uume katika Uislamu

(Imetafsiriwa)

Uke na uume ni miundo mizito ya kijamii ambayo imekuwa na mabadiliko kadri muda unavyopita, ikiundwa na tamaduni, dini, na fikra tofauti tofauti. Miundo hii inafafanua kile kinachochukuliwa kuwa suluki, dori, na sifa “zinazofaa” kwa wanaume na wanawake katika jamii. Walakini, mitazamo tofauti ya ulimwengu ina tafsiri tofauti za kile kinachojumuisha uume na uke. Makala haya yanaangazia mitazamo ya Kimagharibi na Kiislamu juu ya miundo hii, yakiangazia udhaifu wa mtazamo wa Kimagharibi, hasa kwa kuzingatia sintofahamu za hivi karibuni, kama vile kesi ya bondia wa Algeria anayeshiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Paris, ambayo inasisitiza msimamo tata na aghlabu wa kinafiki wa mtazamo wa Magharibi kuhusu jinsia.

Mitazamo ya Magharibi juu ya Uke na Uume

Katika ulimwengu wa Magharibi, fahamu za uke na uume zimepitia mabadiliko makubwa. Kutoka kwa kanuni ngumu za kijinsia za karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 hadi mnyumbuko zaidi na “jumuishi” wa ufahamu katika nyakati za kisasa, mitazamo ya Magharibi juu ya jinsia imeundwa na mambo ya kihistoria, kitamaduni, kijamii na kisaikolojia.

Kijadi, jamii za Kimagharibi mara nyingi zimesawiri uume na uke kwa maneno ya pande mbili na yanayopingana. Uume ulihusishwa na nguvu, busara, uthabiti, na uongozi, wakati uke ulihusishwa na malezi, huruma, urembo, na unyumba. Miundo hii iliathiriwa na miundo ya mfumo dume ambayo ilifafanua wanaume kama viongozi na watoaji matumizi na wanawake kama wafuasi na waundaji familia. Wanawake walichukuliwa kuwa wenye werevu mchache na wasio na uwezo wa mambo fulani, kama vile kupiga kura na kufanya kazi.

Kwa kuongezeka kwa ufeministi, vuguvugu la haki za kiraia, na wanaharakati wa LGBTQ+ katika karne ya 20, ufafanuzi huu mgumu ulianza kutiliwa shaka na kusambaratishwa. Mitazamo ya kisasa ya Kimagharibi inazidi kuona uume na uke kama fahamu ya nyumbufu, iliyobuniwa kijamii badala ya vibainishi vya kibayolojia visivyo badilika. Jinsia inaonekana kama wigo, ambapo watu binafsi wanaweza kudhihirisha sifa za “kiume” na “kike”, bila kujali jinsia yao ya kibaolojia. Hii imesababisha kukubalika zaidi kwa utambulisho usio wa pande mbili, waliobadili jinsia, na wa ambao hawajaamua jinsia, na kutoa changamoto kwa jozi za jadi za uume na uke.

Mtazamo wa Kimagharibi kuhusu jinsia unasalia kuwa umejaa ukinzani na unafiki, hasa unapotazamwa kupitia jicho la matukio ya hivi majuzi kama vile sintofahamu inayomhusisha bondia wa Algeria kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris. Bondia huyo ambaye ni mwanamke kibaiolojia, amekosolewa na baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na mamlaka za michezo kwa madai ya kumiliki viwango vya juu vya homoni za “kiume” na kupendekeza kuwa asiruhusiwe kushindana na wanawake wengine.

Sintofahamu hii inazidi kupambanua hasa inapounganishwa na ongezeko la kukubaliwa kwa wanawake waliobadili jinsia (wanaume wa kibaolojia wanaojitambulisha kuwa wanawake) katika michezo ya wanawake katika nchi za Magharibi. Sauti nyingi zile zile zinazomkosoa bondia huyo wa Algeria kwa viwango vyake vya kimaumbile vya homoni pia zinatetea kujumuishwa kwa wanawake waliobadili jinsia katika michezo ya wanawake, ingawa wanariadha hawa wanaweza kuwa na faida za kibaolojia kutokana na kubalehe kwa wanaume.

Kizungumkuti hiki kinaangazia kutofautiana kwa kina katika ufahamu wa Magharibi wa uke na uume. Kwa upande mmoja, mwanamke wa kibaolojia aliye na tofauti za kimaumbile za homoni anakosolewa na kuhukumikiwa, wakati kwa upande mwingine, wanaume wa kibaolojia wanaojitambulisha kama wanawake wanakubaliwa kama wanawake kamili, hata kama wanadumisha faida fulani za kimwili. Hii inafichua dosari ya kimsingi katika simulizi ya Kimagharibi: fahamu ya usawa wa kijinsia inapigiwa debe, lakini kibaguzi na mara nyingi kwa gharama ya wanawake wa kibaolojia.

Mitazamo ya Kiislamu juu ya Uke na Uume

Mtazamo wa Kiislamu juu ya uke na uume umekita mizizi katika mafundisho ya Quran, Hadith (maneno na matendo ya Mtume Muhammad), na mtazamo jumla wa Kiislamu wa ulimwengu (Tawhid). Uislamu unatoa mfumo makhsusi wa kuelewa dori za kijinsia, majukumu, na madhihirisho, ambao mara nyingi hutofautiana na dhana za kisasa za Magharibi.

Kanuni za Msingi

Katika Uislamu, wanaume na wanawake wote wanaonekana kuwa sawa mbele ya Mwenyezi Mungu (Allah), lakini wanachukuliwa kuwa na dori na majukumu tofauti, yenye kukamilishana. Ukamilishano huu hauonekani kama daraja bali kama uwiano uliowekwa na Mungu ambapo kila jinsia inatimiza dori yake ndani ya familia na jamii. Quran inasema,

[وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ]

“Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.” [Quran 30:21].

Uke katika Uislamu

Uke wa Kiislamu unasifiwa kwa sifa kama vile haya, huruma, malezi na nguvu za kiakhlaki. Fahamu ya haya inasisitizwa hasa kwa wanawake katika suluki na mavazi. Hata hivyo, haya hii hauonekani kuwa ishara ya udhaifu au ukandamizwaji; badala yake, ni chaguo makini kudumisha utu na kulinda nafsi kindani na kinje.

Uislamu pia unatambua dori muhimu ya mwanamke katika jamii zaidi tu ya majukumu ya kinyumbani. Wanawake kama Khadija binti Khuwaylid (ra), mke wa kwanza wa Mtume Muhammad (saw), walikuwa wafanyibiashara wanawake wenye mafanikio na wanaheshimika katika historia ya Kiislamu. Aisha binti Abi Bakr (ra), mke mwengine wa Mtume (saw), anajulikana kwa mchango wake wa kielimu na anachukuliwa kuwa mmoja wa watu muhimu sana katika fiqhi ya awali ya Kiislamu.

Uume katika Uislamu

Uume wa Kiislamu mara nyingi huhusishwa na sifa kama vile nguvu, ujasiri, haki, na uadilifu wa kimaadili. Hata hivyo, sifa hizi huchochewa na mkazo wa unyenyekevu, upole, na huruma. Mtume Muhammad (saw) anachukuliwa kuwa kielelezo bora cha uume wa Kiislamu, akichanganya nguvu na uongozi na huruma, unyenyekevu, na heshima kwa wanawake. Wanaume kwa jumla huonekana kama watoaji matumizi na walinzi katika familia, lakini hii inasawazishwa na msisitizo wa ushirikiano, wema, na majukumu ya pamoja. Kwa mfano, Mtume Muhammad mara nyingi alisaidia kazi za nyumbani na alisisitiza umuhimu wa kuwatendea wanawake kwa heshima na utu.

Hitimisho

Sintofahamu inayomzunguka bondia wa Algeria kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris inaangazia dosari ya kimsingi katika ufahamu wa Kimagharibi wa uke na uume: matumizi yasiyo na mashiko ya kanuni zake yenyewe ambazo aghalabu husababisha matokeo ya kutatanisha. Ingawa mitazamo ya Kimagharibi inazidi kusisitiza uwazi na kuvunjwa kwa kanuni za jadi, mtazamo wa Kiislamu unazingatia usawa, ukamilishano, na mwongozo wa kimungu.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Sumaya Bint Khayyat

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu